Mfanyabiashara maarufu nchini, Mustafa Jaffar Sabodo akizungumza jijini Dar es Salaam, kuhusu wafanyabiashara wanaoficha fedha majumbani na kumshauri Rais John Magufuli abadilishe fedha. (PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA) |
Mfanyabiashara maarufu nchini, Jaffar Sabodo (73), amemshauri Rais John Magufuli abadilishe fedha ili kubana wafanyabiashara wakwepa kodi na kuficha fedha majumbani.
Aidha, amesema kutokana na utendaji wa Rais, haoni sababu za vyama vya upinzani kuendelea kumpinga, na badala yake waache siasa na waungane naye kujenga Tanzania mpya.
Kauli ya mfanyabiashara huyo iliungwa mkono na wachumi waliozungumza na gazeti hili kubainisha kuwa njia nzuri zaidi ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupunguza masharti kwa benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye benki iwe kubwa jambo ambalo litafanya watu wakiweka fedha benki wapate faida.
Sabodo alitoa ushauri huo jana alipozungumza na JAMBO LEO katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Dar es Salaam, ambapo alisema licha ya hatua nzuri za Serikali ya Rais Magufuli kiuchumi na kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu na ufisadi, wapo walioficha mabilioni ya fedha nyumbani badala ya benki ili kukwepa kodi.
Sabodo akisisitiza jambo. |
Aliongeza: “Kwa maoni yangu, hatua hiyo ya kubadilisha fedha ichukue kati ya mwezi mmoja na mmoja na nusu, watabainika wengi walioficha fedha nyumbani na hali ya uchumi itabadilika.”
Akifafanua, Sabodo ambaye ni mzaliwa wa Lindi, alisema India, Pakistan na Venezuela ziliwahi kukumbwa na hali kama iliyopo sasa nchini, lakini hatua ya kubadilisha noti ilizisaidia kuimarisha uchumi na bajeti zao.
“Watu wanaiba fedha nyingi, wanazificha chini ya magodoro, ili kumaliza hali hiyo ni muhimu noti zikabadilishwa hali itakayomlazimisha kila aliyeficha fedha kuzitoa, hapo wapo watakaokimbia nchi,” alisema Sabodo huku akitaja baadhi ya watakaokimbia hatua hiyo ikichukuliwa.
Sabodo alitoa kauli hiyo wakati Rais Magufuli ameshatoa kauli kuwataka walioficha fedha majumbani kuziacha ziingie kwenye mzunguko huku akionya wasipofanya hivyo anaweza kuamua kuzibadili ili wakose mahali pa kuzipeleka.
Magufuli alitoa kauli hiyo Septemba kwenye mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi ambapo alisema watu hao wamekuwa na utaratibu wa kutoa fedha zao benki na kuzificha kwa kuogopa kuwa atabaini kiasi walichonacho.
Wachumi
Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Profesa Damian Gabagambi alisema: “Kuendesha uchumi hakutakiwi nguvu sana. Uchumi unajengwa kwa imani, mtu yeyote anayeendesha uchumi anatakiwa kuijenga hiyo imani na ikuzwe.
“Chochote kinachofanyika na kuua imani kinavuruga uchumi, ukiona watu wanaficha fedha hilo si tatizo, ni kwamba kuna kitu ambacho ni tatizo, kuficha fedha ndio kujihami kwao.”
Alisema njia nzuri ya kufanya watu walioficha fedha kuzitoa, ni BoT kupunguza masharti inayowekea benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye benki iwe kubwa, jambo ambalo litafawanya watu kutoficha fedha kwa maelezo kuwa wakipeleka fedha kwenye benki hizo, watapata faida.
Alisema riba inayotozwa kwenye benki inapangwa na BoT na kuitaka benki hiyo kufanya marekebisho ili kusaidia wanaoweka fedha kwenye benki kupata faida.
“Ila kama wana hakika fedha zimefichwa na wahusika hawawezi kuzitoa, njia pekee ni kutishia kuchapisha, ingawa hiyo ni njia ya haraka sana. Pamoja na hayo, muhimu ni kuhakikisha chanzo cha watu kuficha fedha kinajulikana,” alisema
Mhahidhi Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Haji Semboja alisema: “Katika uchumi ambao unakwenda vizuri na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa fedha zinafanya kazi, suala hilo (kuficha fedha) haliwezi kujitokeza kwa maana mwenye fedha atajua jinsi ya kuziweka.
“Katika uchumi ambao watu wamekaa na kuhodhi fedha majumbani mwao ukitaka fedha hizo ziingie kwenye mzunguko basi unazibadilisha. Watu watazileta kwa nguvu maana hawatakuwa na ujanja. Ila kubadili fedha kuna sababu nyingi.”
Alisema sababu nyingine ni kutaka kubadili fedha ili kuwa na mwonekano mpya, pamoja na ubora wake ikiwa za awali zilikuwa zikichakaa mapema.
“Watu kukaa na fedha ndani ni kutoelewa mifumo ya kisasa ya kibiashara, watu wanaofanya hivyo ni wanaofanya shughuli ambazo haziko kwenye mfumo wa ulipaji kodi,” alisema.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.