ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, April 3, 2025

BENKI YA CRDB YATAMBULISHA MKOPO WA KIDIJITALI WA 'JINASUE'

 

Katika mpango wake wa kuongeza ujumuishaji wa wananchi kiuchumi, Benki ya CRDB imezindua huduma ya mikopo ya Jinasue inayowalenga wateja wake wote wenye uhitaji wa fedha.

Huduma hiyo iliyozinduliwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili itawaruhusu wateja wa benki wenye salio dogo kwenye akaunti zao kuliko muamala wanaotaka kuifanya au wateja wanaohitaji fedha kutokana na dharura walizonazo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Adili amesema ujumuishi wa kifedha ni ajenda ya kimkakati ndani ya Benki ya CRDB inayoamini suala hilo ni msingi wa mapinduzi ya kiuchumi katika jamii yoyote.

“Tunayo mikopo inayowalenga baadhi ya wateja wetu kama vile watumishi, wanafunzi wa vyuo vikuu na wastaafu pamoja na wafanyabiashara. Tumegundua kuna watu ambao hawapo kwenye makundi hayo ambao wanahitaji uwezeshaji hivyo kuja na Jinasue, mikopo inayomlenga kila mteja wa benki yetu,” amesema Adili.
Mikopo hiyo, amesema itakuwa inatolewa kwa kushirikiana na kampuni ya CreditInfo na itatolewa kupitia SimBanking kuwawezesha wateja wetu kumudu gharama za huduma, bidhaa, na ankara mbalimbali wanapokuwa na changamoto za kifedha.

Kupitia SimBanking, wateja watapata mikopo ya Jinasue kwa urahisi kuanzia Shilingi 1,000 hadi Shilingi milioni 1 kwa riba ya asilimia 8 tu. Ili kupata mkopo huu, mteja anatakiwa kuwa anatumia akaunti ya Benki ya CRDB na amejiunga na huduma ya SimBanking.

“Mkopo wa Jinasue ni suluhisho muhimu kwa wateja wanapokabiliwa na changamoto za kifedha wakati wa kulipa ankara na huduma muhimu. Huu ni mkopo wa haraka, wa kidijitali, na wa gharama nafuu ambao utawasaidia wateja wetu kukabiliana na changamoto za uhaba wa fedha,” amesema Adili.

Kwa muda mrefu, Benki ya CRDB imekuwa ikibuni huduma za aina tofauti zinazolenga kukidhi mahitaji ya wateja wake huku ikiwekeza nguvu katika matumizi ya teknolojia.

Katika jitihada hizo, mwaka 2017, ilizindua “salary advance,” mikopo inayowalenga wafanyakazi na watumishi wa umma inayotolewa hadi shilingi milioni 3 kwa riba ya asilimia 5 tu, na mwaka 2019 ikazindua “boom advance,” kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu ikitolewa kuanzia shilingi 1,000 hadi shilingi 150,000 na kurejeshwa hadi kwa siku 60 tangu walipochukua mkopo.

Mwaka 2020 Benki ya CRDB ilitambulisha sokoni “pension advance,” mikopo mahsusi kwa ajili ya wastaafu wanaoruhusiwa kukopa kuanzia shilingi 5,000 hadi shilingi milioni 1.

ZAIDI YA WAFANYABIASHARA 100 KUHUDHURIA JUKWAA LA BIASHARA NA UWEKEZAJI NCHINI ISRAEL

 

Na Pamela Mollel,Arusha


Zaidi yawafanyabiashara na wajasiriamali 100 kutoka nchini wanatarajia kuhudhuria jukwaa maalumu la kimataifa linalohusu maswala ya uwekezaji nchini Israel kwa ajili kubadilishana uzoefu na fursa za miradi ya uwekezaji zinazoweza kutekezwa na wataalamu hao katoka nchi hizo mbili.

Wafanyabiashara hao wanatarajia kukutana katika mji wa Tel-aviv nchini Israel june 8 hadi 14, 2025 katika jukwaa la Biashara na Uwekezaji ya Tanzania-Israel (TIBIF) .

Lengo kubwa katika jukwaa hilo ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Israel, kukuza ushirikiano na ubunifu lakini pia kubadilishana fursa za uwekezaji na miradi inayoweza kutekelezwa na nchi hizo mbili.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT) Isaac Mpatwa amesema kuwa wameandaa safari hiyo kwa ajili ya kuwapa fursa wajasiriamali na wafanyabiashara kukutana, kujitambulisha, na kuchunguza ushirikiano unaowezekana na wenzao wa Israel katika Nyanja mbalimbali.

"Tunawapeleka wafanyakabiashara wetu nchini Israel ili kuwaunganisha na masoko, miradi, mitaji, fedha, mafunzo, na ushauri wa kibiashara katika sekta mbalimbali za uwekezaji wa elimu, ufugaji, uvuvi, viwanda, teknolojia na utalii” amesema na kuongeza

“Tunataka wafanyabiashara wetu wapate nafasi ya kukutana na wenzao wa Israel kupitia mikutano midogo midogo ya kibiashara ‘Business to Business Meeting[B2B]' iliwaweze kufaidika na fursa za biashara zinazofanana na wenzao”

Mpatwa amesema kuwa hayo yote yanafanyika kwa ushirikiano na serikali chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uwekezaji, na Wizara ya Mambo ya Nje.

“Ushirikiano huu unalenga kubadilishana maarifa, miradi, na uzoefu kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuhakikisha wafanyabiashara wetu wanaungwa mkono na mifumo rasmi ya kiuchumi na unatoa fursa za kufanikisha makubaliano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara na serikali, au serikali za nchi washirika na nchi yetu”.

Mpatwa ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mtandao wa kuwaunganisha wafanyabiashara na wajasiriamali na fursa mbalimbali za kiuchumi ndani na nje ya nchi iliyopewa jina la ‘KLI Alumni Connect’.

Mtandao huo utawahusisha wafanyabiashara waliopitia programu za uongozi wa Biashara na ujasiriamali katika kipindi cha miaka mitatu kilichoendeshwa na KLNT kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Regent kilichoko nchini Marekani.

Mpatwa amesema mtandao huo utakaowakutanisha wahitimu wa elimu ya vitendo ya biashara na ujasiriamlali kutoka kituo cha kibiashara cha Business Development center (BDC) Tanzania unalenga kuwawezesha kukuza na kuimarisha biashara zao walizonazo.

"Kupitia KLI Alumni Connect, tunawapa wahitimu wetu fursa ya uunganishwa na ekosistemu ya biashara, mabenki, taasisi za maendeleo ya teknolojia, na wadau wa ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya mataifa 100 duniani tulizo na mahusiano nazo”.

Amesema hiyo itawawezesha kupata Elimu zaidi, mitaji, ubunifu, teknolojia, vifaa, na masoko ya kimataifa.

Mmoja wa wafanyabiashara wahitimu katika programme hiyo, Rephrine Kombe amesema mafunzo hayo ya wiki 20 yamewasaidia kuwapa ujasiri wa kuwasilisha mawazo yao na kuboreshwa na wataalamu hao wa biashara na kuwasaidia kuanza safari rasmi ya kibiashara.

"Mimi nilikuwa na wazo tayari, hivyo nikasaidiwa kuboresha na wakufunzi wetu ambao ni maprofesa wa biashara, na sasa nimefanikiwa kuwa na biashara halisi, na zaidi nimefanikiwa kuingia kwenye mfumo rasmi wa kiserikali" amesema Rephrine ambae ni Mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza taulo za kike cha Reepads’ .

Aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Programe hiyo, Meya wa jiji la Arusha Maximmilian Iranghe amesema kuwa elimu hiyo ya ujasiriamali ya vitendo ni nzuri ambayo inasaidia pia serikali kukuza ajira na kukua kiuchumi kwa jamii.

“Kadri wananchi wake wanavyokua na uchumi mzuri ndivyo na serikali inavyozidi kukua hivyo niwapongeze sana KLNT na niseme kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono wafanyabiashara na wajasiriamali wote nchini hasa katika kutatua changamoto zao wanazokumbana nazo ili kukuza biashara zao”.

Pia amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanatumia fursa ya uwekezaji wa nyumba za wageni ili kuchangamkia fursa ya utalii inayozidi kukua kila kukicha huku changamoto kubwa ikiwa malazi.

“Tena uwekezaji huo muanze sasa hivi maana mwaka 2027 kuna utalii mkubwa wa mikutano na wa michezo ambazo tutakuwa na mkutano mkubwa wa wadau na wataalamu wa nyuki duniani watakaokutana Arusha unaojulikana kama ‘Apimondia’ lakini pia michuano ya kombe la Afrika ‘Afcon’ hivyo changamkeni hela zinakuja” amesema Meya huyo.

Wednesday, April 2, 2025

ZAIDI YA WANANCHI 9,450 KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAJI WILAYA YA KOROGWE

 


Na Oscar Assenga, TANGA


ZAIDI ya Wananchi 9,450 wa wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga wanatarajiwa kuondokana na changamoto ya upatkanaji wa maji baada ya Serikali kuzindua mradi wa Kitaifa wa Ujenzi wa Visima 900 ambao unalenga kutatua changamoto hiyo.

Kati ya visima hiyo Mkoa wa Tanga watapata visima 53 ambavyo vitajengwa kila jimbo

Akizungumza mradi huo katika Kijiji cha Makorora wilaya Korogwe Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Burian alisema kwamba visima 8 vimejengwa na kati ya hivyo vitano vimejengwa katika Jimbo la Korogwe Vijiji na Vitatu Korogwe mjini.

Alisema kwamba hatua hiyo ni juhudi za Serikali za kuhakikisha wana watua ndoo kichwani wakina mama hapa nchini kwa kuwekwa huduma hiyo karibu na maeneo yao ili kuwaondolea adha ambazo walikuwa wanakumbana nazo awali.

“Leo hii tumekuja kushuhudia katika jimbo la Korogwe Visima vilivyochimbwa na hivyo yote ni kuhakikisha tunamtua Ndoo kichwani Mama kama ilivyo azma ya Rais wetu Dkt Samia Suluhu tumefanya hivyo kuonyesha maji yamefika kwa wananchi”Alisema

Awali akizungumza Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo alisema kwamba wataendelela kuboresha huduma za maji katika maeneo ya vijiji kwa kuendeleza miradi ya maji kila eneo ambalo halijaunganishwa na huduma hiyo

Alisema huduma hiyo iwafikie ndani ya muda mfupi ili waweze kuondokana na adha ya kufuata maji umbali mrefu na hivyo kuwawezesha kushiriki kwenye shughuli nyengine za maendeleo.

Lengo la Serikali ni kuwapatia maji wananchi kwa asilimia 85 vijiji na aslimia 95 maeneo ya mijini





Tuesday, April 1, 2025

TAASISI ZOTE MWANZA ZATAKIWA KUJISAJILI PDPC

 


NA ALBERT G.SENGO/MWANZA Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni suala nyeti kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia kunakosababisha utoaji huduma nyingi kuhamia kwenye mifumo ya kielektroniki hivyo kulazimu kuanzishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya Mwaka 2022, Sura ya 44.