ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, March 8, 2025

HADITHI YA JINSI WIMBO WA SHAGGY (IT WASN'T ME') ULIVYOTENGENEZWA.

 


The Story of 'It Wasn’t Me' by Shaggy.

Wakati Shaggy akirekodi albamu yake ya Hot Shot, yenye mikwaju kama "It Wasn't Me" na "Angel", lebo hiyo iliikataa kama albamu ya kutupa isiyo na manufaa na "hakuna hits" humo ndani yaani ni kama album ya kupoteza muda tu hivyo "It wasn't Me" haikutolewa hata kama single.

Lakini mfululizo wa ajali za kufurahisha na siyo mbaya, ikiwemo upakuaji haramu kwa njia za kiwizi na kiudukuzi mitandaoni, ilipelekea kuusukuma wimbo "It Wasn't Me" kuwa moja ya vibao vya kwanza viliyopelekwa sokoni kwa njia ya kimagendo na kugeuka kuwa muhimu kwenye menyu za ma-Dj wengi duniani.

Mtayarishaji VICE anakutana na Shaggy kwenye kumbukumbu ya miaka 20 ya album 'Hot Shot' ambayo inaambatana na kutolewa kwa albamu yake mpya kabisa ya Hot Shot 2020, na kuhadithia jinsi wimbo "It Was'nt Me" ilivyowafungulia dunia. Click here to subscribe to VICE: http://bit.ly/Subscribe-to-VICE
Kutoka katika picha za kumbukumbu mwanahabari Albert G. Sengo (left) na mwanamuziki toka nchini Marekeni 'Shaggy' alipokuja jijini Mwanza mnamo mwaka 2011 na kupiga bonge moja la show katika Tamasha la  'Serengeti Fiesta 2011'
Kabla ya kutoa burudani katika tamasha la Fiesta, Shaggy alihudhuria tamasha la asili ya watu wa kanbila la Wasukuma linaloitwa Bulabo na kusimikwa kwa kupewa hadhi ya Utemi wa Sukuma kupitia jina lake hili hilo maarufu na kuitwa "Ng'wana Shaggy"

MAMA KOKA AUNGURUMA AUNGANA NA WANAWAKE KIBAHA MJI MAADHISHO YA SIKU YA MWANAMKE DUNIANI

 


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA 

Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Mama Selina Koka amewahimiza wanawake kuachana na kuwa na tabia ya kuwa  tegemezi na badala yake wahakikishe  wanachapa kazi kwa ushirikiano wa pamoja katika shughuli zao mbali mbali za maendeleo  kwa lengo la kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na wimbi la umasikini.

Mama Koka ameyabainisha hayo  alipokuwa mgeni rasmi wakati wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ambapo ambayo yamefanyika katika  ukumbi wa Kibaha shooping Moll na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali, viongozi wa vyama, wajasiriamali  pamoja na wanawake kutoka makundi tofauti katika Halmashauri ya Kibaha mji.
Amesema kwamba kupitita maaadhimisho hayo wanawake wanapaswa kubadilika na kuwa na kupendana wenyewe kwa wenyewe ikiwa pamoja na kuweza kuchangamkia fursa za mikopo ambayo itaweza kuwasaidia  kukuza mitaji yao na kuiendeleza katika suala zima la kufanya biashara zao.

"Nimefarijika sana kushiriki na wanawake wenzangu katika siku hii ya maadhimisho ya siku ya mwanamke dunia lakini kitu kikubwa ninachowaomba mnatakiwa kuwa na ushirikiano na upendo wa pamoja katika mambo mbali mballi ikiwa pamoja na kuchangamkia fursa za mikopo ambayo itaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika  kuendeshea biashara zao  na hatimaye kujikwamua kiuchumi,"amesema Mama Koka.
Pia amewahimiza wanawake hao kuhakikisha kwamba wanakuwa na malezi bora kwa watoto wao ikiwa pamoja na kuwalinda kwa pamoja bila ya kuwa na ubaguzi wowote na kuwapatia haki zao zote za msingi ikiwemo elimu sambamba na mahitaji mengine yanayostahili.

Katika hatua nyingine amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutenga fedha amabzo zimeweza kusaidia katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo na kuwaomba wanawake kumpa sapoti ya kutosha katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kumpa kura nyingi za kishindo.

Kwa upande wake mkuu wa  Idara ya maendeleo ya jamiikatika Halmashauri ya mji Kibaha    Leah Lwaji  amesema kwamba lengo kubwa ni kuwawezesha wanawake katika makundi mbali mbali katika kuwainua katika nyanja ya kiuchumi pamoja na kuwakumbusha umuhimu wa haki, usawa pamoja na uwezeshaji katika kuchochea suala zima la maendeleo  endelevu kwa wananchi.

"kupitia maadhimisho haya tunawakumbusha wanawake kuhakikisha umuhimu wa haki saawa pamoja na uwezeshwaji,kwa lengo la kuweza kuchochea ukuaji katika sekta ya uchumi, maendeleo jumuishi na ustawi wa jamii, kwa maendeleo  endelevu kwa wanawake, ili waweze kufikia malengo yao.

Aidha amesema kwamba Halmashauri ya Kibaha mji bado inaendelea na uhamasishaji na uelimishaji kwa wananwake juu ya umuhimu wa kondoa mila ambazo zimepitwa na wakati amabpo imefanikiwa kupita na kutoa elimu katika kata 14 ambapo jamii imefanikiwa kupata elimu katika nyanja ambali mbali ikiwemo ufundi, uashi, makenika pamoja na mambo ya umeme.

Kadhalika amesema kwamba Halmashauri ya Kibaha mji imeendelea kutekeleza agizo la Rais Samia la kutenga asilimia 10 yanayotokana na mapato yake ya ndani, kwa kila mwaka kwa ajili ya kuwaapatia makundi ya wanawake, vijana pamoja na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuweza kuwawezesha kichumi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Mwajuma Nyamaka amewapongeza wanawake na kuwataka kuhakikisha kwamba wanajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ikiwa pamoja na kumpa sapoti Rais Samia Suluhu ili aweze kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Dangini Mfaume Kalanguti wamewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha kwamba wanaweka misingi mzuri  ya kuchapa kazi kwa bidii na kuachana na kuwa tegemezi ikiwemo  kuwalea na kuwalinda watoto katika masuala mbali mbali ya ulinzi na usalama.
 
Kauli mbiu ya mwaka huu  ya siku ya mwanamke Duniani inasema kwamba Wanawake na wasichana tuimarishe Haki, usawa na uwezeshaji ambapo pia imeambatana na maonesho mbali mbali kutoka kwa wajasiriamali wa Halmashauri ya Kibaha mji.

SIMBA SC YATISHIA KUTOINGIZA TIMU KWA MKAPA LEO DHIDI YA YANGA

 

KLABU ya Simba imetishia kutocheza mechi ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi ya Yanga leo baada ya usiku wa jana kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam kwa mujibu wa kanuni.






RAIS DKT. SAMIA AKISHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Akishiriki Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoani Arusha, leo tarehe 08 Machi, 2025.

Friday, March 7, 2025

RC MTANDA ATOA WITO KWA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi nchini katika uchaguzi mkuu 2025 kwani Serikali imejipambanua kwenye kukuza usawa, haki na uwezeshaji kwa jamii.

Mhe.Mtanda ametoa wito huo jana Machi 06, 2025 katika uwanja wa mpira wa Nyamagana wakati akihutubia wanawake na wananchi walioshiriki maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya wanawake ngazi ya Mkoa.


Mtanda amesema wanakwake ni jeshi kubwa nchini hivyo likitumika vizuri litaleta maendeleo na Serikali inaendelea kutoa usawa wa kijinsia kwenye uongozi na ndiyo maana hata Mwanza wapo viongozi wengi wa kike na 43% ya viongozi ni wanawake nchini.


"Tunazo bilioni 2.4 kwa ajili ya mikopo kwa walemavu tena kwa jinsia zote na kundi hili siyo lazima waombe mkopo kwa vikundi hata mmoja mmoja na jumla ya wataalamu wa afya 3201 wameajiriwa kuanzia 2021 hadi 2025 na kufanya huduma za afya kuimarika zaidi mkoani Mwanza." Mhe. Mtanda.

Akisoma risala ya wanawake wa Mkoa huo Mwalimu Sophia Turuya amesema wanawake nchini ni wengi zaidi ya wanaume kwa uwiano wa zaidi ya milioni moja hivyo kundi hilo likipewa fursa litakua ni chachu ya maendeleo.


Aidha, ameipongeza Serikali kwenye uboreshaji wa huduma za afya na akawasilisha ombi la kuongezwa kwa wataalamu wa afya na mazingira pamoja na kuweka mazingira rafiki ya kupata nishati safi ya kupikia pamoja na mabweni ya wasichana ili watoto wa kike wasome katika mazingira salama.

Vilevile, ameutaja mfuko wa maendeleo ya wanawake kupitia vikundi vya ujasiriamali kama mkombozi wa mikopo kwa masharti nafuu kwa wanawake ambao unawapatia mitaji kupitia mikopo itokanayo na mapato ya ndani ya halmashauri.


Katika kunogesha maadhimisho hayo yenye kauli mbiu 'wanawake na wasichana 2025, tuimarishe haki, usawa na uwezeshaji' michezo mbalimbali imerindima kama kuvuta kamba, mbio kwenye magunia, kufukuza kuku na washindi wamejipatia zawadi nono.

MC KIANDA ATAMANI TUZO YA MC WA TAIFA

 



Na Oscar Assenga, TANGA.

MSHEHERESHAJI aliyeibuka kinara katika Tuzo za MC Bora wa Mkoa wa Tanga 2025 Giliad Kianda “MC Kianda” amesema kwa sasa malengo yake anayatazama kuwania tuzo bora za Taifa kutokana na umahiri wake na ubunifu katika utekelezaji wa kazi zake.

Kianda aliyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa mashindano ya Tuzo la Tanga Awards na kufanikiwa kuibuka na Tuzo ya MC Bora kwa Mkoa wa Tanga baada ya kupigiwa kura na wadau mbalimbali.
 
Alisema kwamba wanawashukuru wana Tanga kwa kumsapoti mpaka akafanikiwa kuibuka na ushindi katika shindano hilo kwani bila wao asingeweza kupata mafanikio aliyoyapata huku akiwahaidi kile ambacho walikiona kwake wategemee makubwa zaidi.

“Niwaambie tu kwanza wadau wangu nawashukuru sana na niwahaidi wategemee kazi nzuri zinakuja kutokana na ubunifu ambao utakuwa kipaumbele lakini pia niwashukuru waandaaji wa tuzo hizo KEBI na timu yake nawashukuru”Alisema MC Kianda.

Aidha alisema utolewaji wa Tuzo katika Tasnia mbalimbali nchini ikiwemo washereheshaji wa matukio mnbalimbali ikiwemo Harusi imetajwa kuwa chachu ya kuwapa motisha kufanya kazi kwa kujituma na ubunifu.

Awali akizungumza mshindi wa Tuzo mbili za Uandaaji wa Video mwaka 2024/2025 na upigaji wa Picha Mwaka Production aliwashukuru wapiga kura maana watu wanaona kazi zao na wanapiga kura na juhudi zao na maarifa ndio zimewaweka kuwa namba moja.

Katika tuzo hizo zile ambazo zimeshindanishwa ni za Heshima pamoja na utambuzi wa mchango wa wasanii mbalimbali katika mkoa wa Tanga ambazo zinatajwa kwenye kuwa chachu katika kuongeza ubunifu na ufanisi zaidi katika kazi zao.




HALMASHAURI KUU YA CCM KIBAHA MJI YAWAPONGEZA DED,MBUNGE KOKA NA DC KIBAHA KWA KUTEKELEZA ILANI

 

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John (kushoto) akitunukiwa tuzo na Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu cha Utekelezaji wa Ilani ya CCM  kwa kipindi cha Julai 2024  hadi Desemba 2024 kilichohudhuria na viongozi wa chama pamoja na serikali kwa ajili  namna ya ilani ya chama ilivyotelekezwa katika miradi ya mbali mbali ya  maendeleo.

VICTOR MASANGU, KIBAHA

Halmashauri kuu ya Chama cha mapinduzi (CCM) Kibaha  kwa pamoja imeridhishwa na miradi mbali mbali ya maendeleo katika sekta mbali mbali ikiwemo maji, elimu, afya miundombinu ya barabarara pamoja na hudumu  nyingine za maendeleo iliyotekelzwa kwa kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Disemba mwaka 2024.

Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu cha Utekelezaji wa Ilani ya CCM  kwa kipindi cha Julai 2024  hadi Desemba 2024 kilichohudhuria na viongozi wa chama pamoja na serikali kwa ajili  namna ya ilani ya chama ilivyotelekezwa katika miradi ya mbali mbali ya  maendeleo.

Nyamka amesema kwamba wameweza kupita katika maeneo mbali mbali kwa ajili ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo ambapo kwa  kauli moja yameipitisha kutokana na kuona kazi nzuri ambayo yameifanya katika utekelezaji huo wa miradi ambayo itaweza kuwa mkombozi mkubwa katika kuwasaidia  kwa kiais kikubwa wananchi kuweza  kupata huduma kwa urahisi katika mahitaji mbali mbali.

Aidha Nyamka amebaisha kwamba katika kikao hicho  wamewez kumpongeza  kwa dhati Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John kwa kuweza kupambana na kuweza  kusimamia kwa vitendo  utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) kwani miradi mbali mbali imeweza kutekelezwa.

Aidha kikao hicho kimempongeza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri  ya Kibaha mjini Dkt. Rogers Shemwelekwa  kwa kuwekakuweka mikakati mizuri ambayo imeweza kuongeza chachu zaidi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya ndani ikiwemo sambamba na kusimamia maslahi ya watumishi wake.

Pia Mwenyekiti huyo hakusita kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Mhe:Silvestry Koka  kwa kutekeleza majukumu yaoke ipasavyo ya kuwatumikia wananchi ikiwemo suala zima la kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo hali amabayo imechangia kwa kiais kikubwa kuweza kuleta chachu ya maendeleo.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka amesema kwamba ameweza kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo kwani miradi mingi katika sekta mbali mbali ya maji, afya, elimu, miundombinu ya barabara pamoja na mambo mengine ya huduma za kijamii imeweza kutekelezeka  kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wake Katibu wa chama caha mapinduzi (CCM) Issack Kaleiya amesema kwamba miradi hiyo amabyo walipita kwa ajili ya kukagua ni moja ya utekeelzaji wa ilani ya chama na kwamba itaweza kuwa ni mkombozi mkubwa katika kutatua kero na changamoto  mbali mbali za  wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amebainisha kwamba katika Halmashauri ya Kibaha mji Ilani ya chama imeweza kutekelezwa katika miradi mbali mbali ya maendeleoa na kumshukuru kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Sauluhu Hassan kwa kuweza kutenga fedha ambazo zimekwenda kutekeleza miradi  ya maendeleo.

Tuesday, March 4, 2025

MOHAMED IQBAL DAR, MBUNIFU WA JINA LA TANZANIA AFARIKI DUNIA

 


Mohammed Iqbal Dar, aliyebuni jina la Tanzania, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 jijini Birmingham, Uingereza, ambako aliishi tangu mwaka 1965.

Dar amefariki baada ya kuugua kwa takriban miaka 10, kipindi ambacho alikuwa hawezi kutembea na alikuwa chini ya uangalizi wa karibu nyumbani kwake.

Alizaliwa Agosti 8, 1944, mkoani Tanga. Baba yake, Dk. Tufail Ahmad Dar, alikuwa daktari mashuhuri aliyewahi kufanya kazi katika mikoa ya Tanga na Morogoro.

Mohammed Iqbal Dar alipata elimu yake ya msingi na sekondari katika Shule ya Aga Khan, kabla ya kuendelea na masomo yake katika Shule ya Sekondari Mzumbe mwaka 1964.

Akiwa mwanafunzi Mzumbe, aliona tangazo katika gazeti la The Standard likiwahamasisha wananchi kupendekeza jina jipya la taifa lililoundwa baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kuna nyakati kulizuka mzozo juu ya nani ndiye alikuwa mbunifu wa jina Tanzania.

Kwa bahati ya kipekee, pendekezo lake la jina Tanzania lilichaguliwa kuwa jina rasmi la nchi, na alitunukiwa tuzo ya Shilingi 200 pamoja na medali iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Habari wakati huo, Sheikh Idrisa Abdul Wakil.

Kifo cha Mohammed Iqbal Dar ni pigo kwa historia ya taifa, kwani mchango wake uliasisi utambulisho wa nchi inayojivunia jina la Tanzania hadi leo.

KOCHA ALIYECHEMKA MANCHESTER UNITED BENNI McCATHY SASA NDIYE KOCHA MKUU MPYA WA TIMU YA TAIFA YA KENYA, HARAMBEE STARS


Gwiji wa soka wa Afrika Kusini Benni McCarthy ametambulishwa kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars.

Enzi zake akiwa Man United katika benchi la ufundi.

Mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 47 amesaini kandarasi itakayomfikisha hadi kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika la TotalEnergies (AFCON) za 2027 ambazo Kenya itaandaa kwa pamoja na majirani zake Uganda na Tanzania.


McCarthy, ambaye kituo chake cha mwisho cha kazi kilikuwa na Manchester United ya Ligi Kuu ya Uingereza kama kocha wa mashambulizi, alitajwa rasmi na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Jumatatu jioni.


"Nimefurahi kuwa hapa, na ninajivunia kuchukua changamoto hii nikiwa na timu ya taifa ambayo ina uwezo mkubwa," McCarthy alisema alipokuwa akitambulishwa.


Rais wa FKF Hussein Mohammed anaamini kuwa McCarthy ndiye mbadala kamili wa Engin Firat aliyejiuzulu mwishoni mwa mwaka jana.


“Tuna imani kuwa Benni ndiye mtu sahihi wa kuiongoza timu yetu ya taifa mbele. Uzoefu wake, maono na kujitolea kwake kuendeleza soka la Kenya vinapatana kikamilifu na matarajio yetu. Tulikuwa na orodha ndefu ya makocha ambao walikuwa na nia lakini tulipoangalia kile anacholeta mezani, tuliamini kuwa ulikuwa uamuzi sahihi,” Hussein alisema.


Mtaalamu huyo anakuja moja kwa moja kufanya kazi, huku Kenya ikitarajiwa kuvaana na Gambia ugenini na kuwakaribisha Gabon mwezi huu katika raundi mbili zijazo za kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA la 2026.


Mtaalamu huyo pia anakodolea macho matokeo mazuri kwa Harambee Stars katika michuano ya TotalEnergies Afrika (CHAN) ambayo itaandaliwa kwa pamoja na Kenya, Uganda na Tanzania mwezi Agosti.

"Inawezekana kushinda michezo miwili na kukusanya pointi sita na kisha tunaweza kuona ni wapi hilo linatupeleka," McCarthy alisema kuhusu mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia. Anaongeza; "Tunahitaji tu kubadilisha mawazo ya wachezaji na sio kukata tamaa nyumbani. Kampeni hii inaweza kufanikiwa na chochote kinawezekana. Tutafanya kazi kwa bidii na wachezaji na wafanyikazi na tunaangalia uwezekano wa kumaliza kundi katika nafasi mbili za juu.

Kuhusu matamanio yake ya awali kwa CHAN, McCarthy alisema; “Kama waandaji, bila shaka tunataka kujieleza vyema na kufanya kila tuwezalo kama timu kuwafanya Wakenya wajivunie. Lengo la CHAN na AFCON mnamo 2027 bila shaka ni kuona timu ikicheza katika hatua za mwisho iwe nusu nusu au hata fainali. Kwa kufanya kazi kwa bidii, inawezekana."

Gwiji huyo wa Bafana Bafana amewahi kuzifundisha Amazulu na Cape Town City katika nchi yake ya asili ya Afrika Kusini, na kuipeleka timu ya kwanza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ya CAF ya TotalEnergies kwa mara ya kwanza kabisa.

Kama mchezaji, McCarthy alikuwa mshambuliaji aliyepambwa, na alikuwa mfungaji bora wa pamoja kwenye AFCON ya 1998. Katika ngazi ya klabu, alishinda Ligi ya Mabingwa ya UEFA akiwa na FC Porto na pia alikuwa na kazi ya kutunga akiwa na Blackburn Rovers na West Ham nchini Uingereza kabla ya kumaliza soka yake ya kucheza nyumbani akiwa na Orlando Pirates mnamo 2013.


Anakuja kwa kazi yake ya kwanza ya usimamizi wa timu ya taifa na ataungana na watu wanaowafahamu, Vasili Manousakis kama Kocha Msaidizi, Moeneeb Josephs kama Kocha wa Makipa, na Pilela Maposa kama Mchambuzi wa Utendaji.

BENKI YA CRDB, UNDP zazindua programu kuwasaidia wafanyabiashara kufikia Soko Huru la Afrika (AfCTA)

 

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (wa pili kushoto) akikata utepe kuashiria kuzindua programu ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kushiriki fursa zilizopo katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) inayotekelezwa na CRDB Bank Foundation pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa (UNDP). Wengine katika picha ni Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa (wa pili kulia), Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa (kulia) pamoja na Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Taasisi ya CRDB Bank Foundation (CBF) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa (UNDP), leo wamezindua mwongozo uliorahisishwa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati nchini wenye fursa za kuwaunganisha na Soko Huru la Afrika (AfCTA) utakao wawaongezea uwezo na maarifa zaidi ili waweze kupanua biashara zao kote barani Afrika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo ambao baadaye ulifuatiwa na semina fupi kwa wajasiriali hao, uliofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Benki ya CRDB, Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe. Exaud Kagahe alisema “Serikali inajua faida za mkataba huu ndiyo maana Bunge liliidhinisha mnamo Septemba 2021, na hivyo kuifanya nchi yetu kustahiki kunufaika na Soko Huria la Afrika. Uamuzi huu wa serikali unalenga kufungua fursa kwa wajasiriamali wetu nje ya mipaka yetu ya kitaifa,”

Aliendelea kusema "Ili kuchukua fursa hizi kikamilifu, watu wetu lazima wawe na taarifa sahihi, maarifa muhimu, na ujasiri wa kuvuka mipaka kutafuta fursa hizi popote zinapojitokeza ndani ya mataifa 55 yetu Bara la Afrika. Kinachoendelea katika semina ya leo ni sehemu ya mikakati ya kuwawezesha wajasiriamali wetu kushindana na wenzao sokoni.”

Akielezea jukumu la CRDB Bank katika programu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, TullyEsther Mwambapa alisema taasisi yake imejipanga kuhakikisha inatoa elimu ya fedha, mafunzo ya biashara na mitaji wezeshi itakayo wawezesha wajasiriamali kunufaika na Soko Huria la Afrika (AfCTA) linalokadiriwa kuwa na watu zaidi ya bilioni 1.4.

Kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UNDP), Mkurugenzi Mkaazi wa Shrika hilo, Shigeki Komatsubara alieleza fursa zinazoambatana na soko huru la AfCTA ikiwamo kuongezeka kwa biashara za ndani, kuvutia uwekezaji, na kuchochea mabadiliko ya kiuchumi hasa kwa wanawake wajasiriamali kote barani Afrika.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa (wa pili kulia), Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa (kulia) pamoja na Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara wakipiga makofi wakati watazama video fupi katika hafla ya uzinduzi wa programu ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kushiriki fursa zilizopo katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) inayotekelezwa na CRDB Bank Foundation pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa (UNDP).


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe akizungumza na washiriki wa semina kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kushiriki fursa zilizopo katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) inayotekelezwa na CRDB Bank Foundation pamoja na UNDP.




Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa akizungumza na washiriki wa semina ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kushiriki fursa zilizopo katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) inayotekelezwa na CRDB Bank Foundation pamoja na UNDP.


Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara akizungumza na washiriki wa semina kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kushiriki fursa zilizopo katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) inayotekelezwa na CRDB Bank Foundation pamoja na UNDP.











Sehemu ya washiriki wa semina ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kushiriki fursa zilizopo katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) inayotekelezwa na CRDB Bank Foundation pamoja na UNDP.




Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa (wa tatu kulia), Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa (wa pili kulia), Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara (wa tatu kushoto), Mkuu wa Uendeshaji CRDB Bank Foundation, Joyceline Makule (wapili kushoto), Mkuu wa Biashara changa Benki ya CRDB, Fadhil Bushagama pamoja na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo (wa kwanza kulia) wakiwa katika pic ha ya pamoja na washiriki wa semina ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kushiriki fursa zilizopo katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) inayotekelezwa na CRDB Bank Foundation pamoja na UNDP.