ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, March 13, 2022

KAULI YA MAJALIWA KUHUSU WAFUGAJI KUTOKA NGORONGORO WANAOHAMIA HANDENI.

 


Waziri mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima kushirikiana na wakuu wa wilaya za mkoa huo katika mpango wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya wafugaji kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na kutoa elimu na taarifa kwa wananchi kuhusu mpango huo.


Akizungumza na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali kwenye ziara yake ya siku moja katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni kwa lengo la kuwasikiliza wananchi na kukagua ujenzi wa nyumba hizo leo Jumapili Machi 13, 2022, Majaliwa amesema ni lazima wananchi kuanzia ngazi ya wilaya, kata mpaka vijijiji pamoja na viongozi wao wapewe taarifa kuwa ni kitu gani kinaendelea kwenye maeneo.


“Hapa kuna wenyeji mkuu wa wilaya, wabunge, viongozi wa halmashauri na vijiji, mkuu wa mkoa kaeni chini muwambie ni kitu gani kinafanyika kwenye eneo lao, kwamba kuna mradi huo ili na wao waweze kutoa ushirikiano kwenye kupokea wageni wanaofika hapo,”amesema Majaliwa.


Kauli hiyo ya Majaliwa imekuja baada ya mwenyekiti wa kijiji cha Msomera, Martin ole Ikayo kumueleza waziri mkuu  kuwa hawana taarifa kamili kuhusu ujio wa wageni hao ila kwa kuwa yeye amewapa  taarifa basi huduma za kijamii ziboreshwe kwenye kijiji chao.


Amesema idadi ya watu itaongezeka hivyo ni vizuri serikali iharakishe kuboresha huduma zote muhimu katika sekta za afya, elimu, maji na matumizi bora ya ardhi ili kusitokee tatizo lolote baadaye. 


Mbunge wa Handeni vijijini, John Sallu amemuomba waziri mkuu kwa kuwa wageni hao wanafikia Handeni basi fursa zinazopatikana serikali iangalie ni jinsi gani wananchi wa Handeni nao watanufaika nayo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.