ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, August 17, 2018

KIKWETE AMTEMBELEA TENA KIGWANGALLA, YUKO FITI KURUHUSIWA WAKATI WOWOTE.


RAIS Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete amemtembelea na kumjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum kitengo cha Taasisi ya Mifupa MOI, hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine tena.

Hii inakuwa ni mara ya tatu kwa Kikwete kumtembelea Dk Kigwangalla ambapo awali alimtembelea Agosti 8, 2018 alipokuwa amelazwa Wodi ya Mwaisela akipatiwa Matibabu ya awali na juzi Agosti 15, 2018 katika wodi ya Taasisi ya Mifupa MOI.

Akiwa hospitaini hapo mapema jana, Kikwete ameweza kumjulia hali na kubadilishana nae mawazo mbalimbali huku akimtakia unafuu aendelee na majukumu yake ya kila siku na akimpongeza kwa shughuli zake anazozifanya katika kuinua sekta ya Utalii pamoja na kulinda rasilimali za Maliasili.

“Nikutakie kheri. Nashukuru kwa kukuta unaendelea vizuri sasa na nilikuja ukiwa upo unaongea ukiwa umelala kitandani na kwa sasa nimekuja tena umeweza kuimarika na hata kutembea na kukaa kama hivi hongera sana” alieleza Kikwete wakati akimjulia hali Waziri Kigwangalla wodini hapo.

Tayari jopo la Madaktari bingwa wa MOI wamebainisha kuwa Dkt. Kigwangalla kwa sasa anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani ambapo kwa sasa sehemu zilizobakia ni mkono wake wa kushoto ambao kila siku unaendelea kuimarika.

Hata hivyo, Dkt. Kigwangalla amemweleza Kikwete kuwa kwa sasa hali yake inaendelea kuwa vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani huku akiendelea na mazoezi kidogokidogo.

Aidha, jioni ya jana Dkt. Kigwangalla ameweza kufanya mazoezi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa moja kuanzia kwenye viunga vya Hospitali hiyo na kuzunguka maeneo yanayozunguka Muhimbili na baadae kupanda kwa kutumia ngazi katika jengo anapopatiwa matibabu kwa miguu mpaka gorofa ya sita.

Waziri Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari mnamo Agosti 4, 2018 huko Manyara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo katika ajali hiyo iliyokuwa na watu 6, Afisa Habari wa Wizara hiyo Hamza Temba alifariki dunia huku watano wakijeruhiwa akiwemo yeye anaendelea na matibabu Hospitalini hapo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.