ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, August 18, 2018

SIMBA BINGWA NGAO YA JAMII 2018-2019

 SIMBA SC wamefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Hiyo inakuwa mara ya nne kwa SImba SC kutwaa Ngao ya Jamii, baada ya 2011 wakiifunga Yanga 2-0, 2012 wakiifunga Azam FC 3-2 na mwaka jana wakiwafunga tena mahasimu wao wa jadi, kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.


Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Elly Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma wote wa Dar es Salaam, na Ferdinand Chacha wa Mwanza, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.


Mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere alianza kuifungia Simba SC dakika ya 29 kwa shuti kali kutokea pembezoni mwa Uwanja kushoto, baada ya kuwatoka mabeki wa Mtibwa Sugar na kipa wao, Benedictor Tinocco kufuatia kazi nzuri ya Hassan Dilunga.
 Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Nicolas Gyan, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, James Kotei, Hassan Dilunga/Muzamil Yassin dk78, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi/John Bocco dk66 na Shiza Kichuya/Shomari Kapombe dk73.
 Mtibwa Sugar: Benedict Tinoco, Rogers Gabriel, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Cassian Ponera, Hassan Isihaka, Shaban Nditi, Ismail Aidan, Salehe Hamis/Ally Makalani dk 85, Kelvin Sabato, Awadh Juma/Juma Luizio dk63 na Salum Kihimbwa/Haroun Chanongo dk73.
  Kelvin Sabato Kongwe au Kiduku akaisawazishia Mtibwa Sugar dakika ya 33 baada kupokea pasi nzuri ya Saleh Hamisi na kufumua shuti zuri akiwa anatazamwa na mabeki wa Simba SC.

Wakati refa Sasii anajiandaa kupuliza filimbi ya kukamilisha kipindi cha kwanza, Hassan Dilunga akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya dakika 45 stahili za mchezo.

Dilunga aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar mwezi uliopita tu baada ya awali kuchezea Ruvu Shooting, Yanga SC na JKT Ruvu, alifunga bao hilo kwa shuti lililowababatiza wachezaji wengine kufuatia pasi ya Mganda, Emmanuel Okwi.


 Kipindi cha pili mchezo uliendelea kupendeza, Simba SC wakisaka mabao zaidi na Mtibwa Sugar wakitafuta bao la kusawazisha lakini hakuna timu iliyofanikiwa kutikisa nyavu. 

Mtibwa ilipata pigo baada ya kiungo wake, Awadh Juma kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake imechukuliwa na Juma Luizio dakika ya 63, wote wamewahi kuchezea SImba SC.

Nahodha wa leo wa Simba SC, Emmanuel Okwi naye akashindwa kuendelea na mchezo dakika ya 66 akimpisha Nahodha wa klabu, John Bocco. 

MAKONDA AWAAHIDI MAKUBWA WASANII.
NA ZEPHANIA MANDIA/GSENGOtV
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo ameungana na maelfu ya wakazi wa jiji hilo kwenye Tamasha kubwa la Burudani Komaa Concert 2018 lililoandaliwa na kituo cha utangazaji cha E FM/TV E ambapo amesema serikali ya mkoa huo itaendelea kutoa ushirikiano kwa wasanii kwakuwa sanaa ni Ajira rasmi inayowasaidia vijana wengi.

Akizungumza na maelfu ya wananchi hao Makonda amewaomba waendelee kumpa ushirikiano wa kutosha Rais Dkt. John Magufuli huku akipongeza maendeleo makubwa yaliyopatikana tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani.

Aidha Makonda amewapongeza E FM kwa kuandaa tamasha hilo lililotoa fursa kwa wananchi wanyonge kupata burudani huku akiwakumbusha wananchi kuhakikisha wanafanya Usafi wa mazingira wanayoishi.

Pamoja na yote Makonda amewahimiza wananchi kuhakikisha wanalinda Amani, usalama na kuwakumbuka kwenye Maombi viongozi wote wa Taifa.

MKUU WA WILAYA YA KWIMBA ALA KIAPO NA KUKABIDHIWA MAJUKUMU MAZITO 16 AGOSTI 2018NA ZEPHANIA MANDIA/GSENGOtV
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe.John Mongella amemwapisha Mkuu mpya wa wilaya ya Kwimba Mhe.Senyi Simon Ngaga na kumtaka  akatimize vyema majukumu yake ikiwemo kupambana na mauaji yatokanayo na imani za ushirikina.

Hafla ya kumwapisha Mhe. Ngaga ambaye amechukua nafasi ya Mhe. Mtemi Msafiri aliyehamishiwa Chato mkoani Geita imefanyika leo Agosti 16, 2018 katika ofisi za Mkuu wa Mkoa Mwanza.

Friday, August 17, 2018

SIMBA KUIKABILI MTIBWA NGAO YA JAMII, BILA YA BOCCO, KAPOMBE.NA GSENGOtV

Klabu ya Simba FC ya Dar es salaam imewasili jijini Mwanza hii leo tayari kuvaana na wanatamtam wa Manungu Mtibwa Sugar kwenye mnatanange wa Ngao ya Jamii unaoarajiwa kuchezwa jumamosi hii kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akiongea na wanahabari muda mfipi baada ya kwasili Kocha mbelgiji Patrick Aussems  amesema kuwa klabu hiyo licha kuwakosa nahodha John Boko, Shomali Kapombe ambao wote ni majeruhi amebainisha utayari wa kikosi chake na kujinasibu kuondoka na kombe hilo ikiwa ni  kujiweka tayari kunyakua tena kombe la ligi kuu msimu ujao.

KAULI YA ATCL KUHUSU DREAMLINER KUTOONEKANA HEWANI.

SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) limezungumzia kutosafiri kwa ndege yake mpya aina ya Boeing 787-7 Dreamliner, iliyoanza kazi mwishoni mwa mwezi uliopita.

Tangu ilipoanza safari zake Julai 29, ndege hiyo imekuwa ikifanya safari kati ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza kila siku asubuhi na jioni.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Ladislaus Matindi alisema juzi kuwa, hakuna ndege yao ambayo imekwama mahali popote na hata Dreamliner ambayo shirika limeisimamisha kwa makusudi kutokana na matakwa ya kiufundi.

“Tunazo ndege nne, tatu aina ya Bombardier Q400 zinaruka na kufanya safari zake kama kawaida, Dreamliner tumeisimamisha sisi wenyewe kwa ajili ya matakwa ya kiufundi, kwa hiyo iko chini kuanzia jana (Agosti 14), leo (Agosti 15) na kesho (Agosti 16),” alisema Matindi wakati akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam, juzi.

Alisema nia ni kuangalia sehemu za marekebisho katika ndege hiyo ikiwemo suala la WiFi ambayo inatakiwa kufanyiwa marekebisho madogo na mambo mengine yanayohusiana na uendeshaji kwa kuwa safari zinazofanyika sasa ni za majaribio na mafunzo kwa marubani.

“Ndege ilisimamishwa ili kufanyia marekebisho ambayo yanatakiwa katika uendeshaji. Hayo yanayosemekana siyo kweli na kesho (jana) tutakuwa tumemaliza na tutaendelea na safari za Dreamliner,” alisema.

Awali, baadhi ya taarifa zilisambaa mitandaoni zikidai ndege hiyo ilikuwa na matatizo yaliyosababisha abiria waliotakiwa kusafiri nayo kukwama hadi wakatafutiwa ndege nyingine.

Matindi alisema ATCL walipanga kuwa matengenezo yangefanyika baada ya wiki tatu, lakini mafundi waliomba yafanyike mapema kwa sababu wanakaribia kuondoka, hivyo ikabidi shirika lifanye uamuzi wa ghafla.

“Marekebisho yalifanywa baada ya kukamilika kwa safari moja ya kutoka Mwanza kurudi Dar es Salaam, hivyo hakuna abiria yeyote aliyetelekezwa wala kushushwa uwanja wa ndege kama inavyoelezwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mawasiliano wa ATCL, Joseph Kagirwa alisema abiria wote ambao walitakiwa kusafiri na Dreamliner kwa safari zao, baadhi yao walisafirishwa na Bombardier na wengine walipandishwa katika ndege za mashirika mengine.

“Tulifanya mawasiliano na abiria wetu siku moja kabla, kila mmoja alipigiwa simu kuelezwa dharura iliyojitokeza, hakuna mtu aliyetozwa nauli zaidi na ofa zetu zinaendelea kama kawaida,” alisema Kagirwa.

“Kesho Dreamliner inarejea katika safari zake kama kawaida na ndege itakuwa imejaa.”

Abiria waliokwama

Baadhi ya wasafiri ambao walitarajia kusafiri na ndege hiyo kutoka Kilimanjaro kwenda Dar es Salaam juzi, walilazimika kukaa uwanjani kwa zaidi ya saa nane.

Abiria waliozungumza na gazeti hili walilalamikia kutopewa taarifa mapema juu ya ndege hiyo iliyotakiwa kuondoka uwanjani hapo saa sita mchana, lakini haikufika.

“Tuko uwanjani hapa toka saa nne na tulitakiwa tuondoke kuelekea Dar es Salaam majira ya saa sita mchana, lakini hadi sasa bado hatujaondoka,” alisema mmoja wa abiria ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Baadaye abiria huyo alisema waliondoka kwa makundi kwa kutumia ndege za mashirika mengine.

Abiria huyo alisema kundi la kwanza liliondoka uwanjani hapo saa 12 jioni na la mwisho liliondoka saa mbili usiku.

“Baadhi ya abiria wameshasafiri kwa kutumia ndege za kampuni nyingine, lakini abiria 15 kati ya 50 tuliotarajia kusafiri kwa ndege hiyo bado tupo uwanjani, hatujui hatima yetu,” alisema abiria huyo kabla ya baadaye kusema walifanikiwa kuondoka saa mbili usiku.

KIKWETE AMTEMBELEA TENA KIGWANGALLA, YUKO FITI KURUHUSIWA WAKATI WOWOTE.


RAIS Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete amemtembelea na kumjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum kitengo cha Taasisi ya Mifupa MOI, hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine tena.

Hii inakuwa ni mara ya tatu kwa Kikwete kumtembelea Dk Kigwangalla ambapo awali alimtembelea Agosti 8, 2018 alipokuwa amelazwa Wodi ya Mwaisela akipatiwa Matibabu ya awali na juzi Agosti 15, 2018 katika wodi ya Taasisi ya Mifupa MOI.

Akiwa hospitaini hapo mapema jana, Kikwete ameweza kumjulia hali na kubadilishana nae mawazo mbalimbali huku akimtakia unafuu aendelee na majukumu yake ya kila siku na akimpongeza kwa shughuli zake anazozifanya katika kuinua sekta ya Utalii pamoja na kulinda rasilimali za Maliasili.

“Nikutakie kheri. Nashukuru kwa kukuta unaendelea vizuri sasa na nilikuja ukiwa upo unaongea ukiwa umelala kitandani na kwa sasa nimekuja tena umeweza kuimarika na hata kutembea na kukaa kama hivi hongera sana” alieleza Kikwete wakati akimjulia hali Waziri Kigwangalla wodini hapo.

Tayari jopo la Madaktari bingwa wa MOI wamebainisha kuwa Dkt. Kigwangalla kwa sasa anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani ambapo kwa sasa sehemu zilizobakia ni mkono wake wa kushoto ambao kila siku unaendelea kuimarika.

Hata hivyo, Dkt. Kigwangalla amemweleza Kikwete kuwa kwa sasa hali yake inaendelea kuwa vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani huku akiendelea na mazoezi kidogokidogo.

Aidha, jioni ya jana Dkt. Kigwangalla ameweza kufanya mazoezi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa moja kuanzia kwenye viunga vya Hospitali hiyo na kuzunguka maeneo yanayozunguka Muhimbili na baadae kupanda kwa kutumia ngazi katika jengo anapopatiwa matibabu kwa miguu mpaka gorofa ya sita.

Waziri Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari mnamo Agosti 4, 2018 huko Manyara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo katika ajali hiyo iliyokuwa na watu 6, Afisa Habari wa Wizara hiyo Hamza Temba alifariki dunia huku watano wakijeruhiwa akiwemo yeye anaendelea na matibabu Hospitalini hapo.

BRIGEDIA JENERALI MWANGELA AKAGUA MIRADI NA KUWAASA WATUMISHI WILAYANI SONGWE

 Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela akikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Mbuyuni Wilayani Songwe, kituo hicho kilipokea shilingi milioni 400 kutoka serikali kuu na kinatarjiwa kukamilika mwezi ujao.
 Wananchi wa Kata ya Mbuyuni Wilayani Songwe wakijitolea shughuli mbalimbali za ujenzi katika Kituo cha Afya Mbuyuni ambapo serikali kuu ilitoa shilingi milioni 400 na kituo hicho kinatarajiwa kukamilika mwezi ujao.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela akikagua mradi wa maji Mbuyuni ambao ulikamilika mwaka 2014 lakina bado wananchi hawapati maji kutokana na maji katika chanzo hicho kuwa na rangi mbaya, Brigedia Jenerali Mwangela amemuagiza mhandisi wa maji wilayani humo kufaya utafiti wa chanzo kingine haraka. 

MKUU wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela jana jioni amehitimisha ziara yake ya siku mbili Wilayani Songwe, ambapo amekagua miradi kumi ya maendeleo na kisha kuzungumza na watumishi na watendaji wa taasisi mbalimbali zilizomo wilayani humo.
Brigedia Jenerali Mwangela akiwa ameambatana na baadhi ya maafisa wa Mkoa wa Songwe akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe wametoa maelekezo yaliyohusu kuboresha utendaji kazi kwa watumishi wa Wilaya ya Songwe.
Amesema “nimegundua kila ambacho alinieleza Mkuu wa Mkoa aliyestaafu kuhusu wilaya ya Songwe ni sahihi, upungufu alio uona nami pia nimeuona, napenda kusema mlikuwa mnamuona ni yeye Mkali ila mimi nasema alikuwa Mvumilivu”.
Brigedia Jenerali Mwangela amesema hatosita kumsema na kumchukulia hatua mtendaji anayeenda kinyume na sheria na taratibu za utumishi wa umma hivyo basi watumishi hao wabadilike na kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano, watembelee na kukagua miradi inayotekelezwa wilayani humo.
Aidha amempongeza Mkuu wa Shule ya Sekodari ya Kanga wilayani humo ambapo alifanya ziara ya kushtukiza na kuwakuta walimu wote wapo darasani wanafundisha na mwalimu mkuu huyo akiwa anafundisha huku akisimamia ujenzi wa mabweni shuleni hapo, amemshauri mwalimu huyo kutumia wataalamu wa ujenzi wa wilaya ili Kusimamia ubora.
Baada ya kutembelea Daraja la Kikamba linalounganisha kata ya Kapalala na Gua, Brigedia Jenerali Mwangela amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Songwe Kumsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi wa daraja hilo kwa muda uliopangwa ambao ni Septemba 7, mwaka huu.
Katika kituo cha Afya Mbuyuni amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo kuhakikisha ujenzi unapokamilika, vifaa tiba, dawa na wataalamu wa Afya wawepo ili kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wananchi na meneja wa Tanesco kwa kushirikiana na Mkoa kuhakikisha kituo hicho kitakapoanza kutoa huduma kiwe na umeme.
Brigedia Jenerali Mwangela amemtaka mhandisi wa maji Wilayani humo kufanya utafiti wa haraka wa chanzo kingine cha maji kwa ajili ya mradi wa maji Mbuyuni kwakuwa wananchi wamekataa kuyatumia maji ya chanzo cha awali kutokana na maji hayo kuwa na rangi mbaya.
Ameongeza kuwa wataalamu waliofanya utafiti awali hawakutendea haki taaluma yao na hivyo kusababisha hasara kwa serikali huku wananchi wakiendelea kupata kero ya maji tangu mradi huo ukamilike mwaka 2014.
Brigedia Jenerali Mwangela amemtaka Afisa Afya wa Wilaya ya Songwe kutoa elimu kwa wananchi ili wajenge vyoo bora, elimu ya masuala ya lishe, pia ahamasishe upimaji afya zao hususani kwa magonjwa yasioambukiza kama tezi dume, kisukari, VVU pamoja na kufanya tohara.
Ameongeza kwa kuwataka watunze mazingira na kuendelea kusimamia agizo la katazo la ukataji ovyo miti kwa ajili ya biashara ya mkaa, aidha ameelekeza wananchi wanaruhusiwa kuvuna miti katika maeneo maalumu yaliyotengwa na wakala wa huduma za misitu (TFS).
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Mathias Nyange amewataka watumishi kuacha utoro kwakuwa wengi wao ifikapo siku ya ijumaa hutoroka na kuelekea Mkoa wa jirani walipoweka makazi yao.
RPC Nyange amesema, “nitamshauri Mkuu wa Mkoa vikao viwe vinafanyika siku ya Jumamosi ili kufuta utoro huu, nawashauri watumishi unapopangiwa kituo cha kazi ndio kwenu papende, ufanye kazi kwa bidi”.
Ameongeza kuwa serikali inatukanwa kutokana na uzembe wa baadhi ya watumishi hivyo wajitume wabadilike na wafanye kazi kwa ushirikiano hasa katika kumsaidia mwananchi masikini apate maendeleo.

UJAMBAZI WA SILAHA UMEPUNGUA NCHINI-IGP.


 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akisalimiana na Maofisa waliopo Shule ya Polisi Moshi zamani CCP wakati wa ziara ya kikazi kuangalia mwenendo wa mafunzo chuoni hapo na kuzungumza na Wakufunzi wa chuo hicho. (Picha na Jeshi la Polisi).
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akikagua gwaride baada ya kuwasili Shule ya Polisi Moshi zamani CCP kwa ziara ya kikazi kuangalia mwenendo wa mafunzo chuoni hapo na kuzungumza na Wakufunzi wa chuo hicho. (Picha na Jeshi la Polisi).
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Polisi Hamis Issah na RPC Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ramadhan Nganzi wakati wa Ziara yake ya kikazi Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha. (Picha na Jeshi la Polisi).
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akisalimiana na Wakazi wa Kata ya Mto wa Mbu Wilayani Monduli wakati alipokwenda kuzungumza nao wakati wa Ziara yakeya kikazi Mkoa wa Arusha yenye lengo la kutatua changamoto za uhalifu (Picha na Jeshi la Polisi).
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akizungumza na  na Wakazi wa Kata ya Mto wa Mbu Wilayani Monduli katika mkutano wa hadhara wakati wa Ziara yakeya kikazi Mkoani Arusha yenye lengo la kutatua changamoto za uhalifu (Picha na Jeshi la Polisi).
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Karatu Bi. Theresia Mhongo wakati wa Ziara yake ya kikazi Mkoani Arusha yenye lengo la kutatua changamoto za uhalifu (Picha na Jeshi la Polisi)
Na Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro ametoa onyo kali kwa majambazi na wahalifu wengine hususani wanaotumia silaha za moto kuacha mara moja kabla ya kukutana na moto mkali wa Jeshi la Polisi ambapo pia ametoa wito kwa wazazi kuwakanya watoto wao kujihusisha na vitendo hivyo.

IGP Sirro ameyasema hayo wakati akizungumza na Wakazi wa Mto wa Mbu Tarafa ya Manyara Wilayani Monduli Mkoani Arusha wakati wa Ziara yake mkoani humo yenye lengo la kubaini changamoto za kiuhalifu na kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema hivi sasa ujambazi wa kutumia silaha umepungua kwa kiasi kikubwa na baadhi ya matukio ambayo yamekuwa yakijitokeza yanaendelea kudhibitiwa na Jeshi la Polisi.

“Nawasihi wanaofikiria kuendelea kufanya vitendo vya uhalifu ikiwemo vya utumiaji wa silaha na kuua watu waache mara moja kwa kuwa wakikutana na moto wa Jeshi la Polisi wasije wakajilaumu mana kwa sasa moto wetu ni mkali hivyo nawashauri wazazi wakanye watoto wao” Alisema Sirro.

Aidha amewataka Wakazi wa Mto wa mbu Wilayani Monduli kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa kuwa usalama umeimarishwa katika kupambana na wahalifu waliokuwa wakifanya vitendo vya kuwaua watu hususani wanawake ambapo katika kipindi cha hivi karibuni kuliripotiwa matukio kadhaa ambayo yalileta wasiwasi katika eneo hilo muhimu kwa utalii.

Amewataka Viongozi wa Vijiji na Kata kuhakikisha kuwa suala zima la ulinzi na usalama linatiliwa mkazo ili kuhakikisha hakuna mhalifu katika maeneo yao na wageni wanapoingia wachukue taarifa zao mapema.

Kwa Upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Mto wa Mbu Bi. Kuluthum Hassan alisema Wahalifu wanaouza bangi, pombe ya gongo na dawa za kulevya wanaendelea kuwafichua ili wafikishwe katika vyombo vya dola na hivi sasa wanaendelea na mipango ya ujenzi wa kituo kikubwa cha Polisi kitakachoendana na hadhi ya eneo hilo.

Nao wananchi mbalilmbali wa Mto wa mbu wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha kuwa maeneo hayo yanakuwa salama wakati wote hususani kipindi hiki cha watalii wengi katika maeneo hayo na wameahidi kuchangia ujenzi wa kituo cha Polisi ili kuboresha usalama katika eneo hilo.