ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, May 3, 2014

WASICHANA 30 JIJINI MWANZA WAPATIWA MAFUNZO YA SIKU TANO KUHUSU ELIMU YA UKATILI WA KIJINSIA MAJUMBANI.

Mkurugenzi wa Shiriki la KIVULINI Bw Ramadhan Masele akisisitiza jambo wakati akifunga mafunzo maalum kwa wasichana 30 walio na umri kati ya miaka 18 mpaka 25 kutoka wilaya ya Ilemela na Nyamagana za jijini Mwanza hapo jana. Wasichana hao wamepewa mafunzo kuhusu ukatili wa kijinsia majumbani pamoja na Kingono lengo likiwa ni kuzalisha waelimisha rika wengi zaidi mitaani na kutengeneza jamii isiyokuwa na ukatili wa kijinsia na kingono kwa kwa watoto wa kike.
Mkufunzi wa Masuala ya Kijinsia Bi. Tumaini Kyola akitoa mafunzo kwa kundi la Wasichana 30 ambao hawako mashuleni juu ya mbinu mbalimbali za kuelemisha jamii kuhusu masuala Ukatili wa Majumbani na wa kingono pia. Wasichana hawa wanategemewa kwenda kuwafundisha wasichana wenzao wa mitaani, kila mmoja amepewa lengo la kufikia wasichana 50. 
Baadhi ya wasichana 30 wakiwa makini kufuatilia mafunzo waliokuwa wakipatiwa na mkufunzi wao (hayupo pichani), hili ni kundi la kwanza kwa wasichana waliokuwa nje ya shule ambapo mafunzo ya kundi la pili kwa wasichana waliopo mashuleni yanatarajiwa kuanza mwezi wa sita kwa kushirikisha shule zipatazo 40 toka wilaya za jiji la Mwanza.

Wasichana thelathini pamoja na Mkufunzi wao na baadhi ya maafisa wa Kivulini wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mafunzo hayo ya siku tano hapo jana katika ukumbi wa VETA jijini Mwanza.


MKURUGENZI wa shirika la kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI lenye makao yake makuu jijini Mwanza Bw. Ramadhan Masele amefunga rasmi mafunzo ya siku tano yanayolenga  kuwajengea wasichana uwezo wa kutoa elimu juu ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia chini ya mradi wa kuwashirikisha vijana kuzui Ukatili wa majumbani ikiwa ni pamoja na ukatili wa  kingono kwa watoto wa kike na wasichana.  

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo Bw. Masele aliwataka washiriki wote kutumia elimu hiyo muhimu waliyoipata kutoa elimu na kuongeza uwelewa zaidi kwa jamii yao kuanzia ngazi ya familia, marafiki na vikundi mbalimbali na kuwa chachu ya mabadiliko  juu ya kupigania haki za wanawake na wasichana wanaonyanyaswa kijinsia katika jamii zao.

“Imani yangu ni kuwa semina hii itakuwa ni kiwanda kizuri cha kuwatengeneza nyinyi wote kuwa mabalozi wazuri katika jamii, baada ya mafunzo haya tunaamini kuwa mtakuwa chachu ya mabadiliko katika kutetea na kulinda haki za wanawake na wasichana kwa kukemea, Kupinga, kuripoti na kuzuia aina zote za ukatili wa majumbani na kingono kwa wasichana na wanawake na kutoa taarifa pindi vitendo hivi vinapotokea” alisema Bw. Masele

“Kila mmoja aliyehudhuria mafunzo haya  kwa nafasi aliyonayo tunaamini anaweza kuwa chachu ya mabadiliko endapo atatimiza wajibu wake kwenye eneo analoishi. Hili suala la ukatili wa kijinsia si suala geni nchini hasa eneo hili la kanda ya ziwa hivyo kuna kila sababu ya kuzidisha mapambano dhidi yake, cha muhimu ni kuzingatia mafunzo mliyopewa na muwezeshaji wenu” aliongeza Bw. Masele.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa muda wa siku 5 kwa vijana 30 wa kike wenye umri kati ya miaka 18-24 kutoka wilaya mbili za Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza. Lengo la Mafunzo ni kuwajengea vijana uwezo wao binafsi na uwezo wa kuelimisha jamii hasa Vijana wenzao  kupambana na kupinga Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika maeneo wanayoishi.

Mafunzo yalianza Jumatatu tarehe 28 Aprili, 2014 mpaka tarehe 2 Aprili, 2014 katika Ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi, VETA kilichopo Nyakato nje kidogo ya jiji la Mwanza.

Takwimu zinaonyesha bado jamii inakabiliwa na ukatili mkubwa wa kijinsia ambapo ubeberu wa wanaume pamoja na mila na desturi potofu zimeonekana kukandamiza jinsi ya kike zaidi kuliko jinsi ya kiume, ukatili huo ni wa kijamii, kiuchumi pamoja na kisaikolojia hivyo kunaitajika juhudi za dhati na makusudi kuweza kukabiliana na tatizo lilopo kwa jamii.

Akimalizia mawaidha yake kwa washiriki Bw. Masele alisema lengo la mafunzo hayo ni kuona mabadiliko katika mfumo juu ya kujali na kuheshimu haki za mwanamke na wasichana, kwani jamii nyingi zinapambana na mifumo miwili mikubwa, ambayo ni mfumo dume ambao umekuwa ukiwakandamiza wanawake katika jamii na mfumo wa kitabaka unaoongeza nafasi kati ya matajiri na masikini.

Shirika la KIVULINI kwa kushirikiana na Asasi ya Vijana  inayojulikana kama Wadada Centre for Solution Focus Approach ndio waandaji wa mafunzo hayo kupitia mradi wa kuwashirikisha vijana kuzui Ukatili majumbani na Ukatili wa Kingono chini ya ufadhili wa Shirika la terre des hommes ch (tdhschweiz) - Fursa kwa Vijana  la nchini Switzerland

Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kutetea pamoja na kulinda Haki za Wanawake na Wasichana. Shiriki la Kivulini linahamasisha jamii (Wanawake, Wanaume na Vijana ) kulinda, kutetea Haki za Wanawake na Wasichana kwa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Makao makuu ya shirika yapo jijini Mwanza, Wilaya ya Ilemela, Tanzania.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.