ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, January 29, 2022

MASHABIKI WA YANGA WAITEKA MWANZA KWA BURUDANI V MBAO FC

 LEO Januari 29 Yanga itakuwa kwenye kazi ya kusaka ushindi mbele ya Mbao FC ambayo nayo pia inaska ushindi kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya 32 bora, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Hiki hapa kikosi cha Yanga kinachotarajiwa kuanza mchezo unatarajiwa kuchezwa saa 10:00 jioni:- Mshery Aboutwalib Paul Godfrey Yassin Bakari Mwamnyeto Dickson Job Zawad Mauya Sure Boy Jesus Moloko Ambundo Farid Mussa Fiston Mayele Akiba Johora Bryason Bacca Balama Ngushi Ushindi Nkane Kaseke

Friday, January 28, 2022

TFRA YAWASHAURI WAKULIMA KUNUNUA MBOLEA KWA PAMOJA

SHEHENA: Shehena ya mbolea ikiwa katika moja ya maghala yaliyopo mkoani Mbeya tayari kwa matumizi wakati wa msimu wa kilimo.

Mkaguzi wa mbolea Allan Mariki, akikagua ubora wa mbolea katika moja ya ghala la kuhifadhia mbolea ili kuhakikisha kuwa  mbolea inayowafikia wakulima imekidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kupitia vyama vya ushirika inawahamasisha wakulima nchini kununua mbolea kwa pamoja kutoka kwa wazalishaji/makampuni yanayoingiza mbolea moja kwa moja badala ya mkulima mmoja mmoja kununua kutoka kwa wafanyabiashara wa kati ili kununua mbolea hiyo kwa bei ya jumla  na hivyo kuipata kwa bei ya chini tofauti na kila mkulima akinunua kiasi kidogo cha mbolea.

 

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na ununuzi wa Mbolea wa Pamoja, Joseph Charos alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo mwishoni mwa wiki.

 

Charos alieleza kuwa, Kutokana na bei za mbolea katika soko la dunia kuendelea kuwa juu, bei za soko la ndani pia zimeendelea kupanda. Alisema, kwa mfano, wastani wa bei ya mkulima (Retail price) kwa mbolea ya Urea umepanda kutoka Sh. 53,318 mwezi Desemba, 2020 na kufikia Sh. 104,069 mwezi Desemba, 2021 kwa mfuko wa kilo 50, wakati wastani wa bei ya mbolea ya DAP umepanda kutoka Sh. 66,995 mwezi Desemba, 2020 hadi Sh.  109,179 mwezi Desemba, 2021 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na ongezeko la 95% na 63% mtawalia.

 

Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa bei za mbolea zilizokuwa zikitangazwa na soko la dunia katika kipindi cha Julai - Desemba 2021, kwa wastani bei za mbolea zilizoingia nchini zilikuwa nafuu ambapo kwa mbolea ya UREA, bei ya chanzo (FOB) katika soko la dunia kwa mwezi Julai hadi Desemba ilikuwa kati ya dola za marekani 420 hadi 1,000 kwa tani wakati wastani wa bei hadi hapa nchini (CIF Value) kwa mbolea iliyoingia katika kipindi hicho ni kati ya dola za marekani 570 hadi 1,398 kwa tani.

Akielezea kwa upande wa DAP, Charos alisema bei ya chanzo (FOB) katika soko la dunia kwa mwezi Julai hadi Desemba ilikuwa kati ya dola za marekani 550 hadi 912 kwa tani wakati wastani wa bei hadi hapa nchini (CIF Value) kwa mbolea iliyoingia nchini katika kipindi hicho ni kati ya dola za marekani 659 hadi 810 kwa tani.

Kufuatia bei za mbolea kuwa juu kwenye soko la dunia, soko la ushindani nchini limesababisha wafanyabiashara wafanye jitihada za kutafuta mbolea kutoka kwenye vyanzo vyenye bei nafuu ili kupunguza bei ya mbolea kwa wateja wao. 

Akihitimisha taarifa yake Charos alisema, Kwa ujumla, bei za mbolea zilizoingia nchini katika kipindi cha Julai - Desemba 2021 zimepanda kwa mbolea zote zikilinganishwa na bei za kipindi kama hiki mwaka 2020/2021.

Aliongeza kuwa, wastani wa bei ya kufikishia mbolea ya DAP hapa nchini (CIF) kwa mwezi Desemba, 2020 ilikuwa dola za kimarekani 362 ikilinganishwa na wastani wa dola za kimarekani 810 kwa mbolea iliyoingia mwezi Desemba, 2021 sawa na ongezeko la 123%, ambapo kwa mbolea ya Urea, bei ya kuifikisha hapa nchini (CIF) kwa mwezi Desemba, 2020 ilikuwa dola za marekani 310 wakati bei ya mbolea iliyoingia chini mwezi Desemba, 2021 ni dola za marekani 1,398 sawa na ongezeko la 350%.

Hata hivyo, mamlaka inaendelea na juhudi za kuwahamasisha wakulima kupitia vyama vya ushirika na wataalam wa kilimo, kutumia mbolea mbadala katika shughuli za kilimo zinazopatikana kwa gharama nafuu na kuwataka kuzingatia ushauri wa wataalam.

SERIKALI YAUHAKIKISHIA MGODI WA NYANZAGA MAZINGIRA RAFIKI YA UWEKEZAJI.

 

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amefanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi kutoka mgodi wa Nyanzaga (Nyanzaga Mining Company Limited) uliopo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza lengo ikiwa ni kupata mrejesho wa maandalizi ya awali kabla ya mgodi huo kuanza uzalishaji.

Dkt. Biteko amefanya mazungumzo hayo akiwa ziarani Kahama mkoani Shinyanga na kutumia fursa hiyo kueleza utayari wa Serikali kuweka mazingira rafiki kwa mgodi huo ikiwemo kufikisha huduma muhimu kama nishati ya umeme, maji na barabara ili kurahisisha shughuli kuanza.

Ujumbe huo kutoka mgodi wa Nyanzaga ukiongozwa na Meneja Mkuu, Damien Valent umemhakikishia Waziri Biteko kuwa maandalizi ya ufunguzi wa mgodi huo yanaendelea vyema ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya ardhi ili kuwalipa fidia wananchi watakaopisha shughuli za mgodi.

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Afisa Madini Mkazi Mkoa wa kimadini Kahama Mhandisi Jeremiah Hango, Kamishna Msaidizi Wizara ya Madini Maruvuko Msechu, Kamishna Tume ya Madini Janeth Lekashingo, Afisa Mahusiano mgodi wa Nyanzaga Paul Gongo na Katibu wa mgodi huo Chelestino Malile.

Mgodi wa Nyanzaga ni miongoni mwa migodi minne iliyokabidhiwa leseni za uchimbaji madini mwezi Disemba mwaka jana katika hafla iliyoshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo unatarajiwa kuendeshwa kwa ubia kupitia kampuni ya pamoja baina ya Serikali na mwekezaji iitwayo Sotta Mining Corporation Limited ambapo Serikali ina hisa za asilimia 16 na mwekezaji asilimia 84.
Na Mathias Canal na George Binagi, Kahama- Shinyanga
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko (kushoto) akizungumza na ujumbe kutoka mgodi wa Nyazanga ukiongozwa na Meneja Mkuu wa mgodi huo, Damien Valent (wa tatu kulia).
Viongozi kutoka mgodi wa Nyanzaga wakiongozwa na Meneja Mkuu wa mgodi huo, Damien Valent (kushoto), Afisa Mahusiano baina ya mgodi na Serikali Paul Gongo (katikati) na Katibu wa mgodi Chelestino Malile (kulia).
Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Madini wakifuatilia kikao hicho. Kutoka kushoto ni Katibu wa Waziri wa Madini Mhandisi Kungulu Kasongi, Afisa Madini Mkazi Kahama Mhandisi Jeremia Hango, Kaimu Kamishna Wizara ya Madini Maruvuko Msechu na Kamishna Tume ya Madini Janeth Lekashingo.

Thursday, January 27, 2022

DKT. GWAJIMA KUANZISHA MADAWATI YA KIJINSIA VYUO VIKUU

Na WMJJWM-DSM

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Dkt.Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali imejipanga kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia zinazowakabili Baadhi ya Wanafunzi waliopo Vyuo Vikuu hapa nchini ili kunusuru kushuka kwa ufanisi wa masomo.


Amebainisha hayo jijini Dar es salaam katika Uzinduzi wa Dawati la Jinsia kufuatia utekelezaji wa mradi wa kutetea haki za Jinsia wa unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO ). 


Dkt. Gwajima  amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayo ongozwa na Mhe.Rais  Samia Suluhu Hassan imejipanga kupambana na Ukatili wa Kijinsia.


"Kuna matukio mengi ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii ikiwemo Vyuoni na shuleni hivyo kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kuanzisha Madawati ya Jinsia yanayofanya kazi kwa  mfumo wa kupima ufanisi wake ili isije ikawa tumefungua kwa mazoea yakakosa tija" amesema. Dkt. Gwajima.

Aidha Dkt Gwajima amesema, Serikali imetekeleza mambo mengi katika kupambana na ukatili wa kijinsia mathalani kukuza uelewa wa wananchi kutoa taarifa za matukio, Madawati ya Jinsia 420 yameundwa kwenye Vituo vya Polisi na 153 kwenye Jeshi la Magereza, Kamati 18,186 za Ulinzi wa Wanawake na Watoto zimeanzishwa nchini, Vituo vya huduma kwa wahanga vimeanzishwa kwenye hospitali 14, Sheria ya msaada kwa wahanga na 1 ya mwaka 2017 imetungwa na mambo mengine mengi.


Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.Omari Kipanga, amesema kuwa mradi wa ‘03plus’ utanufaisha Vyuo Vikuu vya Dar Es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Serikali ya awamu ya sita imejipanga kikamilifu kuondoa changamoto ya ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwakilishi wa UNESCO nchini Tirso Santos amesema kwamba lengo la kuleta mradi huo ni kutaka kuona wanafunzi wa kike waliopo vyuo vikuu wanasoma kwa kujiamini


MWANZA KAA TAYARI NA 'PRE VALENTINE DAY PART'

 


Event : PRE VALENTINE DAY PART


LOCATION : CLUB ELEVATE 


AFRICAN PRINTEMPS CULTURAL TRAVEL LIMITED, Will reward the best appearance  couple to visit Serengeti national Park 2days one night.


All couple are welcomed. 


@apc_travels 

@clubelevate_tz 


#AchaTutrend 

#Worldwide 🌍

RAIS SAMIA AWATAJA WANAOMTULIZA UBONGO WAKE.

 

🖐🏾Heri ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
#ShikaNeno
#TendaNeno
#Kaziiendelee
#HappyBirthday Mhe. @samia_suluhu_hassan
.
.
.
#JEMBE™

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata keki kama ishara ya kusherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa leo tarehe 27 Januari, 2022 Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa wajukuu zake ndiyo tiba yake kuu pale kichwa chake kinapokuwa kimejaa kwa mambo mengi hasa akiwa Dar es Salaam.


Hayo ameyabainisha hii leo Januari 27, 2022, wakati akisherehekea siku yake ya kuzaliwa jijini Dodoma, ambapo ametimiza umri wa miaka 62.


"Ukiona kichwa kimejaa zaidi tiba yangu ni wajukuu, napiga tu simu nileteeni hao kwahiyo wanakuja kwa masaa kadhaa hasa nikiwa Dar es Salaam, piga kelele panda shuka, pigishwa mbio kwenye ngazi wakirudi wanakokaa basi ubongo umepumzika," amesema Rais Samia

Monday, January 24, 2022

MKE, MUME WASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI MWANZA.


Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watano wakiwemo mke na mume kwa tuhuma za kuhusika kwenye mauaji ya watu watatu wa familia moja katika mtaa wa Mecco mkoani Mwanza.


Kwenye tukio hilo lililotokea Jumanne Januari 18, 2022 mfanyabiashara, Mary Charles (42), mtoto wake, Jenifa Fredy (22) na msaidizi wa kazi za ndani, Monica Jonas walipoteza maisha baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na shingoni.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anzi amesema watuhumiwa wanadaiwa kutekeleza mauaji hayo Jumanne Januari 18 mwaka huu huku chanzo kikitajwa kuwa ni mgogoro wa kibiashara kati ya watu hao.


“Marehehemu (Mary Charles) alikuwa akiwatumia watuhumiwa fedha kwa ajili ya kwenda kumnunulia mazao mkoani Kigoma lakini mara ya mwisho baada ya kutumiwa fedha watuhumiwa hawakufanya hivyo, alipoanza kuwadai walishindwa kumlipa fedha hiyo wakaamua kumfanyia kitendo hicho,” amesema Ng’anzi.


Ng’anzi amewataja watuhumiwa hao kuwa ni mkazi wa Utemini kata ya Buhongwa jijini humo, Thomas Songay (26), mke wake, Hajir Thomas (23), Deoglas Malengwa (31), Emmanuel Lugaila (36) na Emmanuel Mathew, 19.


“Katika mahojiano yaliyofanywa watuhumiwa wamekiri kutenda tukio hilo. Aidha silaha aina ya panga lililotumika kutekeleza tukio hilo limepatikana na tumelipeleka kwenye ofisi ya mkemia mkuu kwa ajili ya kuoanisha vinasaba vya marehemu,” amesema Ng’anzi


Amesema watuhumiwa hao walikutwa na baadhi ya vielelezo vilivyotambuliwa na ndugu wa marehemu kuwa ni Jokofu moja aina ya Kyoto, Godoro, TV mbili aina ya Singsung nchi 18, Radio mbili na Jiko la kupikia vinavyodaiwa kuporwa na watuhumiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo.


Pia amesema baada ya uchunguzi kufanyika, maofisa wa jeshi hilo walipata simu simu tatu za marehemu zikiwa zimefukiwa katika nyumba ya mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo.


“Watuhumiwa hawa watafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilisha upelelezi wa tukio hili kwa hatua zaidi za kisheria,” amesema Nganzi

MBUNGE NEEMA LUGANGIRA AWASILISHA MAPENDEKEZO YA KUFANYIWA KAZI ILI KUIMARISHA USTAWI WA NGOs KWA KATIBU MKUU DKT ZAINABU CHAULA

MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Kundi la Asasi za Kiraia NGOs Tanzania Bara, Mhe Neema Lugangira kulia akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainabu Chaula leo Jumatatu 24 Januari 2022, katika Ofisi za Wizara iliyopo Mji wa Magufuli, Mtumba, Dodoma.


MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Kundi la Asasi za Kiraia NGOs Tanzania Bara, Mhe Neema Lugangira kulia akiwa kwenye picha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainabu Chaula leo Jumatatu 24 Januari 2022, katika Ofisi za Wizara iliyopo Mji wa Magufuli, Mtumba, Dodoma mara baada ya kumaliza mazungumzo yao
MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Kundi la Asasi za Kiraia NGOs Tanzania Bara, Mhe Neema Lugangira kulia akiagana na  Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainabu Chaula leo Jumatatu 24 Januari 2022, katika Ofisi za Wizara iliyopo Mji wa Magufuli, Mtumba, Dodoma mara baada ya kufanya mazungumzo naye

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Kundi la Asasi za Kiraia NGOs Tanzania Bara, Mhe Neema Lugangira amewasilisha mapendekezo ya maeneo ambayo yanayohitaji kufanyiwa Maboresho ili kuimarisha Ustawi wa NGOs hapa Nchini.

Mbunge Neema aliwasilisha mapendekezo hayo  alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainabu Chaula leo Jumatatu 24 Januari 2022, katika Ofisi za Wizara iliyopo Mji wa Magufuli, Mtumba, Dodoma.

Alisema mambo hayo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa  mwaka huu 2022 ambayo ni pamoja na kuandaa Mpango wa Kuwajengea Uwezo NGOs za Mikoani ili waweze kujiendesha kwa Mujibu wa Sheria. 

Mbunge huyo alisema suala lingine ambalo walilizungumza ni kuandaa Mikutano ya Kimkakati na Wadau wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika maeneo mahsusi ikiwemo Maboresho ya Kanuni za Usimamizi wa Fedha za NGOs

Alisema Maboresho mengine aliyowasilisha ni katika Kodi kwa Wafanyakazi Wanaojitolea
(Volunteers) na Maboresho ya Kodi ya Mapato (Income Tax) kwa Kundi hili la NGOs.

Hata hivyo Mbunge Neema Lugangira aliwasilisha shukrani kutoka Sekta ya Azaki (NGOs) kwenda kwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujibu kilio cha muda mrefu na kuunda Wizara Mpya inayosimamia Masuala ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Sekta ipo tayari kushirikiana kwa karibu na Wizara hii muhimu.

Katika hatua nyengine Mbunge Neema Lugangira alimpongeza sana Dkt. Zainab Chaula kwa Kuteuliwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kuwaKatibu Mkuu wa Wizara hii mpya na muhimu sana.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii Dkt. Zainab Chaula amuhakikishia Mbunge huyo kuwa Ofisi yake ipo wazi kwa ajili ya majadiliano na kubadilishana mawazo hivyo anawakaribisha sana Wadau wa Sekta ya NGOs ili kwa pamoja walete mageuzi ya kimaendeleo katika Masuala yote ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. 

Dkt Chaula amewahikikisha Sekta ya NGOs atashirikiana nao kwa karibu ili kwa pamoja waweze Kuimarisha Mazingira Wezeshi kwa Ustawi wa NGOs ambao ni Wadau muhimu katika Utekelezaji wa Mipango ya Wizara yake.

Kwa kuhitimisha, Dkt. Zainab Chaula, Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii  Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumy amesisitiza kuwa Ofisi yake ipo wazi kwa ajili ya majadiliano na kubadilishana mawazo hivyo anawakaribisha sana Wadau wa Sekta ya NGOs.