Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
Mheshimiwa Paul Makonda leo amepokea Vitanda 150 na Magodoro 150 vyenye
tamani ya zaidi ya shilingi Million 300 kutoka kampuni ya mafuta ya
Camel chini ya Kampuni tanzu za Amsons Group iliyomua kuunga mkono
juhudi za Mkuu wa Mkoa katika kuboresha sekta ya Afya.
Vitanda hivyo ambabyo pia vina Magodoro pamoja na Mashuka yake
vitapelekwa kwenye Wodi mpya ya Mama na Mtoto iliyojengwa kwenye
Hospital ya Amana chini ya ufadhili wa kampuni ya Amsons Group ambayo
ujenzi wake umekamilika kwa Asilimia mia moja.
Akizungumza baada ya kupokea Vitanda hivyo, Makonda amesema amedhamiria
kuhakikisha changamoto zote zinazoikabili sekta ya Afya katika Mkoa wa
Dar es Salaam zinamalizika ili kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora
za afya.
“Sitaacha kutafuta kwaajili ya Wananchi wa Dar es salaam, nitabisha hodi
kila panapostahili ili mradi Wananchi wangu wawe wanapata huduma za
Afya katika mazingira mazuri ili siku moja waone kazi kubwa inayofanywa
na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dr. John Magufuli” Alisema
Makonda.
“Tumedhamiria kuhakikisha Mama,Mtoto na Wananchi wote wa Mkoa wa Dar es
salaam wanapata huduma bora, na huduma bora zipo kwenye Afya,kama
Wagonjwa wasipopata huduma bora inakuwa ni tatizo,tayari kama
mnavyofahamu tuna Majengo ya kisasa tunayoendelea kujenga Chanika,
Amana, Temeke na Mwananyamala ambapo kukamilika kwake yataongeza tija ya
upatikanaji wa huduma za bora za Afya, sasa Vitanda hivi 150 ni tafsiri
tosha kuwa vinakwenda kupunguza adha kwa kinamama wanaokwenda
kujifungua kwenye Hospital ya Amana” Aliongeza Makonda.
Kwa upande wake Suleiman Amour meneja uendelezaji wa biashara kampuni ya
Camel Oil amesema vitanda hivyo ni uendelezaji wa kutoa mchango wao
kuunga mkono juhudi za mkuu wa mkoa za kuhakikisha wananchi wa Dar es
salaam wanapata huduma bora za afya.
Ikumbukwe kuwa Kampuni tanzu ya Mafuta na Saruji za Amsons Group ndio
wanaojenga wodi za mama na motto kwenye Hospital za Amana, Temeke na
Mwananyamala baada ya mkuu wa Mkoa kuwashirikisha dhamira yake ya
kumaliza kero kwenye sekta ya Afya.