ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, December 24, 2016

ASKARI POLISI WILAYA YA RORYA WALALAMIKIWA KWA KUNYANYASA WANANCHI NA BODABODA.

Askari wanapopata fedha za waendesha badaboda hufanya tendo la kugawana na hata kudiliki kununua bidhaa kwa fedha ambayo wameipata kwa mazingira yenye kunyanyasa bodaboda na wananchi kwenye maeneo ya magulio, minada na masoko maeneo mbalimbali ya Kata za Jimbo la Rorya kama walivyonaswa na camera yetu  hivi karibuni maeneo ya gulio na mnada wa Nyamaguku.
2
3
4
5
6

 Na Peter Fabian, RORYA.

ASKARI Polisi wa Kanda maalumu ya Tarime na Rorya waingia matatani ni baada ya kudaiwa kuwanyanyasa wananchi wa baadhi ya maeneo ya Kata za Jimbo la Rorya Mkoa wa Mara wanapokwenda kwenye magulio na minada ya mifugo huwavizia maeneo ya porini na kuwakamata na kuwashikilia hadi wanapotoa fedha ndipo huwaachia .

Wakizungumza na GSENGO BLOG kwa nyakati katika maeneo ya Kata za Shirati, Utegi, Labwoli, Kumuge, Kisumwa, Nyamuga wakiomba kuhifadhi majina yao kwa kuhofia kukamatwa na askari Polisi wamelalamikia kuwepo kero hiyo na unyanyasaji unaofanywa na askari hao hasa siku za magulio na minada ya Nyamaguku, Shirati, Mtana na Randa.

Ni askari wa Trafiki na Polisi kutoka Kituo cha Polisi Shirati wakiwa wamezingilwa na wananchi na waendesha pikipiki baada ya kuzikamata bodaboda zao na kuzishikilia huku ikidaiwa kuwatoza fedha kwa nguvu bila kuwapatia stakabadhi (risti) iwapo walibainika kuwa na makosa ambapo utaratibu hutozwa faini na kuandikia stakabadhi badaboda hao, lakini sasa ni tofauti imedaiwa kuwa ni kero na unyanyasaji kwa badaboda katika magulio, masoko na minada ya mifugo maeneo ya Shirati, Nyamaguku, Utegi, Randa, Mtama Jimbo la Rorya, umedaiwa kugeuzwa mradi wa kujipatia fedha, badaboda huwafukuza kwa gari la OCD Utegi, OCD Shirati na OCD Kinesi wa Kanda Maalum ya Tarime na Rorya huku askari Polisi wa kawaida wao hutumia pikipiki kuwafukuza hadi porini na huwapiga wanapowakamata na huwasababishia ajari na kuwaacha wakiwa majeruhi kama walivyonaswa na camera yetu hivi karibuni huko Shirati.
“Siku ya gulio na mnada wa mifugo katika maeneo ya Nyamaguku, Shirati, Mtana na Randa wananchi, wafanyabiashara  na waendesha pikipiki (bodaboda) askari polisi huja kwa wingi wakiwa na silaha kwenye pikipiki (bodaboda) sita wakiwa wamebebana wanazokuwa wamezikamata kwa wananchi na wengine kwenye magari ya Polisi PT 1691ya Kanda maalumu Tarime na Rorya na PT ya OCD Utegi,”alieleza mmoja wa wananchi.

Aidha mmoja wa wananchi hao alieleza kwamba askari hao wamekuwa wakivizia siku za magulio, minada na masoko ambapo huwaja kwa wingi na wamekuwa na tabia ya kuwaamusha usiku wa kuanzia saa 10:00 alfajiri hadi saa 2:00 asubuhi wakidai wanasaka nyavu haramu na samaki wachanga na wakikosa huwavizia badaboda na kuwafukuza kwa gari na pikipiki hadi wawapatie fedha.

“Hii ni kero kubwa kwa vijana waendesha bodaboda na wananchi wanaotumia usafiri huo umeonekana kuwa ni mradi wa askari Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya ambao wamekuwa wakiwakamata na kuwaomba fedha na wanapokosa huwaomba hadi kuku na hata wanapodai stakabadhi (risti) huambiwa kwa kufokewa huku wakitishiwa pikipiki zao kwenye magari,”alisema Kiongozi wa bodaboda mmoja.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Rorya Mkoa wa Mara, Lameck Airo (CCM), aliwaeleza waandishi kuwa amekuwa akipata malalamiko ya wananchi na viongozi wa vijiji na Kata kuwepo kwa maaskari wanaowanyanyasa na kuwakamata waendesha bodaboda kwa kuwavizia maeneo ya porini na kuwakamata kisha kuwatoza fedha hadi kuwaomba kuku na mbuzi bila kuwambia makosa yao.

“Nimekuwa nikikutana na Wakuu wa Polisi kila mara na hata kumueleza Kamanda wa Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya (RPC) Andrew Sata lakini hali hiyo husitishwa kwa muda wa wiki moja hadi mbili lakini huibuka kwa nguvu kubwa na hii imekuwa kero kwa wananchi na hasa bodaboda kweli wananyanyasika kwa kukamatwa na kuombwa fedha zisizokatiwa stkakabadhi,”alisema.

Mbunge Airo ameeleza kuwa kufatia hatua ya wananchi hao kulalamika atalifikisha suala hilo kwa IGP, Ernest Mangu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba pamoja na uongozi wa Serikali Mkoa wa Mara kwa kuwa askari hao katika baadhi ya vituo wamekuwa wengi zaidi ya mahitaji ambapo alitolea mfano wa Kituo cha Kinesi kina sakari zaidi ya 100 ambao kazi kubwa kwao ni kutafuta fedha kwa wananchi.

“Tunashukuru askari Polisi waliokuwa wameletwa kwa wingi wakati wa kuanzishwa Kanda maalumu kwa lengo la kuzuia wizi wa mifugo na mapigano ya wakurya na wajaluo wakati ule ambapo walisaidia sana na kumaliza lakini sasa wameonekana askari hao kuwa kero ya kunyanyasa wananchi kwa vitendo hivyo na hili linahitaji askari hao wapelekwe kwenye mahitaji,”alisisitiza.

Naya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya (RPC), Andrew Sata alipotafutwa kwa njia ya simu alisema kwamba taarifa hizo ndo kwanza anazisikia na kuomba alifanyie kazi suala hili na kisha atalitolea taarifa na kwa sasa hawezi kulizungumzia kwa kuwa ni kipindi cha sikukuku na kazi kubwa ni kuimalisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya Kanda hiyo.

NANI KAKWAMBIA ETI WATU HAWATOENDA MAKWAO MSIMU HUU...? MAGARI YAFURIKA MOSHI FOLENI YATISHA.

MOSHI:- Mji wa Moshi umekuwa na msongamano mkubwa wa magari katika barabara kuu ya kuingia mjini kutokea Dar es Salaam.
Msongamano huo wa ongezeko la magari unalosababishwa na utamaduni wa wenyeji wa Mkoa Kilimanjaro, kurejea nyumbani kutokea mikoa mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

Awali, ilitarajiwa kusingekuwapo na ongezeko hilo la wageni kwa mwaka huu, kutokana na ugumu wa maisha uliotokana na kupungua kwa mzunguko wa fedha mitaani.

Hata hivyo, juzi saa 12.00 jioni hadi saa 2.00 usiku, kuliibuka msongamano wa magari kuanzia eneo la Mbwaharuki hadi Magereza Barabara Kuu ya Dar es Salaam- Moshi.

WATU WAWILI WANASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA KUCHOMA OFISI YA SHULE MKOANI SHINYANGA.

Jeshi la polosi mkoani Shinyanga linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuchoma ofisi ya mwalimu mkuu shule ya msingi Ibanilo iliyoko katika kijiji cha Igembya kaya ya Nyida wilayani Shinyanga.
ITV imefika katika shule hiyo na kukuta wakazi wa maeneo hayo wakiwa katika hali ya taharuki huku wakidai kuwa kumekuwepo na mgogoro wa ardhi unaufukuta muda mrefu kati wakazi wawili ambao majina yao yamehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi na uongozi wa shule hali ambayo imekuwa ikisababisha vitisho vya mara kwa mara na uharibifu wa mali za shule.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ibanilo Bw.Shabani Jumanne ameainisha hasara iliyotokana na kuchomwa kwa ofisi hiyo na kuomba msaada wa haraka kwa wadau wa elimu kabla shule hazijafunguliwa mwezi January Mwakani huku diwani wa kata ya nyida Mh.Selemani Segeleti sakikiri kiwepo kwa mgogoro wa muda mrefu ambao amekua akiushughulikia bila mafanikio.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa jeshi mla polisi mkoani Shinyanga ACP Muliro Jimanne Muliro amesema licha ya kuwakamata watu hao wawili kwa tuhuma za kuhusika kuchoma na kuharibu mali ya umma jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili na hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo watuhumiwa kufikishwa mahakamani.

RAIS ATOA ZAWADI YA KRISMAS KWA WAZEE WASIOJIWEZA.

Rais John Pombe Magufuli ametoa msaada wa chakula na vinywaji baridi kwa wazee wanaoishi katika kambi ya Bukumbi mkoani Mwanza ikiwa ni zawadi ya Christmas. 

Friday, December 23, 2016

SABODO AMSHAURI RAIS MAGUFULI ABADILISHE FEDHA.

Mfanyabiashara maarufu nchini, Mustafa Jaffar Sabodo akizungumza jijini Dar es Salaam, kuhusu wafanyabiashara wanaoficha fedha majumbani na kumshauri Rais John Magufuli abadilishe fedha. (PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA)

Mfanyabiashara maarufu nchini, Jaffar Sabodo (73), amemshauri Rais John Magufuli abadilishe fedha ili kubana wafanyabiashara wakwepa kodi na kuficha fedha majumbani.

Aidha, amesema kutokana na utendaji wa Rais, haoni sababu za vyama vya upinzani kuendelea kumpinga, na badala yake waache siasa na waungane naye kujenga Tanzania mpya.

Kauli ya mfanyabiashara huyo iliungwa mkono na wachumi waliozungumza na gazeti hili kubainisha kuwa njia nzuri zaidi ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupunguza masharti kwa benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye benki iwe kubwa jambo ambalo litafanya watu wakiweka fedha benki wapate faida.

Sabodo alitoa ushauri huo jana alipozungumza na JAMBO LEO katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Dar es Salaam, ambapo alisema licha ya hatua nzuri za Serikali ya Rais Magufuli kiuchumi na kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu na ufisadi, wapo walioficha mabilioni ya fedha nyumbani badala ya benki ili kukwepa kodi.

Sabodo akisisitiza jambo.
“Rais anafanya kazi nzuri, lakini ni wengi walioficha fedha nyumbani. Watanzania wanakufa njaa, wengine wameficha fedha. Hapo nashauri Rais abadilishe fedha hasa noti za Sh 5,000 na Sh 10,000. Hatua hiyo itasaidia kukabili ubadhirifu unaofanywa na watu wenye nia mbaya, lakini pia inaweza kuokoa uchumi na kufikia ndoto ya kuwa na Tanzania Mpya,” alisema Sabodo.

Aliongeza: “Kwa maoni yangu, hatua hiyo ya kubadilisha fedha ichukue kati ya mwezi mmoja na mmoja na nusu, watabainika wengi walioficha fedha nyumbani na hali ya uchumi itabadilika.”

Akifafanua, Sabodo ambaye ni mzaliwa wa Lindi, alisema India, Pakistan na Venezuela ziliwahi kukumbwa na hali kama iliyopo sasa nchini, lakini hatua ya kubadilisha noti ilizisaidia kuimarisha uchumi na bajeti zao.

“Watu wanaiba fedha nyingi, wanazificha chini ya magodoro, ili kumaliza hali hiyo ni muhimu noti zikabadilishwa hali itakayomlazimisha kila aliyeficha fedha kuzitoa, hapo wapo watakaokimbia nchi,” alisema Sabodo huku akitaja baadhi ya watakaokimbia hatua hiyo ikichukuliwa.

Sabodo alitoa kauli hiyo wakati Rais Magufuli ameshatoa kauli kuwataka walioficha fedha majumbani kuziacha ziingie kwenye mzunguko huku akionya wasipofanya hivyo anaweza kuamua kuzibadili ili wakose mahali pa kuzipeleka. 

Magufuli alitoa kauli hiyo Septemba kwenye mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi ambapo alisema watu hao wamekuwa na utaratibu wa kutoa fedha zao benki na kuzificha kwa kuogopa kuwa atabaini kiasi walichonacho.

Wachumi
Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Profesa Damian Gabagambi alisema: “Kuendesha uchumi hakutakiwi nguvu sana. Uchumi unajengwa kwa imani, mtu yeyote anayeendesha uchumi anatakiwa kuijenga hiyo imani na ikuzwe.

“Chochote kinachofanyika na kuua imani kinavuruga uchumi, ukiona watu wanaficha fedha hilo si tatizo, ni kwamba kuna kitu ambacho ni tatizo, kuficha fedha ndio kujihami kwao.”

Alisema njia nzuri ya kufanya watu walioficha fedha kuzitoa, ni BoT kupunguza masharti inayowekea benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye benki iwe kubwa, jambo ambalo litafawanya watu kutoficha fedha kwa maelezo kuwa wakipeleka fedha kwenye benki hizo, watapata faida.

Alisema riba inayotozwa kwenye benki inapangwa na BoT na kuitaka benki hiyo kufanya marekebisho ili kusaidia wanaoweka fedha kwenye benki kupata faida.

“Ila kama wana hakika fedha zimefichwa na wahusika hawawezi kuzitoa, njia pekee ni kutishia kuchapisha, ingawa hiyo ni njia ya haraka sana. Pamoja na hayo, muhimu ni kuhakikisha chanzo cha watu kuficha fedha kinajulikana,” alisema

Mhahidhi Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Haji Semboja alisema: “Katika uchumi ambao unakwenda vizuri na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa fedha zinafanya kazi, suala hilo (kuficha fedha) haliwezi kujitokeza kwa maana mwenye fedha atajua jinsi ya kuziweka.

“Katika uchumi ambao watu wamekaa na kuhodhi fedha majumbani mwao ukitaka fedha hizo ziingie kwenye mzunguko basi unazibadilisha. Watu watazileta kwa nguvu maana hawatakuwa na ujanja. Ila kubadili fedha kuna sababu nyingi.”

Alisema sababu nyingine ni kutaka kubadili fedha ili kuwa na mwonekano mpya, pamoja na ubora wake ikiwa za awali zilikuwa zikichakaa mapema.

“Watu kukaa na fedha ndani ni kutoelewa mifumo ya kisasa ya kibiashara, watu wanaofanya hivyo ni wanaofanya shughuli ambazo haziko kwenye mfumo wa ulipaji kodi,” alisema.


PETE YA ALMASI YAMPONZA MKE WA MUGABE AAMRISHWA KURUDISHA NYUMBA TATU.

Pete hiyo ilikuwa ni kama zawadi kwa Mke wa rais Mugabe, Bi Grace, kuadhimisha miaka 20 ya ndoa.
Jaji mmoja nchini Zimbawe amemwaagiza mke wa rais Robert Mugabe, Grace Mugabe, kurudisha nyumba tatu alizompokonya mfanyabiashara nmoja raia wa Lebanon, kufuatia zabuni ya pete ya almasi ya gharama ya dola milioni 1.35.

Kulingana na kesi iliyowasilishwa na mfanyabiashara huyo, Bi Mugabe alitaka kurudishiwa pesa baada ya pete hiyo ya almasi iliyonunuliwa mjini Dubai. ilipowasilishwa kwake baada ya kutengenezwa na mtu tofauti.

Wakati Jamal Ahmed alishindwa kulipa pesa hizo kwa akaunti mjini Dubai, na licha ya yeye kusema kuwa pesa hizo zilitumwa kupitia kwa benki moja ya Zimbabwe, Bi Mugabe alichukua kwa nguvu nyumba zake tatu mwezi Oktoba.

Jaji Clement Phiri alisema kuwa Bi Mugabe pia ni lazima ahakikishe kuwa wafanyakazi wote waliokuwa wakihudumu kwenye nyumba hizo wamerudishwa kazini.

Pete hiyo ilikuwa ni kama zawadi kwa mke wa rais Mugabe, Bi Grace, kuadhimisha miaka 20 ya ndoa.

BURIANI MPOKI BUKUKU.



Marehemu Mpoki Bukuku, wakati wa uhai wake
Marehemu Mpoki Bukuku, wakati wa uhai wake.

Dar es Salaam. 
Mpigapicha maarufu Mpoki Bukuku amefariki dunia leo katika Taasisi ya Mifupa (MOI), alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma (MOI) Almas Jumaa.
"Ni kweli Mpoki amefariki dunia mchana huu, alipokelewa jana usiku baada ya kupata ajali ya gari maeneo la Mwenge  ITV, taarifa zaidi tutazitoa baadaye," alisema Almas.
Mpoki Bukuku amewahi kufanya kazi kama Mpiga Picha Mkuu katika gazeti la Mwananchi, linalochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Pia amewahi kufanya kazi magazeti kadhaa likiwemo Majira na Nipashe.

SHIRIKA LA NDEGE LA ETIHAD LAINGIA MAKUBALIANO YA KIHISTORIA NA 'Precision Air'

KATIKA hatua za kuhakikisha inayafikia maeneo mengi Afrika Mashariki, Shirika la Etihad la Umoja wa Falme za nchi za Kiarabu limeingia makubaliano na Shirika la ndege la hapa nchini Precision Air ambayo yamelenga kupanua huduma zaidi ndani na nje ya Tanzania.

Makubaliano hayo yanatoa fursa kwa, Shirika la Ndege la ‘Precision Air’ ambalo linaongoza kwa utoaji huduma hapa nchini kuweza kutoa huduma za moja kwa moja katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu na zaidi.

Kupitia makubaliano hayo, Shirika la Ndege la Etihad litaweka alama yake ya kibali EY kwenye ndege za ‘Precision Air’ zinatoa huduma kati ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza, Mtwara, Nairobi, Zanzibar na Pemba, Vilevile kwenye ndege zinazotoa huduma kati ya Nairobi, Kilimanjaro na Zanzibar.

Aidha, Precision Air pia itaweka alama yake ya PW kwenye Ndege za Etihad zinazotoa huduma zake za kila siku kati ya Dar es Salaam na Abu Dhabi ikiwa ni hatua ya kuhimarisha uhusiano kati ya Afrika Mashariki na Falme za Kiarabu.

Kwa mujibu wa Ofisa Mkuu wa Mipango na Mikakati wa Shirika la ndege la Etihad, Kevin Knight, ‘Precision Air’ ni shirika lenye ubunifu wa hali ya juu ambalo limeweza kuibuka na tuzo mbalimbali katika utoaji wa huduma bora za anga.
Makubaliano yetu leo yanadhihirisha kuwa ndoto ya Shirika la Ndege la Etihad ya kuhimarisha huduma katika Ukanda wa Afrika Mashariki inazidi kukua.
“Huu ni mfano mzuri zaidi katika kuifikia mipango mikakati yetu ya kufanya kazi na wadau ili kutimiza dhamira yetu na kutoa huduma bora za kibiashara na usafiri wenye raha kwa chaguo bora zaidi,” aliongeza Ofisa huyo.
Naye Sauda Rajabu ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mkuu wa Precision Air Services PLC,alisema, “Hii ni hatua muhimu na mpya kwa Precision Air, na tunafurahi sana kufanya kazi na Shirika la Ndege la Etihad katika ushiriiano huu. Tunatazamia kuwakaribisha abiria wengi zaidi wa Shirika la ndege la Etihad kwenye ndege zetu na ni furaha yetu kuendelea kuzifikia fursa nyingi zaidi katika hatua ambayo itasaidia kuhimarisha uhusiano wetu kwa mipango ya muda mrefu.

“Kwa kupitia ushirikiano huu, tunawasaidia wateja wetu wa safari za ndani kujipatia fursa zaidi ya kwenda Abudhabi, na kusafiri maeneo zaidi ya 100 duniani kupitia mtandao mpana wa Shirika la ndege la Etihad ambao ni Afrika Mashariki ya Kati, Afrika, Ulaya, Asia, Australia na Marekani,”
Tangu jana abiria wameanza kukata tiketi za safari kutoka kwa mawakala au katika ofisi za mashirika haya kwa ajili ya safari za Januari 11, mwakani na kuendelea.

Shirika la Ndege la Etihad kwa sasa linatoa huduma katika nchi kumi barani Afrika 10 Afrika ikiwemo Johannesburg, Nairobi, Entebbe, Dar es Salaam, Khartoum, Casablanca, Rabat, Lagos, Cairo na Mahé, Seychelles.


 Kuhusu Shirika la Ndege la Etihad

Shirika la Usafiri wa Anga la Etihad (EAG) linafanya shughuli zake ulimwenguni kote likifanya biashara kupitia mashirika yake manne ambayo ni; Shirika la Ndege la Etihad, The National Airline of The United Arab Emirates, Etihad Engineering, Hala Group na Airline Equity Partners.
Shirika limewekeza kwenye mashirika saba mengine ambayo; Airberlin, Air Serbia, Air Seychelles, Alitalia, Jet Airways, Virgin Australia na Swiss-based Darwin Airline, inayofanya kazi chini ya  Etihad. 

Shirika la Etihad lenye makao makuu yake Abu Dhab limejiwekea malengo ya kuhudumia abiria  na usafirishaji mizigo maeneo zaidi ya  110 na kutoa huduma bora ya usafirishaji mizigo Mashariki ya Kati, Afrika, Ulaya, Asia, Australia na Amerika. Shirika lina ndege za Airbus na Boing 120, ikiwa na zingine 204 ambazo bado zinatumika kwa sasa;  ikiwamo  71 Boeing 787s, 25 Boeing 777Xs, 62 Airbus A350s na 10 Airbus A380s.

Kwa maelezo zaidi tembelea: www.etihad.com

KIUNGO WA ZAMANI WA TAIFA STARS ATHUR MWAMBETA ANAOMBA MSAADA.

 Wachezaji wa zamani wakiongozwa na Kitwana Manara wakimjulia hali,Athur Mwambeta,ambaye amekatwa miguu yote miwili

Na Humphrey Shao,Globu ya Jamii.

Kiungo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania na Simba Sports iliyokuwa ikiitwa Senderland ,Athur Mwambeta amewaomba wadau mbalimbali wa mchezo wa soka nchini na Chama cha Mapinduzi (CCM) kumsaidia kupata chombo cha usafiri kitakachomtoa sehemu moja mpaka nyingine mara baada ya kukatwa miguu yote miwili kutokana na maradhi yanayomkabili.
 


Mwambeta amesema hayo leo jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Globu ya jamii katika hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo amelazwa katika jengo la Kibasila ward namba 11, ambapo anaendelea na matibabu mara baada ya kukatwa mguu ijumaa iliyopita.
 


"Nimeugua maradhi haya pindi tu nilipoacha kucheza mpira hali iliyopelekea kukatwa mguu wangu wa kwanza mwaka 2015 na mwaka huu ijumaa iliyopita ndipo nilipokatwa mguu wangu wa pili na kubaki kama hivi mnavyoniona, kwani siwezi tena kusogea kutoka sehemu moja kwenda nyingine kama ilivyokuwa awali hivyo kwa yoyote anaeweza kunisadia naomba ajitokeze " amesema Mambeta.
 


Amesema kuwa anaomba wadau kumchangia kupitia nambari hii 0714435312 ili aweze kujikwamua katika changamoto mbalimbali za kimaisha.
 


Pia alitoa wito kwa wapenzi na wanachama wa CCM kujitokeza kumsadia kwani wao ni moja ya watu waliokuwa wahamasishaji wakubwa kupitia TANU mpaka ilipozaliwa CCM walitumia mpira kama sehemu ya hamasa.

Thursday, December 22, 2016

NKUNDA STAR - DIMAGA JEMBE LIVE

Published on Dec 22, 2016
Ni msanii ambaye kwa mara ya kwanza ngoma yake Jembe fm ililetewa na msikilizaji kwa njia ya simu, kupitia kitengo cha muziki ilikuwa ni haraka sana kubaini sanaa ya ukweli iliyotumika katika kazi husika. 

Ndipo hatua ya kumsaka Nkunda Star ikaanza ...kipindi hicho hatukujua hata jina la msanii huyu kwani track yake ilitumwa kwa whatssup bila jina ...ila taarifa zikajulikana tu kwamba dogo yuko shy ......ndani ya siku mbili tu mara baada ya tangazo la kumsaka kupitia kipindi cha HOT STAGE kinachohusika na Muziki wa Hip hop...Taarifa jamaa zilifikia .....jamaa alifunga safari hadi Mwanza studio za Jembe Fm.

Huko ndiko safari nyingine ya muziki wake ikaanza

BAN ATOA WITO KWA PANDE ZOTE DRC KUSULUHISHA MGOGORO KWA AMANI..

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeondoka Ban Ki-moon ametoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro wa kisiasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutatua mgogoro huo kwa njia za amani.
Wito huo wa Ban umekuja baada ya watu  zaidi ya 26 kuripotiwa kuuawa katika maandamano yalioyaoanza Jumatatu dhidi ya Rais Kabila baada ya muhula wake wa uongozi kumalizika.
Taarifa ya msemaji wake imemnukuu Katibu Mkuu akizitaka pande zote zinazohusika katika upatanishi na usuluhishi kuafikiana kwa njia ya amani na kujaribu kutatua masuala yanayohusiana na mipango ya mpito kuelekea uchaguzi mkuu kwa mujibu wa katiba ya DRC.
Ban ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuweka mbele maslahi ya nchi na raia badala ya maslahi yao binafsi.
Amemsihi Waziri Mkuu Samy Badibanga kuchukua hatua madhubuti kwa mujibu wa makubaliano ya kisiasa ya tarehe 18 Oktoba huku akisisitiza umuhimu wa vikosi vya usalama nchini humo kujizuia kuchukua hatua zinazoweza kusababisha vifo kama vile vilivyoripotiwa kwenye mji mkuu Kinshasa.

Ban ameitaka serikali ya Kinshasa  kwa mara nyingine tena kukuza na kulinda haki za binadamu na kuzingatia uhuru wa kimsingi uliotajwa katika Katiba.
Maandamano dhidi ya rais Kabila mjini Kinshasa
Kambi kuu ya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewataka wananchi kutomtambua tena Joseph Kabila kama rais wa nchi hiyo na imewahimiza kuonesha upinzani wao dhidi ya Kabila kwa njia ya amani.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), Etienne Tshisekedi, ameitaja hatua ya Rais Kabila ya kuwa madarakani kwa awamu ya tatu kuwa ni kinyume cha sheria na kwamba jitihada zake za kutaka kubakia madarakani ni mapinduzi ya kijeshi.