ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, July 22, 2023

MAKALA:KAMPUNI YA TAIFA GESI YANUNGANA NA SERIKALI KUDHIBITI WIMBI LA UKATAJI WA MITI MKOA WA PWANI.

 


Na Victor Masangu,Pwani 

Mkoa wa Pwani umetajwa kuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na hii ni kutokana na kuwepo kwa wimbi kubwa la wananchi kukata miti ovyo pamoja na kutumia kwa kasi matumizi ya mkaa hali ambayo imesababisha kila kukicha hali ya mazingira kuwa mbaya zaidi na maeneo mengine kuwa kama jangwa.

Mkoa wa Pwani umeonekana kinara zaidi kwa uharibifu wa mazingira na hii yote ni kutokana na  wananchi kuamua kwenda katika baadhi ya maeneo na kuamua kukata miti hiyo kwa ajili ya matumizi ya mkaa,pamoja na kuni kitu ambacho kinachangia zaidi hata kupotea kwa uoto wa asili.


Uchunguzi ambao umefanyika na mwandishi wa habari hizi umeweza kubaini kwamba katika baadhi ya halmashauri tisa ambazo zipo katika Mkoa wa Pwani baadhi yake zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mazingira kuharibika kutokana na changamoto hiyo ya ukataji wa miti ovyo na wengine bila hata ya kuwa na vibali maalumu.

Changamoto ya ukataji wa miti ovyo bila ya kuwa na vibali uchunguzi umebaini  nayo ndio imekuwa ni chanzo kikubwa ya baadhi ya watu hasa katika maeneo ya vijijini kwenda katika maeneo hayo na kukata miti kinyemela hasa katika nyakati za usiku na baada ya hapo kutumia miti hiyo kwa matumizi ya mkaa pamoja na kuni bila kujua madhara yake katika siku za zijayo.


Kutokana na hali hiyo pia imebainika kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakishirikiana na madereva wa pikipiki maarufu (boda boda) kwa ajili ya kusafirisha magunia ya mkaa hasa katika nyakati za usiku wakisafirisha magunia hayo kuyapeleka katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es salaam kwa lengo la kuweza kujipatia kipato.


Pamoja na hali hiyo mwandishi wa habari hizi aliweza kujionea jinsi ya magunia zaidi ya nane hadi kumi yakiwa yamepakiwa katika baadhi ya  boda boda uku wakiwa wanatumia njia za vichochoroni ili kukwepa kukamatwa na mamlaka husika kwani wengine hawana vibali kwa kusafirisha nishati hiyo ya mkaa.

Lakini pamoja na serikali kupiga marufuku uharibifu wa mazingira ovyo bila kuzingatia sheria na taratibu lakini bado kuna baadhi ya madereva wa boda boda kuendelea kushirikiana na baadhi ya watendaji katika kuendelea kukata miti ovyo ili kuweza kupata kuni pamoja na mkaa bila ya  kujali kabisa athari zake.

Kutokana na kuendelea na wimbi hilo la ukataji wa miti ovyo umesababisha pia kwa kiasi kikubwa kuharibu miundombinu ya barabara kutokana na kuchimba mashimo makubwa kwa ajili ya kuweza kuchoma miti hiyo ili kupata mkaa bila kuangalia ni namna gani wananchi wenye makazi yaliyo jirani kutokana na kufuka kwa moshi wakati wa kuni au magogo hayo yanapochomwa moto.

Boda boda hao pia wamekuwa wakivunja sheria za barabarani huku wakiwa wamebeba magunia hayo mpaka wanashindwa kukaa vizuri katika kiti na wakati mwingine wamekuwa wakisababisha ajali na baadhi yao kupata majeraha na vilema vya kudumu kutoka na kazi hiyo wanayoifanya.


Baadhi ya madereva wa boda boda ambao wanajishughulisha na kusafirisha nishati hiyo ya mkaa kwa masharti ya kutotajwa majina yao wamesema kwamba wameamua kujikita katika kazi hiyo kutokana na kukabiliwa na changamoto ya fursa za ajira lakini serikali ikija na mpango wa kuwasaidia wapo tayari kuachana na uharibifu wa mazingira.


Wamesema kwamba wengi wao wamekuwa wakienda katika maeneo ya vijijini na kushirikiana na wahusika katika kukata miti hiyo kwa lengo la matumizi ya nishati ya mkaa pamoja na kuni ambazo zimekuwa zikitumika hasa katika maeneo ya vijijini.


"Kutokana na kazi hii ya kubeba magunia ya mkaa tunapitia changamoto nyingi sana ikiwemo kukamatwa na mamlaka husika TFS na wakati mwingine tunapewa adhabu na kutulipisha faini kwani tumeshakatazwa kufanya kazi hii bila ya kuwa na vibali kwa hiyo serikali ikiweka mazingira vizuri ya nishati mbadala basi sisi tupo tayari kwa matumizi mengine ya gesi,"wamebainisha boda boda hao.

Kadhalika wamebainisha kuwa baadhi ya boda boda hao wamesema kwamba rafiki zao wameshaamua kuachana kabisa na shughuli hizo za kusafirisha mkaa kutokana na kuona athari zake mbali mbali ikiwepo suala la kupata ajari na kukamatwa kila kukicha.

Wakitoa ushuhuda mwingine wameongeza kuwa wakati mwingine wamekuwa wakikimbizana na TFS na kusababisha kuanguka na mwisho wa siku wanataifishwa magunia hayo ya mkaa na hatimaye kujikuta wanaingia hasara kwani wakati mwingine wanapigwa na pikipiki kuchukuliwa.

Mmoja mwingine wa boda boda anayeishi Wilaya ya Kibaha amesema kuwa alishakumbwa na mkasa wa kukamatwa na TFS pindi alipokuwa amebeba mkaa na alipokonywa pikipiki yake lakini alipata msaada wa kupatiwa elimu juu ya matumizi mabaya ya uharibifu wa mazingira.


Aidha dereva huyo akusita baadhi ya wadau mbali mbali ambao waliweza kumsaidi kwa dhati kuweza kumpa elimu zaidi ya madhara ya uharibifu wa mazingira pamoja na umuhimu wa kutumia nishati mbadala ya Taifa gas ili kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni.

Nao baadhi ya wananchi wa Mkoa ambao wameachana kabisa na matumizi ya kuni pamoja na mkaa wamesema kuwa ujio wa uwepo wa nishati ya Taifa gas umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa changamoto ya uharibifu wa mazingira katika maeneo mbali mbali.

Pia wananchi hao wameishauri serikali kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi hasa wa vijijini juu ya madhara ya ukataji wa miti ovyo sambamba na kuweka mipango madhubuti ya kuzalisha mitungi ambayo itakuwa na ujazo wa aina tofauti ili kumudu gharama za kununua.

Kwa Upande wao wadau wa mazingira katika Mkoa wa Pwani waliomba mamlaka zote zinazohusika ikiwemo TFS kuongeza nguvu zaidi katika kudhibiti hali ya uharibifu wa mazingira ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji kwa kushirikiana na wananchi wenyewe.

Pia hawakusita kuwatoa mawazo yao kwa kuwataka  Wakala wa misitu TFS kutokaa barabarani kwa ajili kuwakamata madereva wa boda boda na badala yake wafanye ziara katika maeneo husika lengo ikiwa ni kuwadhibiti wale wote ambao wanafanya uharibifu kwa kukata miti ovyo.


Katika kuliona hilo serikali imezindua kampeni maalumu ya utunzaji wa mazingira na matumizi sahihi ya nishati mbadala ambayo imezinduliwa hivi karibuni katika shule ya sekindari Ruvu ambayo itasaidia kuachana na matumizi ya mkaa na miti.

Kuzinduliwa kwa kampeni hiyo kwa kuanzia katika Mkoa wa Pwani imeanza kuzaa matunda kutoka na wadau wa mazingira,halmashauri mbali mbali kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mtaa na vijiji kuanza juhudi za kurudisha hali halisi kwa kuanza kupanda miti.

Pia kumekuwepo na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya hali nchi hivyo serikali kuzindua kampeni hiyo pia itaweza kuwa mkombozi kutokana na ushirikiano ambao umeshaanza kufanyika kuanzia ngazi za chini hadi ngazi za juu.

Nao baadhi ya mama lishe wanaofanya biashara zao katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Pwani wamenufaika na matumizi ya nishati mbadala ya gesi wamesema imeweza kuwasaidia kuondokana na kutumia kuni na mkaa kwani itasaidia kuunga juhudi za serikali katika kutunza mazingira.

Pia Mama lishe hao wameipongeza serikali kwa kuleta nishati mbadala na kuiomba iweze kubuni zaidi mitungi mingine midogo ambayo wataweza kuinunua kwa bei nafuu ili kuweza kuachana kabisa na matumizi ya mkaa na kuni.

"Baadhi yetu hapo awali sisi mama lishe katika miaka ya nyumba tulikuwa tunatumia kwa wingi matumizi ya kuni lakini wakati mwingine madhara yake ni makubwa kutokana na kupuliza moto hivyo ule moshi ulikuwa unatuingia kwenye kifua ni hatari kwa afya hivyo nishati hii mbadala ya gesi  ni sahihi zaidi,"wamesema mama lishe.

Katika kutekeleza kampeni hiyo serikali kupitia Waziri  wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk.Selemani Jafo amesema kwamba mpango huo utasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuwahimiza wananchi waweze kutunza mazingira katika maeneo yao.

Aidha Waziri huyo amesisitiza kwa kunahitajika juhudi za ushirikiano kutoka kwa mamlaka mbali mbali zinazohusika ikiwemo TFS,WWWF, na wadau wengine wa mazingira ili kuweza kufanikisha zoezi la kampeni hiyo ikiwa pamoja na wananchi.


Jafo amebainisha kuwa kuwepo kwa nisgati mbada ya Taifa gesi kutaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kupunguza zaidi wimbi la ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira na kuongeza kuwa serikali itakuwa mstari wa mbele katika kutimiza azma ambayo imejiwekea ya kudhibiti uharibifu wa mazingira.

Amebanisha hivi karibuni kampeni hiyo imezinduliwa Wilayani Kibaha katika shule ya sekondari Ruvu hivyo ni vema wahusika hususan Taifa gesi wanapaswa kuangalia namna ya kufunga mitambo katika shule za sekondari ili waweze kutumia nishati hiyo mbadala.



"Hivi karibuni niliweza kupata fursa ya kuhudhuria uzinduzi wa kampeni ya utunzaji wa mazingira kwa hivyo sisi kama serikali  ninawaomba wahusika aa Taifa gesi kuweka mipango ya kufunga mitambo ya gesi katika shule mbali mbali za sekondari na taasisi za umma hii itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira,"amesema Waziri Jafo.



Amefafanua kuwa ana imani kwamba mitambo hiyo ya gesi ikifungwa katika shule hasa za bweni kutakuwa ni njia moja wapo ya juhudi za kupunguza wimbi la ukataji wa miti ovyo na kuondokana na matumizi ya mkaa pamoja na kuni ambapo pia itapunguza gharama za matumizi.


Dk. Jafo amesema kwamba pia kuzinduliwa kwa kampeni hiyo ya utunzaji wa miti   pia itasaidia  kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yamekuwa na athari katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo katika Mkoa wa Pwani.

"Bado kuna shule za sekondari bado kwa sasa zinaendelea na matumizi ya nishati ya kuni pamoja na mkaa lakini nina imani kampeni itaweza kuleta mabadiliko chanya ya kuweza kutumia nishati mbadala kuliko kutumia kuni kwani ndio chanzo cha uharibifu wa mazingira,"anasisita Jafo.



Waziri Jafo ameipongeza kwa dhati juhudi ambazo zimefanywa na Kampuni ya Taifa gesi kwa kuanza utekelezaji wa agizo la Serikali la matumizi ya Nishati Mbadala kwa kuanza kufunga mtambo wa gesi katika shule hiyo.


Jafo meongeza kwamba kati ya mikoa  minne hapa nchini ambayo imeathirika kwa uharibifu wa Mazingira Pwani ni mojawapo ambapo alimpongeza Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge kwa jitihada anazozifanya za kusimamia kampeni ya kupanda miti.


Katika hatua nyingine Waziri Jafo amewasisitiza zaidi wananchi wa Mkoa wa Pwani na hawatajikita kwenye matumizi ya nishati mbadala mabadiliko ya tabia ya nchi yataendelea kuleta athari kubwa.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nikson Saimon amebainisha changamoto kubwa iliyopo ya Wilaya yake ipo karibu jirani na Jiji la Dar es Salaam hivyo kusababisha uharibifu wa mazingira.

Mkuu huyo alisema kuwa hata hivyo bado kuna juhudi za makusudi ambazo zimeshaendelea kufanyika katika kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira linafanyika katika halmashauri zote ikiwemo kupanda miti katika maeneo ambayo yameathiliwa zaidi.


 Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaji Abubakar Kunenge amewataka viongozi na watendaji wote wakiwemo wa Chama kuhakikisha wanatekeleza maelekezo yote ambayo yanatolewa na Rais wavawamu ya sita Dkt.Samia Suluhu katika kujikita katika kupambana na ukataji wa miti ovyo.

"Maagizo ambayo yanatolewa lazima tuyafangie kazi likiwemo hili la Mkoa wetu kukabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira na katika hili mimi naomba tulifanyie kazi kuanzia katika ngazi za chini hadi za juu," anasema Kunenge.



Pamoja na hayo Kunenge amewahiza wananchi wote kuachana kabisa na vitendo vya uharibifu wa mazingira  kwa kukata miti na kuchoma mkaa na badala yake  kujikita zaidi kupanda miti ili kurudisha uoto wa asili.


Mkuu huyo wa Mkoa anasema katika kutimiza mpango wa serikali kwa Sasa tayari wameshaendelea kufanya kampeni ya utunzaji wa mazingira ambapo wameshafanikiwa kupanda miti zaidi ya milioni 9.7.



Katika hatua nyingine anasema kwamba kampeni hiyo ambayo imezinduliwa katika Mkoa wake utaweza kuleta matokeo chanya katika suala zima la kupambana wimbi la ukataji wa miti kiholela na kuweka mipango zaidi katika kupanda miti na kutunza mazingira.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo katika kuunga mkono juhudi za serikali wamepiga marufuku kwa madereva wa boda boda kupakia magunia ya mkaa na kutasafirisha kuelekea Jijini Dar es Salaam.

Kamanda huyo anasisitiza kuwa kumekuwepo kwa ajali nyingi ambazo chanzo chake kinasababishwa na na baadhi ya madereva wa  boda boda kuvunja sheria za barabarani huku wakiwa wamepakia nishati hiyo ya mkaa zaidi ya magunia name.

Jeshi hilo la Polisi Mkoa wa Pwani limesema litaendelea kudhibiti upakiaji holela wa mkaa huo pamoja na kuwakamata wale wote ambao watabainika kwenye kinyume na kuongeza wataendelea kutoa elimu kwa madereva hao juuu ya madhara ya ukataji miti.

Wananchi wa Wilaya ya Mkuranga  na Rufiji  nao hakusita kuzungumzia madhara ambayo yamewakumba kutokana na tatizo la ukataji wa miti ikiwemo suala la uharibifu wa mazingira pamoja na kupoteza uoto wa asili.


Hivi karibu serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Taifa gasi ilizundua kampeni maalumu kwa ajili ya utunzaji wa mazingira pamoja na matumizi ya nishati mbadala iliyofanyika katika shule ya sekondari Ruvu Wilayani Kibaha mkoani Pwani lengo ikiwa ni kuondokana na kuthibiti matumizi ya kuni na mkaa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.