ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, January 30, 2016

MAHAKAMA YA MAFISADI YAIVA, JANUARY MAKAMBA ASEMA WALIMTAKA RAIS KAMA MAGUFULI NA WAMEMPATA, PATA DONDOO ZA MAGAZETI HAPA.

Mahakama ya mafisadi yaiva, January makamba asema walimtaka Rais kama Magufuli na wamempata, pata dondoo za magazeti hapa.

BODI YA SHULE YA PAMBA YAVUNJWA.Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo amevunja bodi ya shule ya sekondari Pamba iliyopo jijini Mwanza na kumvua madaraka mkuu wa shule hiyo Aidan Dotopery pamoja na walimu wengine wawili kutokana na kushindwa kusimamia vyema matumizi ya fedha na mali za shule zao. 

Walimu wengine waliovuliwa nyadhifa zao na mkuu huyo wa mkoa ni pamoja na mkuu wa shule ya sekondari Nyakurunduma January Luganyika na mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nyamagana Masau Mtakilolwa. 

 Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza kufanya ziara katika shule hizo na kuonyesha kutoridhishwa na mazingira ya uwekezaji kwenye vitega uchumi vya shule ya sekondari ya Pamba, huku baadhi ya nyaraka pamoja na mikataba ambayo shule hiyo imefunga na wafanyabiashara hao ikiwa imegubikwa na utata.

Moja kati ya masuala yaliyochomoza kwenye kikao kilichofanyika shuleni hapo hata hatua ya yaivunja bodi ya shule ni madai ya tuhuma za kuingiza shule katika mkataba tata wa ujenzi wa maduka 65....CHEKI VIDEO HAPO JUU.

Friday, January 29, 2016

SUMAYE AIANGUKIA SERIKALI WANANCHI KUVAMIA SHAMBA LAKE LA EKARI 33 MABWEPANDE JIJINI DAR ES SALAAM

 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda akisalimiana na Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye  Dar es Salaam leo asubuhi mara baada ya kuwasili eneo la Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kuangalia eneo la ekari 33 la Sumaye lililovamiwa na wananchi.
 WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye (wa pili kulia), na mke wake mama Esther (kushoto), wakimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (kulia) eneo la shamba lake la ekari 33 lililopo Mabwepande Manispaa ya Kinondoni lililovamiwa na wananchi walipotembea eneo hilo Dar es Salaam leo asubuhi.
 Hapa Sumaye na viongozi wengine wakitafakari jambo.
 DC Makonda akihutubia katika mkutano huo. Kulia ni Diwani wa Kata ya Mabwepande, Suzan Masawe.
 Mheshimiwa Sumaye (kushoto), akiongoza kuonesha mpaka wa shamba lake.
 Mhe. Sumaye akielezea uhalali wake wa kumiliki eneo hilo.
 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mji Mpya,  Justine Chiganga (kulia), akizungumza katika mkutano huo 
 Moja ya kibanda kilichojengwa na wananchi waliovamia eneo la Mhe Sumaye.
 Baadhi ya vibanda vilivyojengwa na wananchi katika eneo la Sumaye.
 Askari Polisi wakiimarisha ulinzi wakati wa mchakato wa kutembelea eneo hilo lililovamiwa.
 Wananchi wa eneo la Mabwepande wakiwa kwenye mkutano huo.
 Mkazi wa eneo hilo Athuman Mnubi akielezea jinsi walivyovamia eneo la Sumaye.
 Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabwepande Abdalla Omari Kunja akizungumza katika mkutano huo.
 Diwani wa Kata ya Mabwepande, Suzan Masawe akizungumza katika mkutano huo.
Ofisa Ardhi Manispaa ya Kinondoni, Matinga Ernest akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya Ardhi katika Manispaa hiyo.

Dotto Mwaibale

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, ameiangukia serikali na kuomba msaada baada ya wananchi kuchukua sheria mkononi na kuvamia eneo lake la ekari 33 lililopo Mabwepande katika Manispaa ya Kinondoni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Serikali imemuahikikishia Sumaye kuwa haina mpango wa kumkandamiza mtu mnyonge wala tajiri hivyo itahakikiha inatoa haki kwa kila mmoja baada ya wiki mbili kwa kua imesikiliza pande zote mbili katika mgogoro huo. 

Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya wananchi wa kitongoji  cha Kimondo mtaa wa mji mpya Kata ya Mabwepande na Sumaye  Dar es Salaam leo asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda alisema ili kumaliza mgogoro huo ambao Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye ameiomba serikali kuingilia kati ni lazima busara kutumika.

Alizitaka pande hizo mbili kuiachia serikali kwa wiki mbili ili kutafuta njia bora ya kumaliza tatizo hilo huku wananchi wakitakiwa kuache kuendelea na ujenzi na kugaiana maeneo katika shamba hilo.

“Serikali ya Rais Magufuli ni sikivu na ndio maana ilikuwa tayari kumsikiliza Waziri Mkuu wetu Mstaafu Sumaye na kusikiliza wananchi ili kutenda haki tunatambua migogoro ya ardhi ilivyokuwa na athari kwa jamii hatuna mpango wa kumkandamiza tajiri wala mnyonge,”alisema.

Alisema katika eneo hilo anajua jinsi wananchi walivyotumia nguvu katika kuwekeza ujenzi na rasilimali zao lakini kwa sasa wasitishe shughuli hizo na kuendelea kugawana maeneo na Sumaye pia kuacha uwekezaji ili kutafuta suluhu.

Zipo njia nyingi tutazitumia kumaliza mgogoro huu ikiwemo kufuata sheria kwa kuangalia iwapo mzee wetu alikiuka taratibu kweli za kumiliki ardhi kama ilivyodaiwa na wananchi hatua gani serikali tuchukue,”alisema.

Alisema pia wanaweza kukaa na Sumaye na kuzungumza naye ili kukubali hasara kwa kutoa eneo kidogo na kuwapatia wananchi  hao ambao hawana makazi au Manispaa kutafuta eneo mbadala na kuwauzia kwa bei nafuu.

Alizitaka pande hizo mbili kutambua umuhimu wa kulinda amani katika mgogoro huo kwa changamoto zilizopo kutatuliwa bila kutumia nguvu.

Makonda pia aliagiza serikali ya kijiji kufanya utambuzi wa wananchi hao wenye makazi katika shamba la Sumaye.

Awali katika mkutano huo Sumaye alimueleza Makonda jinsi serikali ilivyo na kazi ngumu ya kushughulikia migogoro ya ardhi na kuomba kutumia busara zake kumpatia eneo hilo analomiliki kihalali.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kama nilivyokueleza awali serikali yetu inakazi ngumu sana hasa kutokana na viongozi wa chini kutokuwa wasikivu na wakweli eneo hili namiliki kihalali nina nyaraka zote na ninalipia kila mwaka na nilikuwa katika mpango wa kutafuta wafadhili ili kuliendeleza kwa kujenga Chuo Kikuu,”alisema.

Alisema  yeye na familia yake waliuziwa eneo hilo toka mwaka 1997 na anaamini serikali itatenda haki.

 Diwani wa kata hiyo Suzan Masawe alisema anauthibitisho kuwa eneo hilo lilikuwa pori na Sumaye alilitelekeza kwa muda mrefu na kusababisha uhalifu ikiwemo wanawake kubakwa,mali za wizi kufichwa na uhalifu mbalimbali.

Alisema kutokana na hatua hiyo   walimtafuta Sumaye lakini hakuwa na ushirikiano kwakuwa hata alipofanya uwekezaji kwa kuchimba kisima cha maji alikataa kuwapa wananchi .

Suzan alisema kutokana na hasira za wananchi hao kwa kukosa huduma za kijamii kwa muda mrefu ikiwemo eneo hilo kutokuwa na shule,Zahanati wala kituo cha polisi waliamua kuvamia na kujigaia maeneo. 

Mmoja wa wananchi hao Athuman Mnubi alikiri kweli hawana umiliki halali wa eneo hilo na katika hatua ya kutafuta makazi walivamia msitu huo uliotelekezwa na Sumaye.
Alisema wanaamini kutokana na ahadi ya serikali ya Rais Magufuli katika kupora maeneo yaliyotelekezwa  na wawekezaji watasaidiwa.

WAKATI huo huo Makonda alisimamisha na kukamata baadhi ya malori ya kokoto na mchanga, wafanyakazi na Mwekezaji wa kigeni kutoka India  Sules Waljan wanaochimba mchanga,kokoto na kifusi katika eneo la Mabwepande.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuona uharibifu mkubwa wa mazingira na alipowahoji wafanyakazi na Mwekezaji huyo kama wanavibali walisema hawana.

Makonda amewafikisha watuhumiwa hao kituo cha polisi cha Wazo Hill ili kutoa maelezo ya kina na kusema kuwa serikali inatumia gharama kubwa kwa uhalibifu huo wa mazingira ambao pia unafanywa katika vyanzo vya maji na matengenezo ya madaraja yanayoharibiwa ni makubwa.

SAMATTA DILL DONE KLABU YA KRC GENK.

Mbwana Samatta, amewasili nchini Ubelgiji tayari kujiunga rasmi na Klabu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.
Samatta aliondoka nchini juzi saa 6:00 usiku kuelekea Ubelgiji ili kukamilisha taratibu za kujiunga na klabu hiyo mpya ya Genk, baada ya bosi wa TP Mazembe, Moise Katumbi, kukubali kumuuza.
Meneja wa mshambuliaji huyo, Jamal Kisongo, alisema amewasiliana na Samatta na kumweleza kwamba amefika salama na ameanza kufuata taratibu zote ili aweze kufanya kazi nchini humo.
Alisema mara baada ya kuwasili, alitakiwa kufuatilia kibali cha kazi ambacho kitamruhusu kufanya kazi katika klabu hiyo mpya na muda wowote ataanza mazoezi.
“Kuhusu Hati ya Uhamisho wa Kimataifa) (ITC), Katumbi (Moise) amemhakikishia kuituma kwa klabu hiyo, kwani kabla ya kuondoka juzi aliongea naye na kumpa baraka zote za maisha mapya katika Klabu ya Genk,” alisema.
Kisongo alisema kwa kuwa bosi huyo wa TP Mazembe ameridhia kumuuza Samatta kwa Genk, siku chache zijazo anatarajia kwenda nchini Ubelgiji kwa ajili ya kusaini mkataba ambao atafaidika nao ikiwa mshambuliaji huyo atauzwa kwa klabu nyingine.
Samatta ambaye alitwaa tuzo ya kuwa Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani, alikubali kujiunga na timu ya KRC Genk na kugomea ofa zilizotolewa na klabu za Nantes na Olympique Marseille za Ufaransa

TAKUKURU YATANGAZA KIAMA KWA WALA RUSHWA HASA WATUMISHI WA UMMA.

 Kaimu Mkurugenzi Mkuuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru), Kamishna Valentino Mlowola (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisini jijini Dar es Salaam leo asubuhi kuhusu mikakati mbalimbali ya taasisi hiyo ya kupambana na rushwa nchini hasa kwa watendaji wa Umma na kesi zinazochunguzwa ili watuhumiwa wafikishwe mahakama wakati wowote baada ya kukamilika kwa uchunguzi wake.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo. Kulia ni John David wa Gazeti la Majira.
 Mwendeshaji wa Mtandao wa Fullshangwe, John Bukuku (kulia), akiuliza swali katika mkutano huo.
Baadhi ya wakurugenzi wa Taasisi hiyo wakiwa katika mkutano huo.

Na Dotto MwaibaleTAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru), imetoa onyo kwa taasisi nyeti nne hapa nchini ikiwemo wanaohusika na matumizi ya fedha za Umma kufuata sheria, taratibu na kanuni.Pia,Takukuru inashughulikia kukamilisha kesi kubwa 36, zinazowahusu watumishi wenye ushawishi na hadhi kubwa hapa nchini ambapo kati ya hizo zipo zilizokamilika na kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.Akizungumza jijini Dar es Salaam leo , Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Valentino Mlowola alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kwa wananchi kuwajulisha matendo ya rushwa na ufisadi yanayoendelea hapa nchini.Alisema kutokana na hali ya wananchi kuona nia ya serikali ya awamu ya tano katika kushughulikia matatizo ya rushwa na ufisadi hapa nchini ametoa ovyo kwa maofisa wa umma wanaofanya rushwa na ufisadi kuwa sehemu yao ya kazi na miradi ya kuwaingizia kipato."Natoa onyo kwa maofisa wa umma ambao wamefanya rushwa na ufisadi kuwa ni sehemu ya kazi zao na miradi ya kuwaingizia kipato, wajitafakari kabla hawajaamua kujihusisha na vitendo vya rushwa,"alisema.Alisema  hawatasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watumishi watakaojiingiza katika kulihujumu taifa na wananchi kwani wananchi wanakiu ya kupata maendeleo na maisha bora na kuwataka watambue wananchi wa jana si wa leo kwani wamedhamiria kuunga mkono juhudi za serikali yao.Mlowola alitoa ovyo kwa maofisa maduhuli na watekelezaji wa jukumu la kukusanya kodi za wananchi kwa kutomuonea mtu haya kwa atakayejihusisha na ubadirifu wa fedha na mali ya umma."Wakusanye kodi halali ya serikali kwa kufuata sheria, taratibu na Kanuni zinazowaongoza kukusanya kodi, tutachukua hatua stahiki pale kutakapokuwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni zilizopo,"alisema.Pia, Mlowola alitoa ovyo kwa watakaohusika kwenye matumizi ya fedha za umma kwamba wafuate sheria, taratibu na kanuni  zinazowaongoza kwani taasisi hiyo haitawavumilia watakaokiuka fedha za serikali isiyo halali.Mbali na hilo, pia Kaimu huo alitoa onyo kwa watumishi wa umma wenye jukumu la kuhudumia mahitaji ya umma kwa kutojihusisha na rushwa kwa kutekeleza majukumu yao katika muda uliotakiwa, weledi na uaminifu.Alisema taasisi hiyo haipo kwa lengo la maslahi ya watu wabadhilifu wa mali ya umma kwani uchunguzi wa kesi ya kuisababishia hasara serikali shilingi bilioni 8.5 kutokana na ukwepaji wa kodi wa kampuni ya Mafuta ya Lake Oil kwa kufanya udanganyifu kuuza mafuta ndani ya nchi Petrol lita 17,461,111.58 kwa kudanganya zilisafirishwa umefikia hatua nzuri."Takukuru imekamilisha shauri la hili na mtuhumiwa wamepewa miezi miwili kurejesha mikononi fedha zote na kuwarudisha mahakamani endapo watashindwa kurejesha kiasi hicho,"alisema.Alisema mbali na shauri hilo, wapo kwenye hatua nzuri ya kukamilisha uchunguzi wa kesi ya hati fungani ya malipo yaliyolipwa na kampuni ya Enterprise Growth Markert Advisor(EGMA), kiasi cha dola 6,000,000 kwa lengo la kuisaidai Tanzania kupata mkopo wa dola 600,000,000."Takukuru imebaini fedha hizo dola 6,000,000 zilitakatishwa na watumishi wa umma wasio waaminifu wakishirikiana na baadhi kutoka sekta binafsi huku wakijua fedha hizo wamezipata kwa njia haramu,"alisema.Akizungumzia hatua aliyochukua rais, Dk. John Magufuli kwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Mhandisi Benhadard Tito kwa tuhuma zinazomkabili tayaari wanachunguza shirika hilo la reli.Alisema kulikuwepo na ukiukwaji wa kuwapata wazabuni kwenye ujenzi wa reli ya kisasa ya kimataifa(Standard Gauge) unaosimamiwa na Shirika la Hodhi la Reli Nchini(RAHCO), wanamekamatwa ikiwemo raia wa Kenya aliyekuwa kwenye mchakato huo, Kanji Muhando.Kaimu huyo alisema shauri la kesi ya mabehewa ya kokoto 25 ya shirika la reili nchini (TRL), ya kukiuka sheria ya manunuzi ya umma Na.21/2004 pamoja na kanuni zake kutoka kampuni ya Hindustha Engineering and Industries Limited limekamilika."Uchunguzi umekamilika na tumeshapeleka kwa mkurugenzi wa Mashtaka kuomba kibali cha kuwafikisha watuhumiwa waliobainika kujihusisha na matendo ya rushwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za ununuzi wa umma mahakamani,"alisema. Alisema rais alijipa kazi ya kutumbua majipu hivyo aliwasihi watumishi wa taasisi hiyo kutumikia wananchi kwa eledi huku akibainisha tayari wanatekeleza azma na dhamira ya rais ya kupambana na rushwa.Akitolea ufafanuzi swala la kumsubiri rais kutumbua majipu ndio taasisi hiyo ifanye ufafanuzi, Mlowola alisema taasisi hiyo imejipanga vilivyo tangu Novemba 20 mwaka jana wakati rais alipohutubia bungeni alipoonesha dhamira ya na nia ya dhati ya kupambana na rushwa na ufisadi bila kumuonea mtu haya."Nitoe rai kwa wananchi kutoa taarifa ili tuweze kujua kabla hatujapigwa, tukiweza kuisaidia serikali kuokoa fedha kabla hatujapigwa zitasaidia wananchi  kutoa elimu bure, upatikanaji wa dawa na mishahara mizuri,"alisema.Alisema tayari wameshaanza kuchunguza madai ya aliyekuwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kwani tayari wapo hata viongozi wakubwa."Siwezi kusema kuwa kulikuwa na ulegevu, na hatua zimechukuliwa nchini imefikisha mhakamani mawaziri ila nchi ipo kwenye ufagio mpya hivyo tumeweka nguvu zaidi na hali zaidi,"alisema. Akizungumzia maofisa takukuru waliofukuzwa kazi a rais baada ya kukiuka maagizo ya rais ya kupata kibali cha kusafiri nje, alisema maofisa hao walikwenda kwenye mkutano wa taaisis za kupambana na rushwa uliofanyika Congo-Kinshasa.

NITAYATUMBUA MAJIPU MADOGOMADOGO KWA WATUMISHI WAZEMBE.

Mzindakaya akizungumza na watumishi wa idara ya uvuvi.

Na Shushu Joel,Busega.
MKUU wa wilaya ya Busega Paul Mzindakaya.amesema kuwa wakati Rais wa Jamhuli wa muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipambana na rushwa kubwa na matumizi mabaya ya madaraka kwavigogo,ofisi yake nayo imeanza kupambana na mambo hayo kwa wafanya kazi wake.
DC Mzindakaya akizungumza na walimu hawako pichani.
Alisema kuwa wakati Rais Magufuli akitumbua majipu makubwa yeye kwa upande wake  atatumbua majipu madogomadogo ili kuweka nidhamu ya kazi kwa wafanyakazi iweze kuwepo na pia hata kuizidi ilie kauli mbiu ya Rais ya hapa kazi tu.

Yunah aliyasema hayo alipokuwa na kikao kazi ambacho pia kiliwashilikisha watendaji wa kata na vijiji,wafanyakazi wa afya,wakuu wa idara,maafisa kilimo kata na wenyeviti wa vijiji kilichofanyika katika kijiji cha Bulima,kata ya Nyashimo wilayani Busega, chini ya mkuu wa wilaya hiyo,Paul Mzindakaya.
Mkuu wa wilaya Paul Mzindakaya akisisitiza jambo kwa watumishi wa afya

MKURUGENZI huyo aliongeza kuwa mtumishi yeyote Yule wa serikali katika halmashaul hiyo ambaye hatoweza kwendana na kasi anayoinyesha Rais Magufuli hatutomvumilia hata kidogo na wala hata kumuonea haya yeyote ile  katika utendaji wa kazi za halmshaul hizo.

Aidha Yunah alisema kuwa hayuko tayari kumfumbia macho mfanyakazi wake ambaye ataonyesha zaili kashindwa kuondena na kasi ya Rais ni bora akajiondoa kabisa mapema katika kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati Hivyo siko tayari kuwajibishwa kwa kuwafumbia macho watumishi au wasaidizi wengine katika halmashaul yangu alisema Yunah.

Aliwata watumishi hao kuwa na nidhamu ya hali ya juu kazini,kuhudumia wananchi vile ipasavyo na kwa muda mwafaka, kuwa waadilifu  ikiwa na na kuheshimu matumizi pia matumizi ya fedha za umma.

Aliongeza kuwa kila mtumishi anatakiwa kuwa tayari na mabadiliko  ambayo tayari yamesha anza kuonekana na pia kuondoa fikra ambazo watakuwa nazo.

N kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo Paul Mzindakaya aliwata watumishi wote ndani ya wilaya yake kuiweza kutambua wajibu wao walionao  katika kutimiza majukunu yao katika kuwatumikia wananchi .

Mzindakaya aliongeza kuwa naye kwa upande wake yuko tayari kutumbua kila aina ya jipu lolote lile liwe gumu au jepesi nah ii ni kutokana na kasi iliyopo sasa katika nchi yetu chini ya Rais Dkt Magufuli, Hivyo amempongeza Dkt Magufuli kwa kasi aliyoionyesha na kumtaka aweze kuongeza nguvu zaidi ili kupambana zaidi na kwa upande wangu nitaanza kwa kutoa mifano kwa yeyote atakayekeuka kasi iliyopo sasa alisema.

KERO SUGU TANESCO ZAFUNGUA KINYWA CHA MAMA HUYU.

Mteja Ambwene Kyoga


Dotto Mwaibale

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) Wilaya ya Charambe Temeke jijini Dar es Salaam limelalamikiwa na mteja wake mmoja kwa kushindwa kumfungia umeme kwa wakati licha ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Mhongo kuagiza wateja wapya kufungiwa umeme katika kipindi kifupi.


Malalamiko hayo yametolewa na mteja wa shirika hilo Ambwene Kyoga ambaye amelipa sh. 320,960 kwa ajili ya kuwekewa umeme na kupatiwa lisiti namba TDB 16841 kwa ajili ya nyumba yake iliyopo Mbagala Kuu Bucha.


Ambwene alisema sasa anaingia mwaka wa pili bado haja fungiwa umeme kwani mwaka jana mwanzoni alipeleka maombi yake ofisi za shirika hilo za Kurasini lakini alipofuatilia aliambiwa faili lake limepotea hivyo aende ofisi za Charambe ambapo alilipa fedha hizo Desemba 28 mwaka jana tangu hapo licha ya kupelekewa nyaya amekuwa akizungushwa kwa kuambiwa nguzo inayotakiwa achukulie umeme imeoza ingawa inaendelea kutumika.


"Watu wa dharura wamekwisha toa taarifa kuhusu nguzo hiyo lakini bado haijabadilishwa jambo linaloweza kuleta maafa iwapo ikianguka na kibaya zaidi wamekuwa na maneno mengi badala ya kazi sijui wanataka kujenga mazingira ya rushwa" alilalamika Kyoga.


Kyoga alisema waziri wao Mhongo anafanya kazi kwa kujituma na alimsikia katika vyombo vya habari akiagiza kuwa ndani ya wiki moja mwombaji wa umeme awe amefungiwa lakini anashangaa Tanesco Charambe jinsi wanavyofanya kazi kwa kusuasua.


Msemaji wa Tanesco ofisi za  Charambe ambaye alifahamika kwa jina moja la Mugaya alipopigiwa simu jana ili kuzungumzia suala hilo simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila ya kupokewa hata hivyo gazeti ili linaendelea kumtafuta.

AIRTEL FURSA IMETUMIA Shs. MILIONI 7 KUBADILI MAISHA YA MPISHI WA KEKI JIJINI DAR.

Meneja wa Huduma kwa Jamii wa Airtel, Hawa Bayumi (wanne kutoka kushoto), akimkabidhi kijana Diana Mosha, msaada wa vifaa mbali mbali vya kutengenezea keki kupitia mpango wa Airtel ‘FURSA Tunakuwezesha’, katika hafla fupi iliyofanyika nyumbani kwao Ilala jijini Dar Es Salaam jana. Wanaoshuhudia ni wafanyakazi wa Airtel waliohudhuria hafla hiyo.
Meneja wa Huduma kwa Jamii wa Airtel, Hawa Bayumi (pili kushoto), akimkabidhi kijana Diana Mosha, msaada wa vifaa mbali mbali vya kutengenezea keki kupitia mpango wa Airtel ‘FURSA Tunakuwezesha’, katika hafla fupi iliyofanyika nyumbani kwao Ilala jijini Dar Es Salaam jana. Wanaoshuhudia ni (kulia) ni Meneja mauzo wa Airtel Dar Es Salaam ,James Moillo na wafanyakazi wengine wa Airtel.
Kijana Diana Mosha (kushoto), akifafanua jambo baada ya kukabidhiwa msaada wa vifaa mbali mbali vya kutengenezea keki kupitia mpango wa Airtel ‘FURSA Tunakuwezesha’, kwa meneja masoko kanda ya Dar Es Salaam James Moillo (pili kushoto) katika hafla fupi iliyofanyika nyumbani kwao Ilala, Dar Es Salaam jana. Wanaoshuhudia ni meneja masoko wa Airtel kanda ya Mbagala, Saleh Safi akifuatiwa na   meneja wa huduma kwa Jamii wa Airtel, Hawa Bayumi.

Airtel FURSA Imetumia Shs. Milioni 7 kubadilisha maisha ya Mpishi wa Keki jijini Dar.
Dar es Salaam, Jumatano, Januari 27, 2016, kufuatia uzinduzi wa hivi karibuni wa Airtel FURSA msimu wa mbili, Airtel inaendelea kugusa maisha ya vijana nchini Tanzania na kuwawezesha kufikia matarajio yao ya ujasiriamali. Leo Airtel FURSA imemfikia kijana  Diana Moshi, mwenye umri wa miaka 22 anayejihusisha na upikaji wa keki jijini Dar Es Salaam. 

Diana amepokea  ruzuku katika mfumo wa vifaa vya kufanyia kazi vikiwemo trei za keki, mashine za kuchanganyia unga wa keki, mashine za kupambia keki, jokofu na jiko la gesi .Mbali na vifaa hivyo Diana atapokea mafunzo maalum ya ujasiriamali na ushauri wa biashara ya keki kutoka kwa mtaalam maalum na maarufu wa biashara ya keki hapa jijini.

Kutoka alipoanzia akiwa na mtaji mdogo sana wa kuanzia biashara, Diana aliendelea kuwa makini na kutilia mkazo wa ndoto yake. Pamoja na ukosefu wa vifaa Diana hakukata tamaa bali alijifunza kupitia kwa jirani na kukodisha vifaa vya kufanyia kazi kutoka kwa wafanyabiashara wengine. 

Akiwa na furaha kubwa alisema; "Niliona Airtel FURSA kama fursa ambayo inaweza kusaidia kupunguza mapambano na kuongeza matumaini yainua biashara yangu, ninashukuru kwamba leo Airtel FURSA  imenifikia na kuweza kubadilisha maisha yangu. Nimeanza nikiwa na mtaji mdogo sana lakini leo Airtel imenidhihirishia kwamba kufanya kazi kwa bidii na uvumilivu inaweza kutimiza ndoto yako ".

Diana aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa vile yeye sasa anauwezo kwa kuwa na zana madhubuti za kuzalisha zaidi. "Ninaamini katika kipindi cha muda mfupi nitaweza kuzalisha zaidi na kuajiri wengine ili kusaidia biashara yangu. Mimi ni shuhuda wa kweli kabisa  wa walengwa wa Airtel FURSA walioomba na kupata msaada . Ninaahadi kusaidia jamii yangu inayonizunguka kwa sababu ninaelewa fika ni jinsi gani vijana wenzangu wanavyopata tabu huko mtaani na sitaacha kuendelea kuwahamasisha. "

Akikabidhi vifaa hivyo meneja wa huduma kwa jamii wa Airtel Bi Hawa
Bayumi alimpongeza Diana kwa kufwata ndoto zake na kuhimiza vijana wengine kuiga mfano wa Diana. 

Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano  Bi Bayumi alisema "Diana ametutia nguvu na kuweza kushiriki sehemu ya safari ya ndoto zake kwani ameanza akiwa hana kitu , si kwa mtaji tu lakini hata uzoefu wa kufanya biashara hii. Lakini leo hii ameweza kuuza keki kupitia mitandao na kujipatia hela. Tunaamini vifaa tunavyompatia Diana leo vitabadilisha maisha yake na kuinua biashara yake na kuongeza wateja wengi zaidi.

Tunawahimiza vijana wengi hapa nchini kuchangamkia Airtel FURSA si tu inayotolewa kwa vitendea kazi bali na elimu ya biashara ambayo imekuwa ikitolewa nchi nzima hapa Tanzania,  pia kwa kupata maelekezo ya biashara kupitia mitandao yetu ya kijamii inayosadia kuelekeza  vijana jinsi ya kukuza biashara zao, kujenga fursa kwa ajili ya wengine na kuwa na huduma na jami zao zinazowazunguka.

Airtel, kwa mara nyingine tena katika mpango wake wa Airtel FURSA umeahidi kuendelea  kugusa maisha ya wa Tanzania kwa kuwawezesha vijana kupitia Airtel FURSA. Hadi sasa Airtel imeweza kufikia vijana  zaidi ya 2,500  nchini Tanzania na na imeahidi kufikia vijana zaidi ya 1500 katika kipindi cha miezi sita ijayo.
MWISHO.

WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI MKOANI KIBAHA WAPO HATARINI KUPOTEZA MAISHA KUTOKANA NA MIUNDOMBINU KUWA MIBOVU.

NA VICTOR MASANGU, PWANI

SHULE ya msingi ya mkoani iliyopo Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo uhaba wa madawati, madarasa  pamoja na miundombinu ya madarasa kuwa mibovu na vyoo kuwa na nyufa hali ambayo inatishia usalama wa maisha yao kutokana na mazingira wanayosemea ni   hatarishi na  sio rafika kwao.  

 Hali hiyo imebainika baada ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikio kufanya ziara ya kushitukiza katika shule  hiyo na kuweza kujionea ubovu  wa majengo hayo  wanayoyatumia katika shule hiyo kuwa ni chakavu kutokana na kutofanyiwa ukarabati kwa kipindi kirefu.

Mkuu wa shule hiyo Pregua  Mseja amekiri kuwepo kwa hali hiyo ambapo alisema   kwamba licha ya  shule hiyo kukabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombini lakini bado inakabiliwa na uhaba wa madawati pamoja na nyumba sita vya madarasa vina vuja maji kutokana na mapaa yake kutoboka hivyo wanafunzi wananyeshewa  na mvua.

“Kwa sasa Mkuu wa Mkoa shule hii ina changamoto nyingi sana kwani licha ya ubovy wa majengo pamoja na vyoo bado mambo ya msingi yanahitajika kwa shule hii ili wanafunzi waweze kujisomea katika mazingira mazuri kwa mfano sasa kuna madasara sita ambayo yanavuja kweli wanafunzi wananyeshewa na mvua,” alisema Mseja.

Akizungumzia kuhusiana na fedha ambazo tayari wameshakwisha zipokea katika shule hiyo kutoka serikalini kwa ajili ya uendeshaji wa elimu bure alisema  kwamba  wameshapokea kiasi cha shilingi laki 437 ambazo zitatumika katika mahitaji mbali mbali ikiwemo suala la utawala michezo pamoja na mahitaji mengine ya msingi.

 Baada ya Mkuu wa Mkoa kumaliza kufanya ukaguzi katika maejengo ya utawala, madarasa ya wanafunzi pamoja na kutembelea vyoo vinavyotumiwa na wanafunzi hao alitoa agizo kwa halmashauri ya mji wa Kibaha kuhakikisha wanatafuta fedha haraka  iwezekanavyo kwa ajili ya kukarabati miundombinu hiyo ili kuwatendea haki ya msingi watoto hao.

Ndikiro alisema kuwa majengo hayo yanatakiwa kufanyiwa ukarabati wa haraka na kwamba halmashauri ya mji wa Kibaha ihakikishe inatafuta fedha ambazo zitaweza kusaidia katika kukarabati miundombinu hiyo ya majengo ili watoto waweze kujisomea katika mazingira mazuri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kibaha Mauld Bundala aliunga mkono kauli ya Mkuu wa Mkoa ambapo alisema anaskitishwa sana na kuona wanafunzi wnasoma katika majengo amabyo yana nyufa kwani kunaweza kupelekea watoto hao kuangukiwa na majengo.

Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Kibaha Grory Diamunye ambao nao walikuwepo katika ziara hiyo alisema atalivalia njuga suala hilo na kuahidi kulishughulikia haraka sana ili wanafunzi hao waweze kusoma katika mazingira ambayo ni rafiki kwao kwani kufanya hivyo kutaweza kuwafanya waongeze hata kiwango cha ufaulu.

Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 764 kwa sasa bado inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madawati, madarasa, matundu ya vyoo, uchakavu wa miundombinu ya majengo ahali mbayo inwapa wakati mgumu wanafunzi hao kusoma katika mazingira ambayo ni hatari kwa masiha yao.

MABONDIA KUTWANGANA DAR LIVE MARCH 12


Bondia Iddi Mnyeke kushoto akitunishiana misuli na Mohamed kashinde wakati wa utambulisho wa mpambano wao jana katika GYM Uhuru viwanja vya basket mpambano utakaofanyika march 12 katika ukumbi wa Dar live mbagala Picha na SUPER D BOXING NEWS

Na Mwandishi Wetu

MABONDIA mbalimbali watazitwanga march 12 katika ukumbi wa Dar live mbagala akizungumza mbele ya waandishi wa habari mratibu wa mpambano uho

Rajabu Mhamila 'Super D' amewasainisha mabondia mbalimbali kuzipiga siku hiyo ambapo bondia Ibrahimu Maokola 'Simba wa Mbagala' atazipiga na Joseph Sinkala kutoka Mbeya mpambano wa ubingwa raundi kumi kg 74 utakaosimamiwa na kamisheni ya ngumi za kulipwa 'TPBC'  kinachongozwa na Rais Chaurembo Palasa

aliendelea kwa kusema siku hiyo bondia Iddi Mnyeke kg 61 atamenyana na Mohamed Kashinde wakati Pius Kazaula kutoka Morogoro atakumbana na Karage Suba katika uzito wa kg 66

wakati Shabani Kaoneka atakumbana na Said Seleman mpambano wa raundi sita kg 72 na Ambokile Chusa atavaana na Seleman Galile katika mpambano wa raundi sita kg 74

 pia kutakuwa na mapambano mbalimbali yatakayo sindikiza mpambano uho 

siku hiyo kutakuwa na uzwaji wa DVD za ngumi  mabingwa wa Dunia akiwemo mpya za masumbwi kati ya bondia Amir Khan vs Nichlaus Maidana na Floyd mayweather vs Nichlaus Maidana one and two Manny Paquaio, Floyd Maywether, Roy Jones,Miguel Cotto,Linox Lewis, David Haye,Mohamed Ali

ASKARI AUAWA AKITUHUMIWA KUFANYA UJAMBAZI.

Askari polisi wilayani hapa, Nobart Chacha (25) ameuawa kwa kupigwa risasi akituhumiwa kupora mali za mfanyabiashara wa madini kwa kutumia silaha za jadi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema jana kuwa askari huyo aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani na mgongoni.

Diwani wa Kata ya Machimboni, Raphael Kalinga alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Ibindi kilichopo Kata ya Machimboni wilayani Mlele.

Alisema askari huyo akiwa na wenzake walifika kijijini hapo kwa lengo la kumpora mfanyabiashara huyo wa madini ambaye pia anamiliki mashine za kusaga nafaka.

Kalinga alisema askari huyo na watuhumiwa wengine walivunja mlango wa mbele wa nyumba ya mfanyabiashara huyo wakati amelala chumbani.

“Baadaye waliingia ndani walimwamuru mfanyabiashara huyo kukaa kimya, lakini hakutii agizo na badala yake alichukua bunduki yake aina ya Shortgun na kumpiga askari huyo kifuani na mgongoni,” alisema.

Alisema baada ya kuona askari huyo amepigwa risasi, watuhumiwa wenzake walimchukua na kwenda kumtupa kwenye kichaka kilicho umbali wa mita 200 kutoka kwenye eneo la tukio na kisha kutoweka.

Alisema wakazi wa kijiji hicho ndiyo waliomtambua askari huyo baada ya kufuatilia michirizi ya damu na kuukuta mwili wake wake ukiwa kichakani na kutoa taarifa polisi. Alisema polisi walifika kwenye eneo hilo baada ya muda mfupi na kumtambua askari huyo.

Thursday, January 28, 2016

BUNGE LA LEO MBOWE JICHO KWA JICHO NA WAZIRI MKUU.

Mhe. Mbowe ahoji juu ya suala la la jeshi la polisi kuweka makatazo kwa baadhi ya vyama vya kisiasa kutokufanya kazi za kisiasa.

Waziri mkuu Mhe. Kassim Majaliwa atoa ufafanuzi juu ya namna ya kuboresha ukusanyaji wa mapato mbalimbali.

ATHARI ZA MVUA JIJINI DAR ES SALAAM LEO

 Vijana wakiwa wamekaa nje baada ya nyumba wanazoishi kujaa maji maeneo ya Jangwani jijini Dar es Salaam kufuatia mvua zilizonyesha leo.
 Kituo cha daladala za kwenda Gongolamboto cha Suwata Kariakoo kikiwa kimejaa maji hivyo  kuleta adha kwa watumiaji kufuatia mvuo hizo.
 Dimbwi la maji likiwa mbele ya jengo la Yanga.
 Daraja la Jangwani na Kituo cha mabasi ya mwendokasi kikiwa kizingirwa na maji.
 Magari yakipita kwenye dimbwi la maji barabara ya mtaa wa Lindi Ilala.
 Moja ya vibanda wanavyoishi wananchi waliobomolewa eneo la Kinondoni Mkwajuni maji yakipita katikati yake jambo ambalo ni hatari kwa watu wanaoishi ndani humo.
 Nyumba ikiwa imezingirwa na maji eneo la Mchikichini Ilala kufuatia mvua hiyo iliyonyesha leo
Vijana wakiuangalia Uwanja wa Klabu ya Yanga ulivyojaa maji.


SERIKALI ITATUWE NA HILI LA UPUNGUFU WA VYUMBA VYA MADARASA NA MADAWATI.

Lupemba shule ya msingi iliyoko wilayani Magu mkoani Mwanza, wakipata masomo.

SHULE YA MSINGI LUPEMBA ILIYOKO MAGU YAKABILIWA NA UHABA WA MAJENGO NA MADAWATI.
NA Shushu Joel,Magu
TUMEZOEA kusikia shule zilizoko vijijini ndani ndani ndizo zinakabiliwa na tatizo la madawati na majengo,lakini kumbe hata zile za karibu na mijini bado ni shida kwani shule ya msingi Lupemba iliyoko wilayani magu mkoani mwanza inakabiliwa na matatizo hayo

Shule hiyo iliyoko karibu kabisha na ofisi za mji mdogo wa halmashauri ya magu,inapungukiwa madawati zaidi ya 400 na majengo ya madarasa yasiyopungua 5, licha ya kuwa karibu na ofisi hizo, lakini cha kushangaza zaidi hakuna kiongozi wa aina yeyote ile ambaye amefikilia chochote kile juu ya kutatua tatizo hilo linalowakabili wanafunzi hao wanaosomea kwenye mahema na matofali.

Shule hii ya Lupemba ilifunguliwa rasmi miaka michache tu iliyopita,pamoja na upungufu wa madawati na majengo bado pia inakumbwa na tatizo la upungufu wa walimu kwani waliopo ni walimu 8 tu wanawake ni 5 na 3 ni wanaume huku shule ikiwa na jumla ya wanafunzi 620.

Hayo ni baadhi tu ya matatizo yanayoikabili shule hiyo ya msingi Lupemba ambayo idadi kubwa ya wanafunzi wanaishia kukaa chini na kusomea kwenye mahema na huku wakiendelea na shughuli zao zingine za darasani kama ilivyozoeleka kwa wanafunzi wetu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Daniel Matemi anathibitisha uwepo wa tatizo hilo katika shule yake na kusema kuwa suala hili hata yeye amelikuta katika shule hiyo ingawa amekwisha lifikisha katika sehemu husika ila mpaka sasa bado hakuna lolote lililofanyika.

“Tumewabana sana wazazi wa wanafunzi wetu katika michango mbalimbali japo tuweze kuinusuru shule hii lakini suala hili linakuwa ngumu kwa upande wa wazazi hao nah ii ni kutokana na siasa chafu zilizopo katika kijiji hiki na hili ni kutofautiana kwa vyama kati ya mwenyekiti wa shule na mwenyekiti wa kijiji ndio changamoto kubwa inayochangia kuwaumiza wanafunzi hao.

Mkuu huyo aliongeza kuwa kilichobaki kwa sasa ni kuwaomba wafadhili walio na moyo ili wajitokeze kuweza kuifadhili shule hii na kuweza kuinusuru katika janga hili kwani kipindi hiki cha mvua sijui itakuwaje kwa wale wa darasa la 5,6 na 3 ambao wanasomea kwenye mahema,kwa kusema ukweli watoto hawa wanapata taabu sana.

Shule ya msingi lupemba wilayani Magu inasikitisha.
“Ndugu mwandishi kama unavyojua sisi wenyewe hatuna cha kuwasaidia,kama unavyofahamu kuwa mwanafunzi anayekaa chini unamkosesha mambo mengi sana” alisema mkuu huyo wa shule.

Kwa ujumla hali hii inawafanya wanafunzi hao kupunguza uwezo wao wa kufanya vizuri darasani.

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi wilaya ya magu Yesse Kanyuma alipohojiwa juu ya shule hiyo alisema kuwa yeye si msemaje juu ya hilo na wala ajui lolote kuhusu shule hiyo ya lupemba.

N kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Ntinika  Paul alipopigiwa simu yake ili kuthibitisha kwa habari ya shule hii simu yake iliiita bila kupokelewa.