|
Mkurugenzi wa Wilaya ya Magu Bi. Naomi Nnko (L) akitoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali kikaoni. |
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu limemwagiza Mkurugenzi Mtendaji
wake Naomi Nnko kuwachukulia hatua za kimaadili maafisa wake wa Idara ya Fedha
wanaojihusisha na njama ya kuikosesha mapato Halmashauri hiyo kupitia vyanzo
vyake vya mapato vilivyopo.
Hatua
hiyo inafuatia kikao cha Baraza hilo kilichoketi jana Wilayani humo na baadhi
ya Madiwani kuhoji chanzo cha mapato cha soko kuu la Mjini Magu kuingiza kiasi
cha shilingi laki sita kwa miezi miwili badala ya kukusanya kiasi hicho kwa
mwezi mmoja hali iliyobainika kuwepo mwanya wa kufujwa kwa fedha za mapato ya
chanzo hicho na watumishi wa halmashauri idara ya fedha..
Diwani wa Kata ya Ngasamo Wilayani Busega Jejeje Manyama aliunga hoja ya iliyotolewa na Diwani Mwenzake Julias Ngongoseke wa Kata ya Lubugu (UDP) kutoa hoja ya kutaka kufahamu nini kimepelekea chanzo hicho kukusanya mapato madogo ili hali kilikuwa na wakala wa kukusanya mapato aliyekusanya kiasi cha shilingi 600,000/= kwa mwezi na sasa kushuka hadi shilingi 310,000/-kwa mwezi jambo ambalo lilitakiwa kutolewa majibu na Mkurugenzi Nnko.
Akijibu hoja hiyo Mkurugenzi huyo alikiri kwa wajumbe wa baraza hilo kuwepo mapungufu ya kiutendaji katika Idara hiyo ya fedha na kuomba apewe muda wa kufanyia marekebisho ikiwemo kufatilia kwa ukaribu mapato ya vyanzo mbalimbali ili kuondoa mwaswali mengi kutoka kwa waheshimiwa madiwani ambao wameonekana kukelwa na majibu ya kila yasiyojitosheleza.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Boneventura Kiswaga (CCM) ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Uchumi na Fedha alisema kwamba kamati yake imeshitushwa na taarifa hizo za kukusanywa mapato kidogo ikiwemo kumuondosha wakala aliyekuwa anakusanya mapato ya soko hilo Samson Merthusela (Mtu binafisi) ambaye hata hivyo hakuwa na mkataba wowote wa Halmashauri hiyo bali kwa makubaliano.
Kiswaga aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo kwamba Idara hiyo ya fedha inaonekana kufanya mambo kienyeji sana na kutofuata taratibu na kanuni zilizopo za Halmashauri hiyo ikiwemo ya mikataba inayoingia na Makampuni na Mashirika mbailimbali kutofuatwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
“Nakuagiza Mkurugezi,pamoja na kukiri udhaifu yaliyopo kwenye Idara hiyo ya fedha sasa kuwa makini na anza kufatilia kwa ukaribu na kuhakikisha mikataba iliyopo ya halmashauri inaheshimiwa na kufuatwa na wanaingia kisha kushindwa kuitekeleza basi taratibu za kisheria zichukuliwe ikiwemo kushikilia dhamana aliyoiweka wakati wa kuingia mikataba hiyo na halmashauri”alisema
Mwenyekiti huyo alimtaka Mkurugenzi Mtendaji kupitia upya vyanzo vya mapato vilivyopo na kuangalia upya uwezekano wa kuviboresha vya na kupeleka mapendekezo kwenye kikao cha baraza kitakachofuata ili madiwani waitambue kabla ya kuipitia na kulidhia kuiboresha jambo ambalo litaiwezesha halmashauri hiyo kukusanya mapato mengi zaidi ili kufikia malengo ya kutoa huduma kwa wananchi wake.
Hatua hiyo imeonyesha kuwepo baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wasio waaminifu katika Idara ya fedha ,udhandisi wa barabara na majengo,kilimo,ardhi na maendeleo ya makazi, ugavi na manunuzi kutokana na hoja za mara kwa mara za madiwani kushutumu kuwepo uzembe na miradi mingi kujengwa chini ya viwango kila vikao vya baraza vinapofanyika hali ambayo Mwenyekiti Kiswaga ameonya na kumtaka Mkurugenzi Nnko kuwachukulia hatua watumishi na Wazabuni na kuzuia dhamana zao ikiwemo kuwaondosha watakaoshindwa kufuata taratibu kwa kuzigatia sheria za kazi na mikataba.
Mkurugenzi Nnko alisema kwa wajumbe wa kikao hicho kwamba tayari hatua za kuwafukuza kazi zimeisha tekelezwa na kuwataja waliofukuzwa kuwa ni Winfrida Sanga,Josephat Kajilo,Mathias Bulashila,Bertha Sahani,Emmanuel Mashimba,John Shilunga,Reuben Selestine na John Chululuka huku Samson Aron (Afisa Mtendaji wa kijiji) akihukumiwa kwenda jela miezi 9 kwa kosa la kuiba na kuuza chakula hicho baada ya kufunguliwa kesi na kufikishwa Mahakama ya Wilaya hiyo.
Nnko aliwataja watumishi wengine wa Halmashauri waliochukuliwa hatua ni pamoja na Lutundula Mabimbi aliyekuwa Afisa Kilimo na Mifugo wa Wilaya hiyo aliyefukuzwa kazi mwezi uliopita kwa kukiuka taratibu za kazi kufatia taarifa ya tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma za kugawa Power Trel 6 na Pikipiki 6 zikiwa na mapungufu ya vifaa kubainika huku aliyekuwa Afisa Ugavi na Manunuzi Mbrose Monyiaichi akishushwa cheo baada ya kubainika kuhusika na mapugufu hayo.
Aidha kikao hicho kilipokea taarifa ya kufukuzwa kazi kwa watendaji wa vijiji vinane Wilayani humo waliobainika kufuja fedha za chakula cha msaada kilichotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kisha kusambazwa na halmashauri kwa wananchi wa maeneo yao yaliyokumbwa na tatizo la ukame na kusababisha kuwepo njaa kwa baadhi ya wananchi hao na kutakiwa kununua kwa bei ya chini.
Hatimaye kikao hicho kiliahirishwa mpaka tarehe tajwa....