ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, August 15, 2025

80% YA WANANCHI KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA IFIKAPO 2034

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe wakiwa katika foleni kwa ajili ya taratibu za ununuzi wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya shilingi 19,500 kwa jiko Agosti 15, 2025.

 

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe wakijiorodhesha kwa ajili ya ununuzi wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya shilingi 19,500 kwa jiko Agosti 15, 2025.

 

Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt.Joseph Sambali akizungumza wakati wa zoezi la usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Agosti 15, 2025

Afisa Mauzo kutoka Kampuni ya Taifa Gas Limited, Ivon Rukekha (kulia) akitoa elimu ya matumizi ya jiko la gesi kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe waliofika kujipatia majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 wakati wa zoezi la usambazaji wa majiko hayo chini ya uratibu wa REA Agosti 15, 2025


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Shamimu Mwariko amesema kwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) ni dhahiri kwamba lengo la 80% ya wananchi kutumia nishati hiyo litafikiwa ifikapo Mwaka 2034.


Amesema hayo Agosti 15, 2025 wakati wa kutambulisha mradi wa kusambaza majiko ya gesi ya kilo 6 na vichomeo vyake kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 kwa jiko unaoratibiwa na REA na kutekelezwa na Mtoa huduma Kampuni ya Taifa Gas Limited iliyoshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo katika Mkoa wa Katavi.

“Tunaipongeza REA kwa kuja na mkakati huu na kutufikia hapa Mpimbwe, kwani licha ya kwamba sisi tupo katika mikoa ya pembezoni, kwa maana ya Mkoa wa Katavi lakini ni mikoa ambayo imeweza kufikiwa; wananchi wameifurahia huduma ya majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 tu,” alisema Mwariko.

Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kuhakikisha kwamba Tanzania inaningia, inasimamia na inaishi katika mazingira ya Nishati Safi.


“Tunamshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan sio tu kwasababu amekuwa kinara lakini tunamshukuru kwakuwa ameweka mifumo, miundombinu, misingi na mipango mikakati ya kuhakikisha kwamba kweli nchi yetu inafikia kuwa nchi yenye kutumia nishati safi, nishati bora na ya kisasa,” alisema Mwariko.


Alibainisha kuwa Halmashauri ya Mpimbwe tayari imeanza uhamasishaji wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa taasisi zinazotoa huduma ya chakula kwa watu wake zikiwemo shule za msingi na sekondari na kwamba baadhi ya shule ikiwemo shule ya Sekondari Mizengo Pinda tayari imefungiwa mfumo wa Nishati Safi ya Kupikia.


“Hivi tunavyozungumza tayari ofisi za walimu zote za shule za msingi na sekondari wanayo majiko ya gesi kwa ajili ya kuhakikisha wanatumia nishati kupika chakula; kwahiyo kazi iliyopo hapa ni kuhakikisha hata mwananchi wa ngazi ya chini kabisa anaona umuhimu wa utumiaji wa huduma hii na anaitumia bila ya kurudi nyuma,” alibainisha Mwariko.


Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Majimoto, Seltus Mwanampemba alisema tunayo haja ya kutoka kwenye nishati chafu kwenda kwenye nishati safi kwani matumizi ya gesi yanasaidia kuokoa gharama mfano unapotumia mkaa kama ulitaka kuchemsha kikombe cha maji ule mkaa ndio umeupoteza maana yake unatumia gharama kubwa kwa kazi ndogo.


Alisema kumekuwa na mtazamo hasi kwa badhi ya watu kwamba ladha ya chakula inabadilika kwa kutumia nishati safi kupikia jambo ambalo alisema halina ukweli na alitoa wito kwa jamii kuondokana na mtazamo huo kwani yeye anatumia nishati safi kupikia na ladha ya chakula ni ile ile kama wakati ule aliyokuwa akitumia kuni.


Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Majimoto, Dakson Schula alimshukuru Rais MDkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha shule hiyo kupata nishati safi ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi.


“Tunamshukuru Rais Samia, shuleni kwetu tumepata nishati safi ya umeme lakini pia kuna mfumo wa jiko la gesi unajengwa ambao utasaidia kupikia shuleni kwani kwa utaratibu wa hapa shule huwa tunapata chakula,” alishukuru Schula.


Kwa upande wao wananchi walionufaika na majiko ya ruzuku wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kununua majiko walipongeza hatua inayochukuliwa na Serikali ya kuhakikisha wanananchi wa kipato cha chini nao wanafikiwa na wanabadilishiwa maisha yao.


“Tulikuwa tukitumia mkaa na kuni kupikia lakini sasa tunamshukuru Rai Samia na hii kampeni yake ya Nishati Safi kwa wote, katuona akina mama, katusaidia kuondokana na kuni na mkaa; baadhi yetu hatukuwa na uwezo wa kununua majiko ya gesi lakini sasa kwa ruzuku hii kila mmoja atakuwa na jiko la gesi nyumbani kwake,” alisema Editha Kabagi, Mkazi wa Mpimbwe.


“Hakika Rais Samia ni Mama, anauchungu, ametuonea huruma wamama wenzake, kwakweli tumefarijika kwani tulikuwa tunapata shida lakini sasa hali inakwenda kubadilika,” alipongeza Aportuna Simmi, mkazi wa Mpimbwe.

 

Akizungumza kuhusiana na zoezi hilo la usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku, Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt.Joseph Sambali alisema mwitikio wa wananchi ni mkubwa na hilo linadhihirisha kuwa wanadhamira ya dhati kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati ambazo sio safi na salama na kwenda kwenye matumizi ya Nishati Safi.

 


Alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo hasa ikizingatiwa kuwa faida za kutumia Nishati Safi ya Kupikia ni nyingi ikiwemo kulinda afya na kuokoa mazingira.


Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatumia njia mbalimbali katika kuelimisha, kuwezesha na kuhamasisha wananchi ili kufikia lengo la 80% ya wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo Mwaka 2034.

 

Thursday, August 14, 2025

KAMATI YA MTAKUWWA MWANZA YATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WA KULINDA JAMII DHIDI YA UKATILI

 NA ALBERT G.SENGO/MWANZA

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza ndugu Balandya Elikana amewataka wajumbe wa kamati ya ulinzi wa wanawake na watoto (MTAKUWWA) mkoani humo kushirikiana na serikali kuhakikisha wanatambua na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokabili makundi hayo na kuwaondoa kwenye ukatili. Ndugu Balandya amesema hayo leo Agosti 13, 2025 wakati akizindua mafunzo ya siku tatu kwa kamati ya Mkoa ya kupinga na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto NPA-VAWC 2024/25- 2028/29 II.

MHE. RAIS DKT. SAMIA AKIWAVISHA NISHANI YA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI CISM

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Akiwavisha Nishani Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani CISM Ikulu Dar es Salaam, leo tarehe 14 Agosti, 2025.

Wednesday, August 13, 2025

NEEMA LUGANGIRA ATEULIWA BRUSSELS

 



Aliyekuwa Mbunge Viti Maalum, Neema Lugangira amenza kazi jijini Brussels kama Katibu Mkuu wa Women Political Leaders (WPL) — Jumuiya ya Kimataifa ya Viongozi Wanawake: Marais, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri, Wabunge na Mameya/Wenyeviti wa Halmashauri; ambapo wanalenga kuongeza uwakilishi wa wanawake katika siasa na kuimarisha sauti, ushawishi na aina ya uongozi wao katika nyanja na sekta mbalimbali. #UongoziUnaopimika

KAMATI YA MTAKUWWA MWANZA YATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WA KULINDA JAMII DHIDI YA UKATILI

 


Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza ndugu Balandya Elikana amewataka wajumbe wa kamati ya ulinzi wa wanawake na watoto (MTAKUWWA) mkoani humo kushirikiana na serikali kuhakikisha wanatambua na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokabili makundi hayo na kuwaondoa kwenye ukatili.

Ndugu Balandya amesema hayo leo Agosti 13, 2025 wakati akizindua mafunzo ya siku tatu kwa kamati ya Mkoa ya kupinga na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto NPA-VAWC 2024/25- 2028/29 II.

Amesema ni lazima mwanakamati azunguke kwenye jamii ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakwamisha katika kushiriki kwenye kujenga uchumi wao na kuhakikisha wanaweka misingi ya kuondoka changamoto hizo.

"Ukatili kwa wanawake na watoto unazuia maendeleo kwa jamii na nchi kwa ujumla kwani serikali inalazimika kuahughulika na majeraha ya ukatili kama kutibu na kunasihi, hivyo wajumbe nawaomba mkatekeleze wajibu wenu." Amesema Balandya.


Ameongeza kuwa mchanganyiko wa wajumbe kutoka kwenye taasisi na madhehebu ya dini mbalimbali umelenga kuyafikia makundi mbalimbali na kuhakikisha jamii yote inafikiwa na kupatiwa elimu dhidi ya ukatili.

Akizungumzia watoto wanaoishi mtaani, Katibu tawala amesema kila mmoja kwenye eneo lake ahakikishe anafikisha ujumbe kwamba ni vibaya kuwahudumia watoto wanaoomba pesa mtaani kwani inapelekea kuwafanya waendelee kuwepo.


Akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Gabriel Mashauri amebainisha kuwa kwa siku tatu wajumbe watapitishwa katika maeneo 8 ambazo ni afua za kufuata na mwisho wa mafunzo hayo kila mjumbe atajua majukumu yake ya kila siku katika kuhakikisha watoto na wanawake wanakingwa na ukatili.

MGOMBEA URAIS CUF: NIKISHINDA, KEKI YA TAIFA INAWANUFAISHA WOTE

Gombo, ambaye aliambatana na mgombea mwenza wake Husna Mohammed Abdullah, alisema chama hicho kimejipanga kutenda haki kwa Watanzania wote ili wapate stahiki zao katika sekta muhimu kama afya, elimu na maji.
Gombo, ambaye aliambatana na mgombea mwenza wake Husna Mohammed Abdullah, alisema chama hicho kimejipanga kutenda haki kwa Watanzania wote ili wapate stahiki zao katika sekta muhimu kama afya, elimu na maji.

Mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo, ameahidi kwamba endapo atachaguliwa kuwa rais, atasimamia haki na kuhakikisha rasilimali za Taifa zinawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.

Gombo, ambaye aliambatana na mgombea mwenza wake Husna Mohammed Abdullah, alisema chama hicho kimejipanga kutenda haki kwa Watanzania wote ili wapate stahiki zao katika sekta muhimu kama afya, elimu na maji.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea, Gombo alisema kwa sasa haki imekuwa ikipotea katika huduma hizo muhimu, na kwamba atakapopewa dhamana, kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mmoja.

“Sisi kama CUF tunataka kulinda haki ya kupata huduma zote. Keki ya Taifa lazima itanufaishe Watanzania wote ili kuondoa malalamiko ya wananchi,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa sasa kuna baadhi ya makundi ambayo yananufaika zaidi kuliko mengine, jambo linalosababisha malalamiko miongoni mwa wananchi, na CUF inakusudia kuondoa hali hiyo pindi ikishika dola.

KATAVI WAMPA HEKO RAIS SAMIA UMEME VIJIJINI.


Fundi Seremala, Elasto Mwampaya maarufu kama Fundi Lam akiendelea na shughuli zake katika karakana yake ya kutengeneza samani (fenicha) kwa kutumia vitendea kazi vya kisasa vinavyotumia umeme katika Kijiji cha Mapili, Wilaya ya Mlele na kusafirisha katika mikoa mbalimbali kote nchini.

John Julius mkazi wa Kijiji cha Mapili, Wilaya ya Mlele miongoni mwa vijana walionufaika na ajira kijijini hapo baada ya kufikiwa na nishati ya umeme akiendelea na kazi yake ya uendeshaji wa mashine ya kukoboa mpunga.

Mkazi wa Kijiji cha Mapili, Jovina Magupa akiandaa mahindi kwa ajili ya kusaga. Uwepo wa umeme katika kijiji hicho umerahisisha maisha ya wananchi hususan akina mama. 


Fursa lukuki za kiuchumi zaibuliwa

Wananchi waeleza namna maisha yao yalivyobadilika

Wananchi wa Kijiji cha Mapili Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kubadili maisha yao kupitia mradi wa umeme uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Wametoa shukrani hizo kwa nyakati tofauti kijijini hapo Agosti 11, 2025 wakati wa kampeni maalum ya uhamasishaji wa matumizi ya umeme kwa ajili ya shughuli za kiuchumi inayotekelezwa na REA katika maeneo mbalimbali kote nchini.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kabla ya kupata nishati hii ya umeme mazingira hayakuwa mazuri, usiku hatukuwa na mwanga sasa hivi tunaishi kwa amani na hata baadhi ya shughuli za kimaendeleo zinafanyika hadi muda wa usiku lakini pia tunapata habari kwa kutazama luninga muda wowote tunaotaka pia baadhi ya vijana wamepata ajira kupitia umeme,” alisema Mwalimu Mstaafu, Mkazi wa Kijiji cha Mapili, Amos Katawa.

Mrisho Mussa Fundi Uchomeleaji katika Kijiji cha Mapili alisema kabla ya umeme kufika kijijini hapo walikuwa wakilazimika kufanya shughuli zao maeneo ya mjini ambapo ni mbali na kijijini hapo na hivyo kusababisha kupanda kwa gharama ya bidhaa walizokuwa wakizalisha pamoja na kutumia muda mrefu kukamilisha kazi.

“Tulikuwa tunalazimika kutengenezea mageti huko Inyonga na kisha tunasafirisha, hali hii ilikuwa ni usumbufu kwetu hadi kwa wateja wetu, lakini sasa mambo yote tunafanya hapa, hakuna haja tena ya kurudi mjini, nawasihi mafundi na wengine wenye fani zao wasipende kukimbilia mijini; Rais Samia ametuona, kila kitu hapa kijijini sasa hivi kinapatikana,” alisema fundi Mussa.

Kwa upande wake Scholastica Kitwewe, Mkazi wa Kijiji cha Mapili alisema umeme umerahisisha maisha ya wanawake kijijini hapo kwani hapo awali walikuwa wakitumia muda mwingi kuandaa mahindi ya unga kwa kutwanga katika kinu lakini sasa mashine za kusaga na kukoboa nafaka zimefunguliwa kijijini hapo jambo ambalo linarahisisha shughuli zao za mapishi ya kila siku na kuwaokolea muda.


Kwa upande wake, Elasto Mwampaya maarufu kama Fundi Lam ambaye ni Fundi Seremala kijijini hapo alisema kuwa umeme umewezesha kukua kwa karakana yake ya useremala na kwamba hivi sasa anatengeneza fenicha zenye ubora na kuuza katika mikoa mbalimbali kote nchini jambo ambalo halikuwezekana hapo awali kabla ya kufikishiwa umeme.

Alisema umeme umemuwezesha kupanua wigo wa ajira na kwamba katika karakana yake ameajiri vijana wengi na pia anatoa mafunzo kwa vijana namna ya kutengeneza bidhaa kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyotumia umeme.

Akizungumza kuhusiana na umeme kijijini hapo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mapili Anthony Mwijuma, aliipongeza REA kwa kutekeleza mradi huo ambao alisema umekuwa ni neema kwa wananchi wake ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kufikiwa na umeme.


“Wananchi wa Mapili tunasema asante kwa Rais Samia kwani kupitia umeme vijana wamepata ajira, wengine wamebuni miradi na biashara ndogondogo za vinywaji, vifaa vya simu na wengine sasa hivi na mafundi wa kuchomelea hapahapa kijijini,” alisema Mwijuma.

Akizungumza hali ya usambazaji umeme mkoani Katavi, Msimamizi wa miradi ya REA Mkoani humo, Mha. Gilbert Furia, alisema vijiji vyote vina umeme na kazi inayoendelea sasa ni kusambaza umeme katika vitongoji ambavyo havikufikiwa.

“Tunamshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambayo imewezesha kufikisha umeme katika vijiji vyote 49 ndani ya Halmashauri za Mlele na Mpimbwe na sasa tunatekeleza mradi wa kusambaza umeme vitongojini; hadi sasa katika Hamashauri hizi vitongoji 176 kati ya vitongoji 251 vimefikiwa na mradi unaendelea wa kufikisha umeme kwenye vitongoji vilivyobaki,” alisema Mha. Furia

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mlele, Yahaya Mbulu aliipongeza REA kwa kukamilisha mradi wa kufikisha umeme vijijini na alisema kuwa amejionea namna ambavyo kazi ya kufikisha umeme vitongojini ikiendelea kutekelezwa kwa kasi.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia REA; vijiji vyote vimefikiwa; wananchi wa Mlele tunasema asante kwa Serikali maana umeme umeleta fursa, Mlele ya jana sio ya leo, hatua imepigwa,” alisisitiza Mbulu.


RAS PWANI AWAHIMIZA WATUMISHI HALMASHAURI YA MANISPAA YA KIBAHA KUCHAPA KAZI KWA UBUNIFU


 Na Victor Masangu,Kibaha 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, leo ameanza ziara yake ya kikazi katika Halmashauri za Mkoa wa Pwani kwa kutembelea Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Katika ziara hiyo, Mnyema amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuongeza mapato ya Halmashauri pamoja na Mkoa kwa ujumla.
"Naomba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kubuni vyanzo vipya vya mapato. Hili ni miongoni mwa maagizo niliyopatiwa ili kusaidia kuongeza mapato ya Mkoa wetu," alisema Mnyema.

Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa kuendelea kubuni na kusimamia miradi mbalimbali yenye tija, ambayo imesababisha ongezeko la mapato ya Manispaa hiyo kila mwaka.
Mnyema aliwataka watumishi wa Manispaa hiyo kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya utumishi wa umma kwa kuwa na nidhamu, uadilifu, na bidii, ili kutoa huduma bora kwa wananchi. Alisisitiza pia umuhimu wa uwajibikaji na uaminifu katika usimamizi wa fedha za umma, ili kudhibiti upotevu wa rasilimali na kuongeza ufanisi katika miradi ya maendeleo.

Akiwa katika Manispaa ya Kibaha, Katibu Tawala huyo alitembelea na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza – Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya Sofu, pamoja na mradi wa maduka ya biashara ya Kibaha Shopping Mall.
Ziara hiyo inalenga kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kufanya vikao kazi na watumishi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani.

KAYA 3,255 KUNUFAIKA NA MAJIKO YA GESI YA RUZUKU WILAYA YA MLELE

 

Mtaalamu kutoka Kampuni ya Taifa Gas, Emmanuel Humphrey akitoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Usevya wilayani Mlele kuhusiana na matumizi sahihi ya majiko ya gesi wakati wa zoezi la usambazaji wa majiko hayo Agosti 12, 2025 kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19, 500 kwa kila jiko.

Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt.Joseph Sambali (kushoto) akielezea mradi wa usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku kwa Katibu Tawala Wilaya ya Mlele, Yahaya Mbulu kabla ya kuanza kwa zoezi la usambazaji wa majiko hayo wilayani humo Agosti 12, 2025






-Wananchi waipongeza Serikali kwa makati huo


Wananchi Kijiji cha Usevya Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kuhakikisha wanafikiwa na nishati safi ya kupikia kwa bei ya ruzuku.


Wametoa pongezi hizo kijijini hapo Agosti 12, 2025 wakati wa zoezi la usambazaji wa majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita na vichomeo vyake kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 kwa kila jiko.


"Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea majiko haya yanakwenda kurahisisha maisha yetu, majiko haya pia ni mkombozi wa mazingira naamini ukataji wa miti unakwenda kupungua," alisema Davis Majaliwa Mkazi wa Usevya.


Kwa upande wake Christina Sindano mkazi wa Kijiji cha Usevya alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kampeni hiyo ambayo alisema inanufaisha wananchi wake hususan kina mama.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Usevya, Focus Kapongwa alisema wananchi kijijini hapo wamekuwa na mazoea ya kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa lakini kufika kwa mradi kutapunguza ukataji holela wa miti.


"Tunashukuru kwa hii huduma, tumepata shida sana kwenye ununuzi wa mkaa kwani sasa hivi mkaa ni bei ghali na haya majiko yatatusaidia kupunguza gharama ya maisha," alisema Kapongwa.


Akizungumza kuhusu mradi, Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt.Joseph Sambali alisema mradi huo kwa Mkoa wa Katavi unatekelezwa kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa Gas Limited ambapo jumla ya majiko 9,765 ya gesi (LPG) yatasambazwa.


"Majiko haya yanauzwa kwa bei ya ruzuku gaharama zingine zimebebwa na Serikali lengo ni kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa gharama nafuu ambayo kila mwananchi anamudu," alisema Dkt. Sambali


Alisisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili kuepuka watu kujirudia kwani dhamira ni kufikiwa kwa kila mwananchi.


Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Mlele, Yahaya Mbulu alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ikiwemo ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao na kuhifadhi mazingira.


"Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele kwenye Niishati Safi ya Kupikia; inakadiriwa kuwa takribani watu 31,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati isiyo salama," alibainisha Mbulu.


Alitoa wito kwa wananchi kuacha kuharibu mazingira kwa kukata miti badala yake wachangamkie fursa hiyo ya majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku.


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wameachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama.


Monday, August 11, 2025

SHILATU AWEKA HISTORIA UZINDUZI TK MOVEMENT

 


~ Ni uzinduzi ofisi ya kwanza TK Movement 

~ Wananchi wameamua  kuusema ukweli juu ya Dk. Samia

Na Mwandishi wetu

Wananchi wameamua kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanamlinda, kumtetea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa gharama yeyote Ile.

Hayo yamejidhirisha kwenye uzinduzi wa ofisi ya kwanza na ya kihistoria nchini ya TK Movement uliotokana na nguvu za Wananchi ambapo uzinduzi huo wa ofisi umefanywa na Afisa Tarafa Lisekese Emmanuel Shilatu kwenye Kijiji cha Miwale kilichopo Kata ya Msikisi.


Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Msikisi, Shilatu aliwasihi Wananchi kuongeza Utaifa, Uzalendo kwa Taifa lao la Tanzania kwa kujivunia Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kujivunia Serikali yao, kujivunia na kuyasema maendeleo yaliyopatikana nchini.

"Nawapongeza Wananchi wote kuhakikisha upatikanaji wa ofisi ya kwanza ya TK Movement. Ndugu zangu, akitokea Mtu akikwambia Tanzania tuna nini mwambie tuna amani, tuna maendeleo na tuna Rais Samia Mzalendo, Mchapa kazi, hodari, mtekelezaji na mfuatiliaji. Akikuuliza maendeleo yapi mpeleke muonyeshe miradi ya maendeleo ambayo ipo Kila sehemu kwenye sekta za afya, elimu, maji, miundombinu nk. Waonyesheni pembejeo za kilimo mnazopewa bure na Rais Samia. Hakikisheni mnawaeleza Watu utekelezaji wa ilani ya uchaguzi CCM unaofanywa na Serikali" Alisema Shilatu.


"Tunapoelekea kwenye uchaguzi Mkuu huu wa kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais hakikisheni mnadumisha amani na utulivu lakini pia mjiepushe na vitendo vya rushwa." Alisisitiza Gavana Shilatu.

Nae Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Rauphu Said amesema Wananchi wanajivunia Serikali yao napo tayari kuitetea na kumtetea Mhe. Rais Samia.

"Mimi kama kijana na Vijana wenzangu tunayaona maendeleo yanayoendelea kupatikana na kukua nchini yanayotupelekea kuamua kuitetea Serikali iliyopo Madarakani na kumlinda Rais Samia kwa wivu mkubwa." Alisema Rauphu.

TK Movement ni mtandao unaofanya kazi ya kuhamasisha Vijana na Wanawake katika ushiriki wao wa shughuli za maendeleo nchini ili kuchochea Kasi ya maendeleo katika Taifa letu.


Sunday, August 10, 2025

MHE. RAIS DKT.SAMIA AKIWAONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MWILI WA SPIKA MSTAAFU WA BUNGE HAYATI JOB NDUGAI

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Akiwaongoza Waombolezaji Kuuaga Mwili wa Spika Mstafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Job Yustino Ndugai Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma, leo tarehe 10 Agosti, 2025.