|
Mbunge wa Jimbo la Kisesa Luhaga J. Mpina (kulia) akikabidhi mashuka kwa hospitali ya Wilaya ya Meatu kwa Mkurugenzi wa wilaya hiyo Isaya M. Moses. PICHA kwa hisani ya maktaba yetu 2012. |
SAKATA la ukosefu wa dawa katika hospitali zote za umma limetikisa Bunge baada ya Mbunge wa Jimbo la Kisesa(CCM), Luhaga Mpina kutaka bunge hilo liahirishwe ili fedha zinazotumika kuwalipa posho zikusanywe ziende kununua dawa kuokoa maisha ya watanzania wanaokufa kila siku kwa kukosa dawa.
Hatua hiyo ya Mpina ilikuja kufuatia maelezo yaliyotolewa na Serikali kuwa inakwenda kukaa kikao cha kujadili suala hilo majibu ambayo hajakumridhisha mbunge huyo.
Mpina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Uchumi,Viwanda na Biashara alisema watanzania wanaendelea kupoteza maisha huku Serikali ikiendelea kulifanyia mzaha jambo hilo nyeti.
Alisema wakati wa vikao vya kamati za Bunge vilivyokaa Dar Es Salaam wiki mbili zilizopita, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Margareth Sitta na kamati yake waliitaka Serikali ilipe deni ya Sh.bilioni 100 linalodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa(MSD) ili kunusuru vifo vya wananchi wanyonge bado Serikali imeendelea kusuasua katika jambo hilo.
Hata hivyo Mpina alielezea kusikitishwa kwake na Serikali kushindwa kutaja waliohusika kuiba sh.bilioni 37 za kununulia dawa huku pia ikishindwa kutaja hatua ilizochukua dhidi ya watu hao.
Kufuatia hali hiyo alimba Mwongozo kwa Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kukubali kuahirisha mkutano wa 16 na wa 17 wa Bunge hilo ili fedha zilizokuwa zitumike kulipana posho zipelekwe haraka MSD kulipa deni hilo ili kunusuru maisha ya wananchi wasio na hatia wanaondelea kufariki kwa kukosa dawa.
Alisema hospitali zote za Umma zinakabiliwa na ukosefu wa dawa huku kwenye jimbo la Kisesa ikikosekana hata dawa aina ya Oral ya kuzuia kuharisha kwa watoto wachanga ambao nao wanapoteza maisha kwa kukosa dawa hiyo.
"Mheshimiwa Naibu Spika leo Serikali inasema inaenda kukaa kikao wakati hospitali nchi nzima hazina dawa watu wanakufa kwa kukosa dawa,kwa kuwa Serikali imeshindwa kutatua tatizo hili basi mkutano wa 16 na 17 wa Bunge hili liahirishwe ili fedha hizi zitumike kununua dawa zikatibu wananchi hawa waokufa bila dawa" alisema Mpina.
Kufuatilia mwongozo huo, Naibu Spika Ndugai alisema hoja hiyo ya Mpina ni nyeti na kwamba itajadiliwa kwenye Kamati ya uongozi ili kufanya uamuzi.
'Mh Mpina hoja yako ni nzito sasa itabidi ipelekwe kwenye kamati ya uongozi itakayokutana leo jioni (jana) ili kulijadili na kulifanyia uamuzi"alisema Ndugai.
Katika hatua nyingine Mbunge wa Kigoma Kusini(NCCR-Mageuzi), David Kafulila ameliomba bunge kujadili suala la ufisadi wa IPTL kutokana na unyeti wa suala hilo baada ya Serikali kuonekana kuikalia ripoti hiyo isiwasishwe bungeni.
"Mheshimiwa Naibu Spika naomba bunge lako likubali tusimamishe shughuli zote za bunge tujadili suala hili la IPTL ambalo limesababisha wafadhili kukatisha misaada yao na kuathiri mwenendo wa shughuli za Serikali"alisema Kafulila.
Baada ya Kafulila kuomba mwongozo huo, Mnadhimu wa Shughuli za Serikali bungeni, William Lukuvi alisema uchunguzi wa suala la IPTL bado unaendelea kufanywa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali(CAG) na kwamba utakapokamilika ripoti hiyo itawasilishwa bungeni.
Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge alisema taarifa alizonazo uchunguzi wa CAG uko kwenye hatua za mwisho na kwamba utakapokamilika utawekwa wazi.
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alimtaka Naibu Spika aruhusu kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza suala hilo.
Ndugai alisema hoja ya kuundwa Kamati teule nayo itawasilishwa kwenye kikao cha kamati ya uongozi ya Bunge kujadiliwa.
Naye Mbunge wa Nzega(CCM), Dkt. Khamis Kigwangala aliomba mwongozo kuhusu kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga kuhusu baadhi ya Kamati za kutojua mipaka yake.
Kingwangala alimtaka Naibu Waziri huyo kufuta kauli yake bungeni kwani inaweza kuathiri utendaji wa Kamati za Bunge kwa kufanya ionekane hazijui majukumu yake na kusababisha maagizo na ushauri inayokuwa inatoa kuonekana pia ni batili.
Hata hivyo Ndugai alilitolea ufafanuzi suala hilo na kusisitiza kuwa Kamati za Bunge ziko kusheria na zitaendelea kutelekeza majukumu yake bila kuingiliwa na mihimili mingine ya dola.