ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, September 22, 2023

Benki ya CRDB kuendelea kurahisisha ukusanyaji mapato Hospitali ya KCMC

 


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Benki ya CRDB na Hospitali ya Kanda ya KCMC iliyopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, zimeingia makubaliano ya kuendelea kuifanya Benki ya CRDB kuwa mtoaji wa huduma za fedha hasa ukusanyaji mapato hospitalini hapo.

Azma ya Benki ya CRDB siku zote ni kuhakikisha inatoa huduma bora na shindani zinazokidhi mahitaji ya wateja wake ikiamini kuwa huduma bora, za kisasa, jumuishi na rahisi za fedha ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Hivyo, Benki ya CRDB imewekeza rasilimali zake katika ubunifu wa huduma na bidhaa zake, ikiwamo kuanzisha na kuboresha kiendelevu mfumo wa upokeaji na ufanyaji malipo kwa njia za kieletroniki unaotumika kwenye taasisi tofauti ikiwemo hii ya Hospitali ya KCMC.

Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema Hospitali ya KCMC ni moja ya taasisi za mwanzo kuingia ubia na Benki ya CRDB kutumia mfumo huu wa malipo, mwaka 2014. Ubia huu ulienda sambamba na uzinduzi wa kadi maalum ya malipo ya Hospitali ya KCMC iliyopewa jina “TemboCard KCMC.”

Katika mwaka wa kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo hospitalini hapo, zaidi ya shilingi bilioni 4.1 zilikusanywa na mpaka mwaka 2022, makusanyo hayo yameongezeka mara mbili na kufika shilingi bilioni 8.7 kwa mwaka.

“Tangu tulipoingia mkataba na Hospitali ya KCMC kuanza kuutumia mfumo wetu mpaka mwaka jana, tumeiwezesha Hospitali ya KCMC kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 52.8. Hiki ni kiasi kikubwa kukusanywa ndani ya miaka minane na makusanyo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka,” amesema Raballa.

Raballa amesema katika kuimarisha ushirikiano na hospitali na pia ili kusogeza karibu zaidi huduma kwa wateja wake mwaka 2020 Benki ya CRDB ilifungua tawi hospitaini hapo. Tawi hilo linawafaa pia wafanyakazi wa hospitali, wanafunzi wanaojifunza hospitalini hapa, wagonjwa, wafanyabiashra na wananchi kwa ujumla wanaoishi au kupita maeneo ya hospitali.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema kabla hawajaanza kutumia mfumo wa Benki ya CRDB, walikuwa wanakusanya mapato kidogo na kuna nyakati walilipwa hata kwa fedha bandia .

“Kama mnavyofahamu uendeshaji wa hospitali ni wa gharama kubwa, hivyo usimamizi wa mapato ni kati ya vipaumbele muhimu vya hospitali yoyote. Ndio maana leo tupo tena hapa kuuhuisha mkataba wetu ili kuendelea kuwa na ufanisi mkubwa katika ukusanyaji wa mapato yetu,” amesema Profesa Masenga.

Awali, mkurugenzi huyo amesema wahasibu walilazimika kukaa na fedha nyingi kwenye ofisi zao jambo lililokuwa linawaweka kwenye hatari ya kuvamiwa hivyo kupoteza mapato ya hospitali ndio maana mwaka 2004 ilikuwa rahisi kwa menejimenti ya hospitali kushawishika kuingia makubaliano na Benki ya CRDB kutumia teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato na kwamba mfumo huu umeondoa makosa ya kibinadamu kwa kiasi kikubwa hivyo kuongeza makusanyo.

Profesa Masenga pia amesema uhusiano wa Benki ya CRDB na Hospitali ya KCMC hauishii kwenye huduma za benki pekee kwani wao ni miongoni mwa wanufaika wa uwekezaji unaofanywa kwa jamii na Benki ya CRDB.

Profesa Masenga amesema Benki ya CRDB imewajengea eneo la mapumziko kwa wagonjwa na wasaidizi wao, na mara kadhaa imewasaidia vifaatiba na kompyuta ili kuboresha utoaji wa huduma hospitalini.

Kutokana na makubaliana haya, sio hospitali pekee itakayonufaika na mfumo huu bali pia wale wote wanaohudumiwa hospitalini hapa. Malipo sasa yatakuwa yanafanyika kutumia ‘control number’ . Hivyo yeyote anayehudumiwa Hospitali ya KCMC hata hitaji kufanya malipo kwa fedha taslimu, hivyo kuweza kufanya malipo kielektroniki.

Mhudumiwa ataweza kulipa kwa kutumia kadi za benki ikiwemo za Visa na MasterCard, pia ataweza kutumia SimBanking, internet banking na pia CRDB wakala. Malipo haya ya kisasa yanamwezesha mfanya malipo yoyote kulipia huduma ya kwake au ya mtu mwingine moja kwa moja hospitalini, akiwa popote alipo, ndani au nje ya nchi ilimradi awe na control number, ulipo tupo!








Huduma za uzazi wa mpango zaimarika Simiyu, mwanaume aridhia kufunga kizazi

 

Mwanaume mmoja katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ameridhia kufunga mirija ya uzazi kama njia ya kudumu ya uzazi wa mpango, kwa lengo la kuwa na watoto wachache anaomudu kuwahudumia.

Mwanaume huyo, John Sayi (47) mkazi wa Kijiji cha Sulu Kata ya Mbalagani amesema tayari ana watoto sita hivyo ameridhia kwa hiari uamuzi huo baada ya kupata elimu ya umuhimu uzazi wa mpango kupitia vyombo vya habari.

“Nilipata msukumo kutoka kwa baba mzazi ambaye alikuwa na wanawake wanne lakini hakutana kuwa na watoto wengi kwani alizaa watoto sita tu. Wake zake watatu kila mmoja alizaa mtoto mmoja akiwemo mama yangu na mwingine alizaa watoto watatu” amesema Sayi.

Amesema alipata nafasi ya kuongea na baba yake ambaye ametangulia mbele za haki aliyemweleza kwamba alikuwa akitumia njia ya asili ya uzazi wa mpango hivyo na yeye ikamuingia akilini kuwa na watoto wachache.

Mwaka 1998 Sayi alioa mke wa kwanza na kuzaa naye watoto wawili kabla ya kutengana mwaka 2002 ambapo kwa sasa anaishi na mke wa pili aliyemuoa mwaka 2,000 na kujaaliwa kupata watoto wanne hadi alipofunga mirija mwaka huu 2023.

“Wasukuma tuna tabia ya kuzaa watoto wengi, mwanaume ukimwambia mwanamke aache kuzaa anafikiri akifanya hivyo utaendelea kuzaa na wanawake wengine hivyo nilipomwambia mke wangu nataka kufunga uzazi aliamini nimedhamiria kutoendelea kuzaa” amesema Sayi na kuongeza na kukubaliana nami;

“Kwenye tendo la ndoa najisikia vizuri maana kwa sasa nachelewa kumaliza tofauti na hapo awali, wengi hatupendi kumaliza mapema hivyo wanaume wenzangu wasiwe na hofu kwamba ukifunga mirija ya uzazi utapata madhara” ameeleza Sayi.

Inaelezwa watu wengi wamekuwa wakitumia njia za uzazi wa mpango za muda mfupi na muda mrefu ambazo ni pamoja na vidonge, vipandikizi, vitanzi na kondomu tofauti na ilivyo kwa njia ya kudumu ambayo ni kufunga mirija ya uzazi kama alivyofanya Sayi.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH, Mratibu wa afya ya uzazi na mpango mkoa wa Simiyu, Mary Makunja amesema wanawake wanaoongoza kwa kutumia uzazi wa mpango ikilinganishwa na wanaume.

“Kabla ya mradi huduma za uzazi wa mpango zilikuwa asilimia 36 mwaka 2022 lakini kwa sasa (2023) ni asilimia 45 huku idadi ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya/ hospitali ikifikia asilimia zaidi ya 90” amesema Makunja.

Amebainisha kuwa mwitikio wa kutumia njia za uzazi wa mpango za muda mfupi na mrefu ni mkubwa ikilinganishwa na njia ya kudumu; akisema “kwa mwaka idadi ya wanawake wanaoridhia kufunga mirija ya uzazi inafikia 100 huku wanaume wakiwa kati ya mmoja hadi watatu”.

Makunja ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa jamii ya wakazi wa Simiyu kutumia uzazi wa mpango hatua itakayowasaidia kuwalea vyema watoto wao tofauti na ilivyo sasa ambapo mwanamke anaweza kuwa na nzao kati ya saba hadi kumi jambo ambalo ni hatari kiafya.

“Jamii ya watu wa huku asilimia kubwa ni wakulima hivyo wanaona ni fahari kuoa mwanamke zaidi ya mmoja na kuzaa watoto wengi wakiamini watawasaidia kwenye shughuli za uzalishaji mali hivyo tunaendelea kuwaelimisha” amesema Makunja.

Kutokana na umuhimu wa uzazi wa mpango katika kukabiliana na vifo vya uzazi kwa wanawake na watoto, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali likiwemo shirika la JHPIEGO linalotekeleza mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH kuelimisha jamii, kuwajengea uwezo wataoa huduma za afya pamoja na kuboresha huduma katika vituo vya afya na hospitali ili kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mmoja wa wanaume mkoani Simiyu, John Sayi (47) aliyeridhia kutumia njia ya uzazi wa mpango ya kudumu akizungumza na wanahabari waliomtembelea wilayani Maswa kwa ajili ya kufanya naye mahojiano.
Mratibu wa afya ya uzazi na mpango mkoa wa Simiyu, Mary Makunja akizungumzia hali ya utoaji huduma za uzazi wa mpango.

Tuesday, September 19, 2023

MAKTABA YABOMOLEWA KUJENGWA MPYA YA KISASA MWANZA NA CHATO


 NA. ALBERT G.SENGO/MWANZA

Huku akionesha na kuelekeza kwa mkono kupitia picha kubwa ya kwenye bango la ukumbi wa mkutano, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) Dkt. Mboni A. Ruzegea anasema "Kama umepita sasa hivi eneo ambalo kulikuwa na maktaba ya mkoa wa Mwanza, imebomolewa na ujenzi unaendelea"
"Na hii hapa ndiyo picha ya jinsi jengo litakavyokuwa kwa Maktaba ya Mwanza, pindi litakapokamilika, mnaletewa kitu kizuri sana na Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, kizuri ni kwamba pesa zake zilishaidhinishwa kwenye Bajeti ya 2023-2024" na kisha Dkt Ruzegea akaendelea kwa kusema. "Vilevile tutakuwa na maktaba kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa awamu ya 5 Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambayo inajengwa pale Chato, maktaba kubwa nzuri ya mfano itakayobeba kumbukumbu zote za viongozi wa nchi yetu" Taarifa hii imetoka leo Septemba 19 katika Kongamano la Tatu la Kitaifa la Huduma za Maktaba, Tamasha la Vitabu na Usomaji, linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano BOT Kapri Point, Jijini Mwanza. Lengo kuu la Kongamano na Tamasha hili ni kutoa fursa kwa wadau wote wa huduma za maktaba nchini kushiriki, kujadili, kuchangia na kuamua kwa pamoja upatikanaji na utumiaji wa huduma bunifu za maktaba na teknolojia za kisasa nchini kunavyosaidia kujenga ari na utamaduni wa kujisomea. Kongamano hili ni la siku 3, hivyo litadumu kuanzia leo 19 hadi 21 mwezi Septemba 2023. Kauli mbiu ya Kongamano hilo kwa mwaka huu 2023 ni 'Waandishi na Wachapishaji Tukutane Maktaba'

Monday, September 18, 2023

MHE. RAIS SAMIA AKIZUNGUMZA NA WANANCHI WA MTAMA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi wa Mtama leo tarehe 18 Septemba, 2023

KONGAMANO LA HAKI JINAI LAFANYIKA KIBAHA WANANCHI WAELEZA KERO ZAO.

 


Na Victor Masangu,Kibaha 

Wananchi Wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba serikali kuingilia kati changamoto ya baadhi ya askari wa maliasili kuwakamata na kuwapiga bila sababu za msingi baadhi ya  watu wanaobeba mkaa kwa ajili ya matumizi yao binafsi ya nyumbani kitendo ambacho wamedai ni uonevu.

Wananchi hao wameyasema wakati wa kongamano maalumu kwa ajili ya kujadili haki jinai lililofanyika katika stendi ya zamani maili moja Wilayani Kibaha na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali taasisi binafsi,wajumbe wa tume iliyoundwa  pamoja na wananchi.

Wamesema kumekuwepo na ukiukwaji wa sheria na taratibu kwa baadhi ya askari hao wa maliasili kuchukua maamuzi ambayo sio sahihi ya kuwakamata watu ambao hawana hatia na kuwachukulia mkaa kitendo ambacho wamekilaani vikali.

Kadhalika Ally Rashid ambaye ni mwananchi alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda time hiyo ya haki jinai ambayo itaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa changamoto mbali mbali ambazo zinawakabili wananchi hasa katika kupata haki zao za msingi.

Kadhali hawakusita kutoa maoni yao juu ya adhabu kunyonga iwe pale pale na kwamba inatakiwa iundiwe  kitengo chake maalumu  badala ya kuacha jukumu hilo kwa Rais pekee yake na kwamba watu wanaofanya mauaji kwa makusudi adhabu hiyo iwahusu bila ya huruma.

Naye mwananchi mwingine alitejitambulisha kwa jina la  Hawa John alisema kwamba kumekuwepo kwa baadhi ya  polisi jamii nao wamekuwa hawatendi haki pindi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao katika kuwakamata watuhumiwa.

" Hawa polisi Jamii wako sana kwenye kata unapofika kuelezea tukio lako polisi unaambiwa uwape kwanza hela ili wakamkamate mtuhumiwa hili jambo kwetu ni kero tunaomba takukuru pamoja na  Tume ilifanyie kazi"alisema 

Hawa pia alisema lipo suala la baadhi ya Askari wa Jeshi la Polisi kutowalinda watu wanaotoa taarifa za wahalifu linapaswa kuangaliwa Ili kulinda usalama wao kwani wapo wanaopelekewa taarifa kuhusiana na wahalifu lakini haohao Askari wanawataja watoa taarifa.

Naye Ramadhani Maulidi alieleza katika mkutano huo kwamba  anatamani siku moja angeajiriwa na Serikali Ili akafanye kazi ya kunyonga watu waliohukumiwa kutumikia adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia ya kuhusika na mauaji.

Alisema zipo taarifa zinazoelezwa kwenye  vyombo mbalimbali kuwa ni zaidi ya miaka 10 sasa adhabu hiyo imekuwa haitekelezwi huku matukio ya mauaji yakiendelea ni wakati sasa Serikali  kuliangalia suala hilo sambamba na kuajri watu wenye roho ngumu ambao watatekeleza adhabu ya kunyonga.

"Uanakuta mtu ameuwakwa makusudi halafu anaenda kukaa gerezani muda mrefu bila kunyongwa hilo haliwezekani kama mtu amekutwa na hatia ya kuuwa naye anyongwe, siyo unasikia  wanaanza kusema haki za binadamu kwani yeye alipokuwa anauwa alikuwa hajui kuwa kuna haki za binadamu?" alifafanua .

Mjumbe waTume hiyo Dk Laurean Ndumbaro alisema  kutosainiwa kwa adhabu ya kifo kwa watu wanaohukumiwa kutumikia adhabu hiyo kwa muda mrefu sasa kumesababisha uwepo wa mlundikano wa wafungwa na kwamba  mapendekezo yao ni kuona suala hilo linangaliwa upya.

Prof.  Edward Hosea ambaye ni Mjumbe wa Tume ya Haki Jinai alisema.kuwa katika ufuatiliajj wao walibaini kwamba zipo sheria nyingi zinatakiwa kufanyiwa marekebisho Ili kulinda haki za wananchi ikiwemo utitiri wa majeshi uliopo ambaounapaswa kuangaliwa na kuundiwa sheria upya.

Sunday, September 17, 2023

TASAC YATOA ELIMU KWA UMMA KATIKA MAONESHO YA KONGAMANO LA WIKI YA PILI YA UFUATILIAJI (U&T) 12-15 SEPTEMBA 2023 ARUSHA - AICC

 


Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limefanikiwa kutoa elimu kwa umma ikiwa ni moja ya  ya Taasisi za Kiserikali zinazoshiriki maonesho yanayoendelea katika Kongamano la Wiki ya Pili ya Ufuatiliaji (U&T).

Maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya AICC jijini Arusha yalianza tarehe 12 Septemba na kilele chake ni tarehe 15 Septemba, 2023. 

TASAC inashiriki maonesho hayo ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu kazi  na majukumu inayoyatekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415.

Wadau wote mnaalikwa kutembelea banda la TASAC katika eneo zilipo Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Uchukuzi.