ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, October 1, 2025

DK SAMIA:TUTAIMARISHA UKUSANYAJI MAPATO KUEPUKA MIKOPO NA MISAADA YA MANYANYASO

 MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo Serikali itaendelea kuongeza makusanyo ya mapato ndani ya nchi yetu ili kuepuka manyanyaso yanayotokana na mikopo na misaada. 

Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro katika mkutano wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu Dk.Samia amesema kıla ambacho wameahidi kwa wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030 CCM inajua fedha itapatikana wapi.

“Kila tulichokiweka mule katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu tunajua fedha yake ya utekelezaji inatoka wapi lakini nataka niwaambie lingine tumeongeza makusanyo ya mapato. 

“Tunajua hakika fedha zinatoka wapi. Tutakopa ndiyo lakini mikopo ambayo itaheshimu uhuru wa nchi yetu ndiyo tutakayokopa.”

Pamoja na hayo Dk.Samia Suluhu Hassan ametumia nafasi hiyo kuelezea faraja yake kwa wananchi wa Wilaya Mwanga ambayo inatokana na kutimiza mradi ambao marehemu Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Rais mstaafu Cleopa David Msuya ulikuwa mradi wake wa kufa na kupona.

“Alinifuata na akaniomba miradi miwili mradi mmoja maji safi Mwanga - Korogwe na mradi wa pili wa barabara ya Msuya bypass.

“Faraja yangu ni kwamba miradi yote miwili nimeweza kuifanya ameiona kabla ya Mungu hajamchukua kwa hiyo nawashukuru wanamwanga. Niseme kwamba kwenye maji tumeweza kupandisha asilimia ya upatikanaji maji kutoa 77.5 mwaka 2023 hadi 81.9 mwaka jana.

“Miradi 26 imefanyika hapa kwa bilioni 54.2 na mradi wa Same Mwanga Korogwe peke yake una bilioni 304 kwa hiyo ni mradi mkubwa sana. 

“Tumetekeleza mradi huu kwa awamu ya kwanza ambayo tayari maji yameanza kupatikana. Na awamu ya pili ni kwenye maenwo yaliyobaki Same baadhi na kule Korogwe.

“Kama nilivyomuahidi marehemu Mzee Msuya tutakwenda kuukamilisha mradi huu sambamba na ile barabara ya Msuya bypass.”

Wakati huo huo mgombea Urais Dk.Samia amesema Serikali imejenga minara sita ya simu ili kuimarisha mawasiliano ya simu na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi.

“Sasa hivi mambo yote kwenye simu, kununua kwenye simu kutangaza biashara kwenye simu lazima tuhakikishwa network inapatikana kila mahali. “

WANAFUNZI SUA WANG'ARA TUZO ZA UMAHIRI WA HABARI ZA SAYANSI TANZANIA

 Na: Calvin Gwabara – Dar es salaam 

Wanafunzi watatu wa Shahada ya Uzamili ya Taarifa na Menejimenti ya Maarifa (MIKM) kutoka Idara ya Infomatiki na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (DIIT) ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameng’ara kwenye tuzo kubwa zinazotambua mchango wa wanahabari kwenye kuandika taarifa za sayansi na bioteknolojia Afrika kwa upande wa Tanzania (OMAs).


Wanafunzi hao ni Rebecca Kachembeho na Jackline Martine ambao wameibukwa kwa pamoja washindi wa jumla wa tuzo hizo (Overall winner) kwa kuandika taarifa nzuri iliyohusu nafasi ya bioteknolojia kwenye kutatua changamoto za ugonjwa mnyauko wa migomba Mkoani Kagera, Changamoto za wadudu wa Pamba wanaokwamisha tija pamoja na makala kuhusu Bungua wa Mahindi na Viwavijeshi vamizi wanavyorudisha maendeleo ya wakulima nchini.

Mwandishi mwingine ambaye pia ni Mwanafunzi aliyeng’ara kwenye tuzo hizo ni Martinius Sospeter ambaye ameshika nafasi ya pili kwa upande wa magazeti kwa kuandika Makala nzuri iliyoonesha mchango wa Sayansi hasa Bioteknolojia katika kutatua changamoto za upungufu wa chakula zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, wadudu na magonjwa na nafasi ya Bioteknolojia katika kuboresha afya nchini Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya washindi na washindi wote kwenye hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es salaam Mshindi wa jumla Bi. Rebecca Kachembeho amekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kufundisha kozi ya namna ya kuandika habari za sayansi na kutafsiri matokeo ya kisayansi kwa lugha rahahisi kwa jamii ili waweze kuelewa na kutumia matunda ya sayansi.

“Tunakishukuru Chuo Chetu cha Sokoine cha Kilimo kwa kuona umuhimu wa kutufundisha kozi hii na kutupatia mbinu nyingi za namna ya kuwasilisha sayansi kwa jamii, hakika imetupatia mbinu nyingi na maarifa ya kutuwezesha sasa kuitumiakia jamii yetu vizuri kwa kuwafikishia matokeo ya tafiti kwa lugha rahisi ili wayatumie kutatua changamoto zinazowakabili na kuongeza ustawi wao katika nyanja mbalimbali.” Alisema Bi. Kachembeho.

Awali akieleza kuhusu tuzo hizo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amon Nungu amesema tume imekuwa ikifanya kazi na Waandishi wa habari kwa miaka mingi hasa kwa kuwajengea uwezo kuhusu Uandishi wa habari za sayansi na nafasi yao katika kusaidia kufikisha matokeo ya tafiti kwa jamii.

“ COSTECH kupitia Jukwaa la bioteknolojia za Kilimo Afrika (OFAB Africa) tumekuwa tukifanya kazi kubwa sana katika kuwajengea uwezo Wanahabari nchini kwa zaidi ya miaka 15 ya jukwaa hili lakini pia katika kuongeza ari ya kuhamasisha uandishi huo tumekuwa tukitoa tuzo maalumu kutambua mchango wao kila mwaka hapa Tanzania na baadae washindi huenda kushindanishwa Afrika na wamekuwa wakifanya vizuri na wengine kunyakua Tuzo hizo barani afrika kama tulivyosikia Calvin Edward Gwabara kutoka SUAMEDIA aliyeshinda Tuzo ya Afrika mwaka 2018” alifafanua Dkt. Nungu.

Aidha amewahakikishia Wanahabari ushirikiano wa kina katika kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao lakini pia kuendelea kuwajengea uwezo zaidi katika kuandika habari za sayansi nchini ili sayansi iweze kutoa mchango unaostahili kwenye maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Nae Mgeni rasmi katika Tuzo hizo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Prof. John Kandolo amewapongeza washindi hao wote kwa kuandika habari na makala nzuri ambazo zimeweza kushawishi majaji kuzipatia ushindi hasa baada ya kutimiza vigezo vingi vilivyowekwa kuchuja ubora na kuona mchango wake katika maisha ya watu.

“Niwapongeze wote mlioshinda na wale wote zaidi ya 50 mlioshiriki kutuma kazi zenu kwenye tuzo hizi, ninaamini kama hukupata leo basi umefungua mlango wa kujipanga vizuri ili uweze kushinda kwenye tuzi zijazo, lakini niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhabarisha jamii kwenye kutumia matokeo ya sayansi kutatua changamoto zao na kuongeza tija kwao na maendeleo ya Taifa leo” alieleza Prof. Kandalo.

Aidha amesema kuwa maendeleo ya taifa lolote duniani yanategemea matumizi ya Sayansi na teknolojia na ubunifu lakini yatatokea endapo matokeo hayo ya tafiti yatafahamika kwa jamii na kuyatumia kikamilifu kama ambavyo mataifa mengi yaliyoendelea duniani yanavyofanya.

Awali tuzo zilitanguliwa na mafunzo kwa waandishi wa habari ambapo Watafiti nguli wa Bioteknolojia na wabobevu kwenye masuala ya Uandishi wa habari za Sayansi nchni walifundisha mada mbalimbali na kutoa nafasi ya mjadala mpana wa fursa zilizopo, changamoto na hatimae kuweka mikakati ya pamoja.

MATUKIO WAKATI WA UTOAJI WA TUZO HIZO.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amon Nungu  akieleza kuhusu tuzo hizo na mchango wa COSTECH kwa wanahabari na sayansi.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Prof. John Kandolo akizungumza kabla ya kutoa tuzo hizo. 

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakifuatilia mafunzo hayo kabla ya utoaji wa tuzo kuanza.

Bwana Calvin Gwabara akipokea cheti cha ushiriki kutambua mchango wake kwenye tuzo hizo na uandishi wa habari za sayansi.

Mohamed Gojo mmoja wa wanafunzi wa SUA aliyeshiriki kwenye tuzo hizo akipokea cheti chake cha ushiriki.

Mwanafunzi Martinius Sospeter aliyeshika nafasi ya pili kwa upande wa magazeti akipokea cheti chake kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamsheni ya COSTECH.

Washindi wa tuzo hizo kutoka SUA  Bi. Rebecca Kachembeho (wa kwanza kushoto)  Jackline Martine (katikati) na Martinius Sospter (Kulia) wakiwa kwenye piocha ya pamoja mara baada ya kupokea tuzo zao.

Mshindi wa Jumla Bi. Rebecca Kachembeho akiwa ameshika tuzo yake mara bada ya kukabishiwa

Mshindi mwenza Bi. Jacline Martine akiwa kwenye picha na tuzo yake mara baada ya kukabidhiwa kwenye hafla hiyo.

Monday, September 29, 2025

WAZEE ZINGATIENI LISHE BORA KUJIKINGA NA MARADHI - RC MTANDA

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa rai kwa wazee kula vyakula vyenye lishe bora kwa kufuata mlo kamili na kuzingatia makundi yote muhimu ili kujihakikishia afya imara na kuepuka maradhi hususani yasiyoambukiza.


“Wazee tuache tabia ya kula vyakula bila kufuata mlo kamili kwa mfano mtu asubuhi anakula wali, mchana anakula wali na usiku pia anakula wali wakati huo ni wanga ambao kazi yake ni kuleta nguvu na kubadilika kuwa sukari na mafuta hivyo ni vyakula ambavyo havitusaidii kwa afya yetu.” Mhe. Mtanda.


Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa rai hiyo leo tarehe 29 Septemba, 2025 wakati akihutubia katika kongamano la Siku ya Wazee duniani lililoadhimishwa kimkoa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuwakutanisha wazee zaidi ya 200 waliojadili kuhusu mustakabali wa maisha yao.


Aidha, amewahakikishia wazee hao kuwa serikali itaendelea kuboresha maisha yao katika nyanja mbalimbali kama kuwapatia huduma bora za afya bila malipo ambapo akabainisha jumla ya wazee Elfu 97 wametambuliwa na kupewa vitambulisho mkoani humo.


Kadhalika, amewasihi kundi linaloelekea kwenye uzee kuwekeza katika shughuli za uzalishaji mali kama kilimo, uvuvi na ufugaji ili kujiwekea akiba ya uchumi imara wakati wa uzee jambo litakalowasaidia kuondokana na msongo wa mawazo.


Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Jesca Lebba amesema Mwanza yenye vituo 569 vya kutolea huduma unatoa kipaumbele kwa kundi hilo na kwamba jumla ya wazee elfu 78 wamehudumiwa 2024/25 na kupitia mabaraza ya wazee halmashauri zinawawezeshwa kwa kuwahusisha na shughuli mbalimbali za uchumi.


Akiongea kwa niaba ya mwenyekiti, Mzee Juma Ngeleja ametumia wasaa huo kuishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za kijamii kama kujengwa kwa zahamati vijijini na uwepo wa madawati maalumu ya kuwahudumia kwa kipaumbele kwani ni ishara kuwa serikali inajali afya ya wazee.


Oktoba Mosi ya kila mwaka ni siku ya wazee duniani ambapo kitaifa hapa nchini siku hiyo itaadhimishwa kesho kutwa mkoani Ruvuma chini ya Kaulimbiu isemayo ‘Wazee tushiriki uchaguzi Mkuu 2025 kwa ustawi wa jamii yetu’.