ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, September 20, 2019

AHADI YA RAIS MAGUFULI UJENZI WA JENGO LA ABIRIA UWANJA WA NDEGE MWANZA SASA RASMI YAANZA KUFANYIWA


Utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  aliyotoa mnamo tarehe 15 ya Mwezi July 2019, kuiagiza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutoa Sh2.2 bilioni na Manispaa ya Ilemela itoe Sh1.8 bilioni na kufanya jumla Sh4 bilioni kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, hatimaye agizo hilo limeanza kutekelezwa, kwani maandalizi ya awali kuelekea ujenzi wa jengo hilo umeanza mapema hii leo. 

Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella ametembelea eneo lililotengwa kwaajili ya  ujenzi wa jengo hilo la abiria kujiridhisha kwamba kazi imeanza au laa.

Jiunge nasi kushuhudia yaliyojiri.


MBUNGE MGIMWA KUSOMESHA WANAFUNZI KUANZIA KIDATO CHA TANO HADI CHUO KIKUU

Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa akivalishwa skafu na mmoja ya wanafunzi wa shule ya sekondari Ifwagi wakati alipotembelea shule hiyo
Afisa elimu sekondari wilaya ya Mufindi Musa Ally akiongea na wanafunzi wakati wa ziara ya Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa shuleni hapo
Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa akiongea na wanafunzi wa shule ya sekondari Ifwagi alipofanya ziara ya kikazi katika shule hiyo
Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa akiwa sambamba na afisa elimu sekondari wilaya ya Mufindi Musa Ally na mtendaji wa kata ya Ifwagi wakati wa ziara ya mbunge huyo katika shule hiyo

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Ifwagi iliyopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wametakiwa kufaulu kwa kiwango cha kupata daraja la kwanza ili waweze kupata fursa ya kupata ufadhili wa kusomeshwa na Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa.

Akizungumza wakati alipotembelea shuleni hapo Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa alisema kuwa mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza atamsomesha kwa kumlipia baadhi ya mahitaji muhimu kuanzia kidato cha tano hadi chuo kikuu.

“Mimi nipo tayari kuchangia baadhi ya mahitaji kwa wanafunzi watakao faulu vizuri katika mtihani wa mwisho wa kidato cha nne ambapo mnatarajia hivi karibuni mtafanya mtihani huo”alisema Mgimwa

Mgimwa alisema kufanya hivyo kutaongeza chachu ya wananfunzi kusoma kwa bidii na kuwa na ufaulu ambao utaleta maendeleo ya mwanafunzi na shule yenyewe hivyo mnatakiwa kusoma kwa bidii na kuzingatia masomo yenu ili mpate matokeo mazuri ya mtihani wa mwisho.

Aidha Mgimwa alisema kuwa anaendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenda mabweni katika shule mbalimbali za jimbo la Mufindi Kaskazini hivyo hata hapa Ifwagi tunaendelea na ujenzi wa bweni kwa lengo la kuhakikisha tunaboresha elimu na kukuza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hii.

“Nimechangia fedha nyingi kwenye bweni lenu hili ambalo ndio kwanza tumeanza hivyo mtuombee kwa mungu ili tukamilishe ndoto ya ujenzi wa bweni hili na wanafunzi mnatakiwa kudhamini mchangao wa wazazi,walimu,mbunge wenu na serikali kwa ujumla kwa juhudi ambazo zinafanywa kuleta maendeleo” alisema Mgimwa”

Mgimwa aliongeza kwa kusema kuwa katika shule ya sekondari ya Ifwagi amechangia katika ujenzi wa vyoo,bweni,uchimbaji wa kisima pamoja na kushughulikia maswala ya michezo hivyo rai yake kwa wanafunzi ni kuhakikisha wanasoma kwa bidii ili yapatikane matokeo mazuri.

Naye afisa elimu sekondari wilaya ya Mufindi Musa Ally alimpongeza mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini kwa juhudi anazozifanya kuhakikisha anaboresha sekta ya elimu kwa kuchangia kila mara kwenye shule zote zilizopo katika jimbo hilo.

“Huyu mbunge amekuwa msaada sana kwetu maana kila mara tukiomba msaada wowote unahusu elimu amekuwa akitusaidia kwa hali na mali ni tofauti na wabunge wengine hivyo mnapaswa hata kuwaambia wazazi wenu mchango wa mbunge huyu kwenye sekta ya elimu” alisema Ally

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo ya sekondari ya Ifwagi walimpogeza mbunge huyo na kumuomba aendelee kuwasaidia kuboresha elimu kwa kuwa elimu ndi msingi mkuu wa maisha ya mwanadamu

TANZANIA INAVYOPAMBANA NA NJAA ILIYOFICHIKA.

Proteinquellen (Colourbox)
Wataalamu wa masuala ya lishe wanaeleza njaa iliojificha kuwa ni kula chakula na kushiba huku mwili ukiwa haujavuna vya kutosha madini, protini na hata vitamin, hali inayopelekea mwili kuzongwa na maradhi mbalimbali.

Mataifa yanayoendelea yamekuwa yakikabiliwa kwa kiasi kikubwa na matatizo ya lishe kutokana na wananchi wengi kutokuwa na elimu ya kutosha na sahihi juu ya lishe bora katika familia zao, hali inayoathiri kasi ya juhudi za kupambana na njaa iliojificha.
Tanzania  ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na tatizo hilo kwa watu wake hasa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wanawake walio katika rika la kuzaa.
 Utafiti wa wa afya na viashiria vya malaria wa mwaka 2015/16 unaonesha kuwa upungufu wa damu kwa watoto walio na umri wa miezi 6 hadi 59 ni asilimia 58 huku asilimia 2 wakiwa na upungufu wa juu wa damu, asilimia 30 wakiwa na upungufu wa kati na asilimia 26 wakikabiliwa na upungufu wa damu wa kawaida.
Utafiti huo unaonyesha kuwa mkoa wa Shinyanga ndiyo umeathirika zaidi ambapo wastani wa asilimia 71 ya watoto wana tatizo la upungufu wa damu.
Bado utafiti huo unaonyesha kuwa miongoni mwa wanawake walio katika rika la kuzaa la umri wa kuanzia miaka 15-49 asilimia 45 wana tatizo la upungufu wa damu ambapo asilimia 1 wana upungufu wa damu wa juu, asilimia 11 wana upungufu wa damu wa kati na asilimia 33 wakiwa na upungufu wa damu kawaida.
Tansania Jackfruits-Verkäufer in Dar es Salaam (DW/S. Khamis )
Fenesi ni tunda lenye manufaa makubwa katika mwili wa mwanadamu.
Udumavu na utapiamlo kwa dhana ya kitabibu
Wataalamu wa masuala ya lishe waliiambia DW kuwa udumavu ni matokeo ya  utapiamlo mkali unaotokana na mtoto kukosa lishe bora katika kipindi cha siku elfu moja tangu kutungwa kwa mimba.
Hivyo mtu huwa na uzito usioendana na umri wake, katika makala hii Ruthy Mkopi, afisa mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe nchini Tanzania (TFNC) anasema mapambano dhidi ya udumavu laazima yaanze katika siku 1000 za kwanza za binadamu.
"Hizi tunazihesabu tangu kutungwa kwa mimba ambapo hapa mama anatakiwa ale chakula kwa uwiano sawa katika kila kundi la  chakula, kwa maana ya mikunde, asili ya wanyama, mbogamboga, sukari, mafuta pamoja na matunda", alisema mkopi na kuongeza kuwa, "akila kwa mgawanyiko sahihi itasaidia kwa kiwango kikubwa kupata mtoto ambae hajadumaa."
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema utapiamlo ambao matokeo yake ni udumavu hutokana na kutokuwa na usawa katika kiwango cha chakula kinachompa mtu virutubisho mwilini.
Hali hii hutokea kwenye makundi mawili; kwanza kutokuwa na lishe ya kutosha ambako kunajumuisha kudumaa, kuwa  na uzito mdogo usioendana na umri pamoja na kukosa virutubisho vya kutosha.
Pili ni kula vyakula vinavyoleta  unene uliopitiliza na magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha. Na hali hii huwapata zaidi watoto na watu wenye kipato kizuri waishio mjini.
Mkopi anasema "kaya nyingi hasa za mjini zina utamaduni wa kula vyakula vya jamii ya wanga ambavyo ni kama  ugali wa mtama, mahindi, na muhogo na wali, huku akibadilisha mboga peke yake lakini anakuwa amekula chakula cha jamii ya aina moja pekee yake kwa siku nzima”
Simbabwe Kartoffelverkäuferin in Harare UN FAO Hunger und Biosprit (AP)
Mwanamke akiuza viazi.
 Hali ilivyo ndani ya kaya
Katika familia nyingi linalotazamwa ni kula na kila mwanafamilia ashibe kwa kiwango chake pamoja na urahisi wa upatikanaji wa chakula katika jamii husika, ndani ya familia nyingi wanawake walio katika umri wa kuzaa na watoto walio chini ya miaka mitano ndio wanaathirika zaidi na tatizo hili linalotajwa na wataalamu njaa ilio jificha.
Mkazi wa jijini dar  es salaam Siwema Shukuru (33) amezaa watoto wawili na walikumbwa na tatizo la udumavu. Anasema haamini suala la chakula kama linaweza kusababisha mtoto wake mwenye miezi 22, anaeanza kutambaa ashindwe kukua kama watoto wengine walio katika umri wake ambao kwa kawaida wameanza kuzungumza, kukimbia huku na kule kwa kujifunza na hata utundu wenye kugundua zaidi.
"Ni mtoto wangu wa pili wa kwanza alifariki kwa tatizo la upungufu wa damu, sitaki kuamini kama chakula kinasababisha, sababu asubuhi nampa uji wa mahindi ikifika mchana tunakula ugali usiku kwenye saa nne tunakula kama ni wali ama ugali, yeye nilimuachisha kunyonya tangu alipotimiza mwaka mmoja,” anasema siwema.
Hali ya siwema inatajwa na wataalamu kuwaathiri zaidi wanawake walio vijijini ambao wao kwa kiasi kikubwa ndio wanatazamwa kama wazalisaji ndani ya familia, hivyo muda mwingi huwaacha watoto wao wakiwa na kaka ama dada zao na wakati mwingine bibi ama babu zao, ambao huwaachia kama ni viazi au uji hushindia huo hadi nyakati za jioni wanaporejea nyumbani na kuandaa chakula kingine ambacho hakina tofauti katika virutubishi kama walichokula mchana.
Tafiti zinahitaji jitihada zaidi kumaliza tatizo la njaa iliojificha
Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Kim, katika mkutano wake na mawaziri wa fedha kutoka mataifa mbalimbgali uliofanyika mwaka 2016 nchini Marekani alisema kuwa, asilimia 43 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanaokadiriwa kufikia milioni 250 katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati wamedumaa.
Master zum Themenheader Kann Afrika den Hunger stillen? (AFP/Getty Images)
Viazi vitamu vikivunwa shambani.
Alisema watoto hao wanakabiliwa na utapiamlo mkali, unaosababishwa  na umasikini pamoja na ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa kupata lishe bora kwa wanawake na watoto, hasa walio chini ya umri wa miaka mitano.
Kwa nchini Tanzania  utafiti uliofanywa na taasisi ya lishe (TFNC) kwa kushirikiana na ofisi ya taifa ya takwimu (NBS) kuhusu afya na viashiria vya malaria wa mwaka 2015-2016  unaonesha kuwa tatizo la udumavu linakabili zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa na watoto chini ya miaka mitano.
Utafiti huo unaonesha kuwa mkoa wa Rukwa unaongoza kuwa na watoto wengi wenye udumavu kwa kiwango cha asilimia 56 ukifuatiwa na mkoa wa Njombe kwa asilimia 49, Ruvuma asilimia 41, Iringa asilimia 42 na Kagera 42.
Kiuhalisia mikoa hii kwa nchini humo ndio inayoongoza kwa uzalisaji wa chakula hata hivyo ndio inayoonoza kuwa na kiwango cha juu kuwa na hali ya udumavu.
Mkopi anasema matokeo ya utafiti huo yanadhihirisha bado kuna kazi kubwa ya kupambana na  changamoto ya lishe duni inayosababisha  udumavu, uzito pungufu, upungufu wa damu na ukondefu.
Mapambano dhidi ya  njaa iliojificha.
Tatizo la udumavu katika nchi linawaleta pamoja wadau wa masuala ya lishe kwa kuweka mipano na mikakati inayoweza kutekelezeka kuanzia katika ngazi ya familia ili kuepuka udumavu na kutokomeza njaa iliojificha katika kaya.
Meneja wa mradi wa kapu lishe unaoonozwa na kituo ca kimataifa cha viazi lishe (CIP), Hilda Munyua  anasema  tafiti zimewafanya kuingia katika mradi huo ili kupambana na udumavu kwa uwiano sawa wa mijini na vijijini, ambapo wakulima wananweza kupanda mbegu zilizo na virutubiso vinavyohitajika mwilini.
"Mama akikosa afya bora atapata watoto walio na afya dhoofu, lakini na mtoto anapopata udumavu inakuwa ni Athari kubwa sababu ubongo wake unakuwa haujakomaa vilivyo anakuwa na uwelewa duni, sababu ya udumavu na unaweza ukaongea nae anakuangalia tu hata darasani hataweza kufanya vizuri.
Südsudan Hunger Symbolbild (Getty Images/AFP/A. Gonzales Farran)
Utapiamlo na udumavu ni matatizo yanayoikabili Tanzania.
"Katika mradi wetu tunasisitiza wakulima kuwa na mbegu zenye virutubiso vya kutosa sababu atapanda na atakula atauza chakula bora na wengine watapata pia, hii itasaidia kupambana na njaa iliojificha.”
Hata hivyo katika vituo vya afya kwa mijini hali inaonekana kuwa ni nzuri sababu wahudumu wamekuwa wakitoa darasa la lishe bora kwa wananwake wajawazito na watoto hatua ambayo imeleta mapinduzi makubwa katika lishe kwa wanawake na watoto.
Chiku Saalim ambae mwanae ana mwaka mmoja na nusu ameiambia DW kuwa "lishe kwa mtoto wangu ni jambo la kwanza sababu najua akipata maradhi sitaweza kufanya lolote, sitaweza kufanya kazi kumpatia mahitaji yake, atakumbwa na maradhi huku baya zaidi ikiwa ni udumavu,” alisema Chiku na kuongeza kuwa;
"Nimeweka utaratibu maalum wa chakula cha mwanangu, kwa mfano Jumatatu asubuhi akiamka, namlisha uji wa lishe, kisha analala tena, ikifika mchana nampatia parachichi, ndizi, na kiini cha yai la kienyeji ambavyo nakuwa nimeviandaa na kuvisaga kwa pamoja.
"Lakini inapofika  sisi (watu wazima) tunapokula chakula cha mchana unakuta na yeye analilia, basi namlisha japo kidogo, si sana…inapofika saa kumi jioni huwa tayari nimemuandalia chakula cha maharage au choroko ambacho huchanganywa kwa nazi au karanga na kusagwa kwa pamoja,” anasema.
Chiku anasema pamoja na hayo bado huzingatia kuhakikisha anamnyonyesha mwanawe ipasavyo na kumpatia maji ya kunywa ambayo anakuwa ameyachemsha yeye mwenyewe na kuyahifadhi vizuri nyumbani.
Maazimio ya serikali kumaliza njaa iliojificha.
Katika gazeti la mtandao la wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia, wazee na watoto naibu waziri Dokta Faustine Ndugulile anasema: "Zaidi ya asilimia 35 ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano nchini vinachangiwa na matatizo ya lishe duni na katika kipindi cha mwaka 1992 hadi 2015/16 vimepungua kutoka 149 hadi 67 kwa kila vizazi hai 1000.
Hawkers of boiled maize in Tanzania at work (DW/S. Khamis)
Mahindi ni chakula chenye wanga kwa wingi.
"Udumavu umepungua kutoka asilimia 49.7 hadi 34.4 kwa upande wa ukondefu (uzito kwa urefu) kutoka asilimia 7.8 hadi 4.5  kwa upande wa uzito pungufu (uzito kwa umri)  kutoka asilimia 25.1 hadi 13.7. Vilevile mwanamke 1 kati ya 10 ana uzito pungufu wakati asilimia 18 wana uzito mkubwa na asilimia 10 wanakiribatumbo.”
Naibu waziri Huyo aliahidi kuwa watajipanga katika kutoa elimu ya afya kwa umma na kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kumaliza tatizo la udumavu.
Nini kifanyike kupambana na njaa iliojificha?
Shabaha ya shirika la afya duniani WHO ifikapo mwaka 2025 ni kwa kupunuguza kwa idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano waliodumaa kwa nchini Tanzania kwa asilimia 40. Hivyo ni muhimu kwa jamii ya Watanzania kuzingatia lishe bora kwa watoto, wajawazito na  wanawake walio katika rika la kuzaa.
Jean Claude Robyongo, mkuruenzi wa shirika la mbegu la kimataifa la CIAT anasema "lazima jamii ione umuimu wa afya zao na watoto, ambao ni tafa la kesho kwa kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anajiuliza alichokula kinakwenda kutengeneza nini au kinaboresha nini katika mwili wake na watoto wake, tukiwa na utamaduni huo hata walimu shuleni hawatapata tabu kubwa kusomesha watoto wetu.
"Utamaduni huo utasaidia pia watoto watakapokuwa watu wazima kuendeleza katika familia zao, lakini tunajikumbusha kuwa chakula ni tiba tunakula ili kuifanya miili yetu iwe na nguvu, tuweze kufikiri na kutoa maamuzi mazuri na  tuwe na afya njema, tukielewa kwa pamoja tutaacha kula sababu ya kushiba.”
Mwandishi: Hawa Bihoga
Mhariri: Iddi Ssessanga

ROCK CITY MARATHON 2019 YAJA KITALII ZAIDI


Huu ni msimu wa kumi wa mbio hizo za Rock City Marathon ambazo zimekuwa na mwitikio mkubwa,na mwaka huu inataraji kuwa na washiriki zaidi ya elfu tatu ambapo zaidi ya shilingi Milioni 30 kushindaniwa.
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Dr. Phillis Nyimbi ameongoza wadau wa michezo katika uzinduzi wa zoezi la uchukuaji fomu za kujiandikisha kushiriki mbio hizo za kimataifa ambazo kwa mwaka huu 2019 zinatarajiwa kuja na moto zaidi kutokana na hamasa na jinsi wawezeshaji walivyojipanga.


Thursday, September 19, 2019

BAADA YA MIAKA 50 WANAFUNZI WALIOSOMA MWANZA SEKONDARI WAREJEA NA ZAWADI YA UWANJA WA MICHEZO


KATIKA kukabiliana na upotevu wa vipaji vya mchezo wa mpira wa kikapu mkoani Mwanza, wadau mbalimbali wametakiwa kujenga viwanja vya michezo, ili kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji hivyo kwa maslahi ya Taifa.

Ushauri huo umetolewa na mlezi wa chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Mwanza (MRBA) Altaf Mansoor, baada ya uzinduzi wa uwanja wa mpira wa kikapu wa shule ya sekondari Mwanza, uliojengwa na wanafunzi waliohitimu katika shule hiyo yapata miaka 50 iliyopita yaani mwaka 1968.

Uwanja huo umejengwa na wahitimu hao kwa kushirikiana na Kampuni ya Moil, baada ya mkoa wa Mwanza kuyumba katika medani ya mpira wa kikapu, kufuatia timu zilizokuwa zikitamba miaka hiyo kukosa uelekeo, ili kuangalia namna ya kuzijenga.

Wednesday, September 18, 2019

MBUNGE MGIMWA KUTATUA TATIZO LA BARABARA YA MTILI,IFWAGI,LULANDA MPAKA MPANGATAZARA

 Mbunge wa jimbo la Mufindi kaskazini Mahmoud Mgimwa akiongea wa kijiji cha Ibwanzi kilichopo kata ya Ihanu akielezea jinsi ya kutatua changamoto ya barabara kwa kuwa ashapata fedha za kutatulia kero hiyo inayokwamisha maendeleo ya tarafa ya Ifwagi. 
 Mbunge wa jimbo la Mufindi kaskazini Mahmoud Mgimwa akiwa anakagua barabara ya kutoka Mtili hadi Mpangatazara
Kaimu meneja wa TARURA wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Injinia Selemani Mjohi akielezea jinsi ambazo watatengeneza barabara ya Mtili hadi Mpangatazara
Mbunge wa jimbo la Mufindi kaskazini Mahmoud Mgimwa akimuonyesha Kaimu meneja wa TARURA wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Injinia Selemani Mjohi ubovu wa daraja la Nandala

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.


Mbunge wa jimbo la Mufindi kaskazini kutatua changamoto ya barabara kwa wananchi wa tarafa ya Ifwagi kuanzia mwezi wa kumi mwaka huu kwa kuwa changamoto hiyo imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo kwa wananchi wa tarafa hiyo.

Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara ya kata za Mpangatazara,Ihanu na Ifwagi mbunge Mahmoud Mgimwa alisema kuwa changamoto ya barabara imekuwa kero kwa kurudisha nyuma juhudi za maendeleo ya wananchi wa tarafa ya Iwagi.

“Kweli hata mimi nimekuwa nikiiona changamoto hii na imekuwa inaninyima usingizi mara kwa mara kwa kuwa inakwamisha maendeleo ya wananchi kwa kuwa shughuli nyingi za kimaendelo zimekuwa zinategemea barabara kwa kiasi kikubwa” alisema Mgimwa

Mgimwa alisema kuwa wamepata kiasia cha shilingi milioni mia tisa ishirini na moja kwa ajili ya kutengeneza barabara ya kutoka Mtili,Ifwagi,Lulanda hadi Mpangatazara kwa kiwango cha changarawe ili kutatua tatizo hilo kwa muda mrefu.

“Jamani msione nilikuwa sionekani wala siji kwenye mikutano ya hadhara kwa sasbabu barabara hii ilikuwa inaniumiza kichwa ila kwa sasa nakuja kifua mbele na kiburi kwa kuwa tayari fedha nimetafuta na nimewapa hawa TARURA kwa ajili ya kutengeneza barabara hii” alisema Mgimwa

Mgimwa alisema kuwa barabara hiyo itatengenezwa kwa kiwango bora ambacho kinaweza kudumu kwa miaka mitano bili kuharibia kwa kiasi kikubwa bali kutakuwa na matengenezo madogo madogo ambayo hayaepukiki.

Aidha Mgimwa amewataka wananchi ambao wanapitiwa na barabara hiyo kuakikisha kuwa barabara hiyo inatengenezwa kwa kiwango kulingana na gharama ambazo wamezitoa kwa kuwa fedha inayotumika hapo ni kodi ya wananchi na wao ndio wenye mali hiyo.

“Barabara hii ikianza kutengenezwa ni jukumu letu sote kuhakikisha inatengenezwa kulingana na michoro iliyopo kwa mujibu wa mkataba la sivyo wasiipokee barabara hiyo ikikamili,mkipokea barabara ambayo ipo chini ya kiwango hilo litakuwa sio jukumu langu kwa kuwa wajibu wa kutafuta fedha mimi kama mbunge nimeshalifanya” alisema Mgimwa

Kwa upande wake kaimu meneja wa TARURA wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Injinia Selemani Mjohi alikiri kwenye mikutano ya hadhara kupokea fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe.

“Ni kweli mbunge wenu ametafuta fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara hii milioni mia tisa ishirini na moja na tayari zipo benk kwenye akaunti zetu na tunarajia kuanza kuzitumia hivi karibu kwa lengo la kutatua changamoto hii ambao imekuwa kero kwenu” alisema Mjohi

Mjohi aliongeza kuwa tayari walishatangaza zabuni na wameshawapata wakandarasi wawili ambao watahusika kutengeneza barabara hiyo kwa kuwagawana kimeta ambazo zipo kwenye barabara hiyo.

“Niwatoe hofu kuwa wakandarasi wataanza kazi mapema mwezi wa kumi mwaka huu kutengeneza barabara yetu kwa kuwa mwezi huu watasaini mikataba ya kuanza kazi na watapita kila kijiji kutoa taarifa kuwa wanaanza kazi ya ujenzi wa barabara hizo” alisema Mjohi

Mjohi aliungana na mbunge wa jimbo hilo Mahmoud Mgimwa kwa kuwataka wananchi kusimamia utengenezwaji wa barabara hiyo kulingana na michoro watakayo pelekewa ili kuhakikisha ubora wa kutengeza barabara hiyo unazingatiwa na ni jukumu lao.

“Nao baadhi ya wananchi walimpongeza mbunge huyo kwa juhudi anazozifanya kuhakikisha analeta maendeleo kwenye jimbo hilo na kusema kuwa wanamshukuru endapo barabara hizo zitakamilika kutengenezwa” walisema wananchi

MBWANA SAMATTA AWEKA REKODI UEFANi mechi ambayo Mbwana Samatta hataisahau maishani mwake kwa mambo matatu kuwa mtanzania wa kwanza kucheza European Champions League na pia kufunga goli katika mechi yake ya kwanza ya UEFA CL.

Matokeo ya 6-2 dhidi ya Salzburg hayakuwa mazuri lakini Samatta ameandika rekodi binafsi na za kitaifa. Mtanzania gani mwingine anaelekea huko alifika Samatta?.

Pia katika mchezo huo Samatta alionyeshwa kadi nyekundu kabla referee hajaenda kuangalia tukio hilo upya ili kujiridhisha kupitia teknolojia mpya ya VAR ambayo ilimuonyesha haikua straight red card badala yake aliibadi na kumpa kadi ya njano

MAJALIWA AJITAPA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA AHADI ZITE ZA RAIS MAGUFULI.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli ikiwemo ujenzi wa barabara ya Mikumi-Ifakara kwa kiwango cha lami zitatekelezwa, hivyo amewataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao.


Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Mji wa Ifakara pamoja na wilaya ya Kilosa alipokuwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

“Kila alichokiahidi Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli nitakisimamia kuhakikisha kinatekelezwa, hivyo wananchi endeleeni kuiamini Serikali yenu. Serikali yenu ipo makini na ina dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inavyoelekeza.”

Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli iko makini na inaendelea kuchapa kazi kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na mkoa wa Morogoro.

Pia, Waziri Mkuu alisema kila mtumishi wa umma anatakiwa ahakikishe anafanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kuboresha maendeleo ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani ya vijijini.

Waziri Mkuu alisema iwapo watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji zitakuwa historia kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Alisema watumishi wa umma wanapaswa kuwa na nidhamu ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika maeneo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ya afya, elimu na maji. “ Sina mzaha na watakaotafuna fedha hizo.”

MWENYEKITI WA HALMASHAURI WILAYA YA TARIME AGONGA HODI TAMISEMI


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoani Mara Moses Misiwa amehoji suala la Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019-2020 iliyotolewa na Tamisemi kwa nini imetoa fedha nyingi kwa uendeshaji wa halmashauri kuliko fedha za maendeleo kwa wananchi kama ilivyokuwa miaka kabla tokea uchaguzi wa 2015.

Tuesday, September 17, 2019

MBWANA SAMATTA AWA MTANZANIA WA KWANZA KUCHEZA UEFA


Leo usiku timu ya Genk anayocheza Mtanzania, Mbwanna Ally Samatta wataanza kucheza mechi ya kwanza kwenye UEFA dhidi ya Salzburg.

Nyota wa Kitanzania na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayekipiga na klabu ya Genk anapata mafanikio makubwa kama Mtanzania kucheza Ligi ya Mabigwa Ulaya.

Samatta akiwa kinara wa mabao msimu uliopita ndani ya Genk aliiwezesha klabu yake kupata nafasi ya kushiriki Uefa Champions League, baada ya Genk kunyanyua kombe la ligi kuu Ubelgiji, hii ni mara ya kwanza Genk kushiriki bila kupitia hatua ya mtoano.

Lakini taarifa mbaya ni kwamba, kunauwezekano wa Samatta kukosa mchezo wa leo dhidi ya Salzburg, kutokana na majeraha ya goti aliyopata kwenye mechi ya Tanzania dhidi ya Burundi kufuzu Kombe La Dunia

Monday, September 16, 2019

UZINDUZI WA RADA MBILI ZA KUONGOZEA NDEGE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli azindua Rada mbili (2) za kuongozea ndege za Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanajaro (KIA). Hafla inayofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam .

Sunday, September 15, 2019

DUH..! MRADI WA MAJI ULIOSHINDWA KUKAMILIKA MIAKA SABA WAKAMILIKA NDANI YA MIEZI MIWILI


Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa (Mb) amezipa mamlaka za maji zinazotumia bei za kukadiria (flat rates) miezi mitatu kuhakikisha wateja wote wamefungiwa dira za maji ili kila mteja alipe gaharama ya maji kwa kiasi alichotumia. Pia ameziagiza mamalaka za maji za mikoa kuhakikisha wanadhibiti upotevu wa maji na kuongeza mtandao wa maji ili kujiongezea mapato.

Profesa Mabarawa ametoa maagizo hayo Jumamosi ya tarehe 14 Septemba 2019 alipokuwa akizinduzi wa mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima kata ya Kikubiji, Wilayani Kwimba Mkoa wa Mwanza.

Hii ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Vijiji vya Shilima, Mhande na Izizimba. 
Mradi wa maji wa Shilima ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na ulitakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita. Hata hivyo, kutokana na udhaifu wa Mkandarasi pamoja na usimamizi mbaya haukuweza kukamilika.

Waziri Mbarawa tarehe 3 Julai, 2019 akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Kwimba alitoa ahadi ya kukamilisha mradi huo kwa kutumia wataalamu wa ndani kwa kuhakikisha wananchi wa Kijiji cha Shilima wanapata maji katika kipindi cha miezi miwili, yaani hadi kufikia tarehe 3 Septemba, 2019, ahadi ambayo ilikamilika tarehe 25 Agosti, 2019 siku tisa kabla ya tarehe ya makubaliano.

Wakati akisoma taarifa ya Mradi, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kwimba Mhandisi Boaz Matundalo amesema kuwa, Kijiji cha Shilima kina wakazi wapatao 7,526 ambapo mradi huu wenye magati 35 una uwezo wa kuhudumia wakazi 8.750 ikiwa ni wastani wa watu 250 kwa kila gati.

Mradi wa maji wa Shilima umetekelezwa na wataalamu wa ndani kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA)

TAHARUKI: KUNDI LA TEMBO LAVAMIA MAKAO MAKUU YA JIMBO LA WAZIRI MPINA/ WANANCHI WAPAZA SAUTI

KUNDI la Tembo kutoka Pori la Akiba la Maswa (Maswa Game Reserve) lililoko wilayani Meatu mkoani Simiyu limevamia Makao Makuu ya Jimbo la Kisesa mji wa Mwandoya na kuzua taharuki kubwa kwa wananchi wa eneo hilo.

Kundi hilo la Tembo wapatao 34 waliingia katikati ya Kijiji cha Mwandoya ambako shughuli za kiuchumi na kijamii zilisimama kwa muda kufuatia taharuki hiyo huku wananchi wa eneo hilo wakiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kuzuia tembo hao wasifike kwenye makazi ya watu kwani ni wanyama wakali wanaweza kuleta madhara makubwa kwa binadamu na uharibifu wa mali.


Pia Wananchi hao wameshukuru Mbunge wa Jimbo hilo, Mheshimiwa Luhaga Mpina kwa hatua aliyochukua ya kuanzisha operesheni ya kuwafukuza tembo hao inayoendeshwa na vijana wa jimbo hilo wakishirikiana na Askari wa Pori la Akiba la Maswa ili kupunguza madhara yatokanayo na wanyama hao

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwandoya Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu, Kibona Jackson Bujoma amesema kundi hilo la tembo lilizua taharuki kubwa na kushukuru kikosi cha doria kilichoundwa Mhe Mpina kuwezesha kuwafukuza tembo hao na kuwarejesha hifadhini bila kuleta madhara kwa wananchi.

Kibona alisema pia tayari Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Mpina ameshaunda vikundi vya vijana sita kutoka kila kijiji kiichopo kando ya hifadhi hiyo ambapo watakuwa wanashirikiana kufukuza tembo na askari wa Pori la Akiba la Maswa

PROFESA MBARAWA AZIAGIZA MAMLAKA ZA MAJI NCHINI


  Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akikata utepe kuzindua rasmi mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima, Kata ya Kikubiji, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza.
 Baadhi ya wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi wa mradi wa maji wa Shilima
 Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) (mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa maji Shilima.

Mamlaka za maji zinazotumia bei za kukadiria (flat rates) kote nchini zimepewa miezi mitatu kuhakikisha zinawafungia dira za maji wateja wao wote ili kila mteja alipe gharama ya maji kwa kiasi alichotumia.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa (Mb) alitoa agizo hilo Septemba 14, 2019 alipokuwa akizindua mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima Kata ya Kikubiji, Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza. 

Waziri Mbarawa alisema Serikali imetenga Bilioni moja kusaidia mamlaka za maji ambazo hukadiria matumizi ya maji wateja wake badala ya kutumia dira ya maji ili kuepuka kumbebesha mteja mzigo usiyo kuwa wake. 

Waziri Mbarawa vilevile ameziagiza mamlaka za maji za mikoa kuhakikisha zinadhibiti upotevu wa maji kwani maji mengi yanapotea kabla ya kufika kwa wananchi sambamba na kuongeza mtandao wa maji ili kuwaunganisha wananchi wengi zaidi.

Akizungumzia mradi wa maji wa Shilima, Profesa Mbarawa alisema ujenzi wake ni utekelezaji wa Sera ya Maji pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayoelekeza kuwapatia  huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85 wakazi wote waishio vijijini ifikapo mwaka 2020.

Aliongeza kuwa uzinduzi wa mradi huo ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Vijiji vya Shilima, Mhande na Izizimba.

Alibainisha kwamba mradi wa maji wa Shilima ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na ulitakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita. Hata hivyo, kutokana na udhaifu wa Mkandarasi aliyekuwa anautekeleza pamoja na usimamizi mbovu haukuweza kukamilika kwa wakati. 

Waziri Mbarawa aliwapongeza wote walioshiriki kwenye ujenzi wa mradi kwa namna mbalimbali na kwa ushirikiano waliotoa kwa kipindi chote cha ujenzi wake hadi unakamilika kwa wakati kama alivyokuwa ameelekeza.

Akizungumzia ujenzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa ujenzi, Mhandisi Anthony Sanga alisema walizingatia agizo la Waziri Mbarawa na kwamba mradi huo ulikamilka tarehe 25 Agosti, 2019 kabla ya muda uliyokuwa umeelekezwa.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kwimba, Mhandisi Boaz Matundalo alisema kuwa Kijiji cha Shilima kina wakazi wapatao 7,526 ambapo mradi huu wenye magati 35 una uwezo wa kuhudumia wakazi 8.750 ikiwa ni wastani wa watu 250 kwa kila gati.

Waziri Mbarawa tarehe 3 Julai, 2019 akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Kwimba alitoa ahadi ya kukamilisha mradi huo kwa kutumia wataalamu wa ndani kwa kuhakikisha wananchi wa Kijiji cha Shilima wanapata maji katika kipindi cha miezi miwili, yaani hadi kufikia tarehe 3 Septemba, 2019, ahadi ambayo hata hivyo ilikamilika tarehe 25 Agosti, 2019 siku tisa kabla ya tarehe ya makubaliano.

MWAKYEMBE AWAPA 5 WAZEE WA KIMASAI KWA KUDUMISHA MILA.


Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amepongeza wazee na viongozi wa kimila wa kabila la kimasai kwa kuendeleza na kuhifadhi mila na desturi.

Hayo ameyasema leo Ngaramtoni, Jijini Arusha wakati wa kufunga mafunzo ya kimila kwa vijana wa kimasai na kueleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kumjenga kijana kuwa mtu mwenye maadili na kuheshimika kwa jamii yake.

“Mafunzo haya mliyoyapata kutoka kwa viongozi wenu na Wazee wa kimila yanawajenga kuwa rai wema na wenye maadili katika kujenga taifa letu ” Dkt. Mwakyembe

Aidha aliongeza kwa kueleza kuwa Wizara inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Wazee wa Kimasai kwa kuhakikisha mila na desturi ya mtanzania inatunzwa na kuendelezwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Pia Dkt. Mwakyembe ameahidi kushirikiana kwa karibu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi katika kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za mila yanahifadhiwa vizuri bila kuingiliwa na watu.

Vilevile aliwapongeza viongozi wa Jeshi la Tanzania kwa kuruhusu maeneo ya kijeshi ambayo ni ya kihistoria kuendelea kutumika ajili ya masuala ya kimila na kuzitaka taasi nyingine ambazo zina maeneo hayo kuiga mfano huo .

AZAM FC YAKUNG'UTWA NYUMBANI - KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA.

Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Triangle United wamepoteza kwa kukubali kufungwa goli 1 kwa bila.

Bao pekee la Triangel United ya Zimbabwe lilifungwa dakika ya 34 na Ralph Kawondera kutokana na uzembe wa safu ya ulinzi wa Azam FC.

Licha ya Azam FC kupewa sapoti kubwa na mashabiki waliojitokeza uwanja wa Azam Complex hayakuzaa matunda kwani safu ya ulinzi ya Triangle United ilikuwa ngumu na ikajilinda na hatari zote.

Sasa Azam FC ina kazi nzito ya kwenda kutafuta matokeo ugenini kwenye mchezo wa marudiano unaoatarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 27-29 nchini Zimbabwe.

HUYU NDIYE ANSSUMANE FATI - KINDA WA KATALUNYA.

Anssumane Fati ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka 16, alizaliwa tarehe 31 October 2002 kule nchini Guinea-Bissau, alijiunga na academy ya Barcelona (La Masia) mwaka 2012.

Mtoto ana balaa kubwa sana huyu ni ingizo moja matata sana ndani ya kikosi cha Barcelona akitokea La Masia.

Jana amepiga goli moja dakika ya pili tu na kutoa pasi kwa Frankie de Jong iliyozaa goli la pili dakika ya saba wakati Barcelona ikiwaangamiza Valencia 5-2 ndani ya Camp Nou.

Ni mtu mwenye kasi, anaweza kumiliki mpira, anapiga mashuti, akiingia kwenye box anakuwa mwiba mkali zaidi. Ni mchezaji wa viwango sana, kama atajitunza na kulinda kipaji na kiwango chake Anssumane Fati anaweza kuja kuwa moja ya wachezaji wakubwa sana ambao majina yao yataimbwa na wazungu muda wote.
Shida sasa wale watu weupe ambao Salamba aliwaomba viatu (utani) tayari wamemshawishi abadilishe uraia wake na muda wowote anaweza kuwa Mhispania. Wakati huo huo wakoloni wa zamani wa Guinea-Bissau Taifa la Ureno nao wameonyesha nia ya kutaka kumshawishi Anssu abadilishe uraia wake na kuchezea timu ya vijana ya nchi hiyo.

Kwa upande wake Anssu yuko tayari kubadilisha uraia na kuwa raia wa Hispania na kama atafanikiwa basi ataanza kukitumikia kikosi cha Hispania katika fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 nchini Brazil kuanzia tarehe 26 October mpaka tarehe 17 November 2019.

Anssumane Fati mpaka sasa hajachezea timu ya Taifa lolote hivyo anayo nafasi ya kuchagua ni Taifa gani alitumikie kati ya mataifa matatu ya Guinea Bissau (taifa ambalo amezaliwa), Ureno (taifa lililotawala Guinea Bissau enzi za ukoloni) na Hispania (taifa ambalo ameishi tangu akiwa na miaka 6).

Anssumane Fati anakuwa mchezaji kijana mdogo zaidi wa pili katika historia ya Barcelona kuingia kwenye kikosi cha wababe hao wa Katalunya wa kwanza alikuwa ni Vicenç Martínez mwaka 1941, yeye alianza kuichezea Barcelona mechi ya kwanza akiwa na miaka 16 na siku 280 huku Anssu yeye akiichezea Barcelona mechi ya kwanza ya Laliga akiwa na miaka 16 na siku 298.

Fati ndiye mchezaji kinda zaidi ambaye amecheza mechi katika Ligi Kuu ya Hispania Laliga na kufunga goli la mapema zaidi dakka ya 2 na kutoa pasi ya goli dakka ya 7 katika mechi moja. Amefanya hivyo kwenye mchezo kati ya Barcelona dhidi ya Valencia tarehe 14 September 2019 katika uwanja wa Camp Nou.

Anssumane Fati pia anakuwa mchezaji kinda zaidi wa kwanza mwenye umri wa miaka 16 akitumikia kikosi cha Barcelona (senior team) kufunga goli akiwa na kokisi hicho.

Anssumane Fati alianza maisha yake ya soka pale familia yake ilipohamia nchini Hispania kitongoji cha Herrera katika mji wa Sevilla akiwa na umri wa miaka 6. Wakati kaka yake mkubwa Braima alipojiunga na Sevilla mwaka 2009 yeye Anssumane alikuwa akicheza katika timu za watoto za CDF Herrera mpaka mwaka 2010 alipojiunga na timu za watoto za Sevilla mpaka mwaka 2012. Anssumane Fati alijiunga na academy ya Barcelona La Masia mwaka 2012 na amekuwa akicheza kwenye timu za vijana za Barcelona mpaka tarehe 24 July 2019 aliposaini mkataba wa kuitumikia "Barcelona senior team" mpaka mwaka 2022.

Kijana anajua sana kufunga aisee ndio maana wazungu wameamua kumpa uraia na sasa wanachofanya Barcelona ni kumuanzisha kwenye mechi za La Liga ili aendelee kuwa fiti kabla ya kwenda Brazil kama kila kitu kitakuwa sawa katika dili lake la kuitumikia timu ya Taifa ya vijana ya Hispania.

Anssumane anacheza nafasi ya kiungo wa pembeni namba 11.

Huyo ndio Anssumane Fati chaguo la Ernesto Valverde kinda mwafrika anaepasua vichwa vya wazungu.

Ndimi,
Emmauel M. Makalla.
0716605949