|
Makamu wa rais Dkt. Bilal akizungumza wakati wa Kilele cha maadhimisho ya sherehe hizo kwenye Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza leo, Juni 5. |
HOTUBA YA MHE. DKT. MOHAMMED GHARIB
BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE KILELE
CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI,
TAREHE 5 JUNI, 2014 MKOANI MWANZA
Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi
Mungu mwingi wa rehema, kwa kutujaali uzima na afya njema, na kutuwezesha
kukusanyika hapa, kushuhudia tukio hili adhimu.
Nitumie nafasi hii kuushukuru uongozi wa
Mkoa wa Mwanza, mikoa jirani, na wadau mbalimbali walioshiriki kwa njia moja
ama nyingine, kufanikisha Maadhimisho haya, ambayo yamefana sana. Hongereni sana! Niwashukuru pia kwa mapokezi
makubwa na moyo wa ukarimu, mliouonesha kwangu na ujumbe wangu, tangu
tulipowasili hapa. Asanteni sana!
Ndugu
Wananchi;
Mabibi
na Mabwana;
Leo Watanzania tunaungana na jamii ya
kimataifa duniani kote kuadhimisha kilele cha Siku ya Mazingira Duniani. Siku
hii muhimu huadhimishwa kwa lengo la kukumbushana na kuelimishana kuhusu
umuhimu wa mazingira na wajibu wa jamii katika kuyatunza kwa manufaa ya vizazi
vya sasa na vijavyo.
Ujumbe wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka
huu ni: ”Chukua Hatua Kukabiliana na
Mabadiliko ya Tabianchi” (Raise
Your Voice, Not the Sea Level). Kitaifa, kaulimbiu inayoongoza maadhimisho
haya ni “Tunza Mazingira ili Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi”. Kaulimbiu
hii inatukumbusha kuchukua hatua na wajibu tulionao wa
kukabiliana na athari za Mabadiliko ya
Tabianchi.
Ndugu Wananchi;
Tunafahamu kwamba, mabadiliko ya tabianchi
yanachangiwa na mrundikano wa hewa ukaa inayotokana na shughuli za maendeleo
inayofanywa na binadamu kama vile viwanda, kilimo, usafirishaji n.k. Sehemu
kubwa, yaani asilimia 97, inachangiwa na nchi zinazoendelea. Ingawa mrundikano
uliopo sasa umesababishwa na nchi zilizoendelea. Nchi masikini kama Tanzania
ndizo zinazoathirika kwa kiwango kikubwa.
Athari za mabadiliko ya tabianchi sasa ni dhahiri katika maeneo mengi duniani
kote. Tumeshuhudia ukame uliokithiri, majira ya mvua yasiyotabirika, mafuriko, kuongezeka
kwa joto duniani, kuongezeka kwa kina cha bahari na kuzama kwa baadhi ya visiwa vidogo; kukauka
kwa vyanzo vya maji na kupungua kwa kina cha maziwa. Wananchi wanaoishi katika
maeneo hayo, ni wahanga na mashuhuda wa matukio hayo ya kusikitisha. Katika
baadhi ya maeneo maisha ya watu, mifugo na mali zao, vimepotea kutokana na
athari hizo.
Ndugu
Wananchi;
Nchi yetu imeshuhudia athari za mabadiliko
ya tabianchi katika sekta zote za uchumi. Baadhi ya sekta za uchumi zinazoathirika
zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni Sekta ya Kilimo, Nishati, Maji, Miundombinu,
Mifugo, Afya na Maliasili. Nitafafanua kama ifuatavyo:-
Sekta ya Kilimo: Sekta hii imeathirika sana kutokana na ukosefu wa mvua
za uhakika na ukame wa mara kwa mara unaosababisha uzalishaji hafifu wa mazao
ya kilimo hivyo kuchochea tatizo la njaa nchini na kulazimisha Serikali kuwapa
chakula wananchi ambao wana uwezo wa kuzalisha na kujilisha wenyewe.
Sekta ya Nishati: Sote tunatambua kuwa nchi yetu imekuwa ikitegemea zaidi
nishati ya umeme unaotokana na nguvu za maji kwa miaka mingi. Kutokana na
mabadiliko ya tabianchi, vina vya maji katika mabwawa ambayo ni vyanzo vikuu
vya nishati ya umeme, vimekuwa vikishuka hadi kufikia chini ya viwango hususan
katika msimu wa kiangazi, hivyo kuathiri upatikanaji umeme katika maeneo mengi
nchini.
Miundombinu: Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi
ya mafuriko. Kwa mwaka huu, mafuriko yamegharimu maisha ya Watanzania wenzetu na
kuharibu miundombinu na makazi ya watu huku yakiacha madhara makubwa katika
mashamba yao. Kwa mfano katika Jiji la Dar es Salaam, zaidi ya Shilingi Bilioni
20 zitahitajika kurejesha miundombinu ya barabara. Aidha, mafuriko yaliyotokea
Morogoro mwaka huu yameleta hasara kubwa kwa Taifa.
Sekta ya Mifugo: Taifa
limeshuhudia kuongezeka ukame mara kwa mara ulioleta maafa makubwa kwa jamii za
wafugaji katika mikoa ya Kaskazini mwa nchi yetu kwa mifugo mingi kufa kwa
kukosa maji na malisho, tatizo ambalo limesababisha hata migongano kwenye
matumizi ya ardhi. Kutokana na ukame uliotokea mwaka 2006, Serikali ilibidi
kuwafidia na kuwapa ruzuku wananchi waliopoteza mifugo yao yote.
Sekta ya Afya: Athari za kiafya
zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi, zimeripotiwa nchini ikiwa ni pamoja
na ugonjwa wa malaria ambao umesambaa katika maeneo yenye baridi hususan maeneo
ya miinuko (Nyanda za Juu Kusini, Kilimanjaro, Arusha na Lushoto) ambayo awali
hayakuwa na ugonjwa huu. Kwa takribani mwezi mmoja sasa, nchi yetu inakabiliana
na ugonjwa wa “Dengue” unaosabishwa na virusi vinavyoenezwa na mbu aina ya “Aedes.”
Mbu hawa huzaliana kwa wingi katika vipindi vya mvua nyingi.
Sekta
ya Maji:
Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, vyanzo vingi vya maji nchini vimekuwa
vikipungua kwa kasi kubwa. Kwa mfano, tangu mwaka 1972 kiasi cha maji katika
mto Mara, kimeshuka kwa asilimia 68 hususan, katika msimu wa kiangazi,
ikiashiria uwezekano wa kuathiri idadi ya wanyama wanaotegemea mto huo katika mifumo
Ikolojia ya Serengeti. Aidha, kiasi cha maji katika mito ya Kilombero na Rufiji
kimepungua kwa asilimia 8 tangu mwaka 1972. Vile vile, vina vya maji katika
Ziwa Victoria, Tanganyika, Manyara, Rukwa na Jipe, vimeendelea kupungua kwa
kasi kubwa.
Sekta ya Maliasili: Sote tunafahamu, Tanzania ina maliasili nyingi katika misitu, mapori na
maji. Katika maeneo haya kuna mimea, wanyamapori, samaki, wadudu, na viumbe
wengine wa majini na nchi kavu. Baadhi ya mimea, wanyamapori na viumbe wengine
ni wachache na hawapatikani popote duniani isipokuwa hapa nchini kwetu. Viumbe
wengi hawa, sasa wako hatarini kutoweka kutokana na uharibifu wa mazingira na
athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ndugu
Wananchi;
Mabibi
na Mabwana;
Ili kupunguza au kudhibiti athari hizi za mabadiliko
ya tabianchi, zinazotishia jitihada zetu za kujiletea maendeleo, ni muhimu tuchukue
hatua za kuhakikisha tunatunza na kuhifadhi mazingira yetu. Tupande miti na
kutunza misitu yetu ili itusaidie kunyonya hewa ukaa zinazosababisha mabadiliko
ya tabianchi. Katika ngazi ya Kimataifa, tutaendelea kuzishinikiza nchi
zilizoendelea, kuchukua hatua mahsusi za kupunguza uzalishaji wa gesijoto na
kusaidia nchi zinazoendelea kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ndugu
Wananchi;
Ndugu Wananchi;
Pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, mazingira ni sehemu ya
maisha ya binadamu, na ndio uhai wa Taifa
lolote lile. Binadamu hawezi kuishi bila ardhi, maji, mimea na hewa. Hata hivyo
pamoja na umuhimu huo, tunaendelea kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira
katika nchi yetu kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo; Kilimo kisichoendelevu
kinachofanyika katika maeneo ya vyanzo
vya maji, kwenye vilele na miteremko mikali ya safu za milima; Matumizi mabaya ya dawa za kilimo,
mifugo na za viwandani; Kilimo cha umwagiliaji
kisichoendelevu; Matukio ya moto na uchomaji moto misitu; Uchimbaji madini
usioendelevu na mrundikano wa taka katika maeneo ya miji na makazi yetu.
Vilevile, wingi wa mifugo inayozidi uwezo wa malisho, husababisha upungufu wa
maji na malisho, hivyo kuchangia migongano baina ya wadau mbalimbali katika
matumizi ya ardhi.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Sote kwa pamoja tunao wajibu wa kutafuta ufumbuzi
wa kudumu wa matatizo haya, kila mmoja kwa nafasi yake. Yako mambo mengi ambayo
yanahitaji mikakati ya kudumu ili kuhakikisha kwamba shughuli za maendeleo ya
kiuchumi haziathiri mazingira. Mambo
haya ni pamoja na:-
i)
Kuhifadhi
ardhi na kupanda miti;
ii)
Kudhibiti
uchomaji moto ovyo;
iii)
Kuhifadhi
vyanzo vya maji, milima na misitu ya asili;
iv)
Kudhibiti
uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya makazi na viwandani;
v)
Ujenzi
na matumizi ya vyoo bora;
vi)
Kudhibiti
kilimo na uchimbaji madini usioendelevu;
vii)
Kudhibiti
matumizi mabaya ya dawa za mifugo na
kilimo;
viii)
Kuimarisha
vikundi vya usimamizi wa uvuvi;
ix)
Kuanzisha
au kuimarisha kamati za mazingira katika ngazi zote;
x)
Kusimamia
uzalishaji bora usiochafua mazingira kwenye viwanda vyetu; na
xi)
Kulinda
mazingira ya maeneo ya pwani, bahari, mito, maziwa na mabwawa.
Ndugu Wananchi;
Kazi ya kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya
mazingira, inahitaji juhudi za vyombo mbalimbali katika ngazi zote. Niombe
vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali na asasi za kiraia, tusaidiane katika
hili.
Hatuna budi kushirikiana ili kutekeleza
Sheria na Kanuni za hifadhi ya mazingira katika kila ngazi ya uongozi kote
nchini. Aidha, katika kila ngazi hizo, pawe na mipango ya matumizi bora ya ardhi; mikakati
bora ya kudhibiti uvuvi haramu na ufugaji usio endelevu. Wizara na taasisi
husika kwa kushirikiana na jamii yote, ziendeleze mafanikio yaliyokwishapatikana
kwa kusimamia ipasavyo Sheria na Kanuni zilizopo.
Aidha, Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti
iendelezwe na juhudi zielekezwe katika kuitunza na kuihudumia miti iliyopandwa.
Ningependa kusisitiza kwamba utamaduni tuliouanza wa kupanda miti, kutunza misitu
na uoto wa asili, tuuendeleze na kuudumisha. Nitumie fursa hii, kupongeza mikoa
iliyovuka malengo ya upandaji miti Milioni 1.5 kwa kipindi cha mwaka
2012/2013. Mikoa hiyo ni Kagera, Mbeya,
Njombe, Ruvuma, Iringa na Tanga.
Ndugu
Wananchi;
Katika Maadhimisho haya, tuzo zimetolewa kwa washindi wa ngazi ya Kitaifa, waliojitokeza
katika Mashindano ya Tuzo ya Rais ya Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Kupanda na
Kutunza Miti, ambayo hutolewa kila baada ya miaka miwili. Nitumie fursa hii,
kupongeza mikoa 17 iliyoshiriki katika mashindano haya. Mikoa hiyo ni:- Dodoma,
Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro,
Mwanza, Mtwara, Pwani, Ruvuma,
Shinyanga, Simiyu na Tanga. Natoa
wito kwa Mikoa ambayo haikushiriki, wahakikishe wanahamasisha wananchi wao
kushiriki mashindano haya.
Nitumie fursa hii kuwapongeze washindi wa Tuzo hii, kwa juhudi kubwa
walioifanya katika kuhifadhi vyanzo vya maji, kupanda na kutunza miti. Washindi
hawa wawe mfano wa kuigwa na jamii yote ya Watanzania. Vilevile, niwapongeze
wale wote waliojitokeza kushiriki mashindano haya, hata kama hawakuibuka
washindi, ujasiri mliouonesha ni kielelezo tosha kuwa ni wana mazingira nambari
moja. Natoa wito kwa wananchi kote
nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano ya Tuzo hii itakayotolewa tena
tarehe 5 Juni, 2016, Mwenyezi Mungu akitujalia uzima.
Ndugu
Wananchi;
Wageni
Waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, kwa mara
nyingine, napenda kuushukuru na kuupongeza
Uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa maandalizi mazuri ya Maadhimisho ya Siku ya
Mazingira nchini. Nizipongeze tena taasisi,
vikundi na watu binafsi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha maadhimisho haya.
Napenda niwakumbushe jambo moja muhimu sana, katika kufanikisha suala
zima la Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira yetu; Ili tufanikiwe katika jambo
hili; Lazima
tuifanye kila siku kuwa Siku ya Maadhimisho ya Mazingira Duniani. Tuchukue Hatua
Kutunza Mazingira yetu ili Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Mwisho kabisa, Kwa heshima kubwa na taadhima natamka kwamba; Maadhimisho ya Siku ya
Mazingira Duniani yamefikia Kilele.
Ahsanteni
sana kwa kunisikiliza.