Saturday, July 24, 2010
BANGO
PICHANI BAADHI YA ASKARI WA KULINDA AMANI NCHINI SOMALIA.
Wanajeshi wawili kutoka Uganda wanaolinda amani nchini Somalia chini ya Muungano wa Afrika wameuawa mjini Mogadishu.
Askari hao waliuawa katika mapigano kati ya vikosi vya AU na wapiganaji wa kiislam wa al-Shabaab.
Msemaji wa Muungano huo amethibitisha kujeruhiwa kwa wanajeshi wengine watatu.
Kwa mjibu wa jeshi la Muungano wa Afrika majeshi yamelazimika kuondoka katika ngome yake katika mji wa Mogadishu na kuelekea vitongojini ili kuwasaka wapiganaji hao.
Suala la hali ya usalama nchini Somalia huenda likawa ajenda kuu katika kikao cha viongozi wa nchi na serikali wa Muungano wa Afrika kitakachoanza mjini Kampala, Uganda wikendi hii
HABARI KWA HISANI YA BBC.
CLEORHAS ANGELLO RUGALABAMU.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa salamu za rambi rambi na pole kutokana na kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza, Bw. Cleophas Angello Rugalabamu kilichotokea mapema jana nchini India ambako alikuwa anatibiwa.
Bw. Rugalabamu (64) alilazwa katika Hospitali ya Appolo mjini Chennai tangu Juni 20 mwaka huu na alifariki dunia leo alfajiri.
Mipango inafanywa ya kurejesha maiti yake nchini kwa ajili ya mazishi. Katika salamu zake alizozituma kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Yohana Balele, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Pinda alisema kifo cha Bw. Rugalabamu kimeleta majonzi makubwa.
“Alikuwa kiongozi hodari na muaminifu. Kwa niaba ya Serikali na kwa niaba yangu mimi mwenyewe binafsi, natoa rambirambi na pole kwa familia ya marehemu, ndugu jamaa na marafiki kutokana na msiba huo.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,” Waziri Mkuu alisema katika salamu hizo.
Imetolewa na: Ofisi ya Waziri Mkuu
S.L.P. 3021
DAR ES SALAAM
Jumatano Julai 21, 2010
Wednesday, July 21, 2010
BANGO
KUTOKA MKUTANO WA UKIMWI VIENNA.
Watafiti wanasema jeli yenye dawa zinazopunguza makali ya ukimwi inayofanyiwa majaribio nchini Afrika kusini inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa wanawake kuambukizwa virusi vya Ukimwi, inapotumiwa kila mara kabla ya tendo la ngono.
Shirika la afya duniani WHO na lile la kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa UNAIDS yametaja matokeo ya uchunguzi huo uliofanyiwa wanawake karibu 900 kama yenye mafanikio.
Jeli hiyo imetengenezwa hususan kukabili uambukizaji wa virusi vya Ukimwi, na imechanganywa na dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo ARVs.
Akizungumza katika mkutano huo wa Vienna, aliyekuwa rais wa Marekani Bill Clinton ametoa wito wa uwajibikaji zaidi na utumiaji bora wa fedha za kufadhili harakati dhidi ya kuenea virusi vya HIV.