ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, November 15, 2024

PROF:JANABI MLOGANZILA YAJIZATITI VILIVYO KUPUNGUZA VIFO VYA WATOTO WACHANGA 'NJITI'

 


NA VICTOR MASANGU, KIBAMBA 


Wataalam wa afya nchini wamesisitizwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania maisha ya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda ili kupunguza vifo vya watoto hao na kuweza kufikia malengo ya mpango mkakati wa mwaka 2030 wa kuwa na vifo vya watoto wachanga chini ya vifo 12 kwa kila vizazi hai 1000 .

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua maadhimisho ya kuelekea siku ya mtoto aliyezaliwa kabla ya muda (njiti) yaliyofanyika katika Hopsitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila ambayo yameshirikisha wataalam wa afya wa watoto wachanga kutoka MNH Upanga &Mloganzila.

Prof. Janabi ameeleza kuwa, inakadiriwa kwamba kwa kila watoto 1000, kuna watoto wachanga wapatao 24 wanaofariki ndani ya siku 28 za kwanza na kwamba mikakati ya kupunguza vifo hivi haiwezi kuwa endelevu bila kushirikiana wadau katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuboresha ujuzi wa kuhudumia watoto hao.

Amefafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikiratibu progamu mbalimbali ambazo lengo lake ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na wale wa chini ya miaka mitano, program hizo ni kama kumsaidia mtoto kupumua baada ya kuzaliwa, kupanua huduma za watoto wachanga kwa kujenga wodi za watoto wachanga (Neonatal Units) katika hospitali za mikoa na wilaya, pamoja na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ya namna ya kuhudumia watoto wachanga (Essential newborn care).

Kwa upande wake Daktari Bingwa Bobezi wa watoto wachanga MNH Upanga Dkt. Martha Mkony amesema katika Afrika karibu mtoto mmoja kati ya kumi huzaliwa kabla ya wakati ambapo watoto hao ukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na matatizo ya kupumua, maambukizi , matatizo ya chakula na hatari za ukuaji wa muda mrefu.
“Hata hivyo pamoja na kuwepo kwa changmoto hizo lakini bado kuna matumaini kupitia juhudi za Serikali kwani kuna maboresho ya kutia moyo katika utunzaji wa watoto wachanga nchini kwa kuboresha vituo vya afya na hospitali za kuhudumia watoto wachanga na kujengwa pamoja na kusomesha wataalam wa afya’’ameeleza Dkt. Mkony

Aidha maadhimisho hayo yameenda sambamba na uzinduzi wa kitengo cha kuhifadhi na kuratibu maziwa ya mama (Lactational Management Unit)  kwa la kuhakikisha watoto hao wanapata maziwa ya mama zao kwa wakati kwakua watoto wanaozaliwa kabla ya muda wanakua na uzito mdogo ambao unasababisha kuhitaji kiasi kidogo cha maziwa, kwahiyo hata kama mama anauwezo wa kutoa maziwa mengi kiasi kinachobaki kinahifadhiwa hivyo ni rahisi mama akiruhuisiwa kurejea nyumbani anakwenda na maziwa yake. Hii inasaidia mpango wa kuhakikisha watoto wachanga wanayonyeshwa miezi sita bila kupewa chochote.

RAMOVIC WA TS GALAXY AFRIKA KUSINI NDIYE KOCHA MPYA WA YANGA

 MJERUMANI mwenye asili ya Bosnia and Herzegovina, Sead Ramovic (45) ndiye kocha mpya wa mabingwa wa Tanzania, Yanga anayechukua nafasi ya Muargentina Miguel Angel Gamondi aliyefukuzwa baada ya msimu mmoja na nusu kazini.

Ramovic anajiunga na Yanga akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini, klabu yake ya kwanza kufundisha kama Kocha Mkuu baada ya kustaafu soka mwaka 2014.

Alizaliwa wa Stuttgart, Ujerumani Magharibi na kisoka aliibukia FC Feuerbach kama kipa, kabla ya kuhamia SpVgg Feuerbach mwaka 1995, Stuttgarter Kickers mwaka 1999, VfL Wolfsburg mwaka 2001 na mwaka 2004 alijiunga na Borussia Mönchengladbach alikocheza hadi 2005 akahamia Kickers Offenbach.

Julai 2006 alijiunga na Tippeligaen Tromsø IL ya Norway hadi 2010 akaenda kudakia Sivasspor ya Uturuki hadi 2011 akahamia  Metalurh Zaporizhzhia ya Ukraine kwa muda mfupi kabla ya kutimkia FK Novi Pazar ya Serbia. 

Novemba 17 mwaka 2011 alijiunga na Lillestrøm SK ya Norway kwa ajili ya msimu wa 2012 kabla ya kuhamia Vendsyssel ya Denmark msimu wa 2013, baadaye Strømsgodset ya Norway pia kabla ya kustaafu Mei 21 mwaka 2014.

Ramović aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Bosnia na Herzegovina mwaka wa 2004 na kujumuika kikosini mara kadhaa, japokuwa hakuwahi kudaka hata mechi moja.

Amekuwa akiifundisha TS Galaxy yenye maskani yake Kameelrivier, Manispaa ya Nkangala jirani na Siyabuswa, Mpumalanga tangu mwaka 2021 na baada ya msimu uliopita kuiwezesha kumaliza nafasi ya sita ambayo ni rekodi kwa klabu hiyo - anahamia Yanga yenye maskani yake makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, Ilala Jijini Dar es Salaam.

YANGA YAMFUTA KAZI GAMONDI NA MSAIDIZI WAKE MSENEGAL

 KLABU ya Yanga imeachana na kocha wake, Muargentina Miguel Angel Gamondi pamoja na msaidizi wake, Moussa N’Daw baada ya msimu mmoja na nusu wa kuwa timu hiyo.

Yanga inaachana na Gamondi baada ya timu kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara wakifungwa 1-0 na Azam FC Novemba 2 na Tabora United 3-1 Novemba 7 zote Uwanja wa Azam FC Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Gamondi anaondoka Yanga akiiacha na mataji matatu aliyoikuta nayo, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama CRDB Bank Federation Cup.

Zaidi Miguel Angel Gamondi atakumbukwa daima katika historia ya Yanga baada ya kuiongoza timu hiyo kuichapa Simba mabao 5-1 Novemba 5 mwaka jana Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

NAIBU WAZIRI MKUU ATOA SALAMU ZA POLE KWA KATIBU WA MKUU WA MKOA WA MWANZA.


 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko jana alhamisi ya tarehe 14 Novemba, 2024 alifika nyumbani kwa Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ndugu Matia Levi na kuwafariji kufuatia kufiwa na mtoto wake  Faith Matia, aliyefariki Jumatano tarehe 13 novemba, 2024.


Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.

 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza na waombolezaji waliofika nyumbani kwa Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ndugu Matia Levi (wa kwanza kulia aliyekaa) na kuwafariji kufuatia kufiwa na mtoto wake  Faith Matia, aliyefariki Jumatano tarehe 13 novemba, 2024.

 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akipata maelezo  kutoka kwa Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ndugu Matia Levi (aliyeketi na mkewe)  kufuatia kufiwa na mtoto wake  Faith Matia, aliyefariki Jumatano tarehe 13 novemba, 2024.
 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akiagana na  Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ndugu Matia Levi, mara baada ya kufika nyumbani kwa katibu huyo kutoa rambirambi zake na kuwafariji kufuatia kufiwa na mtoto wake  Faith Matia, aliyefariki Jumatano tarehe 13 novemba, 2024.
 Wakati huo huo salamu za Mkurugenzi wa Makampuni ya Jembe ni Jembe Group Dr. Sebastian Ndege naye katuma salamu zake za rambirambi juu ya msiba huo uliotokea Jumatano tarehe 13 novemba, 2024.

MSANII WA MWANZA NDANI YA RWANDA - AWACHANA WASANII / MSIJIFUNGIE NDANI KAMA MISWAKI

 


Anaitwa Fivara anatokea Rock City Jijini Mwanza.

HOSPITALI YA TAIFA MLOGANZILA YABORESHA ZAIDI HUDUMA ZA KIBOBEZI KWA WAGONJWA WA KISUKARI

 


NA VICTOR MASANGU 


Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila imeanzisha huduma mbili mpya za ubingwa bobezi kwa wagonjwa wa kisukari, huduma hizo ni pamoja na huduma ya matibabu ya magonjwa ya miguu yatokanayo na ugonjwa wa kisukari pamoja na huduma ya kliniki maalum ya kisukari kwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 25 maarufu huduma ya mpito.

Kuanzishwa kwa huduma hizo hospitalini hapa ni mwendelezo wa Serikali wa kuboresha huduma za afya nchini ikiwemo kuanzisha matibabu ya ubingwa bobezi ambayo hayapatikani hapa nchini ikiwa ni mkakati wa kuwapunguzia usumbufu wananchi na gharama za kutafuta huduma hizo nje ya nchi.

Akizindua kliniki hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam MNH ambaye pia ni Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Kisukari na Homoni Dkt. Faraja Chiwanga amesema huduma hizo zitaongeza wigo wa huduma hospitalini hapa ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji uliofanywa na serikali yao.


“Kwa mfano kiliniki hii ya mpito ni ya kwanza kabisa hapa nchini, itakuwa inahudumia vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 25 ambao wanahitaji uangalizi na ushauri tofauti ukilinganisha na wagonjwa waliopo katika makundi mengine” Dkt. Faraja Chiwanga

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kisukari na Homoni, Dkt. Aidan Banduka amesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wanaohudumiwa katika kliniki hiyo kutokana na ubora wa huduma zinazotolewa ambapo kwa siku wanaona kati ya wagonjwa 80 hadi 160 ambapo kuanzia tangu Disemba, 2022 hadi mwaka 2024 wamehudumia wagonjwa zaidi ya 30,000 ambapo kati ya hao 6,535 ni wapya.

Dkt. Banduka ameongeza kuwa jamii inapaswa kujikinga na ugonjwa huu kwa kufuata mtindo bora wa maisha kwa kuzingatia lishe bora, kupunguza matumizi ya chumvi, mafuta, kuacha matumizi ya tumbaku na unywaji wa pombe uliopitiliza na kufanya mazoezi mara kwa mara.

Uzinduzi wa huduma hizo umeenda sambasamba na maadhimisho ya siku ya kisukari duniani ambayo huadhimishwa Novemba 14 kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu 2024 ni kisukari na afya bora, ikihimiza kuongeza ufahamu wa athari za kisukari kwa afya ya mwili na akili kwa wagonjwa wenye kisukari.

Wednesday, November 13, 2024

UWT KIBAHA MJI YAFANYA ZIARA BABU KUBWA KATA YA MKUZA KUVUNJA MAKUNDI

 


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA

Jumuiya ya umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi (UWT) Wilaya ya Kibaha mji  imeamua kufanya ziara maalumu kwa ajili ya kuwahimiza wanachama wao kuhakikisha  kwa sasa wanavunja  makundi yote  na badala yake  wanapaswa kuungana kwa pamoja kwa ajili ya  kushinda kwa kishindo  katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na  Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja  wakati  alipofanya ziara yake maalumu yenye lengo la kukutana na baadhi ya wanawake wa kata ya Mkuza kwa ajili ya  kujadili mambo mbali mbali ikiwemo suala la kutoa msisitizo wa kuvunja makundi pamoja na kuwapa hamasa wagombea ambao wameteuliwa na chama kuweza kujitosa katika uchaguzi huo bila woga.


 Ziara hiyo ambayo imewakutanisha  viongozi mbali mbali wa UWT Kata ya mkuza pamoja na  baadhi ya wanawake wengine ambao wameteuliwa na chama kwa ajili ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kuwakumbusha  wale wote ambao wameshindwa katika kura za maoni  wawe mstari wa mbele kwa ajili ya kuweza kuwasapoti  kwa kiasi kikubwa wale ambao wameteulina kugombea katika nafasi mbali mbali.

"Mchakato wa kura za maoni umemalizika katika chama na ndio maana mimi kama Mwenyekiti wenu wa UWT nimeambatana na katibu kwa lengo la kufanya ziara hii na kutoa hamasa ya wagombea wote wanawake ambao wameweza kuteuliwa na chama kutorudi nyuma na kwamba wawe mstari wa mbele wa kuweza kujitokeza katika nafasi zao ambao wanaziwania katika uchaguzi wa serikali za mitaa ikiwemo pamoja na kuvunja makundi ambayo yalikuwepo hapo nyuma,"alisema Mwenyekiti Mgonja.

Mwenyekiti huyo aliongeza kwamba lengo lao kubwa kama UWT ni kuendelea kupita katika maeneo mbali mbali kwa ajili ya kuwahimiza wanawake wote  ambao wameteuliwa na chama kuhakikisha wanaweka misingi imara katika kukilindana kukiteteaa chama hivyo wanapaswa kujitokeza kwa wingi  bila woga wowote katika zoezi zima la uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuweza kuchukua mitaa yote na kushinda kwa kishindo.

Katika hatua nyingine Mgonja aliwahimiza wanawake wote wa UWT katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchagzi wa serikali za mitaa kuwa makini sana na kujitahidi kuepukana na propaganda mbali mbali ambazo zinatolewa na vyama vingine vya upinzani na kwamba wazipuuze na waweke misingi na kutokisaliti chama chao.

Kwa upande wake Katibu wa (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini Cecilia Ndalu ambaye aliambatana na Mwenyekiti katika ziara hiyo amesema kwamba  wanawake ni jeshi kubwa na lengo la chama ni kuhakikisha kwamba  inashinda kwa kishindo katika mitaa yote katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa.

TOSCI YATEKELEZA PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI (AFDP) KWA VITENDO

 

Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na wataalam kutoka Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu wametembelea Taasisi ya Udhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) Mkoani Morogoro.

Mfuko huo wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unajenga maabara ya kisasa ya uchambuzi wa Ubora wa Mbegu kwa ajili ya Taasisi hiyo kwenye makao makuu yake yaliyopo katika chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA).

 Kufika Kwa Ujumbe huo Mkoani Morogoro, ni sehemu ya ziara  ya kikazi ya kutembelea maeneo yanayotekeleza Programu hiyo,Tarehe 8 Novemba 2024.



Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)







Tuesday, November 12, 2024

MUSWADA WA KUSAIDIWA KUFA UNA ULINZI MKALI, MBUNGE ASEMA.

 


Watu wazima ambao wanaugua mahututi ambao wanatarajiwa kufariki katika muda wa miezi sita wataweza kuomba usaidizi ili kujikatia uhai chini ya mapendekezo ya sheria ya Uingereza na Wales.

Chini ya mswada uliochapishwa Jumatatu , madaktari wawili wa kujitegemea watalazimika kuridhika kuwa mtu anastahiki na amefanya uamuzi wake kwa hiari. Maombi pia yatalazimika kuidhinishwa na jaji wa Mahakama Kuu.

Mbunge wa chama cha Labour Kim Leadbeater, ambaye amewasilisha mswada huo, alisema unajumuisha "ulinzi mkali zaidi popote duniani".

Hata hivyo, wapinzani wa kusaidiwa kufa wameibua wasiwasi kwamba watu wanaweza kuhisi kulazimishwa kukatisha maisha yao.

Sheria za sasa nchini Uingereza zinazuia watu kuomba msaada wa kimatibabu ili kufa.

Muswada huo utahitaji wale wanaoomba kusaidiwa kufa:

  • Awe na umri wa zaidi ya miaka 18, mkazi wa Uingereza na Wales na amesajiliwa na daktari kwa takriban miezi 12
  • Kuwa na uwezo wa kiakili wa kufanya uamuzi kuhusu kukatisha maisha yao
  • Eleza matakwa ya "wazi, yaliyotulia na yenye habari", isiyo na shuruti au shinikizo, katika kila hatua ya mchakato.

Lazima kuwe na pengo la siku saba kati ya tathmini za madaktari wawili na siku 14 zaidi baada ya uamuzi wa jaji kabla ya mtu kusaidiwa kufa, isipokuwa wakati kifo cha mtu kinatarajiwa mara moja.

Mtu huyo ataruhusiwa kubadilisha mawazo yake wakati wowote na hakuna daktari ambaye atalazimika kushiriki katika mchakato huo.

Sheria bado inakataza madaktari au watu wengine kukatisha maisha ya mtu. Iwapo vigezo na ulinzi vyote vinatimizwa, nyenzo vya kukatisha maisha ya mtu lazima vijidhibiti vyenyewe.

Chini ya mswada huo daktari anaweza tu kuandaa dawa/tembe au kumsaidia mtu kumeza.



JESHI la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia dereva wa bodaboda, Juma Afyusisye (38), mkazi wa Iwambi mkoani humo kwa tuhuma za kummwagia mafuta ya petroli na kumchoma moto mtoto (jina linahifadhiwa) kisa Sh. 10,000. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Benjamin Kuzaga, alisema tukio hilo lilitokea Jumanne wiki hii. “Sababu za tukio hilo ni baada ya mtuhumiwa kumpa mtoto huyo Sh. 10,000 akanunue maandazi ya Sh. 5,000 dukani, lakini mtoto akatumia fedha hiyo kwa matumizi yake, hakurudi na hiyo fedha,” alisema Kamanda Kuzaga. Alisema mtoto huyo wa kiume ambaye ni mwanafunzi darasa la pili katika Shule ya Msingi Iwambi, amejeruhiwa maeneo mbalimbali mwilini. Alisema baada ya mtoto huyo kurudi nyumbani akiwa hana fedha wala maandazi aliyotumwa, mtuhumiwa alijichukulia sheria mkononi kwa kummwagia petroli kwenye shati alilovaa kisha kuwasha kiberiti. “Mtoto amelazwa Hospitali Teule ya Ifisi katika Mji Mdogo wa Mbalizi akiendelea kupatiwa matibabu. Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wazazi au walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, badala yake watafute njia sahihi ya kuwaadhibu watoto pindi wanapokosea,” alishauri. Hata hivyo, Kamanda Kuzaga alisema Jeshi la Polisi halitavumilia wala kufumbia macho vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika jamii, litaendelea kuchukua hatua kali kwa watuhumiwa kwa mujibu wa sheria. Akizungumza akiwa hospitalini, mtoto huyo alisema, alipewa Sh. 10,000 kwenda dukani kununua maandazi na sukari na wakati akirejea nyumbani alipoteza Sh. 200, ndipo mtuhumiwa huyo akakasirika na kuchukua tairi na kumwagia mafuta ya petroli na kuwasha moto kisha kuondoka. "Mjomba Inno alivyoniona akaenda kuwaita watoto wenzake na kunimwagia maji ili kuzima moto, lakini haukuzima alichukua mchanga kunimwagia ukazima. “Nilisikia sauti za dereva akisema ‘hawa watoto wasije wakaleta umbea’ akamwita bosi wake akanichukua na kunipeleka zahanati,” alisimulia mtoto huyo. Mama wa mtoto huyo, Marita Abiud alisema, alipigiwa simu na wasamaria wakimweleza kuhusu tukio hilo na alipofika nyumbani alipata taarifa kwamba, aliyefanya kitendo hicho ni jirani yake, ndipo alipokwenda zahanati na kumkuta mtoto akiwa katika hali mbaya na kumpeleka hospitalini. Baba wa mtoto huyo, Uswege Mwambigila, ameonesha kushangazwa na kitendo cha mtuhumiwa huyo kumchoma moto mtoto wake na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali hasa eneo la kitovu. “Amemwagia mwanangu petroli sijui lengo lake lilikuwa ni nini au alikuwa na nia ya kumuua. Kama ni madai hajarudisha chenji, alipaswa kuja kwa wazazi ili tumlipe, yawezekana alikuwa na lengo la kumuua mtoto wangu,” alidai Mwambigija.

KIVUMBI CHA MBIO ZA COAST CITY MARATHON KUTIMUA RASMI NOVEMBA 30 KIBAHA

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 


Waandaaji wa  Mbio za Coast  City Marathon  Mkoa wa Pwani ambazo huwa zinafanyika kila mwaka Mkoani humo, msimu huu   wamekuja kivingine  baada ya kugeukia maboresho ya miundombinu ya elimu.

Mbio hizo ambazo zinatarajia kufanyika Novemba 30,2024 Kibaha Mkoani humo  zinalenga kukusanya sh. 80 milioni na kwamba pesa hizo zitaelekezwa kuboresha miundombinu ya shule ya Msingi Pangani

Tofauti na misimu miwili iliyopita maboresho mengine katika mbio hizo ni motisha kwa washiriki wote kwani mbali na kupata medali na zawadi mbalimbali pia watanufaika na supu ya pweza,madafu na nyama choma siku ya tukio hilo



Akizungumza leo mjini  Kibaha wakati wa uzinduzi wa dirisha la usajili pamoja na vifaa vitakavyotumika siku ya tukio mwenyekiti wa maandalizi hayo Frank Muhamba amesema kuwa kutokana na umuhimu wa elimu kwa jamii wameona ni vema waelekeze nguvu huko ili kusaidia juhudi za serikali 

Amesema kuwa kufanya hivyo si kuwa uongozi wa shule hiyo uliwaomba bali ni kutokana na uzalendo walionao na wanaamini kuwa kusudio lao litatimia


Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo Afisa elimu msingi Halmashauri ya mji wa Kibaha  Theresia Kyara amesema kuwa ni jambo la kuwapongeza waandaajli hao kwani wanaenda kusaidia kupunguza changamoto zilizopo ndani ya sekta muhimu


Balozi wa mbio hizo Twaha Ambiere amesema kuwa tofauti na awamu zilizopita kwa mwaka huu wameboresha mambo mbalimbali ikiwemo zawadi na motisha kwa washirili wote


Afisa michezo halmashauri ya Mji wa Kibaha Burwan Tilusubya amewataka wakazi wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi ili kujisajili na kushiriki kikamilifu kwenye mbio hizo kwani zinafaida nyingi ikiwemo kujenga afya.