ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, March 12, 2022

RAIS SAMIA AAGIZA ZIANDALIWE KANUNI ZITAKAZOONGOZA MIKUTANO YA SIASA.

 

raispicc

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wajumbe wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa leo tarehe 12 Machi, 2022, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma 

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene kuandaa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi, Machi 12, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus imeeleza kuwa Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo Jumamosi Machi 12, 2022 baada ya kupokea maazimio ya awali kutoka kikosi kazi alichokiteua cha kufuatilia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliofanyika Desemba 15-17, 2021 Dodoma.

Rais Samia amemwagiza Waziri huyo kushirikiana na Tanganyika Lawa Society (TLS) pamoja na Zanzibar Law Society (ZLS) kutengeneza kanuni hizo.

“Kikosi kazi hicho chenye wajumbe 24, na ambacho kinawajibika moja kwa moja kwa Mhe. Rais, kiliwasilisha maazimio hayo Ikulu Jijijni Dodoma. Maazimio hayo yamegawanyika katika makundi matatu ya muda wa utekelezaji” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa azimio la muda mfupi ni uandaaji wa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

“Baadhi ya maazimio ya muda wa kati ni pamoja na rushwa na maadili katika uchaguzi, ruzuku, elimu ya uraisa, huku masuala yanayohusu uchaguzi wa katiba mpya vikiwa ni mpango wa muda mrefu”

MASHINE YA KISASA YA UCHUNGUZI WA SARATANI ILIYOTENGENEZWA NA MWANAMKE YATUA BUGANDO MWANZA


Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) umekabidhi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando mashine ya kisasa ya kufanya uchunguzi wa awali na matibabu ya saratani ya matiti yenye thamani ya Sh800 milioni. Mashine hiyo iliyo vumbuliwa na mwanamke na kutengenezwa na wanawake madaktri ni ya tatu katika nchi za Afrika Mashariki na ya pili nchini imenunuliwa na kutolewa chini ya mradi mtambuka wa saratani nchini (TCCP) unaotekelezwa kwa miaka minne tangu mwaka 2020. Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mashine hiyo katika Hospitali ya Bugando, Meneja wa mradi wa TCCP, Dk Harrison Chuwa amesema mradi huo unalenga kuboresha vifaa tiba vya saratani, kuendeleza matibabu, kutoa elimu kwa watoa huduma ya afya na kufanya utafiti wa saratani nchini. Mkuu wa Idara ya Mionzi wa hospitali ya Aga Khan, Profesa Ahmed Jusabani amesema mashine hiyo ina uwezo wa kufanya uchunguzi wa saratani kwa watu 20 hadi 25 kwa siku.

Mkurugenzi wa huduma ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Tamisemi, Dk Ntuli Kapologwe (wa tatu kulia) akisikiliza maelezo kuhusu mashine ya kufanya uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti kutoka kwa mtaalam wa mionzi Bugando, Dk Margreth Magambo (hayupo pichani). Mashine hiyo imegharimu Sh800 milioni.

RAIS WA NNE ZAMBIA AFARIKI DUNIA.

 


Rais wa Nne wa Zambia aliyehudumu kuanzia mwaka 2008 hadi 2011 Rupiah Banda, amefariki dunia jana jioni Machi 11, 2022, akiwa na miaka 85, baada ya kuugua saratani.


Taarifa ya kifo chake ilitangazwa na Rais wa sasa wa Zambia, Hakainde Hichilema, baada ya kuutangazia umma wa wananchi wake kupitia runinga na kusema kama Taifa wanatambua mchango wake.

JAFO AUNDA TIMU KUCHUNGUZA MABADILIKO MTO MARA.

 


Serikali imetangaza kuunda timu maalum itakayochunguza chanzo cha mabadiliko katika mto Mara yaliyopelekea maji kubadilika kuwa meusi huku viumbe hai wakiwepo samaki kufa.


Akizungumza baada ya kufika katika mto huo kujionea hali halisi leo Jumamosi Machi 12, 2022, Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jaffo amesema kuwa timu hiyo ya ataiunda leo ili ianze kufanya kazi mara moja.


"Nimejionea mwenyewe hali si shwari hapa kwa sababu harufu iliyopo hapa sio ile ninayoikuta kila nikija Mara kwa hiyo lazima Serikali ifanye jambo tena kwa haraka ili tupate majawabu nini chanzo na kipi kifanyike kabla watu hawajaathirika," amesema Jafo. 


Amesema kuwa katika timu hiyo anayokwenda kuunda hivi punde kutakuwepo na wataalam mbalimbali wakiwepo wataalam wa miamba na kemikali ambao watatakiwa kujua kama mabadiliko hayo yamesababishwa na kemikali au miamba.


Awali, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria wa Baraza la Taifa la Mazingira (Nemc), Redempta Samuel amesema kuwa timu ya wataalam ilifika katika eneo la mto huo tangu Machi 10, 2022 kwa ajili ya kufanya uchunguzi.


Amesema kuwa hadi sasa wamekwishachukua sampuli 32 kutoka katika maeneo mbalimbali ya mto huo sambamba na ziwa Victoria na kwamba uchunguzi unaendelea kujua tatizo ni nini.


Katika hatua nyingine waziri Jaffo ameshindwa kuingia ndani ya mto huo kama ilivyokuwa imepangwa awali baada ya eneo la mto katika upande wa pili wa daraja la Kirumi kuzingirwa na kujaa magugu maji yaliyofika katika eneo hilo muda mfupi baada ya waziri kuwasili katika eneo hilo.

KAZI MPYA YA HARMONIZE - Bakhresa (Official Lyrics Video)

 

Bonge moja la ngoma lenye mashairi yaliyokwenda skuli ni Bakhresa.

Friday, March 11, 2022

MWANAFUNZI WA CHUO AKAMATWA AKIUZA MITIHANI

 


Mwanafunzi Oscar Brighton wa mwaka wa tatu katika chuo cha Zetech cha nchini Kenya, anashikiliwa kwa makosa ya kukutwa na mitihani feki ya shule za sekondari za nchini humo ambayo alikuwa akiiuza kwa watahiniwa.


Mbali na hayo kijana huyo pia amekutwa na makosa ya kuuza vyeti feki vya shule ya msingi na sekondari.


Katika mitihani aliyokuwa nayo alikuwa akiiuza kwa kiasi cha shilingi 1600 hadi 2600 za Kenya.

MATUMIZI HOLELA YA DAWA YATAJWA KUSABABISHA UGONJWA WA FIGO.


Matumizi holela ya dawa za asili na vidonge jamii ya 'Diclofenac' ili kupunguza maumivu ya mwili yanaelezwa kuwa kisababishi kikubwa cha magonjwa ya figo nchini.


Mbali na matumizi ya dawa hizo, visababishi vingine ni pamoja na shinikizo la juu la damu, kisukari kisichodhibitiwa, ulevi kupindukia, kukosa mazoezi ya mwili na maambukizi katika njia ya mkojo.


Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Figo duniani kwa mkoa wa Mwanza yaliyofanyika katika hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza Daktari bingwa wa magonjwa ya figo, Dk Ladius Rudovick amesema hospitali hiyo inahudumia wastani wa wagonjwa wenye matatizo ya figo 200 kwa siku.


"Ili kuepuka kuingia gharama kubwa kutibu magonjwa ya figo ni vyema watu wakajijengea utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini iwapo wanatatizo hilo ama lah, hii itasaidia iwapo mtu atakugundulika kuwa na ugonjwa kuanza matibabu kabla haujafika kwenye hatua mbaya," amesema Dk Rudovick.

Pia amesema unene kupindukia unachangia kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa shinikizo la damu ambalo ni miongoni mwa visababishi vya ugonjwa wa figo huku akitoa wito kwa jamii kufanya mazoezi na kupunguza kula vyakula vyenye mafuta ili kuepukana na unene uliopitiliza.


Mkurugenzi wa Tiba Bugando, Dk Bahati Wajanga amesema kwa kutambua umuhimu wa siku ya figo duniani hospitali hiyo inatoa huduma ya ushauri na vipimo bila malipo.


"Ni vizuri wananchi na wakazi wa Kanda ya Ziwa wakajitokeza kuchangamkia fursa hii maana matibabu ya figo ni gharama kubwa lakini wiki hii tunayatoa bila malipo," amesema Dk Wajanga


Naye Mkazi wa Igoma jijini Mwanza Ester Pastory ameishukuru hospitali hiyo kwa kutoa huduma hizo bila malipo huku akisema kufanya hivyo kutasaidia kuokoa maisha ya wananchi walioshindwa kumudu gharama za matibabu hayo.


"Niwaombe wasiishie kutoa huduma hapa mjini, wapanue zaidi na kwenda vijijini ambako kuna wananchi wengi wanaosumbuliwa na tatizo hilo na hawawezi kuja mjini kupata matibabu kwa hofu ya kushindwa kumudu gharama," amesema Ester

Thursday, March 10, 2022

WALIOSAMBAZA VIDEO ZA PROF JAY KUFUATILIWA.

 


Hospitali ya Taifa Muhimbili imelaani na kusema haijashiriki kusambaza video inayomuonesha Professor Jay akipambania uhai wake, katika chumba cha uangalizi maalum (ICU), na kusema hospitali inafuatilia ili kubaini chanzo cha video hiyo na kuchukua hatua stahiki.


Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, na kusema kwamba imesikitishwa na kitendo hicho kwa kuwa ni cha kiwango cha juu cha ukosefu wa maadili.


Aidha, Aligaesha amewaomba wananchi na watumiaji wa hospitali hiyo kuendelea kuwa na imani nayo na kuendelea kuheshimu taratibu za hospitali.

WANAWAKE WAONESHANA UBABE ZIWANI SIKU YA MWANAMKE DUNIANI

 Jijini Mwanza kilele cha maadhimisho mwanamke dunia ni kilitanguliwa na mashindano ya mbio za mitumbwi kwa wavuvi wadogo zilizofanyika pembezoni mwa ufukwe wa Ziwa Victoria eneo la Kamanga Ferry.

Wizara ya Uvuvi na Mifugo kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani FAO na Shirika la EMEDO ndio waandaaji wa maadhimisho hayo ya mwaka huu. Shuhudia jinsi akinamama walivyopambana kuwania fedha kwa kuoneshana misuli ya upigaji makasia.

Wednesday, March 9, 2022

RAIA WA POLAND MLIMA BANGI, JELA MIAKA 30.

 


Mahakama Kuu ya Tanzania, imebariki kifungo cha miaka 30 jela walichohukumiwa Raia wa Poland, Damian Krzystof na mkewe mtanzania Eliwaza Pyuza Aprili 2021 baada ya kutiwa hatiani kwa kulima na kusafirisha bangi.


Hukumu ya rufaa hiyo ambayo nakala yake ilipatikana leo Machi, 9 2022, imetolewa na Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi, ambaye alizitupa sababu 10 za rufaa za wafungwa hao waliokuwa wakitetewa na wakili Median Mwale.


Hukumu iliyowafunga wawili hao ilitolewa Aprili 9, 2021 na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Moshi, Bernazitha Maziku ambaye aliwatia hatiani kwa makosa hayo waliyoyafanya Februari 8,2020 na kuagiza pia mali zao zitaifishwe na serikali.


Mali hizo ni shamba lenye ukubwa wa hekari moja lililopo Njiapanda ya Himo wilaya ya Moshi walipokutwa wakijihusisha na kilimo cha bangi, pikipiki aina ya KTM Adventure yenye namba za usajili MC972 AAD na fedha taslimu Sh26.7 milioni.


Hata hivyo, kupitia kwa wakili Mwale, wafungwa hao walikata rufaa wakisema Hakimu alikosea kisheria kuwatia hatiani wakilalamikia mambo kadhaa ikiwamo na upekuzi na ukamataji mali nyumbani kwao ulifanyika usiku bila kuwapo amri ya mahakama.


Halikadhalika walidai hakimu alikosea kisheria kwa kupokea vielelezo mbalimbali licha ya mnyororo wa makabidhiano kuvunjika, washitakiwa kutopatiwa nakala ya maelezo ya mlalamikaji na Damian na kutoelewa vizuri lugha ya Kingereza na Kiswahili.


Hata hivyo hoja hizo zilipanguliwa na wakili mwandamizi wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Kassim Nassir aliyeiwakilisha Jamhuri, akisema sababu hizo hazina mashiko na kwamba ushahidi uliowatia hatiani washitakiwa ulikuwa ni mzito.


Katika hukumu yake, Jaji Simfukwe baada ya kupitia hukumu iliyotolewa na Hakimu Maziku na sababu za rufaa, mahakama imeridhika kuwa mnyororo wa vielelezo ulizingatia utaratibu wa kisheria na hauacha mashaka kwa upande wa mashitaka.


Kuhusu suala la lugha, Jaji alisema katika usikilizwaji wa shauri hilo kulikuwepo mkalimani na Damian alikuwa na wakili ambaye hakuwahi kuibua suala hilo wakati wa usikilizwaji lakini Damian alikuwa akiwasiliana na mkewe kwa lugha ya Kiingereza.


Akizungumzia suala la upekuzi, Jaji Semfukwe alisema mahakama ina maoni kuwa mazingira ya upekuzi na uchukuaji vielelezo yalikuwa na udharura na kwamba kama ungefanyika utaratibu wa kuomba kibali mahakamani, huenda taarifa zingevuja.


“Kwa kuhitimisha na baada ya kukuona kuwa sababu zote za rufaa zilizoletwa na warufani hazina mashiko, rufaa hiyo inakosa miguu ya kusimama hivyo inakataliwa. Kutiwa kwao hatiani na kifungo walichopewa kinabaki kama kilivyo,”alisema Jaji.


Raia huyo wa Poland na mkewe, walikamatwa Februari 8, 2020 nyumbani kwao eneo la Shirimatunda nje kidogo ya mji wa Moshi wakiwa na mashine za kuchakata bangi na pia walikutwa wakilima bangi hiyo katika kiwanja chao eneo la Njiapanda.


Mbali na maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) kukamata shamba hilo lenye ukubwa wa kati ya hekari moja na nusu likiwa na miche 729, pia walikuta bangi iliyochakatwa na kuchanganywa na asali na Jam.

NDEGE ZA URUSI ZINAWEZA KUZUILIWA NCHINI UINGEREZA.

 


Mawaziri wanafanya kuwa kosa la jinai kwa ndege zinazomilikiwa au kukodishwa na Warusi kuingia kwenye anga ya Uingereza.


Meli zinazomilikiwa na Urusi tayari zimepigwa marufuku kukanyaga maji ya Uingereza, lakini hatua hiyo mpya inalenga ndege za binafsi zilizosajiliwa katika nchi ya tatu iliyokodiwa na matajiri wa Urusi.


Serikali ilisema kuwa vikwazo hivyo vitalenga watu walio karibu na Kremlin. Ndege moja katika uwanja wa ndege wa Farnborough huko Hampshire tayari inachunguzwa.


Mamlaka ya Uingereza imeshikilia ndege ya kibinafsi iliyosajiliwa Luxembourg kuchunguza kama inamilikiwa na Urusi na kuleta abiria wa Urusi nchini Uingereza kinyume na vikwazo.


Serikali pia imetangaza vikwazo vipya vya kibiashara ambavyo vitazuia mauzo yote ya Uingereza ya anga au teknolojia inayohusiana na anga kwenda Urusi, ikijumuisha huduma zinazohusiana nazo kama vile bima.


Akitangaza hatua hizo mpya, Waziri wa Mambo ya Nje Liz Truss alisema mabadiliko hayo yatasababisha "maumivu zaidi ya kiuchumi kwa Urusi na wale walio karibu na Kremlin".


Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono Ukraine na "kufanya kazi kuitenga Urusi katika jukwaa la kimataifa".


Katibu wa Uchukuzi Grant Shapps alisema Uingereza ilikuwa "moja ya nchi za kwanza kupiga marufuku ndege za Urusi na leo tunaenda mbali zaidi kwa kuifanya kuwa kosa la jinai kwa ndege za Urusi kufanya kazi katika anga ya Uingereza".


"Siku zote tutafanya kazi kumnyima [Rais wa Urusi Vladimir] Putin na wasaidizi wake haki ya kuendelea kama kawaida huku raia wa Ukraine wasio na hatia wakiteseka."


Nick Watt, mhariri wa kisiasa wa BBC Two's Newsnight, alisema hatua hizo zitashughulikia "eneo la kijivu" la ndege binafsi ambazo zimesajiliwa katika nchi ya tatu iliyokodiwa na Warusi matajiri.


Alisema ndege hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Farnborough, ambao ni uwanja wa ndege wa binafsi, inachunguzwa na mamlaka kwa sababu inaaminika kutumiwa na oligarch wa Urusi.


Vyanzo vya habari viliiambia Newsnight kwamba kutambua ndege kama ya Kirusi sio tu suala la kuifuata kwenye rada, lakini ni "kazi ya upelelezi" ili kubaini asili yake halisi.


Vikwazo hivyo vipya vimekuja muda mfupi baada ya serikali ya Uingereza kuthibitisha kuwa itapiga marufuku mafuta yote ya Urusi ifikapo mwisho wa mwaka huu, huku hatua sawa na hiyo ikitangazwa na Marekani.

MBUNGE DR KABATI AWAFUNDA WANAWAKE WAACHE ULIMBUKENI.

 

Mbunge wa viti maalum mkoani Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) DR Ritta Kabati akiongea na wanawake wa mkoa wa Iringa wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.Mbunge wa viti maalum mkoani Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) DR Ritta Kabati akiwa na mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake.
 Baadhi ya wanawake wa mkoa wa Iringa wakiwa kwenye maandano ya kusherekea siku ya wanawake duniani.


Na Fredy Mgunda,Iringa.

 

MBUNGE wa viti maalum mkoani Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) DR Ritta Kabati alisema licha ya wanawake kudai masuala ya Usawa wa kijinsia ni muhimu wakatambua kuwa usawa unaozungumzwa ni nafasi katika vyombo vya maamuzi na si katika ngazi ya familia kulingana na mila na desturi Zilizopo

Akizungumzia maadhimisho ya siku ya mwananmke Duniani Dr kabati alisema baadhi ya wananwake wamekosa uelewa wa kutosha kuhusu mkakati wa kufikia lengo la usawa wa kijinsia hali inayochochea wanawake walio wengi kuwa chanzo chas kuvunjika kwa ndoa

Dr Kabati alisema kuwa wanawake wanatakiwa kuendelea kutekeleza wajibu wao kama wanawake katika familia ikiwepo kuwaheshimu na kuwashirikisha kwenye majukumu mbalimbali waume zao ili kudumisha ndoa zao kwa kuwa wanaume ni kichwa cha familia.

Aliwataka wanawake kuacha tabia ya ulimbukeni kutokana na kipato na nyazifa walizonazo katika jamii badala yake wanatakiwa kuendelea kutimiza wajibu kwa wanaume zao kama ambavyo mila na desturi zinavyosema.

Dr kabati alisema kuwa wanawake wengi hawajitambui ndio maana ndoa nyingi kwa miaka ya hivi sasa zimekuwa zikivunjika bila sasababu za msingi kutokana na wanawake kuto waheshimu wanaume zao.

Alisema kuwa analaani tabia ya wanawake ambao wamekuwa wanafanyia tabia za dharau wanaume zao ambao ndio kichwa cha familia na ndio kimekuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya familia hivi sasa duniani.

Dr Kabati alisema kuwa wanawake wanatakiwa kuwatunzia siri wanaume zao hata kama wamewazidi madaraka na kipato hapo ndio ndoa itadumu kwa amani kwa sababu mke unakuwa umeshuka kwa mume wako.

Alisema kuwa jambo la hamsini kwa hamsini kwa ngazi ya familia haliwezekani kutokana na mira na destori za kiafrika kwa kuwa wanawake kutolewa mahari na wanaolewa  hali ambayo inaweka wazi kuwa mwanaume ndio kiongozi mkuu wa familia hata kama kipato chake ni kidogo.

 

Dr Kabati alisema wanawake wengi waliofanikiwa kwenye nafasi mbalimbali ni wale waliojishusha na kuwashirikisha wanaume zao hata kama wanavipato vidogo,kuheshimia na kuthaminia hapo itasaidia kuleta amnai kwenye ndoa.

 

Alimalizia kwa kusema kuwa wanawake wanatakiwa kuhakikisha wanawalea watoto wao kwenye malezi yanayotakiwa katika jamii ili kuwa na kizazi ambacho kitakuwa na maadili katika jamiii.

Tuesday, March 8, 2022

MWANZA WAADHIMISHA KWA KISHINDO SIKU YA WANAWAKE DUNIANI.

 

Matukio mbalimbali katika picha: Maandamano ya wadau mbalimbali kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2022 ngazi ya Mkoa Mwanza yaliyoadhimishwa kwa kishindo katika uwanja wa Nyamagana, Machi 08, 2022 

Shirika la kutetea haki za wanawake na wasichana KIVULINI ni miongoni mwa wadau muhimu walioungana na wanawake mkoani Mwanza kusherehekea Maadhimisho hayo ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel aliyewakilishwa na Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Ngusa Samike.
Maandamano ya wadau wakiingia katika uwanja wa Nyamagana.

Siku ya wanawake ilikuja kutokana na vuguvugu la wafanyakazi mnamo mwaka 1908, na ikatambuliwa rasmi kama hafla ya kila mwaka na miongo kadhaa baadaye, mnamo 1975.

Mnamo mwaka 1908, zaidi ya wanawake 15,000 waliandamana katika jiji la New York kudai muda mfupi wa kufanya kazi, malipo bora na haki ya kupiga kura.

Chama cha Kisoshalisti cha Marekani kilitangaza Siku ya Kitaifa ya Wanawake ya kwanza nchini Marekani mwaka mmoja baadaye.

Mjerumani Marxist na mwanaharakati Clara Zetkin alikuwa mmoja wa waasisi wa utambuzi wa toleo la kimataifa la Siku ya Kitaifa ya Wanawake ya Marekani.


Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akiongoza hamasa kwenye maandamano hayo.
Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi (katikati) wakiwa kwenye maadhimisho hayo.

Kila mwaka Machi 08, Umoja wa Mataifa husheherekea haki zilizopatikana kwa bidii za wanawake- na kuangazia changamoto ambazo bado ziko mbele katika kukomesha ubaguzi wa kijinsia katika karibu nyanja zote za maisha.

"Usawa wa kijinsia wa leo, kesho na endelevu" ndio kauli mbiu ambayo Umoja wa Mataifa umeichagua mwaka huu kuadhimisha kile kinachojulikana rasmi kama Siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Monday, March 7, 2022

UFILIPINO YAONGEZA UMRI WA KUANZA KUJAMIIANA KUTOKA 12-16

 


Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte amesaini sheria inayoongeza umri ambao mtu anaruhusiwa kufanya mapenzi kutoka miaka 12 hadi 16, katika juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia. 


Chini ya Sheria ya Ulinzi Maalum wa Watoto dhidi ya Unyanyasaji, Unyonyaji na Ubaguzi, watu wazima ambao wana uhusiano wa kimapenzi na mtu mwenye chini ya miaka 16, kisheria wana hatia ya moja kwa moja ya ubakaji. 


Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF, kabla ya sheria hiyo, Ufilipino ilikuwa na kiwango cha chini zaidi duniani kwenye umri ambao mtu anapaswa kujamiiana, ikiwa nyuma ya Nigeria ambao kisheria ni miaka 11.

AUAWA BAADA YA KUUZA GARI MNADANI.

 


Mfanyabishara na mkazi wa mtaa wa Kipondoda Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Sita John (45) amefariki dunia na mkewe kujeruhiwa baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Machi 7, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP Stella Mutabihirwa amesema kuwa tukio hilo limetokea Jumamosi Machi 05, 2022 wilayani Manyoni.


Kamanda huyo amesema siku ya tukio mfanyabiashara huyo alienda mnadani kuuza gari yake Sh15 milioni.


“Lakini badala ya kupewa fedha, alipewa ng’ombe (idadi haijajulikana) na fedha kiasi. Watu hawa wanaotaka kujipatia fedha kwa njia ya mkato, hawakujua kwamba mfanyabiashara Sita alipewa ng’ombe na fedha kiasi,”amesema.


Kamanda Stella amesema kuwa mkewe alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali wakati akijihami kwenye tukio hilo.


Kamanda Stella amesema baada aya kupata taarifa ya tukio hilo, Polisi ilifanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye familia ya marehemu ilimtambua.


Amesema watu hao walifanikiwa kupora fedha ambayo kiasi chake bado hakijafahamika.


“Upelelezi juu ya tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na mahojiano na mtuhumiwa aliyekamatwa ili kuwafahamu watu anaoshirikiana nao katika matukio ya wizina mauaji” amesema.


 “Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linaendelea kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Singida kuachana na vitendo vya kujitafutia mali kwa njia zisizo halali,”amesema kamanda huyo.

SHEKHE WA MKOA WA MWANZA ANENA MAZITO KUHUSU KUACHIWA KWA MBOWE

 Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia uamuzi wa Jamhuri kufuata kesi ya tuhuma za ugaidi iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Vilevile Kabeke ameipongeza hatua ya Mhe. Mbowe kuitikia wito wa Mhe. Rais na kukutana naye ikulu mara baada ya kutoka gerezani.

SAMIA ATAJA MKAKATI WA SERIKALI KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM.

 


Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inatambua changamoto wanazokabiliana nazo wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini kote na ndio maana inafanya jitihada za kuhakikisha inaweka mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunza ili kila Mtanzania anufaike na fursa za elimu.

Samia ameyasema hayo leo Machi 7 katika ziara yake maalum katika Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa huku akianisha kuwa jitihada hizo zimelenga kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata elimu bora.

Amesema baadhi ya jitihada hizo ni pamoja na Serikali imeendelea na mpango wake jumuishi wa 2021-2026 ambao utazingatia utoaji wa elimu jumuishi katika ngazi zote za elimu lengo likiwa ni kutoa elimu bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

“Tunafanya hivyo kwa sababu tunatekeleza azimio la kimataifa namba 4 katika maadhimio ya maendeleo endelevu yanayozungumzia elimu ikitutaka kutoa elimu yenye usawa kwa wote,” amesema.

Pia amesema kuwa Serikali imeandaa miongozo kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa elimu maalum na jumuishi nchini.

“Miongozo hiyo ni pamoja na ule wa usimamizi na uwendeshaji wa taasisi zinazotoa elimu maalum na jumuishi wa mwaka 2021 pamoja na ule wa ujenzi wa majengo ya serikali yanayozingatia wanafunzi wa mwaka 2020,”alisema.

MBUNGE ATOA BATI 10,CHAKULA KWA KAYA ZAIDI YA 200 ZILIZOEZULIWA NA UPEPO MKALI ULANGA

 

MBUNGE wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro Mh Salim Alaudin Hasham aliyevaa tisheti nyekundu katikati akiwa na wananchi walioathirika na nyumba zao kuezuliwa na upepo ambapo aliwatembelea na kutoa mabati 10 kwa kaya zaidi ya 200
MBUNGE wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro Mh Salim Alaudin Hasham aliyevaa tisheti nyekundu katikati akiteta jambo na wananchi walioathirika na nyumba zao kuezuliwa na upepo ambapo aliwatembelea na kutoa mabati 10 kwa kaya zaidi ya 200
MBUNGE wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro Mh Salim Alaudin Hasham aliyevaa tisheti nyekundu kulia akiwa na wananchi  walioathirika na nyumba zao kuezuliwa na upepo ambapo aliwatembelea na kutoa mabati 10 kwa kaya zaidi ya 200
MBUNGE wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro Mh Salim Alaudin Hasham aliyevaa tisheti nyekundu akikagua nyumba za wananchi  walioathirika na nyumba zao kuezuliwa na upepo ambapo aliwatembelea na kutoa mabati 10 kwa kaya zaidi ya 200
MBUNGE wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro Mh Salim Alaudin Hasham aliyevaa tisheti nyekundu akikagua nyumba za wananchi  walioathirika na nyumba zao kuezuliwa na upepo ambapo aliwatembelea na kutoa mabati 10 kwa kaya zaidi ya 200
MBUNGE wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro Mh Salim Alaudin Hasham aliyevaa tisheti nyekundu akikagua nyumba za wananchi  walioathirika na nyumba zao kuezuliwa na upepo ambapo aliwatembelea na kutoa mabati 10 kwa kaya zaidi ya 200


MBUNGE wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro Mh Salim Alaudin Hasham ametoa bati 10 kwa kaya zaidi ya 200  ambazo nyumba zao zimeezuliwa na upepo mkali jambo lililopelekea kukosa makazi.

Hatua hiyo inatajwa kwamba itawapunguzia ukali wa maisha wananchi ambao wamekumbana na hali hiyo kutokana na nyumba zao kuezuliwa na upepo mkali

Mbunge Salim Ameyasema hayo baada ya kukagua uharibifu huo uliotokea siku za hivi karibuni na kupelekea vijiji vya Gombe,Mwaya,Kichangani,Mbuga na Kivukoni kupata maafa hayo na baadhi ya wananchi kukosa makazi hadi sasa.

Jimbo hilo la Ulanga limekuwa likipata maafa hayo mara kwa mara kutokana na baadhi ya nyumba kukosa mapaa imara jambo linalopelekea upepo pamoja na mvua kuezua nyumba hizo kirahisi.

Mbunge pia ameahidi kutimiza ahadi  hiyo ndani ya wiki moja ili kila Mwananchi arejee kwenye makazi yake haraka na kuendelea na shughuli zao za maendeleo.

YANGA BARIIIIIIIDI KILELENI

 YANGA YATIFUA NYASI ZA KIRUMBA

_______________ Baada ya dakika 90, ubao wa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza umesoma Geita Gold 0-1 @YangaSc Bao pekee la ushindi limefungwa na Fiston Mayele ilikuwa dakika ya kwanza na liliweza kudumu mpaka dakika ya 90 zinatamatika. Mayele anafikisha mabao 10 na pasi 3 za mabao sawa na Relliants Lusajo wa Namungo mwenye mabao 10. Yanga inafikisha pointi 45 wakiwa kileleni bila kupoteza mchezo wowote. Zaidi sikiliza #SportsRipoti ya @jembefmtz

WAANDISHI WA HABARI MARA KUTEMBELEA MIRADI 41 YA MAJI VIJIJINI

 JUMLA ya Miradi mipya 41 ya Maji yenye thamani ya fedha Bilioni 16.7 zilizotolewa na serikali ili kupunguza adha ya maji inayowakabili wananchi wa vijiji mbalimbali katika mkoa wa Mara, itatembelewa na waandishi wa habari ili kuona hatua ya utekelezaji wake pamoja na kuibua changamoto zinazowakumba wananchi katika upatikanaji wa maji safi na salama.

Baadhi ya Waandishi wa Habari katika mkoa wa Mara wa vyombo vya habari vya Magazeti, Televisheni na mitandao ya kijamii  kutoka gazeti la Habari leo,Uhuru ,Nipashe,Majira,ITV,Azam Tv,Mara Online na Uhuru Digital,watatembelea miradi hiyo ya maji kwa siku sita katika wilaya sita za mkoa huo.

Lengo la kutembelea miradi hiyo iliyopo katika wilaya sita za mkoa huo ambazo ni Musoma,Tarime,Rorya,Serengeti,Butiama na Bunda ,ni kuupasha umma juu ya miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA) ili kuwezesha upatikanaji wa wa huduma ya maji safi na salama.

Pia Waandishi wa Habari wataibua changamoto zilizopo za upatikanaji wa maji unaowakumba wananchi waishio vijijini,kutoa elimu ya umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu ya maji na kuziripoti katika vyombo vya habari ili ziwafikie wananchi na serikali.

Mratibu wa waandishi wa habari watakaoitembelea miradi ya maji,Ghati Msamba ambaye ni mwandishi wa habari gazeti la Uhuru alisema kuwa baadhi ya waandishi waliiomba RUWASA kuwawezesha usafiri ili kuitembelea miradi kuona utekelezaji wake na changamoto za upatikanaji wa maji katika maeneo ya vijijini.

"Tuliomba RUWASA katika mkoa wetu wa Mara kutuwezesha usafiri kutembelea miradi ya maji vijijini kwasababu tulitamani sana kuitembelea miradi ya maji lakini ukosefu wa fedha za usafiri tukakwama ikatubidi tuombe RUWASA.

" Wametukubalia ombi letu,jumatatu tutaizungukia miradi kwa siku sita kwenye wilaya sita kuona inavyofanya kazi na jitihada za serikali katika kutatua changamoto za maji pamoja na kuibua changamoto za maji zinazowakabili wananchi wa vijijini na kutoa elimu ya umuhimu wa utunzaji wa miundombinu ya maji kisha tuandike habari na kuziripoti kwenye vyombo vya habari ili kuifikia jamii na serikali"alisema Msamba.

Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mara,Mhandisi Tulinumpoki Mwakalukwa alisema kuwa waandishi watatembelea wilaya hizo kama walivyoomba ili kuona miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa.

"RUWASA mkoa wa Mara una wilaya 6 za Bunda, Butiama, Musoma, Rorya, Tarime na Serengeti, Kwa mwaka huu 2021/22 tunatekeleza jumla ya miradi mipya 41 yenye thamani ya Sh.16.7 Bilioni. Aidha tumepata nyongeza ya miradi 9 yenye thamani ya sh.4.5 Billion kwa mpango wa COVID-19(Uviko).

"RUWASA ni Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini. RUWASA inasimamiwa na Bodi ya wakurugenzi, na Mkurugenzi mkuu chini ya wizara ya maji,makao yake makuu yapo Dodoma, na ina ofisi ngazi ya mkoa inayoongozwa na Meneja wa Mkoa,na ofisi ya wilaya inayoongozwa na Meneja wa Wilaya" alisema Mwakalukwa.

Meneja huyo alisema kuwa miradi ya maji inasimamiwa na Jumuiya za watumiaji wa maji (CBWSO) vinavyoratibiwa na Meneja wa Wilaya nakwamba waandishi wa habari wataishuhudia miradi hiyo na kupata taarifa kwa kila mradi unaotekelezwa kwenye wilaya hizo.

Mwakalukwa ameongeza kuwa RUWASA inaahidi kutoa  ushirikiano kwa vyombo vya habari kama wadau muhimu wa kuihabarisha na kuielimisha jamii kuhusu ujenzi na uendeshaji wa miradi ya Maji vijijini Ili kuwa na miradi endelevu.