MKURUGENZI wa shirika la kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI lenye makao yake
makuu jijini Mwanza Bw. Ramadhan Masele amefunga rasmi mafunzo ya siku tano yanayolenga
kuwajengea wasichana uwezo wa kutoa
elimu juu ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia chini ya mradi wa
kuwashirikisha vijana kuzui Ukatili wa majumbani ikiwa ni pamoja na ukatili wa kingono kwa watoto wa kike na wasichana.
Akizungumza
na washiriki wa mafunzo hayo Bw. Masele aliwataka washiriki wote kutumia elimu
hiyo muhimu waliyoipata kutoa elimu na kuongeza uwelewa zaidi kwa jamii yao
kuanzia ngazi ya familia, marafiki na vikundi mbalimbali na kuwa chachu ya
mabadiliko juu ya kupigania haki za
wanawake na wasichana wanaonyanyaswa kijinsia katika jamii zao.
“Imani
yangu ni kuwa semina hii itakuwa ni kiwanda kizuri cha kuwatengeneza nyinyi
wote kuwa mabalozi wazuri katika jamii, baada ya mafunzo haya tunaamini kuwa
mtakuwa chachu ya mabadiliko katika kutetea na kulinda haki za wanawake na
wasichana kwa kukemea, Kupinga, kuripoti na kuzuia aina zote za ukatili wa
majumbani na kingono kwa wasichana na wanawake na kutoa taarifa pindi vitendo
hivi vinapotokea” alisema Bw. Masele
“Kila
mmoja aliyehudhuria mafunzo haya kwa
nafasi aliyonayo tunaamini anaweza kuwa chachu ya mabadiliko endapo atatimiza
wajibu wake kwenye eneo analoishi. Hili suala la ukatili wa kijinsia si suala
geni nchini hasa eneo hili la kanda ya ziwa hivyo kuna kila sababu ya kuzidisha
mapambano dhidi yake, cha muhimu ni kuzingatia mafunzo mliyopewa na muwezeshaji
wenu” aliongeza Bw. Masele.
Mafunzo
hayo yamefanyika kwa muda wa siku 5 kwa vijana 30 wa kike wenye umri kati ya
miaka 18-24 kutoka wilaya mbili za Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza. Lengo la
Mafunzo ni kuwajengea vijana uwezo wao binafsi na uwezo wa kuelimisha jamii hasa
Vijana wenzao kupambana na kupinga
Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika maeneo wanayoishi.
Mafunzo
yalianza Jumatatu tarehe 28 Aprili, 2014 mpaka tarehe 2 Aprili, 2014 katika
Ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi, VETA kilichopo Nyakato nje kidogo ya jiji la
Mwanza.
Takwimu
zinaonyesha bado jamii inakabiliwa na ukatili mkubwa wa kijinsia ambapo ubeberu
wa wanaume pamoja na mila na desturi potofu zimeonekana kukandamiza jinsi ya
kike zaidi kuliko jinsi ya kiume, ukatili huo ni wa kijamii, kiuchumi pamoja na
kisaikolojia hivyo kunaitajika juhudi za dhati na makusudi kuweza kukabiliana
na tatizo lilopo kwa jamii.
Akimalizia
mawaidha yake kwa washiriki Bw. Masele alisema lengo la mafunzo hayo ni kuona
mabadiliko katika mfumo juu ya kujali na kuheshimu haki za mwanamke na
wasichana, kwani jamii nyingi zinapambana na mifumo miwili mikubwa, ambayo ni
mfumo dume ambao umekuwa ukiwakandamiza wanawake katika jamii na mfumo wa kitabaka
unaoongeza nafasi kati ya matajiri na masikini.
Shirika
la KIVULINI kwa kushirikiana na Asasi ya Vijana inayojulikana kama Wadada Centre for Solution
Focus Approach ndio waandaji wa mafunzo hayo kupitia mradi wa kuwashirikisha
vijana kuzui Ukatili majumbani na Ukatili wa Kingono chini ya ufadhili wa
Shirika la terre des hommes ch (tdhschweiz) - Fursa kwa Vijana la nchini Switzerland
Kivulini
ni shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kutetea pamoja na
kulinda Haki za Wanawake na Wasichana. Shiriki la Kivulini linahamasisha jamii
(Wanawake, Wanaume na Vijana ) kulinda, kutetea Haki za Wanawake na Wasichana
kwa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Makao makuu ya shirika yapo
jijini Mwanza, Wilaya ya Ilemela, Tanzania.