ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, March 8, 2018

KOROMIJE WAFUNGUKA SABABU SUGU NA VIKWAZO KWA MAENDELEO YA WANAWAKE VIJIJINI KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA.


SIKU ya kimataifa ya wanawake imeadhimishwa leo Alhamisi, duniani kote kwa kufanyika shughuli mbalimbali katika nchi tofauti huku kukitolewa mwito kwenda kwa makundi yote kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii mbalimbali.

Wanawake wa mkoa wa Mwanza nchini Tanzania wameiadhimisha siku hiyo katika kijiji cha Koromije kilichopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza, maadhimisho yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Koromije kwa kuzungumzia changamoto zinazo wakabili wanawake wa Kitanzania hasa wa vijijini katika kujikwamua kiuchumi, hasa ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ya mwaka huu nchini hapa ilijikita kumuangazia zaidi mwanamke wa kijijini.

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema 'Kuelekea Uchumi wa Viwanda, Tuimarishe Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake Vijijini'.

Hakika Imekuwa siku ya utofauti na faraja kubwa kwani Shirika la Kutetea Haki za Wasichana na Wanawake KIVULINI, chini ya Mkurugenzi wake Yassin Ally imeratibu vyema Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ngazi ya mkoa wa Mwanza.

Mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Jinsia wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Constansia Gabusa. 

Kwenye kusanyiko hilo wanawake wameketi kwa makundi, wakitabasamu na nyuso za furaha lakini vichwani mwao kukiwa na mawazo yaliyogubikwa na manung'uniko kutokana na changamoto nyingi zinazo zorotesha ushiriki wao kuelekea Tanzania ya viwanda.

Moja ya Changamoto kubwa ambazo zimeainishwa ni namna ya kupata mitaji kwa ajili ya kuendesha maisha yao kwa wanaotaka kujikita kwenye ujasiriamali husasani upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu.

Teresia Mnaku ni mwanamama mjasiliamali kutoka wilayani Misungwi ambaye alipewa dhamana na wawakilishi wa vikundi vingine kusoma Risala ya maadhimisho, naye anasema "Unakuta Taasisi fulani inatoa mikopo lakini ile riba inakuwa ni kubwa, mama anatakiwa kurejesha  kiasi kikubwa ambacho kwa uwezo wake kwa kipindi kilichowekwa inamuwia vigumu kutimiza, hatma yake muda wa kurejesha mkopo ukiisha, wanakamata mali zake pamoja na uwekezaji wake naye anarudi katika umasikini zaidi kuliko ule aliokuwa nao" 

"Mikopo mingi hutolewa na Ofisi za Halmashauri, ule umbali kutoka kijijini hadi ofisi za mikopo una athari kubwa kwani wadau wa vikundi wasio na mitaji hulazimika kusafiri kwa gharama kubwa kutoka eneo moja hadi jingine, mpaka mkopo utoka wanajikuta tayari wamesha tumia nusu ya fedha ya mkopo huo waliokuwa wakiufuatilia. Ili kuleta maana, nashauri hawa wadau wa mikopo wasogeze huduma hizo vijijini" aliongeza Bi. Teresia.

Nayo maeneo ya kufanyia bishara yanetajwa kama kizuizi kwa wanawake kufanikiwa kuyafikia malengo kwani maeneo mengi ya biashara vijijini siyo rasmi, yana vizuizi vingi na migogoro baina ya watendaji wake na wasimamizi wa sheria, wakati wowote maamuzi yanafanyika kusitishwa matumizi au marufuku kutumika kwa kufanyia biashara.

Hii ina athari kubwa hasa kwa waakinamama ambao wengi wao wanabidhaa zinazo hitaji nguvu ya ziada kuhamishika kama vile mama lishe ambao wengine huishia kumwagwa bidhaa zao na kupoteza mitaji.

Upatikanaji wa leseni na gharama zake hazilingani hata kiduchu na biashara zao kuanzia mitaji hadi vipato.


























Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.