ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, September 12, 2025

SERIKALI YAIPONGEZA BENKI YA CRDB KUFUNGUA OFISI DUBAI

 


Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ally Ussi (wa tatu kushoto) akizindua tawi la Nyakatuntu wilayani Kyerwa. Pamoja naye ni Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mheshimiwa Zaitun Abdalla Msofe (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Wateja wa Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul (wa nne) pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ally Ussi (wa pili kushoto) akifungua pazia kuzindua tawi la Benki ya CRDB Nyakatuntu akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Wateja wa Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul (wa pili kulia), Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mheshimiwa Zaitun Abdalla Msofe (wa kwanza kulia), na Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta (wa kwanza kushoto).

Kyerwa. Tarehe 11 Septemba 2025: Akizindua tawi la Benki ya CRDB Nyakatuntu wilayani hapa, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ally Ussi, ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kufikisha huduma kwa Watanzania waliopo ndani na nje ya nchi akitolea mfano ofisi yake ya Dubai.

Ussi amesema Tanzania ya sasa imepiga hatua kubwa ya maendeleo hivyo wananchi wake wanahitaji huduma bora za benki ili kufanikisha malengo yao ya kibiashara na uwekezaji, mambo yanayowasaidia kuondokana na umasikini.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu hii ya sita chini ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa kiasi kikubwa. Sasa hivi Watanzania wanafanya biashara kuanzia vijijini mpaka mjini. Na zaidi wapo wanaoenda nje ya nchi hasa China, Uturuki na kwingineko. Nawapongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zenu za kuwafuata wananchi. Sio tawi hili la Nyakatuntu pekee, mpango wenu wa kufungua ofisi Dubai utaitangaza nchi yetu pamoja na kuongeza kujiamini kwa wananchi wetu pindi wanapokuwa nje ya nchi yetu,” amesema Ussi.

Kiongozi huyo amesema ni wakati sasa wa Watanzania kuanza kuzitumia vyema fursa za uwekezaji zilizopo nchini kwa kushirikiana na taasisi imara za fedha hasa Benki ya CRDB yenye uwezo wa kuwahudumia wakiwa ndani ya nchi na nje ya mipaka yetu kwa viwango vilevile.

“Tunazunguka Tanzania nzima, naomba niwaambie ukweli wana Nyakatuntu, kila tulipopita, katika halmashauri zote, tumekuta kuna mawakala na tawi la Benki ya CRDB. Uzuri wa benki hii ni kwamba ina matawi mpaka nje ya nchi. Ukiwa hapa Kyerwa hauna wasiwasi kufanya biashara na mtu aliyepo Burundi kwa sababu Benki ya CRDB ipo kule. Malipo yako utayapata kwa urahisi kabisa. Litumieni tawi hili kuimarisha biashara zenu na kukamilisha mipango mingine ya kiuchumi,” amesisitiza Ussi.

Kabla ya kumkaribisha kiongozi huyo wa mbio za mwenge kitaifa, Mkurugenzi wa Wateja wa Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul amesema tawi la Kyerwa linaifanya Benki ya CRDB kufikisha zaidi ya matawi 260 hivyo kuwa benki yenye mtandao mpana zaidi wa matawi nchini kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania.

“Tawi hili lililozinduliwa leo hapa Nyakatuntu litarahisisha upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi na wakazi wa hapa Nyakatuntu, Wilaya ya Kyerwa, Mkoa mzima wa Kagera na Taifa zima kwa ujumla hata wageni kutoka nje ya mipaka yetu kwani mkoa huu unapokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi. tutaendelea kujenga matawi mapya kila mahali panapostahili ili kuwahudumia wateja wetu kwa haraka,” amesema Bonaventura.

Licha ya matawi, Bonaventura amesema Benki ya CRDB imewekeza kwenye ubunifu unaowapa wateja wake majukwaa tofauti ya huduma unaojumuisha CRDB Wakala zaidi ya 35,000 nchi nzima ambao kwa Mkoa wa Kagera wapo 1,173 wakiwamo 93 wanaotoa huduma katika Wilaya hii ya Kyerwa.

Bonaventura pia alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wana Nyakatuntu kulitembelea tawi hilo kwa ajili ya kupata ushauri wa uwekezaji na fursa nyingine akiwaeleza kuwa sasa hivi Benki ya CRDB inauza hatifungani yake CRDB Al Barakah Sukuk inayofuata misingi ya sharia ingawa inawakaribisha hata wale wasio waumini wa dini ya Kiislamu.

“Mwekezaji wa hatifungani hii atapata faida ya asilimia 12 kwa mwaka. Uwekezaji wake unaweza kufanywa kwa shilingi za Tanzania au dola za Marekani. Kwa shilingi, mtu au taasisi inaweza kuwekeza kuanzia 500,000 na dola ni kuanzia 1,000,” ameeleza Bonaventura.

Mwisho, mkurugenzi amewakaribisha wakazi wa Kyerwa kushiriki semina za ujasiriamali zinazotolewa na CRDB Bank Foundation yakilenga kuwapa wananchi elimu ya fedha, uunganishaji wajasiriamali na masoko mbalimbali na utoaji wa mitaji wezeshi kwa wanawake, vijana na makundi maalumu.

“Tunayafanya haya yote kupitia programu yetu maarufu ya Imbeju ambayo mpaka sasa imshatoa mitaji wezeshi zaidi ya shilingi bilioni 23,” amesema Bonaventura.

Thursday, September 11, 2025

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI AWAFUNDA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA TANGA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

Na Oscar Assenga,TANGA.


IKIWA zimesali siku chache kuingia kwenye uchaguzi Mkuu Octoba 29 Ofisi ya Vyama vya Msajili nchini imekutana naviongozi wa vyama vya siasa mkoani Tanga kwa lengo la kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi kuhakikisha vinafuata sheria na kanuni zilizowekwa.

Elimu hiyo ilifanyika leo kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga ikishirikisha viongozi kutoka wilaya za Tanga,Pangani na Muheza.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Afisa kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Edna Assey alisema wameona ni vema katika kipindi cha uchaguzi kusiwe na makandokando kuwa na ustaarabu kwa maana kufuata sheria,kanuni zilizowekwa kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Alisema waliona ni muhimu kukutana na viongozi wa ngazi za wilaya kutokana na kwamba ndio wanasimamisha wagombea ngazi ya kata na wabunge katika maeneo mbalimbali hivyo wanahaki ya kupatiwa elimu hiyo.

“Katika kutoa elimu hii ni kukumbusha sheria zilizopo katika ofisi ya msajili ,sheria ya vyama vyas siasa sura namba namba 257 sheria ya gharama za uchaguzi sura namba 278 sheria hii ndio ambayo zinaiweka vyama vya siasa katika uchaguzi “Alisema

Aidha alisema katika sheria hizo kuna maeneo au vitendo haviruhusiwi kufanywa wakati wa uchaguzi na ndio ilikuwa agenda kuu ya hayo mafunzo na waliona ni muhimu kuwakumbusha na kuwaelimisha wao kama viongozi wanapokwenda kwenye ngazi za kwa wagombea,mawakala,viongozi na timu za kampeni kuwaelewisha kuna makatazo hayo yamefanyika kwenye sheria .

“Tunawaomba mfanye kampeni za kistaarabu,ofisi ya Msajili inawataka kufanya kazi kama chama ,kama taasisi na elimu hii iwafikie walengwa tunategemea itakuwa hivyo hivyo lakini nawasihi kama kuna malalamiko tuyapeleke kwenye kamati za maadili lakini mambo ya kurusha kwenye mitandao ya kijamii sio nzuri”Alisema

Hata hivyo alisisitiza iwapo wataona kuna eneo ambalo lina changamoto ni vema wawandikie au wapeleke kwa msimamizi wa uchaguzi au kamati ya maadili huku akitoa wito wahakikisha jambo hilo linakuwa na ukweli kwa maana sheria inakataza kutoa taarifa za uongo.

Katika hatua nyengine Ofisa Msajili huyo alisema kwamba vyama vya siasa vimekatazwa kunadi sera zinazopingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar pamoja na Sheria zingine za nchi hasa katika kipindi hiki kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Urais,Wabunge na Madiwani.

Alisema kwamba vyama hicho vimekatazwa kuunda vikundi vya ulinzi na usalama vya aina yoyote au kuwa na taasisi inayolenga kufanya majukumu ya Jeshi la Polisi lakini vikosi vingine vya ulinzi na usalama wa nchi.

Awali akizungumza Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tanga Bahati Kahindi alisema kwamba katika semina hiyo watapitishwa kwenye gharama za uchaguzi na mambo ya maadili na kampeni ambayo ni mambo muhimu kuelekea kwenye uchaguzi huo.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa UDP Mkoa wa Tanga Peter Mhina alishukuru kwa mafunzo hayo huku akishauri ni vyema vyama vya siasa kuwezesha kuanzia Rais, Wabunge na Madiwani ili waweze kufikia maeneo mengi na kuzungumza na wananchi kunadi sera.

“Tunaomba tume ituangalie wao wa vyama vya upinzani kwa sababu wote wapo kwenye sheria ya vyama vya siasa na sio chama tawala pekee maana nchi ni ya vyama vingi”Alisema

Hata hivyo kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Tanga Jamali Kimji alishukuru kwa kupatiwa elimu na ofisi ya msajili ambapo alisema ni elimu nzuri kwa sababu wamezungumza sheria katika tararibu zote za gharama za fedha kwa mgombea.

Alisema pia sheria hiyo katika mikutano na mambo mengine ambayo ni jambo nzuri na kampeni zimeshaanza kwa maana vipi vitu wameviona wengine wanafanya bila kujua kuwape elimu ni jambo nzuri na itasaidia kampeni zao kwenda vizuri.

Mwisho.

Wednesday, September 10, 2025

HUDUMA ZA BENKI YA CRDB SASA VIWANGO VYA KIMATAIFA.

 

 Dar es Salaam. Tarehe 8 Septemba 2025: Baada ya saa 72 za maboresho ya mfumo wa uendeshaji wa benki (Core Banking System), huduma za Benki ya CRDB sasa zimerejea zikiwa bora, zenye kasi kubwa zaidi kukidhi viwango vya kimataifa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema Benki iliweka juhudi kubwa kuhakikisha jambo hili linakmailika kwa wakati ili kurejesha huduma kwa wateja na wadau wake wengine katika majukwaa yote kama ilivyoahidi katika taarifa yake kwa umma iliyoitoa Jumatano tarehe 03 Septemba 2025.

“Benki ya CRDB ni taasisi ya kimataifa tukiwa tunatoa huduma nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku tukikamilisha utaratibu wa kuingia Dubai. Huwezi kutoa huduma katika mataifa haya yote bila kuwa na mfumo imara utakaotunza taarifa za wateja na kufanikisha miamala kwa ufanisi mkubwa. Hii ni moja ya sababu iliyotufanya tuboreshe mfumo wetu mkuu wa uendeshaji. Ninafurahi kuwaeleza kwamba zoezi hili limekamilika kwa ufanisi mkubwa,” amesema Nsekela.

Nsekela amesema kilichokuwa kinafanyika ndani ya saa hizo 72 za kuhama kutoka mfumo wa zamani kwenda huu mpya, ni kuhamisha taarifa za wateja wote waliopo na kuruhusu usajili wa wateja wapya ndani na nje ya Tanzania ambako Benki ya CRDB inahudumia.

Kwa kutambua kwamba Benki ya CRDB inahudumia mamilioni ya wateja ambao walipata taarifa za maboresho haya kwa nyakati tofauti, lakini wote walionesha utulivu na kuiruhusu menejimenti itekeleze maboresho yaliyokusudiwa kwa utulivu mkubwa.

“Kwa ukubwa wa maboresho hayo yaliyohusisha kuhama kutoka kwenye mfumo wa zamani kwenda kwenye mfumo mpya, tulilazimika kusitisha huduma matawini na baadhi ya huduma mbadala (alternative channels) kutopatikana kwa muda. Nawashukuru sana wateja wetu kwa uvumilivu na ushirikiano waliotuonesha katika kipindi hiki na ninawaomba radhi kwa changamoto walizokutana nazo kwa muda ambao baadhi ya huduma zetu hazikupatikana,” amesema Nsekela.


Kutokana na kutoa huduma katika mataifa tofauti ambako kuna utofauti wa sheria, lugha na utamaduni, Nsekela amesema mfumo huu unawaruhusu wateja wa Benki ya CRDB kupata huduma kwa lugha waitakayo na sarafu waipendayo.


“Lugha rasmi kwa Tanzania ni Kiswahili na Kiingereza wakati Burundi wanatumia Kifaransa na Kirundi. Ukienda DRC wao wanazungumza Kifaransa na lugha zao nyingine wakati Dubai kuna Kiarabu na lugha nyingine za kimataifa. Huko kote, mteja atahudumiwa kwa lugha anayoitaka na atafanya miamala yake kwa sarafu aipendayo,” amesisitiza Nsekela.

Ili kuwatoa wasiwasi wateja wake hasa walioona mabadiliko kwenye salio na maeneo mengine ya huduma, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile amesema kulitokana na kuhama kutoka mfumo wa zamani na kuingia katika mfumo mpya ambao una usalama wa hali ya juu, wenye uwezo wa kutoa huduma mpya na bunifu za kidijitali na uliojengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

“Wote walioona tofauti kwenye salio na maeneo mengine, wajue kuwa hali hiyo ilitokana na kuhamisha taarifa kutoka mfumo wa zamani kwenda mfumo mpya. Wateja wetu wafahamu kwamba hatukuwa tunaboresha mfumo bali tulikuwa tunahama kabisa kuruhusu viwango vya mataifa mengine na taasisi za kimataifa tutakazokuwa tunashirikiana nazo,” amesema Mwile.

Nsekela amewashukuru wadau walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha maboresho haya ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanzia hatua za mwanzo hadi sasa.

Maboresho haya yamefanyika ukiwa ni mwendelezo wa mapinduzi yanayofanywa na Benki ya CRDB katika kipindi hiki inaposherehekea miaka 30 tangu kuanzishwa kwake ikishiriki kwa kiasi kikubwa katika kukuza kipato cha mwananchi mmojammoja pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa.

Tuesday, September 9, 2025

TANGAZO - SAMIA KUITIKISA TENA NYAMAGANA

 IJUMAA YA TAREHE 13 SEPTEMBA 2025

MWALIMU:- "NIKIWA RAIS NITAZILINDA JAMII ZINAZOIZUNGUKA HIFADHI"

 


Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kuweka utaratibu maalumu utakaozinufaisha jamii zinazozunguka hifadhi za Taifa endapo atachaguliwa kuunda Serikali Oktoba 29, 2025.


Akizungumza leo Septemba 9, 2025 na wakazi wa Kijiji cha Ikoma, kilichopo mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mwalimu amesema Serikali yake itaondoa mifumo kandamizi inayowanyima wananchi haki ya kunufaika na rasilimali asilia walizopewa na Mwenyezi Mungu.

Mwalimu amesema moja ya mikakati yake ni kuruhusu wananchi wa maeneo hayo kupata kitoweo kama swala kwa njia halali na iliyodhibitiwa, jambo analoliona kama njia ya kupunguza ujangili unaozidi kukithiri.

“Wananchi wakitaka kupata kitoweo wanaishia kupigiwa risasi kwa neema ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amewaruzuku. Hivi niwaulize wale wanaoishi karibu na Ziwa Victoria wanazuiwa kwenda kuvua Sangara na Sato? Yaani wao wakavue Sangara na Sato, ninyi mpigwe risasi?" amesema Mwalimu.

Akiwa anatokea Karatu mkoani Arusha alikofanya mikutano ya kampeni za kuomba kura, Mwalimu amelalamikia mfumo wa sasa, akisema unazidisha chuki kati ya wananchi na mamlaka, badala ya kushirikisha jamii katika kulinda maliasili.

Monday, September 8, 2025

MWENYEKITI CHATANDA AUNGURUMA AZINDUA KWA KISHINDO KAMPENI ZA CCM JIMBO LA MKURANGA

NA VICTOR MASANGU/PWANI Mwenyekiti wa umoja wa wanawake Taifa (UWT) Mary Chatanda amewataka watanzania kushikamana na kutobabaishwa na maneno ya upotoshaji yanayo zungumzwa na baadhi ya watu juu ya mambo mazuri ambayo yametekelezwa na Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan katika nyanja mbali mbali. Chatanda ameyasema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa Kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani ambao umefanyika katika viwanja vya Mwandege.

Sunday, September 7, 2025

KUNDI C KAGAME LI KIBABE SANA, NA LEO TENA MECHI ZOTE DROO

 

TIMU ya Mogadishu City FC ya Somalia leo imetoa sare ya bila mabao na Kator FC ya Sudan Kusini katika mchezo wa Kundi C Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mechi nyingine ya Kundi C Kombe la Kagame iliyotangulia mchana hapo hapo KMC Complex timu za Sudan, Alahly Wad Madani SC na Al Hilal Omdurman SC nazo zimetoka sare ya kufungana bao 1-1.
Al Hilal Omdurman SC ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Sunday Damilare, kabla ya Abdelkader Ouabdi kuisawazishia Alahly Wad Madani SC.

Kwa matokeo hayo, timu zote nne zinaendelea kufungana kwa pointi mbili kila moja baada ya kila timu kutoa sare mbili katika mechi mbili za mwanzo kuelekea mechi za mwisho Septemba 10, Al-Hilal Omdurman na Kator na Mogadishu City dhidi ya Madani, zote zitaanza muda mmoja Saa 9:00 Alasiri.

DKT. BITEKO AHIMIZA WANAMICHEZO KUCHUNGUZA AFYA ZAO

 

📌 Tasnia ya Burudani na Michezo kwa mwaka 2024/2025 imekuwa kwa asilimia 18

📌 Watumishi 3,353 washiriki SHIMIWI mwaka 2025

📌 Awahimiza washiriki SHIMIWI kusikiliza kampeni za wagombea na kupiga kura Oktoba 29

📌 Serikali kujenga Kituo cha Kulea Vipaji Mwanza

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa rai kwa wanamichezo kufanya uchunguzi wa afya zao kwa kuhusisha vipimo vyote muhimu ikiwemo vya moyo, damu na viungo vyote vya mwili ili kuhakikisha usalama wa Afya zao.
 
Ameliomba Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) kuendelea kushirikiana na Taasisi za Afya nchini na kuweka mfumo sahihi wa upimaji wa afya kwa wanamichezo.

Dkt. Biteko ametoa rai hiyo Septemba 7, 2025 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati akifungua rasmi mashindano ya 39 ya SHIMIWI yaliyotanguliwa na maandamano ya watumishi wa umma.

Ametaja masuala mengine muhimu ya kuzingatiwa kwa wanamichezo “ Mazoezi ya awali na mbinu nyingine mbalimbali kwa kujenga uimara wa mwili kupitia mazoezi kama vile kukimbia, mazoezi ya nguvu na mazoezi mfano wa hayo. Pia, kuiandaa akili ili kuikabili michezo na mashindano kwa ujumla, wataalamu husema mafanikio huanza katika fikra,” amesema Dkt. Biteko.

 Ameongeza kwa kusema Nimejulishwa kwamba, katika michezo ya mwaka wa jana mlisajili watumishi 2,995. Na mwaka huu 2025 mmesajili watumishi 3,353 kushiriki michezo hii ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 12 hongereni sana,” 

Pia, ameipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na viongozi wa SHIMIWI kwa kazi kubwa ya kuratibu, kusimamia na kuendeleza michezo nchini.

Dkt. Biteko pia amewataka waajiri kutekeleza maagizo ya Rais Samia ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumishi wanaoshiriki SHIMIWI huku akiwaeleza watumishi kuwa Rais Samia anawatakia kila la heri katika michezo yao na kuwa yuko tayari kuendelea kushirikiana nao ili kupata mahitaji yao.

Amesema takwimu zinaonesha kuwa, Tasnia ya Burudani Tanzania ambayo michezo ipo ndani yake imeendelea kukua kwa kasi na kuchangia sehemu muhimu katika Pato la Taifa na kuongeza ajira nchini.
 
Ametolea mfano kwa mwaka 2022/2023 sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 na mwaka 2023/24 kwa asilimia 18. Aidha, uwepo wa watumishi wanaoshiriki SHIMIWU zaidi ya 3,000 Jijini Mwanza umesaidia kutengeneza ajira na kuchangia mzunguko wa fedha. 

“Nawaomba viongozi muweke mikakati ya kuhakikisha manufaa haya yanawagusa Watanzania wa maeneo yote nchini kwa maslahi mapana ya Taifa kwa ujumla,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Halikadhalika amewaasa wachezaji wote kujenga fikra ya kupendana na si kuchukiana baina yao pamoja na kufuata na kuzingatia taratibu zote za michezo.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewasihi wanamichezo hao kuhimizana kushiriki kwa amani katika zoezi la kusikiliza kampeni za wagombe na kukumbushana umuhimu wa kupiga kura.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza katika michezo ambapo inajenga Kituo cha Kulea Vipaji katika Chuo cha Michezo Malya.

Pia, amesema shughuli za kampeni mkoani humo zinaendelea vizuri na Oktoba 29, 2025 wananchi watajitokeza kwa wingi kupiga kura.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuruhusu kufanyika kwa mashindano ya SHIMIWI kwa watumishi wa umma kwa miaka mitano mfululizo kwa kuwa yameendelea kuwa na faida kubwa.

“ Wizara yetu itaendelea kuhakikisha michezo hii inafanyika kwa haki, sisi kama Wizara tunamshukuru Mhe. Rais kwa maelekezo yake na kutoa raslimali fedha ili kukuza sekta ya michezo nchini,” amesema Msigwa.

Ametaja jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya michezo ni pamoja na kukamilisha viwanja na shule za michezo katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika michezo kimataifa katika ngazi mbalimbali.

Katika salamu zake za utangulizi, Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa imefanya shughuli zake kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuleta matokeo chanya.

Awali, Dkt. Biteko ametembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambapo ameelezwa majukumu na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Mashindano ya Michezo ya 39 ya SHIMIWI kwa mwaka 2025 yanayoongozwa na kaulimbiu “ Michezo kwa Watumishi Huongeza Tija Kazini, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 29 Oktoba 2025 kwa Amani na Utulivu  Kazi Iendelee.”yatafikia tamati Septemba 16, 2025.