ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, March 18, 2026

SALA YA EID KWA NGAZI YA MKOA KUFANYIKA NYAMAGANA.

 


Baraza Kuu la Waislam Mkoa wa Mwanza limetangaza kuwa Swala ya Eid itafanyika kimkoa katika Uwanja wa Nyamagana uliopo Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza.


Katika taarifa hiyo, Waislam wote mkoani Mwanza wanaombwa kuhudhuria swala hilo kwa pamoja ili kushiriki ibada hiyo muhimu ya sikukuu.


Baraza hilo limehimiza umoja, mshikamano na nidhamu wakati wa ibada hiyo, pamoja na kuzingatia maelekezo yatakayotolewa na viongozi wa dini na mamlaka husika.

VIKUNDI 41 VIJANA, WANAWAKE NA WATU WENYE ULEMAVU VYANUFAIKA NA MIKOPO YA ASILIMIA 10 ILEMELA

 


Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza , Amir Mkalipa, amevitaka vikundi vilivyopata mikopo ya asilimia 10 katika wilaya hiyo kuhakikisha vinarejesha fedha hizo kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo.


Akizungumza hii leo wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo hiyo iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Mkalipa amesema kuwa halmashauri itafuatilia kwa karibu vikundi vyote vilivyopata mikopo ili kuhakikisha vinarejesha kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa.


Aidha, Mkalipa amewataka maafisa maendeleo wa kata kutoa elimu mara kwa mara kwa vikundi hivyo pamoja na kuvitembelea ili kubaini mapema vikundi vinavyosuasua katika marejesho, na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.


Kwa upande wake, Meya wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Bi. Salah Ngw'ani, ameishukuru halmashauri hiyo kwa utoaji wa mikopo hiyo, akisema kuwa itakuwa chachu ya maendeleo kwa wakazi wa wilaya hiyo.


Jumla ya vikundi 41 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika wilaya ya ilemela vimenufaika na mikopo hiyo  ya alimia 10 yenye thamani ya shilingi milioni 463.

YANGA SC YAAMBULIA SULUHU NYINGINE KWA TRA UNITED ARUSHA

 


MABINGWA watetezi, Yanga SC wametoa sare ya bila kufungana na wenyeji, TRA United katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

TRA United ilicheza pungufu kwa dakika 10 za mwisho kufuatia kiungo wake, Muzamil Yassin Selemba kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 76 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.

 

Majeruhi bado yanaiandama Yanga huku Dube na beki wa kulia Israel Mwenda wote wakitoka uwanjani kutokana na kugongana. Sare hiyo inaifanya Yanga ibaki kileleni kwa pointi zake 37, tisa mbele ya Azam inayoshika nafasi ya pili na JKT Tanzania inayoshika nafasi ya tatu, wakiwa na pointi 28 kila mmoja, huku Simba wakishika nafasi ya nne kwa pointi 27 nayo TRA nafasi ya 10.


Huu unakuwa mchezo wa pili mfululizo kwa Yanga wa ligi bila bao, kufuatia sare ya 0-0 dhidi ya Azam wikendi iliyopita. Baada ya mechi 15 za mzunguko wa kwanza, Yanga imeshinda 11 na kutoa sare nne, huku ikiwa haijafungwa.


Azam wamecheza mechi 14, mechi inayofuata dhidi ya Mashujaa mjini Kigoma kesho, huku Simba wakicheza mechi yao ya 13 dhidi ya Pamba ya Jiji, hiyo ikimaanisha kuonyesha kwa nguvu kwenye michezo hii kunaweza kuwafanya kupunguza pengo la pointi moja tu nyuma ya wapinzani wao hao wa jadi.


SENEGAL WAVULIWA UBINGWA WA AFCON, MOROCCO WAPEWA USHNDI WA 3-0

 


BODI ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeivua Senegal ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na kuwapa wenyeji, Morocco.

Senegal ilitawazwa kuwa bingwa wa AFCON ya 2025 baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Morocco Januari 18, mwaka huu bao pekee la kiungo wa ulinzi, Pape Alassane Gueye anayechezea Villarreal ya Hispania dakika ya 94 katika mchezo uliodumu kwa dakika 120 Uwanja wa Prince Moulay Abdellah Jijini Rabat.

Hata hivyo, CAF imesema kwamba Senegal imepoteza mechi hiyo na Morocco wamepewa ushindi wa mabao 3-0  kwa kutumia Kifungu cha 84 cha Kanuni za AFCON kwa kitendo chao cha kuondoka uwanjani kupinga Penalti waliyopewa Morocco na kusababisha mchezo kusima akwa dakika 14, kabla ya kurejea kumalizia.

Mshambuliaji Brahim Díaz wa Morocco ambaye yeye mwenyewe alichezewa rafu na beki wa Senegal, El Hadji Malick Diouf – alikwenda kupiga penalti kwa staili ya Panenka bahati mbaya ikaokolewa na kipa Édouard Mendy na kuzima ndoto za Simba wa Atlasi kutwaa taji kwa jasho uwanjani.

Tuesday, March 17, 2026

JPM

Monday, March 16, 2026

MIAKA MITANO TANZANIA BILA JPM

 


Miaka Mitano Siku Zaidi ya Siku 1800 Tangu kifo cha Rais Wa Awamu ya Tano Hayati Dkt, John Pombe Magufuli 


#kazinangoma ya 93.7 Jembe Fm inaungana na Familia ya Dkt, John Pombe Magufuli na Watanzania wote katika kumbukizi hiyo 

Kuzifungua kurasa za kumbukumbu, mijadala na simulizi.

Kuanzia Leo.

📅 16–17 Machi 2026

📻 93.7 Mwanza


Usikose.  Kusikiliza vipindi mbalimbali kupitia Jembe Fm🔥📻 Na Kutufatilia kwenye mitandao ya kijamii @jembefmtz 


Follow Us On Social Media

‎Instagram - @jembefmtz

‎Facebook - @jembefmtz

‎X(Twitter) - @jembefmtz

‎TikTok - @jembefmtz

‎Thread - @jembefmtz


#AhsanteKwaTime 

#Familiamoja

#10yrsjembefm 


#JembeFMKurasa1800LiveChato

MVUA MOROGORO YASABABISHA VIFO VINNE

 


Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro zimesababisha vifo vya watu wanne katika matukio tofauti, huku wengine wakijeruhiwa baada ya kupigwa na radi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema watu wawili walifariki dunia baada ya kupigwa na radi wakati wa mvua kubwa katika Kijiji cha Kilosa Mpepo wilayani Malinyi.

Amewataja waliofariki kuwa ni Nindi Masele (15) na Marwa Mwanzilwa (2), wote wakazi wa kijiji hicho, waliopoteza maisha usiku wa Machi 13, 2026 wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha.

Aidha, amesema watu wengine wanne wa familia moja walijeruhiwa katika tukio hilo akiwemo Milembe Dase (27), Kulwa Malembe (38), Milembe Samwel (39) pamoja na Ngolo Nchimwe (1), ambao wanaendelea kupatiwa matibabu.

Ndani ya mwezi mmoja uliopita, tukio jingine la radi lilitokea Februari 23 mwaka huu katika Kitongoji cha Mbesi, Kijiji na Kata ya Utengule, Halmashauri ya Mlimba wilayani Kilombero.

Katika tukio hilo, watu wawili Tano Leonard Lunasi (36) na Ngimila Ndombeji Mashana (27), wote wakulima na wakazi wa eneo hilo, walipoteza maisha huku wengine wawili wakijeruhiwa walipokuwa wakirejea nyumbani kutoka matembezini.

Katika tukio jingine, watu wawili Hamis Yahaya Waziri (45), mkulima mkazi wa Kisaye na Nyerere Katebeka Kidagati (50), mfugaji mkazi wa Mkono wa Mara wilayani Morogoro, wamefariki dunia baada ya kusombwa na maji ya mvua.

Kamanda Mkama amesema watu hao walifariki katika kata za Tegetero na Mkambarani walipokuwa wakijaribu kuvuka maeneo yaliyofurika maji lakini walizidiwa nguvu na kusombwa na maji.

KAMATI BUNGE YARIDHISHWA MRADI FARU MWEUSI, MBWA MWITU

 Faru mweusi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imesema imeridhishwa na uwekezaji wa mradi wa uhifadhi wa faru mweusi na mbwa mwitu katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, na kuiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka husika kuendelea kuwalinda wanyama hao ambao walikuwa hatarini kutoweka.

Akizungumza Machi 15 baada ya kutembelea na kukagua mradi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mary Masanja, amesema kamati imefurahishwa na maendeleo ya mradi huo huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwalinda na kuwahifadhi wanyama hao adimu.

Alisema pia ni muhimu kuangalia uwezekano wa kuwahamishia faru katika hifadhi nyingine kadri idadi yao inavyozidi kuongezeka, ili kuwapa nafasi zaidi ya kuishi na kuongeza fursa kwa watalii kuwaona katika maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini.

“Mradi kwa sasa unaridhisha na ukizingatia kwamba faru ni mnyama aliyekuwa kwenye hatari ya kutoweka. Tunaendelea kuwaalika wananchi watembelee hifadhi hii, na kikubwa tumeielekeza Wizara kuwa mradi huu unahitaji matunzo endelevu. Pale ambapo idadi ya faru itaongezeka, waweze kusambazwa katika hifadhi nyingine ili watalii wanaotembelea maeneo hayo waweze kuwaona kwa urahisi zaidi,” alisema Masanja.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, alisema mradi huo wa faru uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.4 unalenga kuwahifadhi wanyama hao adimu ili waweze kuzaliana na kulinda urithi wa taifa.

Alisema pamoja na juhudi za uhifadhi, mradi huo pia umeongeza thamani ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, kwani watalii sasa wanaweza kufika katika eneo maalumu lenye uzio wa umeme na kupata fursa ya kuwaona faru kwa ukaribu zaidi.

“Kamati wameridhishwa na mradi huu na kutupa maelekezo ya kuendelea kuwalinda wanyama hawa pamoja na kuboresha zaidi mradi huu. Faru waliopo katika mradi huu wamefikia idadi ya 50, hivyo eneo la sasa linaanza kuwa finyu. Kamati imesisitiza kuongeza eneo la uzio, na sisi pamoja na mamlaka husika tunakwenda kulifanyia kazi kwa haraka ili wanyama wapate eneo kubwa zaidi la kuishi na utalii uendelee kuimarika,” alisema Abbasi.

Aidha, aliongeza kuwa Wizara pia inapanga kuongeza magari kwa ajili ya kuwahudumia watalii wanaotembelea eneo la faru pamoja na hifadhi kwa ujumla, kutokana na ongezeko kubwa la watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, hususan wale wanaokuja kuona faru.

Kwa upande wake, mjumbe wa kamati hiyo, Asia Halamga, alisema juhudi za Serikali zimewezesha kuongezeka kwa wanyama waliokuwa adimu kama faru na mbwa mwitu katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

Alitoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ili kufurahia na kuthamini urithi wa rasilimali za asili uliopo Tanzania.

YANGA SC YAAMBULIA SULUHU DHIDI YA AZAM FC

 


MABINGWA watetezi, Yanga SC wamelazimishwa sare ya bila mabao na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku wa Jumapili ya tarehe 15 Machi 2026, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Yanga SC inafikisha pointi 36 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 28 baada ya timu zote kucheza mechi 14.