Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi mbalimbalia Chato waliohudhuria kwenye uzinduzi wa jengo jipya la Benki ya CRDB tawi la Chato, Leo Machi 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akikata utepe ishara ya uzinduzi wa jengo jipya la Benki ya CRDB tawi la Chato, Leo Machi 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi mbalimbalia Chato waliohudhuria kwenye uzinduzi wa jengo jipya la Benki ya CRDB tawi la Chato, Leo Machi 2018
Na Mathias Canal,
Chato-Geita
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe
Maguguli Leo 9 Machi 2018 amezindua jengo jipya la Benki ya CRDB Tawi la Chato
Mkoani Geita.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe Dkt. Magufuli amesema kuwa
uwepo wa Benki hiyo utarahisisha huduma za uhifadhi fedha kwa wafanyabiashara
wa samaki Wilayani Chato sambamba na wananchi ambao kwa kiasi kikubwa katika
msimu wa Kilimo wamenilima Pamba kwa wingi.
Ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kuzifungia baadhi ya
Benki nchini na kuzipa onyo zingine ambazo zilikuwa zinafanya kazi kwa mazoea
na kwenda kinyume na utaratibu wa sheria za uendeshaji.
Alisema ni bora kuwa na Benki chache nchini ambazo zinaweza
kuwahudumia wananchi wengi hususani masikini kama ilivyo CRDB ambayo imewafikia
kwa kiasi kikubwa wananchi vijijini hivyo kuendelea kuzifungia Benki zote
ambazo zimeshindwa kuendesha vyema shughuli zake na kusalia kufanya huduma
Jijini Dar es salaam pekee.
Rais Magufuli ameiomba benki ya CRDB kupunguza riba ya mikopo
kwani ni asilimia 16 pekee ya watanzania ndio wanaohudumiwa kwenye Benki nchini
hivyo ili wananchi wote waweze kukopa na kuweka mitaji yao midogo kwa ajili ya
faida yao ya Sasa na badae ni lazima kuwa na riba rafiki kwa wananchi.
JPM ameipongeza Benki hiyo kwa kuajiri wafanyakazi wapatao 3200
tangu ilipoanza rasmi nchini mwaka 1972 wakati wa utawala wa serikali ya awamu
ya kwanza chini ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeielewa dhana
halisi ya kuwasaidia wananchi vijijini kutokana na usumbufu mkubwa wanaoupata
katika huduma za kifedha.
Alisema kuwa anayo imani kubwa na Benki ya CRDB kwani naye ni
mteja wa benki hiyo hivyo ili kuendeleza mahusiano mema tayari seikali imelipa
Deni lote la shilingi Bilioni 16 ambalo ilikuwa inadaiwa na benki hiyo kutokana
na mikopo katika miaka ya nyuma.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewahamasisha wananchi
kutunza fedha zao benki na kuachana na dhana ya kuhifadhi fedha majumbani jambo
ambalo ni hatari kwa usalama wa fedha hizo na maisha yao wenyewe.
Mhe Magufuli amesisitiza watanzania kuwa wazalendo huku akisema
kuwa anatambua kuwa wapo baadhi ya wananchi ambao wamesalia na jukumu la
kuandika katika mitandao na vyombo vya habari mambo ambayo ni kinyume na
utendaji wa serikali jambo ambalo ni uchonganishi dhidi ya wananchi na serikali
yao.
Aidha, Mhe Rais Magufuli alikataa ombi la Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB Tanzania Dkt Charles Kimei aliyetaka Benki hiyo
kuitwa CRDB JOHN POMBE MAGUFULI-CHATO huku akisema kuwa isalie kuitwa CRDB tawi
ka CHATO.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Tanzania,
Dkt Charles Kimei ametoa pongezi kwa Rais Magufuli kwa kukubali kuwa mgeni
rasmi katika uzinduzi wa Benki hiyo huku akielezea namna ambavyo amekuwa na
dhamira ya dhati ya kuwainua watanzania kupitia rasilimali zao jambo ambalo
litawanufaisha na kuwainua kiuchumi.
Alisema kuwa Benki hiyo itaendelea kubuni njia nzuri za mikopo
huku akisisitiza kuwa Benki hiyo kuendelea kuwasaidia wananchi kupitia SACCOS
zao kupata mikopo nafuu ili kujinufaisha kwa kuwa na uchumi imara
utakaowawezesha kukuza biashara zao.
Sambamba na hayo pia amekubali ombi la Mbunge wa Jimbo la Chato
Mhe Medard Kalemani ambaye ni Waziri wa Nishati la kujenga uwanja wa kisasa wa
Mpira wa miguu ambapo kwa niaba ya Benki hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini
Benki ya CRDB Tanzania Ndg Martin Mmari amekabidhi Hundi la Shilingi
Milioni 50 kwa ajili ya hatua za mwanzo za kuanza ujenzi wa uwanja huo huku akiahidi
Benki hiyo kuwa wadhamini wa timu ya mpira wa miguu ya wilaya ya Chato.
Dhifa ya uzinduzi wa Benki hiyo ulihudhuriwa na viongozi
mbalimbali akiwemo Waziri Wa Nishati Mhe Medard M.Kalemani (Mb), Naibu
Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko (Mb), Mkuu Wa Mkoa Wa Geita Mhandisi
Robert Gabriel, Naibu Waziri Wa fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijazi (Mb), Naibu
Gavana Wa Benki Kuu Tanzania Dkt Bernard
Yohana Kibese, Balozi Wa Denmark nchini Tanzania Mhe Einar Hebogard
Jensen, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi CRDB Tanzania Ndg Martin Mmari,
Mkurugenzi Mtendaji CRDB Tanzania Dkt Charles Kimei, na Wabunge wa majimbo
mbalimbali ikiwemo jimbo la Busanda na Mbogwe.