Mzee Paulo Mawezi maarufu kama Matonya akiwa na mwanae Elizabath wakiwa katika Kijiiji cha Mpamantwa Tarafa ya Bahi Mkoani Dodoma. Picha hii ilipigwa 2010 wakati alipokwenda kwa mapumziko ya sikukuu ya Krismas. Picha na Maktaba
Habel Chidawali, Bahi
LICHA ya umaarufu mkubwa aliokuwa nao na kufahamika katika miji mingi nchini, ombaomba Paul Mawezi maarufu kwa jina la Mzee Matonya, amefariki dunia na kuzikwa katika mazingira ya ufukara mkubwa.
Matonya alizikwa jana kijijini kwake Mpamantwa, Wilaya ya Bahi, Dodoma akiwa amevishwa nguo moja nyeusi, huku mwili wake ukibebwa na watu wasiozidi 20, waliotumia ngozi kuu kuu ya ng’ombe.
Matonya aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kikohozi tangu Mei mwaka huu, alifariki dunia juzi usiku na kuzikwa jana saa saba mchana mita tatu kutoka katika nyumba yake ya tembe alimokuwa akiishi.
Ndugu na jamaa zake wa karibu walisema Matonya ambaye umri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 90, hakuwahi kwenda kutibiwa hospitali kutokana na ukosefu wa fedha.
Mwandishi wetu alishuhudia idadi ndogo ya waombolezaji nyumbani kwa Matonya, huku watoto wake watatu waliokuwapo msibani hapo kati ya watano aliowaacha hai, wakisema kuwa baba yao amefariki kutokana na umaskini na ufukara.
“Hatukuweza kumpeleka hata hospitali kupata vipimo kwani hatukuwa na uwezo wa kwenda mjini Dodoma kutokana na kukosa hata nauli, ndiyo maana tumekuwa kimya hadi Mungu alipomchukua,’’ alisema mmoja wa watoto hao, David Paulo.
Umaarufu wa Matonya
Umaarufu wa Matonya ulitokana na staili yake ya kuomba kwa kulala chali barabarani, huku akiwa ameinua kopo juu bila ya kujali jua au mvua.
Kwa nyakati tofauti alipinga mpango wa Serikali wa kumrejesha kwao Bahi na mara kadhaa alimweleza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusufu Makamba kuwa yeye ni mtoto wa mjini hivyo asingemuweza. Aliingia Dar es Salaam kwa mara ya kwanza Desemba 7, 1961.
Katika siku za karibuni, alikuwa gumzo kwa Serikali na viongozi huku akipachikwa jina la Komandoo na Kiboko ya Makamba.
Baada ya kuondolewa Dar es Salaam, aliweka makazi yake mapya ya kuomba mkoani Morogoro hususan eneo la Darajani, ambako aliendeleza staili ya kuomba akiwa amelala chali na kuinua kopo juu kwa muda mrefu bila kuchoka.
Iliwahi kuvuma kwamba ombaomba huyo alikuwa na utajiri mkubwa, jambo ambalo mtoto wake mkubwa, Elizabeth Paulo alilipinga na kusema kwamba halina ukweli na hakuacha chochote.
Mke wa Marehemu Paulina alisema walitengana na Matonya zaidi ya miaka 37 iliyopita na wakati huo alikuwa na mali nyingi (ng’ombe). “Tulipotengana tu, mimi nilirudi kwetu na watoto wangu walikuwa bado wadogo na bahati mbaya mdogo wake aliyekuwa akitunza ng’ombe (wa Matonya) alifariki dunia na huo ukawa ndiyo mwanzo wa kumaliza mifugo yote kwani watu waliwaiba wote,’’ alisema Paulina.
Matonya alirudi kijijini kwake Mpamantwa kwa ajili ya mapumziko ya Krismasi Novemba, 2010 akitokea Morogoro kama ilivyokuwa kawaida yake na tangu wakati huo hakurudi tena.
Makamba amlilia
Akizungumzia msiba huo, Makamba ambaye alifanikisha mpango wa kumwondoa Matonya Dar es Salaam, alisema amesikitishwa na kifo hicho cha mtu aliyemtaja kuwa alikuwa rafiki yake mkubwa
CHANZO: MWANANCHI