ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, March 19, 2022

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA SIKU YA MISITU DUNIANI.

 MADHIMISHO ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa na Siku ya Misitu Duniani mwaka 2022 yatafanyika Wilayani Magu, mkoani Mwanza yakiongozwa na Kaulimbiu isemayo 'MTI WANGU, TAIFA LANGU, MAZINGIRA YANGU, KAZI IENDELEE'.

Maadhimisho hayo yatafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania yakiwa yameongozwa na malengo makuu mawili ambayo ni kuwakumbusha na kuwahamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa upandaji na utunzaji wa miti kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa bidhaa na huduma za misitu hapa nchini. Akizungumza mbele ya Kamati ya Maandalizi kwa Maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Magu ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo Salum Kalli amesema kwake ni neema kubwa sana na akiishukuru Serikali kwa kuipa fursa wilaya yake kwani kwa kipindi kirefu imekuwa na uhitaji wa miti kutokana na uharibifu wa mazingira uliofanyika. Zoezi la upandaji miti wilayani Magu linatarajiwa kuanza siku hiyo ya Jumatatu ya Tarehe 21 March 2022 kuanzia majira ya saa 12 asubuhi hadi saa 6 mchana, likifuatiwa na mkutano utakaotumika kama darasa la kutoa Elimu iliyojikita katika kukumbusha na kuhamasisha umma wa watanzania juu ya umuhimu wa kupanda miti, kuitunza, na kuihifadhi misitu iliyo katika maeneo yao kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. Kwa kipindi kirefu eneo kubwa la wilaya ya Magu limekuwa kame kutokana na baadhi ya wananchi wake kujihusisha na biashara ya uchomaji mkaa pamoja na uvunaji hovyo wa miti kwaajili ya mbao. Mpaka sasa zaidi ya miti 65,500 imepandwa wilayani humo, huku lengo likiwekwa hadi kufikia tamati ya maadhimisho hayo wilaya iwe imepanda zaidi ya miti laki moja. Maadhimisho hayo ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa ambayo hufanyika Aprili 1 ya kila mwaka sasa yatafanyika Machi 21, 2022 yakiwa yameunganishwa.

BIDEN AMTAKA RAIS XI WA CHINA KUITOISAIDIA URUSI.

 


Rais wa Marekani Joe Biden amemuonya mwenzake wa China Xi Jinping juu ya athari zitakazoikabili Beijing, endapo itatoa msaada wa vifaa kwa Urusi katika uvamizi wake nchini Ukraine. 

Biden ametoa onyo hilo wakati wa mazungumzo kwa njia ya video na rais Xi juu ya mzozo wa Ukraine. 

Msemaji wa Ikulu ya Marekani White House Jen Psaki, amesema rais Biden ameelezea jitihada za Marekani na washirika wake katika kushughulikia uvamizi wa Urusi, ikiwemo kuiwekea vikwazo vikali Moscow. 

Wizara ya mambo ya nje ya China imeandika kwamba rais Xi amemueleza Biden, juu ya kukomeshwa vita ya Ukraine haraka iwezekanavyo na kutoa wito kwa jumuiya ya kujihami NATO kufanya mazungumzo na Moscow, ili kushughulikia kiini cha mzozo wa Ukraine na kupunguza wasiwasi wa usalama wa mataifa hayo jirani.

FAHAMU ZAIDI KUHUSU UGONJWA WA KASWENDE.

 

Kaswende ni ugonjwa unaoambukiza haraka sana, mara nyingi kupitia ngono. Ugonjwa huu huenezwa kwa kugusa moja kwa moja mchubuko wa kaswende (syphilitic sore) uliopo kwenye ngozi. Kwa hiyo njia kuu ni kupitia ngono ya kawaida, ya kutumia midomo na ile ya kinyume na maumbile.

Mara chache ugonjwa huu huweza kuambukiza kwa kubusiana au kugusana miili. Pamoja na kuwa ugonjwa huambukiza kupitia michubuko, mara nyingi michubuko hatarishi haitambulikani. Mtu aliyeambukizwa huwa hajielewi na hivyo kumwambukiza mpenzi wake.

Kaswende haiambukizi kwa kuchangia vyoo, vitasa vya milango, mabwawa ya kuogelea, kuchangia nguo au vyombo vya chakula.

Kaswende husababishwa na bakteria aitwaye Treponema pallidum , ambaye pia huitwa spirochetes kutokana na umbo lake la mzunguko. Viumbe hawa hujipenyeza kwenye ngozi laini inayotanda midomo au sehemu nyeti.

Mwanamke mwenye mimba na ugonjwa huu anaweza kumwambukiza mtoto aliye tumboni kupitia placenta au wakati wa kuzaliwa.

Aina hii ya kaswende huitwa congenital syphilis, na inaweza kusababisha kujifungua mtoto mfu au mtoto akafa muda mfupi baada ya kuzaliwa. Watoto wengi hawaonyeshi dalili wanapozaliwa. Baadaye watoto huota vijipele, hupata matatizo ya meno, na kubonyea kwa mfupa wa pua – hali inayoitwa saddle nose, kuwa viziwi, kuwa na watoto wa jicho na kifafa.

Ugonjwa wa kaswende hugawanywa katika hatua na kila hatua ikiwa na dalili tofauti, lakini wakati mwingine hakuna dalili zitakazojitokeza kwa miaka mingi.

Uambukizaji unatokea kwenye hatua ya kwanza, ya pili na mara chache mwanzoni mwa hatua ya latent phase.

Hatua Ya kwanza Ya Kaswende – Primary Syphilis
Kaswende huanza kama mchubuko mmoja (au zaidi ya mmoja) mgumu usio na maumivu unaojulikana kama chancre kwenye sehemu za siri, kwenye mdomo, au kwenye ngoz,i siku 10-90 (wastani wa miezi 3) baada ya maambukizi.

Mchubuko huu unaweza kubaki hapo bila kuleta usumbufu kwa kipindi kirefu na hata maiaka mingi. Mchubuko huu wa mviringo hutokea kwenye eneo la maambuikizi. Hata bila ya tiba yo yote, mchubuko huu unaweza ukapona wenyewe bila kuacha kovu katika wiki sita.

Hatua Ya Pili Ya Kaswende – Secondary Syphilis
Hatua ya pili inaweza ikadumu kwa mwezi mmoja hadi miezi sita ikianza kama wiki sita hadi miezi sita baada ya maambukizi.

Katika hatua ya pili, vijipele huota mara nyingi vikianzia mgongoni na kuenea mwili mzima, pamoja na kwenye viganja vya mikono na kwenye nyayo. Vijipele hivi huwa vya mviringo vyenye rangi nyekundu au vyenye wekundu wa kahawia.

Michubuko inayofanana na chunjua hutokea kwenye sehemu za midomo na mkundu. Vile kutatokea maumivu ya misuli, homa, kukauka koo, kuvimba tezi, kupunyuka nywele, kukonda na uchovu wa mwili.

Latent Syphilis
Kama tiba ya kaswende ya hatua ya pili haitatolewa, ugonjwa utaendelea kwenye hatua iitwayo latent stage. Katika hatua hii inayoweza kudumu kwa miaka kadhaa, mwili utautunza ugonjwa bila kuonyesha dalili zo zote. Pamoja na kuwa hakuna dalili zo zote zitakazoonekana, ugonjwa huu unaweza kuendelea kwenye hatua ya mwisho.

Hatua Ya Tatu Ya Kaswende – Tertiary syphilis
Asilimia 15 ya watu ambao hawakupata tiba kwenye hatua ya pili ya kaswende watapata kaswende ya hatua ya tatu – tertiary syphilis. Hatua hii inatokea miaka 10 hadi 30 baada ya dalili za mwanzo za kaswende. Dalili za kaswende za hatua hii ni pamoja na kushindwa kumudu matumizi ya viungo vya mwili, ganzi, upofu, ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu, madhara kwenye moyo na mishipa ya damu, madhara kwenye ini, mifupa na maungio ya mifupa. Kifo huweza kutokea kutokana na uharibifu wa viungo vya mwili.

Kuwahi kumpa tiba mgonjwa wa kaswende ni muhimu kwani kuchelewa kunaweza kumletea madhara makubwa ya mwili au kifo. Kama ugonjwa haujazidi mwaka mmoja, mara nyingi dozi moja ya ya penicillin hutosha.

Kaswende iliyoendelea kwenye hatua nyingine, dozi nyingine zitahitajika.

Thursday, March 17, 2022

JAPAN YAZIONA MELI ZA KIVITA ZIKIELEKEA UKRANE.


Meli nne kubwa za kivita za Urusi zimeonekana zikisafiri karibu na visiwa vya Japan vya Honshu na Hokkaido zikielekea Ulaya, Reuters inaripoti.


Picha zilizochapishwa na wizara ya ulinzi ya Japani zilionyesha kile kilichoonekana kama malori ya kijeshi ndani ya meli hizo Zilizokuwa zikipita.


Alipoulizwa iwapo huenda zilikuwa zinaelekea Ukraine, msemaji wa waziri wa ulinzi wa Japan aliambia Reuters, "inawezekana".


Operesheni ya kijeshi ya Urusi haijaenda kama ilivyopangwa hadi sasa, huku vifaa vya kijeshi vikiharibiwa kwa kiwango kikubwa kuliko ilivyotarajiwa, kulingana na wachambuzi wa kijeshi.

Wednesday, March 16, 2022

WATU 52 WAUAWA KASKAZINI MASHARIKI MWA DRC

 


Zaidi ya watu 50 waliuawa kaskazini mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mashambulizi yaliyofanywa na waasi wanaodhaniwa kuwa wa kundi la ADF, chanzo kutoka eneo hilo kilisema Jumatatu.


Christophe Munyanderu anayefanya kazi na shirika lisilokuwa na kiserikali linalotetea haki za binadamu katika mkoa wa Ituri, alisema mauaji hayo ni kufuatia mashambulizi kwenye vijiji kadhaa.


Alisema waasi wa ADF walishambulia vijiji vinne Jumapili na kuua watu 19, katika wilaya ya Irumu.


Jana Jumatatu, waasi hao walishambulia vijiji vingine viwili na kuua watu 33, ameongeza Munyanderu.


Alisema jumla ya watu 52 waliuawa Jumapili na Jumatatu.


Mauaji hayo yanafuatia mauaji ya watu wengine 30 yaliofanywa na waasi wanaoshukiwa kuwa wa kundi la ADF huko Kivu kaskazini mwishoni mwa wiki iliyopita.

DKT GWAJIMA AUNGURUMA LIVE TOKA NEW YORK MAREKANI.

 
Na WMJJWM- New York Marekani

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Tanzania inatambua umuhimu wa  ushiriki wa wanawake kuanzia ngazi ya chini kwenye jamii ambayo itawezesha kupata matokeo chanya yatakayotoa majibu na tija kwa changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, mazingira na majanga kwa kuzingatia usawa wa jinsia.  


Dkt  Gwajima ameyasema hayo akiwa jijini New York nchini Marekani katika Mkutano wa Mawaziri ndani ya Mkutano wa mkutano wa 66 wa hali ya wanawake duniani.

Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa Tanzania inashiriki kikamilifu kwenye juhudi za kutunza mazingira, kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa na majanga na kwa sababu hiyo imesaini makubaliano mbalimbali ikiwemo azimio la Beijing, azimio la umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa(UNFCC), azimio la Kyoto 1997, ajenda 2030 na CEDAW.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima amesema  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan  ameridhia kuwa kinara wa utekelezaji wa jukwaa la kizazi chenye usawa kwenye eneo la uwezeshaji wa haki za kiuchumi, eneo linalolenga kuwezesha uhakika wa upatikanaji wa chakula, uchumi na maisha bora kwa ujumla. 

Waziri Dkt. Gwajima ameongoza ujumbe wa Tanzania New York nchini Marekani kushiriki mkutano wa 66 wa hali ya wanawake duniani uliojumuisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Mwajuma Magwiza, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia Badru Abdulnoo na Maafisa wengine wa Wizara

DKT. KIJAJI AIAGIZA FCC KUFANYA TATHIMINI KATIKA SOKO ILI KUBAINI MAPUNGUFU YALIYOPO KATIKA KUMLINDA MTUMIAJI

 

Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza wakati akifungua Kongamano la wadau katika kilele Cha maadhimisho ya siku ya haki za mtumiaji Duniani leo hii Jijini Mwanza 

Naibu Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BOT), Dkt. Benard Kibesse akizungumza kwenye Kongamano hilo leo hii Ijumanne Machi 15,2022 katika ukumbi wa Gold crest uliopo Jijini Mwanza  

Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (FCT) Salma Maghimbi akizungumza kwenye Kongamano 

Mwenyeki wa Tume ya Ushindani (FCC), Dkt. Aggrey Mlimuka akizungumza kwenye Kongamano la maadhimisho ya siku ya haki za kumlinda mtumiaji Duniani katika ukumbi wa Gold crest uliopo Jijini Mwanza 

Baadhi ya wadau waliohudhulia kwenye Kongamano lililofanyika leo hii Jijini Mwanza 

Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji (mwenye ushungi wa pinki)akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali waliohudhulia Kongamano la maadhimisho ya siku ya haki za mtumiaji Duniani.Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji ameiagiza Tume ya Ushindani (FCC), kufanya Tathimini katika soko ili waweze kubaini mapungufu yaliyopo katika kumlinda mtumiaji sanjari na mtumiaji wa huduma za kifedha ikiwemo huduma za fedha kidigitali.

Maagizo hayo ameyatoa jana jumanne Machi 15,2022 Jijini Mwanza wakati akifungua Kongamano la wadau katika kilele Cha maadhimisho ya siku ya haki za mtumiaji Duniani.

Dk.Kijaji amesema kwa kutambua changamoto zinazoambatana na kuunganika na mifumo ya fedha kidigitali,Kama vile tatizo la usalama hafifu wa kimtandao,ipo haja ya kuliangalia eneo hili kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha mtumiaji wa huduma za fedha analindwa dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza sokoni katika miamala na huduma zinazohisisha matumizi ya fedha kidigitali.

Ameongeza kuwa Tume ya Ushindani ifanye Tathimini ya matokeo ya utafiti husika na kuishauri Serikali kuhusiana na mahitaji mapya ya kisera,kisheria,taratibu na kanuni ili kuhakikisha kuwa jukumu la msingi la kumlinda mtumiaji wa Tanzania hususani kwa sekta zisizo chini ya Mamlaka za udhibiti wa kisekta linaboreshwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC) Dkt. Aggrey Mlimuka amesema kuwa Kongamano hilo ni mwendelezo wa utekelezaji wa jukumu la kupeleka elimu kwa umma kuhusu haki,wajibu na nafuu zinazopatikana kwa watumiaji kupitia sheria namba 8 ya Ushindani ya mwaka 2005.

Dkt Mlimuka ameeleza kuwa Tume hiyo ipo kwenye mchakato wa kurekebisha sheria yake ili kuwezesha kushughulikia masuala ya kumlinda mtumiaji ipasavyo hususani katika kumlinda mtumiaji kidigitali.

“Tanzania tayari tumesha andaa mfumo wa Kitaifa wa kuwainda watumiaji wa huduma za kifedha na nimatumaini yetu kuwa baada ya Kongamano hili watanzania watakuwa wamepata elimu itakayowawezesha kujua haki zao nakuzifuatilia katika kazi zao”,amesema Mlimuka.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (FCT), Salma Maghimbi ametoa wito kwa wanasheria waliohudhulia Kongamano hilo, kutambua kuwa utekelezaji wa sheria ya Ushindani ni fursa muhimu kwao kujifunza zaidi kuhusu kanuni na mbinu za kuendesha mashauri ya Ushindani na kumlinda mlaji ili waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uwasilishaji wa mashauri.

Awali akizungumza katika Kongamano hilo Naibu Gavana wa Benki Kuu (BOT), Dkt. Benard Kibesse amesema utafiti wa fedha za kidigitali unategemea sana uwepo wa mifumo bora ya kisheria na usimamizi ili kuhakikisha wanakuwa na usawa wa watumiaji wa huduma za kifedha.

Monday, March 14, 2022

TASAC YAWATAKA WAFANYABIASHARA MPAKANI KUACHA KUTUMIA NJIA ZA PEMBENI KUPITISHA MIFUGO

 

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Shirika la Meli Tanzania (TASAC) Captain Mussa Mandia kulia akisisitiza jambo wakati wa ziara yake mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Shirika la Meli Tanzania (TASAC) Captain Mussa Mandia kulia akisisitiza jambo wakati wa ziara yake mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Shirika la Meli Tanzania (TASAC) Captain Mussa Mandia kulia akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Tanga Captain Christopher Shalua wakati wa ziara yake mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Shirika la Meli Tanzania (TASAC) Captain Mussa Mandia kushoto akimsikiliza kwa umakini mmoja wa watumishi wanaofanya kazi eneo la mpakani kupitia wakala huo wakati wa ziara yake mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Shirika la Meli Tanzania (TASAC) Captain Mussa Mandia aliyekaa katikati akifuatilia kwa umakini maelezo mbalimbali mara baada ya kufika eneo hilo la mpaka
Watumishi kutoka taasisi mbalimbali zinazofanya kazi mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)

NA OSCAR ASSENGA, MKINGA

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Shirika la Meli Tanzania (TASAC) Captain Mussa Mandia amewataka wafanyabiashara wa mifugo mipakani nchini kutoa ushirikiano kwa wakala huo huku ikiwataka pia kuacha tabia ya kutumia njia za pembeni badala yake wapitishe kwenye mpaka huo ili serikali iweze kupata mapato yake

Captain Mandia aliyasema hayo leo wakati wa ziara yake kutembelea mpaka huo unaotenganisha kati ya nchi ya Tanzania na Kenya eneo la Horohoro ili kuweza kujifunza na kuona shughuli zinazofanyika kwenye maeneo ya mpaka huo.

Akiwa kwenye mpaka huo aliwatataka wafanyabiashara waongeza ushirikiano ili kuiwezesha Serikali iweze kukusanya mapato yake ikiwemo kuacha kutumia njia pembeni kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria

“Kama leo nipo hapa mpakani wa Kenya na Tanzania eneo Horohoro nimeambiwa usafirishaji mifugo umepungua sana kutoka 10,000 mpaka 3000 sawa na asilimia 30 ya mifugo sababu kubwa ni ukwepaji wa kupitisha mifugo kwenye kituo hiki kwa sababu mbalimbali

Mwenyekiti huyo wa bodi alisema wao kama Wakala wataliangalia hilo na kujaribu kuboresha mazingira na kuhakikisha wafanyabiashara wanafaidika na serikali haipotezi mapato.

“Niwaambie kwamba acheni kutumia njia za pembeni mkiwa na malalamiko yenu yafikisheni kwetu nasi tutaona namna bora ya kuboresha biashara ya mifugo hapa mpakani “Alisema Mwenyekiti huyo wa Bodi.

Aidha alionyeshwa kufurahishwa na hatua ya wakala huo mpakani hapo kushirikiana vema na mamlaka nyengine zilizopo mpakani na kuweza kuboresha makusanyo ya kodi ya nchi yetu yameonekana kwa asilimia 500 ndani ya mwaka mmoja.

Alisema hilo ni jambo muhimu na linahitaji kutazamwa kwa jicho zuri zaidi ili kuweza kuliendeleza na kuongeza wigo mkubwa zaidi ya ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Sunday, March 13, 2022

AUAWA UGOMVI WA KUGOMBEA CHENJI YA SHILINGI 400

 


DEREVA wa bajaji na mkazi wa Miyuji, jijini Dodoma mwenye umri wa miaka 22, ameuawa kwa kupigwa na kipande cha bomba la chuma nyuma ya shingo  kutokana na ugomvi uliotokea baada ya kununua sigara na muuzaji kumgomea kurudisha chenji yake Sh 400.


Kamanda ya Polisi, Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga alisema mauaji hayo yalifanyika Machi 3,  mwaka huu katika Mtaa wa Tofiki, Kata ya Viwanda I Dodoma Mjini baada ya kutoa Sh 500 na kununua sigara ya Sh 100.


Alisema mtuhumiwa wa mauaji hayo ana umri wa miaka 22 na mkazi wa Chinyoya. Kamanda Lyanga alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa.


Katika tukio lingine mwanamke mwenye umri wa miaka 40 na mkazi wa Mtumba  ambaye ni mfanya usafi alikutwa mtaroni akiwa ameuawa baada ya kukabwa shingo na kubakwa. Polisi inaendelea kufuatilia tukio hilo la Machi 9, mwaka huu.


Wakati huo huo, polisi kwa kushirikiana na askari wanyamapori walifanya upekuzi kwenye nyumba ya kulala wageni ya Highway iliyopo Kata ya Mtera, Wilaya ya Mpwapwa na kufanikiwa kukamata pembe za ndovu vipande vinne vyenye uzito wa kilogramu 10.65 vyenye thamani ya Sh milioni 69.4.

SIMBA KAMA KAWA YATAKATA KWA MKAPA

 


Klabu ya Simba imejikita kileleni kwenye msimamo wa kundi D la kombe la shirikisho barani afrika baada ya kuchomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya klabu ya Rs Berkane ya Morocco kwenye mchezo uliofanyika katika dimba la Benjamin Mkapa jiji Dar es Salaam.


Mchezo huo ambao ulikuwa ni mzunguko wa nne wa kundi hilo ,goli la Simba lilifungwa na kiungo mshambuliaji kutoka Senegal Pape Ousmane Sakho dakika ya 44 na kuwafanya klabu ya Simba kufikisha alama 7 na kuwashusha RS Berkane waliokuwa wanaongoza wakiwa na alama 6.


Nyota wa Simba Cloutas Chama ambaye kanuni za mashindano zinabana kushiriki mashandano haya kutokana na jina lake kujumuishwa  kwenye usajili wa RS Berkane amesema ushindi huu unawapa nguvu ya kuipigania nembo ya klabu ya Simba kimataifa zaidi.


"tunacheza mechi kwa ajili ya kuipambania klabu yetu na ushindi huu umetupa nafasi kubwa kwenye kundi letu na tutaendelea hivyo hivyo na sasa kundi lipo wazi na tunapaswa kupambana ili kufanya vizuri kwenye michezo inayokuja"amesema Chama


Simba sasa imesaliwa na michezo miwili kwa ajili ya kukamilisha hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika huku mchezo unaofuata Simba wakisafiri kuwafuata klabu ya Asec Mimosas ya Ivory Coast watakaocheza nao mnamo March 20 mjini Abidjan.

KAULI YA MAJALIWA KUHUSU WAFUGAJI KUTOKA NGORONGORO WANAOHAMIA HANDENI.

 


Waziri mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima kushirikiana na wakuu wa wilaya za mkoa huo katika mpango wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya wafugaji kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na kutoa elimu na taarifa kwa wananchi kuhusu mpango huo.


Akizungumza na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali kwenye ziara yake ya siku moja katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni kwa lengo la kuwasikiliza wananchi na kukagua ujenzi wa nyumba hizo leo Jumapili Machi 13, 2022, Majaliwa amesema ni lazima wananchi kuanzia ngazi ya wilaya, kata mpaka vijijiji pamoja na viongozi wao wapewe taarifa kuwa ni kitu gani kinaendelea kwenye maeneo.


“Hapa kuna wenyeji mkuu wa wilaya, wabunge, viongozi wa halmashauri na vijiji, mkuu wa mkoa kaeni chini muwambie ni kitu gani kinafanyika kwenye eneo lao, kwamba kuna mradi huo ili na wao waweze kutoa ushirikiano kwenye kupokea wageni wanaofika hapo,”amesema Majaliwa.


Kauli hiyo ya Majaliwa imekuja baada ya mwenyekiti wa kijiji cha Msomera, Martin ole Ikayo kumueleza waziri mkuu  kuwa hawana taarifa kamili kuhusu ujio wa wageni hao ila kwa kuwa yeye amewapa  taarifa basi huduma za kijamii ziboreshwe kwenye kijiji chao.


Amesema idadi ya watu itaongezeka hivyo ni vizuri serikali iharakishe kuboresha huduma zote muhimu katika sekta za afya, elimu, maji na matumizi bora ya ardhi ili kusitokee tatizo lolote baadaye. 


Mbunge wa Handeni vijijini, John Sallu amemuomba waziri mkuu kwa kuwa wageni hao wanafikia Handeni basi fursa zinazopatikana serikali iangalie ni jinsi gani wananchi wa Handeni nao watanufaika nayo.

MWANDISHI WA HABARI WA MAREKANI AUAWA UKRANE.

 


Mwandishi mmoja wa habari raia wa Marekani, Jumapili aliuawa kwa kupigwa risasi, na mwingine kujeruhiwa katika mji wa Irpin, kitongoji kilicho mstari wa mbele, wa mapigano, kaskazini magharibi mwa Kyiv, nchini Ukraine, madaktari na mashahidi wameliambia shirika la habari la AFP.


Mmarekani huyo ametajwa kama mpiga picha wa video wa miaka 50, Brent Renaud, wa New York.


Danylo Shapovalov, daktari wa upasuaji aliyejitolea kwa ajili ya ulinzi wa Ukraine, alisema mmoja wa Wamarekani alikufa papo hapo, na wa pili kupewa huduma ya matibabu.


Wanahabari wa AFP mjini Irpin, walisema waliuona mwili wa mwathiriwa. Mwathiriwa wa tatu, raia wa Ukraine, ambaye alikuwa kwenye gari moja na Wamarekani, pia alijeruhiwa.


Maafisa wa Ukraine walivilaumu vikosi vya Russia kwa shambulzi hilo, lakini hali halisi haikufahamika mara moja.


Wanahabari wa AFP waliripoti kusikia milio ya risasi mizinga katika eneo hilo.


Kadi ya utambulisho ya New York Times ilikuwa miongoni mwa karatasi alizokuwa nazo mfukoni mwanahabari huyo, na kusababisha kuenea kwa ripoti kwamba alikuwa mfanyakazi wa gazeti hilo.


Hata hivyo, naibu mhariri wa New York Times alisema kwamba Brent, alikuwa mpiga picha na mtengenezaji wa filamu mwenye kipawa ambaye alikuwa amechangia The New York Times kwa miaka ya nyuma.


Mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine yameendelea kushabisha maafa, na kupelekea mailioni ya watu kukimbilia nchi kadhaa, majirani wa Ukraine.

TPC, UZIKWASA WATETA

 

KATIBU Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Tanga (TPC) Mbonea Herman katikati akipokea majarida ya Shirika la Uzikwasa kutoka kwa Meneja wa Radio Pangani FM inayomilikiwa na Shirika hilo kulia ni Mhariri Mkuu wa Radio hiyo Erick Mallya wakati walipofika ofisi za klabu kwa ajili ya kujitambulisha na kuomba ushirikiano na klabu hiyo mapema leo

KATIBU Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Tanga (TPC) Mbonea Herman katikati akipokea majarida ya Shirika la Uzikwasa kutoka kwa Meneja wa Radio Pangani FM inayomilikiwa na Shirika hilo kulia ni Mhariri Mkuu wa Radio hiyo Erick Mallya wakati walipofika ofisi za klabu kwa ajili ya kujitambulisha na kuomba ushirikiano na klabu hiyo mapema leo
KATIBU Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Tanga (TPC) Mbonea Herman katikati akipokea majarida ya Shirika la Uzikwasa kutoka kwa Meneja wa Radio Pangani FM inayomilikiwa na Shirika hilo kulia ni Mhariri Mkuu wa Radio hiyo Erick Mallya wakati walipofika ofisi za klabu kwa ajili ya kujitambulisha na kuomba ushirikiano na klabu hiyo mapema leo