ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, September 12, 2024

MWANASHERIA WA YANGA AFUNGUKA SAKATA LA KAGOMA ATOA TAMKO

 MKURUGENZI wa Sheria wa Yanga, Simon Patrick leo Septemba 12, 2024 amethibitisha kuwa timu yao ilikamilisha mchakato wa kumsajili Yusuph Kagoma mwezi Machi 2024 kutoka klabu ya Fountain Gate.

Akizungumza wanahabari mapema leo, Simon amesema mazungumzo kati ya Yanga na Fountain Gate kwa ajili ya usajili wa Kagoma yalianza Machi 3, 2024

“Yanga ilipewa masharti na Fountain Gate ya kulipa Milioni 30 kumnunua Kagoma. Baada ya makubaliano ya klabu, pande mbili ziliingia mkataba ya mauziano ya mchezaji”
Yusuph Kagoma

“Mkataba halali ulisainiwa na pande mbili. Yanga ilipaswa kulipa fedha kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ikamilishwe kabla ya April 30 na Awamu ya pili ikamilishwe kabla ya Juni 30

Yanga ililipa fedha zote Milioni 30 kabla ya April 30 na Machi 27, 2024 Yanga ilimtumia Kagoma tiketi ya ndege kutoka Kigoma kuja Dar es salaam kwa ajili ya mazungumzo

Mpaka sasa tunaongea Yusuph Kagoma ni mchezaji halali wa Yanga Sc tulimsaini miaka mitatu na tukamtumia hadi tiketi ya ndege kutoka Kigoma nakuja Dar es salaam kuungana na timu kwa ajili ya maandalizi ya msimu huu 2024 – 2025” amesema Patrick Saimon, Mwanasheria wa Yanga

MBUNGE UMMY AMSHUKURU RAIS DKT SAMIA KWA UWEKEZAJI WA BANDARI YA TANGA ULIOLETA TIJA KUBWA KWA WANANCHI

 

MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngamiani Kati wakati wa mkutano wake wa hadhara katika eneo hilo




Na Oscar Assenga,TANGA


MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa uwekezaji mkubwa katika Bandari ya Tanga ambao matunda yake yameanza kuonekana kwa kuiwezesha kupokea shehena kubwa ikiwemo za magari.

Ummy aliyasema hayo leo wakati wa mkutano wake wa hadhara uliofanyika kata ya Ngamiani Kati Jijini Tanga ambapo alisema hilo ni jambo kubwa sana ambalo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa wananchi .

Alisema kwamba uwekezaji huo wa zaidi ya Bilioni 400 uliofanywa na Serikali umekuwa ni chachu kubwa ya kufungua fursa za kiuchumi katika mkoa waTanga na sasa hata Jiji hilo limeanza kubadilika.

Alisema kwamba kutokana na uwekezaji huo utasaidia kuwezesha uchumi wa mkoa wa Tanga kukua kutokana na shehena za mizigo zinapokuwazikishushwa kwenye Bandari hiyo wananchi watanufaika.

"Uwekezaji huu kwetu sisi watu wa Tanga ni mkubwa wenye manufaa makubwa kwani utatusaidia kuweza kurudisha enzi zetu za miaka ya nyuma kukua kiuchumi na hii italeta manufaa kwetu sote hivyo niwatake wana Tanga kuchangamkia fursa hii"Alisema

Aidha alisema kwamba awali kabla ya uwekezaji huo walikuwa wakikosa fursa za kuona meli kubwa zikitia nanga gatini lakini kwa sasa imekuwa ni rahisi kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali.
 
Alisema jambo hilo limesaidia kuwarudisha wafanyabiashara ambao awali walikuwa wakitumia Bandari hiyo na hivyo kupelekea uwepo wa mzunguko wa kibiashara kwenye Jiji hilo.

"Ndugu zangu wakati natafuta kura mwaka 2020 mkoani kwetu hakukuwahi kuwa na meli kubwa tena ambazo zinashusha magari na kutia nanga gatini lakini kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa  Serikali kupitia mimi Mbunge wenu zimeleta matunda na hivyo Rais Dkt Samia Suluhu kutuletea fedha ambazo zimewezesha maboresho makubwa yaliyowezesha meli kubwa kutia nanga"Alisema
 
Hata hivyo aliwataka wakazi wa Jimbo hilo kuchangamkia fursa ya maboresho yaliyofanywa kwa kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ya kiuchumi,ujasiriamali na kilimo kwa lengo la kuweza kujikwamua kiuchumi zinazotokana na uwekezaji huo.

KIBAHA MJI YAPEWA 'TANO'NA KAMATI YA BUNGE YA ELIMU,USIMAMIZI WA MIRADI

 


NA VICTOR MASANGU


Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia Wizara ya Elimu na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeridhika na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Shule ya Shimbo iliyopo Kata ya Mkuza,Halmashauri ya Mji Kibaha

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Husna Sekiboko  amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ndoto na maono yake ni kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata Elimu bora  kwenye Mazingira rafiki ili kuandaa Wataalam kulitumikia Taifa lao na kwamba Kibaha Mji wamesimamia Ujenzi wa shule hiyo kwa viwango na thamani ya fedha inaonekana

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Leah Lwanji ameieleza Kamati kuwa Jumla ya Shilingi 528,998,425 kupitia Mradi wa SEQUIP zilipokelewa  ajili ya Ujenzi wa miundombinu  27  na tayari imekamilika  na tayari Wanafunzi 281 kati yake wavulana 149 na Wasichana 132 wameanza kunufaika kwa kuwapunguzia umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 8 kuifuata shule Mama ya Nyumbu.

Mhe.Hamisi Shabani Taletale ameipongeza Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa Mradi na kushauri kujengwa kwa uzio ili kuwawekea utulivu wanafunzi wakati wa Masomo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Husna Sekiboko ametoa maelekezo ya Kamati kama ifuatavyo;

Mosi, Shule zote nchini ziwe na utaratibu wa kukagua maudhui ya vitabu kama vinaendana na maadili ya Watanzania kuelekeza vitabu vihakikiwe na kugongwa mihuri wa kuridhia Matumizi na Kamishina wa Elimu nchini

Pili,Serikali iangalie upya mgawanyo wa fedha zinazotolewa kwa ajili ya Miradi kwani yapo maeneo wanakamilisha Ujenzi na maeneo mengine hawakamilishi ama Kujenga chini ya Kiwango na kuathiri matarajio na malengo.Ameitaka Wizara ya Elimu kufanya tathmini ya kimaeneo ili fedha zinazotolewa zitosheleze ili kuongeza tija ya Miradi husika


Waziri wa Elimu Prof.Adolf Mkenda ameishukuru Kamati kwa kazi nzuri na kupokea maelekezo yote  ya Kamati kwa ajili ya kufanyia kazi 

Aidha,Mwenyekiti wa Kamati Mhe.Sekiboko amempongeza sana Dkt.Rogers Jacob Shemwelekwa Mkurugenzi wa Mji Kibaha kwa usimamizi mzuri wa Miradi ya Maendeleo kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani kuhakikisha Mabilioni ya fedha yanayotolewa na Dkt.Samia Suluhu Hassan yanafanyakazi zinazoonyesha matokeo kwa Watanzania


MIKATABA YA KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI ZA KUPIKIA KUSAINIWA

 
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage (katikati) akifafanua jambo wakati wa wa Mkutano na Waandishi wa Habari, leo Septemba 11, katika Ofisi za Wakala huo Jijini Dodoma. Wengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Adrophine Tutuba (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano, Martha Chassama. (Picha na REA)

Na Mohamed Saif- Dodoma

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatarajia kusaini mikataba yenye thamani ya shilingi bilioni 50.98 kwa ajili ya kuhamasisha umma kuachana na matumizi ya nishati za kupikia zisizo salama ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi za Kupikia.

Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage amebainisha hayo katika mkutano na Waandishi wa Habari Septemba 11, 2024 Jijini Dodoma.

Alisema utekelezaji wa miradi ya Nishati Safi na zilizoboreshwa za kupikia ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi 2024- 2034 ambao unaelekeza ifikapo Mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi za kupikia.

“Hivi karibuni, Wakala utasaini mikataba kadhaa ya ushirikiano na wadau mbalimbali ambayo yote kwa pamoja imelenga kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi za Kupikia kwa wote kama Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi za Kupikia unavyoelekeza,” alifafanua Mhandisi Advera.

Mhandisi Advera alisema Wakala umefikia makubaliano ya ushirikiano wa utekelezaji wa miradi ya kujenga na kusambaza mifumo ya Nishati Safi za Kupikia na Jeshi la Magereza pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo mifumo mbalimbali ya nishati safi na iliyoboreshwa itafungwa katika taasisi hizo.

Alisema kwa upande wa Jeshi la Magereza (TPS), mikataba itakayosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 35.23 ambapo kati ya fedha hizo 75.5% ambayo ni sawa na shilingi bilioni 26.57 zitatolewa na REA na 24.6% sawa na shilingi bilioni 8.66 zitatolewa na Jeshi la Magereza kwa Mradi utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika Magereza 129 yaliyopo Tanzania Bara.

“Katika mkataba huu na Magereza kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa mifumo ya bayogesi (gesi vunde) 126, usimikaji wa mifumo 64 ya gesi ya LPG, usimikaji wa mfumo wa gesi asilia, usambazaji wa mitungi ya gesi (LPG) ya kilo 15 ikiwa na jiko la sahani mbili ipatayo 15,920 kwa watumishi wa Magereza, usambazaji wa tani 865 za mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kutoka STAMICO,” alifafanua Mhandisi Advera.

Alisema mkataba huo na Magereza vilevile utahusisha pia usambazaji wa mashine 61 za kutengeneza mkaa mbadala, ujengaji uwezo kwa watumishi 280 wa Jeshi la Magereza na usambazaji wa majiko banifu 977 ambapo kati ya majiko hayo, 377 yatatumia nishati ya bayogesi, 256 yatatumia LPG na 344 yatatumia nishati ya mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kwa kuanzia na baadaye kwa mkaa unaotokana na mabaki ya mazao mbalimbali.

Aidha, kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), alisema mikataba itakayosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 5.75 ambapo kati ya fedha hizo 76% ambayo ni sawa na shilingi bilioni 4.36 itatolewa na REA na huku 24% sawa na shilingi bilioni 1.39 itatolewa na JKT.

“Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi katika Kambi 22 za JKT kwa muda wa miaka miwili itakayohusisha ujenzi wa mitambo 9 ya bayogesi, majiko 291 ya kutumia mkaa mbadala (makaa ya mawe na tungamotaka), ujenzi wa mifumo 180 ya kupikia inayotumia LPG na sufuria zake, ununuzi wa tani 110 za mkaa unaotokana na makaa ya mawe, ununuzi wa mashine 60 za kutengeneza mkaa mbadala na mafunzo kwa vijana wapatao 50,000,” alisema.

Mhandisi Advera alisema katika kuwezesha kaya za vijijini na zile zilizopo katika maeneo ya vijiji-miji kutumia nishati safi za kupikia na zilizoboreshwa, Serikali kupitia REA inaendelea kutoa ruzuku katika uuzaji wa mitungi ya gesi (LPG) ya Kilo 6.

Alizitaja kampuni zilizoshinda zabuni ya kusambaza mitungi hiyo kuwa ni Taifa Gas, Manjis, Oryx pamoja na Lake Oil ambapo alisema jumla ya mitungi 452,445 itasambazwa kwa bei ya ruzuku katika mikoa yote ya Tanzania Bara na huku kila wilaya ikinufaika na mitungi 3,255.


TASAC YATOA ELIMU KWA WADAU MBALIMBALI WILAYANI UKEREWE

 







Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) leo tarehe 10.9.2024, limetoa elimu ya ulinzi, usalama na utunzaji wa mzingira ya usafiri majini kwa wadau mbalimbali wa usafiri majini katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe. Elimu hiyo imehusisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na wasafiri na wasafirishaji, wamiliki wa vyombo vya usafiri majini, viongozi wa serikali za Kijiji na wananchi kwa ujumla. 

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika mwalo wa Bukungu Naho. Michael Rogers amesema ”kila mmoja ni balozi wa usalama wa vyombo vya usafiri majini hivyo hatuna budi kuhakikisha vyombo vinakidhi viwango na kuhakikisha vinakuwa na leseni kwa mujibu wa sheria na kupunguza ajali za mara kwa mara kwa kuvaa vifaa vya kujiokolea kwani kila mmoja wetu ni muhimu kwa jamii na taifa kwa ujumla”

Aidha, wananchi wa Ukerewe katika mialo iliyotembelewa na TASAC wamepongeza na kushukuru juhudi za utoaji elimu na kuomba Shirika kuendelea kufanya hivo mara kwa mara ili kuongeza uelewa mpana kwa wananchi juu ya sekta ya usafiri majini.

Zoezi hili la utoaji elimu limeanza Septemba 9 na litafikia tamati Septemba 13,2024.

Wednesday, September 11, 2024

LIJUWE ZAO LA MWANI LINALOONGEZA SIKU ZA KUISHI, KIBOKO YA MARADHI MENGI.

 

 

NA ALBERT G.SENGO/MWANZA

Mwani wa bahari si jambo geni kwa wazawa wa maeneo ya pwani, wengi hukusanya kwa matumizi ya biashara na wachache hujumuisha katika mlo wao.

Ndani ya maonesho ya biashara ya Afrika Mashariki Jembe Fm inapata wasaa kuzungumza na moja ya wakulima na mfanyabiashara wa zao hilo kutoka visiwa vya Zanzibar, ambaye anashawishi watu kujumuisha mwani katika milo yao, akisema kuwa mwani una faida nyingi kwa afya.

Na baadhi wamekua wakiita mwani kama 'Super food', lakini kuna ukweli wa jambo hili?

DAKIKA ZA JIOOOONI MAGOLI YOTE YA TAIFA STARS DHIDI YA GUINEA 2 1

 

TIMU ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars imechukua alama zote tatu dhidi ya wenyeji, Guinea katika dimba la Charles Konan Banny, Yamoussoukro Ivory Coast kwenye mchezo wa Kundi H.

Guinea 1-2 Tanzania
⚽ Bayo 57’
⚽ Feitoto 61’
⚽ Mudathir 88’

Stars imefikisha pointi 4 baada ya mechi mbili inasalia nafasi ya pili kwenye Kundi H alama mbili nyuma ya vinara DR Congo.

𝐅𝐔𝐋𝐋 𝐓𝐈𝐌𝐄: KUFUZU #AFCON 2025
Botswana 🇧🇼 0-4 Egypt 🇪🇬
Gabon 🇬🇦 2-0 Central African Republic 🇨🇫
Liberia 🇱🇷 0-3 Algeria 🇩🇿
Namibia 🇳🇦 1-2 Kenya 🇰🇪
Zimbabwe 🇿🇼 0-0 Cameroon 🇨🇲

Monday, September 9, 2024

REA YAENDELEA KUTEKELEZA DHAMIRA YA RAIS SAMIA KWA VITENDO

 

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage wakati wa uzinduzi wa kipindi maalum Jijini Dar es Salaam cha Pika Kijanja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kinacholenga kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (wa pili kulia) akielekeza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kipindi maalum cha Pika Kijanja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan maarufu kama Azimio la Kizimkazi iliyofanyikia Jijini Dar es Salaam. 
Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla ya uzinduzi wa kipindi maalum cha Pika Kijanja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan maarufu kama Azimio la Kizimkazi iliyofanyikia Jijini Dar es Salaam. 
Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla ya uzinduzi wa kipindi maalum cha Pika Kijanja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan maarufu kama Azimio la Kizimkazi iliyofanyikia Jijini Dar es Salaam. 

Na Mohamed Saif

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kila Mwananchi anatumia Nishati Safi ya Kupikia.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema hayo Jijini Dar es Salaam Septemba 08, 2024 wakati wa uzinduzi wa Kipindi maalum cha Pika Kijanja na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan maarufu kama Azimio la Kizimkazi.

“Mhe. Rais wakati anazindua Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 Mwezi Mei mwaka huu alitoa maagizo maalum kwa REA; kwakuwa tumefanya vizuri katika kusambaza umeme vijijini huku nako kwa kushirikiana na wadau wengine tuhakikishe asilimia 80 ya Watanzania wanatumia Nishati Safi za Kupikia ifikapo mwaka 2034,” alisema Mhandisi Saidy.

Mhandisi Saidy alibainisha kuwa Wakala umeanza kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais kwa namna mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wananchi kutumia Nishati Safi za Kupikia kwa kuondokana na fikra kuwa bidhaa za Nishati Safi ni ghali ama si salama na kwamba chakula kinachopikwa kwa Nishati Safi hakina ladha.

“Tunaendelea kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kwamba suala la ladha ya chakula linategemea umahiri wa mpishi ama viungo vinavyotumika na sio nishati inayotumika kupikia,” alisema Mhandisi Saidy

Mhandisi Saidy alisema Wakala unaendelea kuwezesha upatikanaji wa Nishati Safi za Kupikia kwa kushirikiana na watoa huduma ambapo REA inawapa fursa watoa huduma kujitangaza ili kuwezesha wananchi wengi kufahamu uwepo wa teknolojia rafiki za nishati safi za kupikia.

Alibainisha kuwa Serikali kupitia REA inatoa ruzuku ili kuwezesha wananchi wamudu kununua bidhaa za Nishati Safi za Kupikia na kujionea ubora wa bidhaa hizo kwa lengo la kuendelea kuhamasisha wananchi wengi wahame kutoka kwenye kutumia nishati zisizokuwa salama.

“Serikali imetoa ruzuku ili kila mwananchi aweze kumudu gharama; Mathalan kwenye mitungi ya gesi (LPG) na vichomeo vyake Serikali kupitia REA imeidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 10 kitumike kusambaza Mitungi ya Gesi ya kilo 6 itakayonufaisha watanzania wapatao 452,445 kwa bei ya ruzuku,” alifafanua.

Mhandisi Saidy alibainisha kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya mia moja zianze kutumia Nishati Safi za Kupikia na kwamba katika utekelezaji wake, REA imeandaa miradi ya kufikisha bidhaa na teknolojia za Nishati Safi za Kupikia kwenye taasisi hizo.

“Tunatekeleza agizo la Mhe. Rais na tumeanza na Magereza wao wana maeneo 211 tutakayoyafikishia Nishati Safi za Kupikia pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwenye Kambi 22 na Shule kongwe zipatazo 52; kwa kifupi kila taasisi yenye watu zaidi ya mia itafikiwa,” alisema Mhandisi Saidy.

Sambamba na hilo, Mhandisi Saidy alisema REA inafanya kazi kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo linazalisha mkaa rafiki na kwamba REA inakwenda kuiwezesha STAMICO kununua mashine tatu za kuzalisha mkaa rafiki ili iweze kufikisha huduma kwenye maeneo mengi zaidi.

Aidha, Mhandisi Saidy alisema REA hadi sasa imefanya vizuri kwenye suala zima la kusambaza umeme vijijini ambapo hadi sasa utekelezaji umefika asilimia 99 na kwamba nguvu iliyotumika kusambaza umeme itatumika pia katika kuhakikisha wananchi wote wanapata Nishati Safi za Kupikia.