Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akifungua moja kati ya vitanda 14 vya kujifungulia
vilivyotolewa na Rais Magufuli mapema leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Singida.
Wauguzi wa Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Singida wakifurahia mara baada ya kukabidhiwa vitanda vya
kujifungulia vilivyotolewa na Rais Magufuli.
Mbunge wa Viti Maalum
(CCM) Aisharose Mattembe akizungumza na wauguzi, madaktari na Umoja wa Wanawake
wa Tanzania (UWT) mkoa wa Singida kabla hajakabidhi vitanda 14 alivyopewa na
Rais Magufuli ili avifikishe kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Kaimu Mganga Mkuu wa
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Emmanuel Kimario akimshukuru Rais Magufuli kwa
kuwapatia vitanda vya kujifungulia ili kupunguza uhaba wa vitanda kwa Mkoa was Singida.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akisaidiana na wataalamu wa afya pamoja na Mbunge wa
Viti maalumu Aisharose Mattembe kufunga moja kati ya vitanda 14 vya
kujifungulia vilivyotolewa na Rais Magufuli mapema leo katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Singida.
Halmashauri saba za
Mkoa wa Singida zimeagizwa kununua vitanda kumi kwa ajili ya akina mama kujifungulia
ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe
Magufuli za kuboresha afya ya mama na mtoto.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa agizo hilo mapema leo katika hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Singida mara baada ya kupokea vitanda vya kujifungulia 14,
magodoro 20 na mashuka 50 vyenye thamani ya zaidi ya milioni 121 kutoka kwa
Rais Magufuli.
Dkt Nchimbi amesema
halmashauri zinatakiwa kuiga mfano wa Rais Magufuli anayojali afya kwa ajili ya
wananchi hivyo wanapaswa kutenga kiasi cha shilingi milioni kumi na tatu kwa
ajili ya kununua vitanda hivyo kwa mwaka huu wa fedha.
“Tumezoea kupokea tu
na tumepokea sana vifaa tiba kutoka kwa rais wetu mpendwa Magufuli, hebu
tujifunze upendo wake kwa wananchi, hivyo naagiza kila halmashauri inunue
vitanda kumi vya kujifungulia nadani ya mwaka huu wa fedha”, amesisitiza Dkt
Nchimbi.
Amengeza kuwa akina
mama wajawazito wanatakiwa kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya
kwakuwa kuna huduma bora zaidi huku akiwataka wakunga wa jadi wawasaidie wajawazito
kufika katika vituo hivyo.
Aidha Dkt Nchimbi
amemshukuru Mbunge wa Viti Maalumu Singida Aisharose Mattembe aliaminiwa na
Rais Magufuli na kumtuma kufikisha vitanda hivyo Mkoani Singida huku akimtaka
kuanzisha tunzo ya wakunga watakaosaidia kufikisha akina mama wajawazito katika
vituo vya kutolea huduma za afya.
“Natoa shukrani zangu
za dhati kwa niaba ya wananchi wa Singida kwa Rais Magufuli kwa kuendelea
kutujali wana Singida, pia nakushukuru kwa uaminifu wako mbuge wetu Mattembe
kwa kufikisha vifaa hivi salama ila naomba uanzisishe tunzo ya wakunga wa jadi
watakaowashauri vizuri na kuwafikisha katika vituo vya kutolea huduma za afya
akina mama wajawazito”, amesema Dkt Nchimbi.
Naye Kaimu Mganga
Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Emmanuel Kimario amemshukuru Rais Magufuli
kwa vitanda hivyo vitakavyosaidia kupunguza uhaba wa vitanda, hasa kwa
hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambapo wajawazito wengi wanapenda kujifungulia kwakuwa
na imani napo kutokana huduma bora zinazotolewa.
Dkt Kimario amesema mpaka
sasa bado kuna akina mama wanajifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi jambo
linalohatarisha afya ya mama na motto hivyo wafuate ushauri wa kufika katika
vituo hivyo mara tu wanapo hisi kuwa na ujauzito.
‘Takwimu za kuanzia
kipindi cha mwezi wa saba mpaka wa tisa mwaka huu zinaonyesha kuwa akina mama waliojifungulia
ni 12,431 ambapo kati yao 190 wamejifunguliwa nyumbani, akina mama 78 wamejifunguliwa
kwa wakunga na wengine 258 wamejifungulia
njiani”, amesema Dkt Kimario.
Kwa upande wake Naibu
Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Maulidi Kiaratu amewapongeza wauguzi na madaktari
wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa huduma nzuri wanazotoa hadi kusababisha
wagonjwa wengi kukimbilia hapo.
Amesema, “unakuta
mgonjwa anaacha aspirini pale kituo cha afya Sokoine na kuja hapa Hospitali ya
Mkoa akiwa na imani kubwa hata akipewa dawa ile ile hapa atapata nafuu, hivyo
nawapongeza sana na muendelee na moyo huo wa kuwahudumia vizuri wagonjwa hata
kama tunapata changamoto akati wa kuwalaza wanapokuwa wengi”, amesisitiza
Kiaratu.
Ameongeza kuwa Mbunge
wa Viti maalumu Singida Aisharose Mattembe amekuwa mstari wa mbele katika
kusimamia afya ya mama na mtoto inaboreka Mkoani Singida huku akijitolea vifaa
mbalimbali kama vitanda na mashuka, jambo ambalo ni faraja kwa akina mama na
wananchi wote.