ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, September 22, 2023

Huduma za uzazi wa mpango zaimarika Simiyu, mwanaume aridhia kufunga kizazi

 

Mwanaume mmoja katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ameridhia kufunga mirija ya uzazi kama njia ya kudumu ya uzazi wa mpango, kwa lengo la kuwa na watoto wachache anaomudu kuwahudumia.

Mwanaume huyo, John Sayi (47) mkazi wa Kijiji cha Sulu Kata ya Mbalagani amesema tayari ana watoto sita hivyo ameridhia kwa hiari uamuzi huo baada ya kupata elimu ya umuhimu uzazi wa mpango kupitia vyombo vya habari.

“Nilipata msukumo kutoka kwa baba mzazi ambaye alikuwa na wanawake wanne lakini hakutana kuwa na watoto wengi kwani alizaa watoto sita tu. Wake zake watatu kila mmoja alizaa mtoto mmoja akiwemo mama yangu na mwingine alizaa watoto watatu” amesema Sayi.

Amesema alipata nafasi ya kuongea na baba yake ambaye ametangulia mbele za haki aliyemweleza kwamba alikuwa akitumia njia ya asili ya uzazi wa mpango hivyo na yeye ikamuingia akilini kuwa na watoto wachache.

Mwaka 1998 Sayi alioa mke wa kwanza na kuzaa naye watoto wawili kabla ya kutengana mwaka 2002 ambapo kwa sasa anaishi na mke wa pili aliyemuoa mwaka 2,000 na kujaaliwa kupata watoto wanne hadi alipofunga mirija mwaka huu 2023.

“Wasukuma tuna tabia ya kuzaa watoto wengi, mwanaume ukimwambia mwanamke aache kuzaa anafikiri akifanya hivyo utaendelea kuzaa na wanawake wengine hivyo nilipomwambia mke wangu nataka kufunga uzazi aliamini nimedhamiria kutoendelea kuzaa” amesema Sayi na kuongeza na kukubaliana nami;

“Kwenye tendo la ndoa najisikia vizuri maana kwa sasa nachelewa kumaliza tofauti na hapo awali, wengi hatupendi kumaliza mapema hivyo wanaume wenzangu wasiwe na hofu kwamba ukifunga mirija ya uzazi utapata madhara” ameeleza Sayi.

Inaelezwa watu wengi wamekuwa wakitumia njia za uzazi wa mpango za muda mfupi na muda mrefu ambazo ni pamoja na vidonge, vipandikizi, vitanzi na kondomu tofauti na ilivyo kwa njia ya kudumu ambayo ni kufunga mirija ya uzazi kama alivyofanya Sayi.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH, Mratibu wa afya ya uzazi na mpango mkoa wa Simiyu, Mary Makunja amesema wanawake wanaoongoza kwa kutumia uzazi wa mpango ikilinganishwa na wanaume.

“Kabla ya mradi huduma za uzazi wa mpango zilikuwa asilimia 36 mwaka 2022 lakini kwa sasa (2023) ni asilimia 45 huku idadi ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya/ hospitali ikifikia asilimia zaidi ya 90” amesema Makunja.

Amebainisha kuwa mwitikio wa kutumia njia za uzazi wa mpango za muda mfupi na mrefu ni mkubwa ikilinganishwa na njia ya kudumu; akisema “kwa mwaka idadi ya wanawake wanaoridhia kufunga mirija ya uzazi inafikia 100 huku wanaume wakiwa kati ya mmoja hadi watatu”.

Makunja ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa jamii ya wakazi wa Simiyu kutumia uzazi wa mpango hatua itakayowasaidia kuwalea vyema watoto wao tofauti na ilivyo sasa ambapo mwanamke anaweza kuwa na nzao kati ya saba hadi kumi jambo ambalo ni hatari kiafya.

“Jamii ya watu wa huku asilimia kubwa ni wakulima hivyo wanaona ni fahari kuoa mwanamke zaidi ya mmoja na kuzaa watoto wengi wakiamini watawasaidia kwenye shughuli za uzalishaji mali hivyo tunaendelea kuwaelimisha” amesema Makunja.

Kutokana na umuhimu wa uzazi wa mpango katika kukabiliana na vifo vya uzazi kwa wanawake na watoto, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali likiwemo shirika la JHPIEGO linalotekeleza mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH kuelimisha jamii, kuwajengea uwezo wataoa huduma za afya pamoja na kuboresha huduma katika vituo vya afya na hospitali ili kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mmoja wa wanaume mkoani Simiyu, John Sayi (47) aliyeridhia kutumia njia ya uzazi wa mpango ya kudumu akizungumza na wanahabari waliomtembelea wilayani Maswa kwa ajili ya kufanya naye mahojiano.
Mratibu wa afya ya uzazi na mpango mkoa wa Simiyu, Mary Makunja akizungumzia hali ya utoaji huduma za uzazi wa mpango.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.