ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, March 1, 2024

MGOMBEA CCM AJITOSA KUCHUKUA FOMU KUWANIA NAFASI YA UDIWANI KATA YA MSANGANI



NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 


Mgombea wa nafasi ya kiti cha udiwani kata ya Msangani  Ndg.Yohana Chongela kupitia chama cha mapinduzi (CCM) leo  amechukua fomu rasmi ya kuwania nafasi hiyo katika ofisi za serikali ya kata ya Msangani.

Mgombea huyo ambaye alisindikizwa na umati wa wanachama wa CCM,viongozi mbali mbali pamoja na wananchi kwa lengo la kwenda kushudia namna ya jinsi anavyokabidhiwa fomu hiyo ya kugombea.

 Yohana mara baada ya kuchukua fomu hiyo kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi alitoa pongezi zake za dhati kwa viongozi na wanachama wote kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote za hatua za awali.

Aidha mgombea huyo aliwashuru wale wote ambao wamejitokeza kwa wingi katika zoezi zima la uchukuaji wa fomu na kuwaomba wampe ushirikiano katika kuelekea uchaguzi huo.

"Kwa kweli niwashukuru sana viongozi wa chama changu cha mapinduzi,wanachama pamoja na wananchi wenzangu kwa kuonyesha upendo wenu na kujitokeza katika zoezi hili la uchukuaji wa fomu,"alisema Mgombe huyo.

Katika hatua nyingine aliwaomba wanachama na wananchi wote kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote cha maandalizi ya kufanyika kwa uchaguzi huo.


Mgombea huyo ameweza kusindikizwa na  viongozi mbali mbali  wa CCM, Wanachama na Wananchi wa  wakiongozwa na  Domotila Kondo Katibu wa  CCM Kata ya Msangani ambaye ndiye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM  Kata ya Msangani.

Viongozi wengine wa Chama ambao pia waliweza kumsindikiza mgombea huyo ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Kibaha mjini Mwajuma Nyamka pamoja na makada wengine.

Uchaguzi wa kujaza nafasi ya udiwani katika kata ya Msangani ambayo ilikuwa wazi kufuatia aliyekuwa diwani wa kata hiyo kufariki unatarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.

Wednesday, February 28, 2024

WANANCHI KATA YA MSANGANI KUFANYA UCHAGUZI WA UDIWANI MACHI 20


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA

Uchaguzi wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi  ya udiwani  katika kata ya Msangani iliyopo Halmashauri ya mji Kibaha mkoani Pwani unatarajiwa kufanyika machi 20 mwaka huu.


Akizungumza na mwandiishi wa habari hizi ofisini kwake   Katibu wa chama cha mapinduzi  (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini Issack Kalleiya alisema kwamba katika kuelekea uchaguzi huo tayari wameshapokea majina matatu ya wagombea.


Katibu huyo alifafanua kwamba kamati ya siasa ya Wilaya imeshapokea majina matatu ya wagombea wa nafasi hiyo ya udiwani kutoka kamati ya siasa ya kata ya msangani.


Aidha Katibu huyo alisema kwamba baada ya kupokea majina hayo kamati ya siasa ya Wilaya imeyapitia na kuamua kuyapitisha yote kwa pamoja na kuyawasilisha katika kamati ya siasa ya Mkoa ili yaweze kupitiwa.


Pia aliongeza kuwa majina ambayo yamepitishwa kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo ya  udiwani ni pamoja na Gunze Chongela,Khamis Mwande pamoja na Tatu Ashura.

Kadhalika alisema kwamba baada ya hapo  majina hayo matatu yaliyopendekezwa kupelekwa katika kamati ya siasa ya Mkoa ili  kuweza kuteuliwa na   kwenda   kugombea katika  nafasi hiyo ya udiwani.


Katibu huyo aliwaomba viongozi wote na  wanachama wote wa kata ya Msangani kuungana kwa pamoja na kuvunja makundi na kumpa ushirikiano mtu ambaye atachaguliwa kugombea nafasi hiyo.

Alisema kwamba kwa kuwa zoezi la mchakato mzima wa kuwachagua wagombea hao lilianzia kwao hivyo wanapaswa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na kuwa kitu kimoja kwa maslahi ya chama.


 Katibu huyo alitoa wito kwa wanachama hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi huo wa udiwani kuweka tofauti zao pembeni na kujitokeza kwa wingi pamoja na wananchi katika uchaguzi huo ambao utafanyika Machi 20 mwaka  huu.


Hivi karibuni aliyekuwa diwani wa kata ya Msangani kupitia tiketi  ya chama cha mapinduzi Leonard Mlowe alifariki dunia na hivyo kupelekea nafasi yake kubaki wazi.


                   MWISHO