NA MADUKA ONLINE
NI SIKU ya pili sasa tangu wachimbaji kumi na nne (14) ambapo simanzi, masikitiko yameendelea kutanda baina ya jamii na ndugu wa wachimbaji ambao wamefukiwa na udogo kwenye Mgodi wa RZ uliopo Kijiji cha Nyarugusu Wilaya ya Geita hata hivyo jitihada na zoezi la kuwaokoa bado linaendelea .
Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita, Ofisi ya Madini Kanda ya ziwa magharibi ikiyashirikisha makampuni ya Migodi ikiwemo GGM na Busolwa mine ndiyo wanaosimamia zoezi hilo ambapo imeelezwa hatua iliyofikiwa hadi leo saa 1:30 asubuhi walikuwa wamechimba takribani mita 20 kati ya 30 ili kuwafikia wachimbaji hao.
Kufuatia hatua hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga amewataka ndugu na jamaa wa watu 14 waliofukiwa na kifusi ndani ya Mgodi wa RZ kuwa na subira wakati waokoaji wakiendelea na Zoezi hilo.
“Mimi niwatake ndugu na jamaa kuendelea kuvuta subira wakati waokoaji wakiendelea na kutumia mashine kwa ajili ya kuwaokoa watu waliozama chini ya Mgodi huo jambo ambalo hata Mkoa wa Geita umelipokea kwa masikitiko makubwa sana,’’alisema Kyunga.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ametoa kalipio kali kwa wawekezaji ambao hawajali ustawi wa wafanyakazi wake kwa uzembe ambao unaweza kuepukika na kwamba alisikitishwa sana namna mgodi wa RZ ambavyo ulikuwa haujali masuala ya miundombinu yake.
ZOEZI LA UOKOAJI
Ingawa matumaini ya wengi yamefifia kuwapata ndugu hao kutokana na ugumu wa zoezi zima ila kuna mwanga wa matumaini umeanza kuonekana.
Kamishina wa madini kanda ya ziwa magharibi Bw. Yahaya Samamba amesema zoezi hilo litakamilika na watu watakuwa salama kutokana na hewa wanayoipata kupitia mpira unaoingiza kwa kutumia mashine.
Kamishina msaidizi wa madini kanda ya Ziwa Yahaya Samamba ameendelea kuelezea kuwa pamoja na kuunda kamati ya uokoji wamekutana na changamoto kubwa kwa sababu ya duara walikozama watu hao kuwa chini ya kilomita 35.huku akisema wanaendelea kuomba mashine nyingine kutoka kwa makampuni mengine kama zoezi litaonekana kuwa na ugumu.
“Tumeunda kamati ya uokoji na kamati yetu imehusisha makampuni yote yalioleta mashine zao kwa ajili ya uokoaji huo huku naye akiwataka wananchi kutoanza kutoa lawama kwa baadhi ya vyombo vya Serikali na ngazi nyingine kwenye wizara ya madini,, alisema Samamba.
Diwani wa kata ya Nyarugusu yalipo maafa hayo, Swalehe Juma alisema janga hilo limemnyima usingizi na kwamba siku ya jana alilazimika kukesha na waokoaji.
“Mwandishi nakushukuru kwa kuwa nasi kwenye zoezi hili ni kweli mimi nyumbani ni karibu hata kwa miguu naweza kutembea nikafika lakini siwezi kwenda jambo hili limeninyima raha nitawezaje kwenda kwangu wananchi wangu wako ndani ya shimo,’’alisema Juma.
MAONI YA WANANCHI.
Hata hivyo baadhi ya wananchi waliohudhuria kushuhudia tukio hili la aina yake katika wilaya ya Geita ikiwa ni mwanzoni mwa mwaka wa 2017, walisema lawama kubwa wanazielekeza kwa mamlaka za madini kwa kushindwa kujisimamia katika kuhakikisha uchimbaji ulio imara kwenye migodi unaboreshwa.
“kaka hili jambo linasikitisha sana hebu fikiria tangu usiku wa tarehe 26 saa saba usiku mpaka leo siku nyingine ya tarehe 27 tumekutana tena watu wako ndani ya kifusi je watapona licha ya matumaini tunayopewa…Mimi hapa naelekeza lawama kwa ofisi ya Madini Mkoa wa Geita hawakagui migodi ipasavyo,’’alisema Mkazi wa Nyarugusu Saidi Mrisho.
“Kwanza nashangaa nilimsikia jana kamishina wa madini kanda ya ziwa akisema chanzo ni kutokana na miti iliyokuwa imeshikilia ukuta kuwa imeoza sasa hapa najiuliza je, kazi ya ofisi ya madini nini wanakagua nini na je waliwahi kuwaambia kuwa miti hii haifai katika ukaguzi wao inapaswa serikali nayo iwachukulie hatua kubwa kwa uzembe huu haiwezekani,’’alisisitiza.
Katika shughuli za uokoaji wananchi hawakuacha kuipongeza kampuni ya uchimbaji wa madini ya Busolwa Mine inayomilikiwa na mwekezaji mzawa Baraka kwa kujitolea mashine zake za greda kuhakikisha wanafanikisha adhima ya kuwaokoa watanzania 13 pamoja na raia wa china Bw. Meng Juping, ambaye anadaiwa hakuwa na Radio Call kama ilivyokuwa kawaida yake wakati anakwenda kutekeleza majukumu yake ya uzalishaji wa madini ya dhahabu.
|