Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akiwataarifu wanachama wa Chadema juu ya mkutano wao kuzuiwa kufanyika baada ya Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Shinyanga Mjini,Charles Shigino kuandika barua jeshi la polisi kuwa kuna taarifa za uvunjivu wa amani kwenye mkutano wa Chadema.
CHANZO:- Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Baraza la Uongozi la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Shinyanga limemsimamisha nafasi zote za uongozi Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini, Charles Shigino kutokana na kwenda kinyume cha Katiba ya Chama, Kanuni na Maadili ya Viongozi wa Chama kwa kuzuia mkutano mkuu wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini kwa kuandika barua Jeshi la Polisi akidai kuna dalili za uvunjifu wa amani endapo mkutano ungefanyika.
Akizungumza na Vyombo vya Habari leo Jumanne Januari 21,2020 katika ofisi za CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini,Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi amesema Baraza la Uongozi CHADEMA limechukua hatua hiyo baada ya kukutana katika kikao cha dharura cha kamati tendaji na kubaini kuwa Shigino amekiuka katiba ya chama na kanuni na taratibu za uongozi.
“Baraza limemsimamisha nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama,Ndugu Charles Shigino ambaye alikuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga na Mjumbe wa mkutano mkuu kata ya Ngokolo. Atabaki kuwa mwanachama na tunamuandikia barua ajieleze ndani ya siku 14 kwa nini asifukuzwe uongozi”,amesema Ntobi.
“Tulikuwa na mkutano mkuu wanachama wa Jimbo la Shinyanga Mjini leo katika ukumbi wa Ibanza Hoteli,tumeshangaa kupata taarifa kuwa Jeshi la polisi kupitia kwa mkuu wa polisi wilaya ya Shinyanga kuwa mkutano wetu umezuiwa kufanyika kutokana na barua iliyoandikwa na Shigino aliyeomba polisi wazuie mkutano kwamba kuna hatari na uvunjifu wa amani”,ameeleza Ntobi.
Amesema kutokana na hali hiyo viongozi wa CHADEMA walifika katika kituo cha polisi wilaya ya Shinyanga na kukutana na mkuu wa polisi wilaya (OCD) ambaye aliwaeleza kuwa wamezuia mkutano huo kutokana na barua ya mwenzao na ndipo Kamati tendaji ya Chadema ilipokaa katika kikao cha dharura na baraza la uongozi kuchukua uamuzi wa kumchukulia hatua Shigino.
“Shigino amekiuka maadili ya uongozi,amefanya utovu wa nidhamu,amekisaliti chama na kupanga njama ya kuhujumu chama na kutoheshimu ngazi za juu za uongozi katika chama. Shigino amekuwa na tabia ya kupinga maamuzi ya viongozi wenzake katika chama”,amesema Ntobi.
"
"Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA ya Mwaka 2006, Toleo la 2016. Ibara ya 7.5.4 (h) Baraza la Uongozi Mkoa, ndio Mamlaka ya nidhamu na uwajibishaji wa Viongozi wa Jimbo/Wilaya. (Ibara ya 6.3.6(iv).Kwa maana hiyo, Baraza la Uongozi limechukua hatua za kinidhamu dhidi yake, kwa kuzingatia Ibara ya 6.3.6.(d).
Hivyo, kuanzia leo, tarehe 21.01.2020, Chama kinatoa taarifa kwa umma na Wanachama kuwa Charles Shigino, amesimamishwa ukatibu mwenezi wa Jimbo la Shinyanga Mjini mpaka hapo itavyoamuliwa vinginevyo",amefafanua.
Ntobi amebainisha kuwa mkutano huo mkuu wa wanachama ulilenga kujadili masuala mbalimbali ya kujenga CHADEMA ikiwemo kuwapa wanachama muhtasari wa mambo yaliyojiri katika Mkutano mkuu wa CHADEMA taifa uliofanyika hivi karibuni na kujadili waraka wa Katibu mkuu wa CHADEMA.
Naye Katibu wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Zacharia Obad amesema Shigino anayo nafasi ya kujitetea ndani ya siku 14 na kukata rufaa baada ya siku 30 kuhusu maamuzi yaliyochukuliwa na Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa.
Aidha amesema CHADEMA haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaokwenda kinyume na maadili na katiba ya CHADEMA.
Hata hivyo Shigino akizungumza na Malunde 1 blog amesema kitendo cha kuweka zuio la mkutano wa wilaya ya Shinyanga Mjini kutokana na kwamba viongozi wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga wamekiuka katiba ya Chadema kwa kuitisha mkutano mkuu wa wilaya ambao hawastahili kuuitisha na kuhudhuria labda kama watakuwa wamepewa mualiko wa wageni waalikwa tu.
Shigino amesema kutokana kutoelewana kwake na viongozi wa baraza la uongozi Chadema mkoa wa Shinyanga kuhusu mkutano huo ndiyo kumemfanya aweke zuio kwa kutumia jeshi la polisi kwani hali isingekuwa shwari ndani ya mkutano huo.
“Ni kweli nimeweka zuio la mkutano wa Chadema kuzuia viongozi hawa waliokanyaga katiba ya CHADEMA. Mkutano wao ulikuwa Batili,Wametumia katiba gani hawa viongozi wa mkoa ambao ni viongozi wa baraza la uongozi wa mkoa na vikao vya mashauriano tu kuitisha mkutano wa wilaya halafu wao ndiyo wakawe wageni rasmi na wasemaji kwenye Mkutano mkuu wa wilaya. Kwenye mkutano huo pia waliita waliokuwa wagombea uenyekiti serikali za mitaa kuhudhuria mkutano..Sasa hapa wametumia katiba gani?,amehoji Shigino.
“Bado sijapata barua ya kusimamishwa uongozi. Lakini hawa Viongozi wa baraza la uongozi Chadema mkoa siyo wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya, Wamepata wapi haya mamlaka ?.Nitaripoti kwa viongozi wa Kanda ya Serengeti kilichotokea. Nataka nijue nani anatakiwa kutumbuliwa kati yangu na wao ambao wamekanyaga katiba?”,amesema.
Hata hivyo Shigino amesema yeye bado ni mwanachama wa CHADEMA na atabaki kuwa CHADEMA na ataendelea kuwa katibu Mwenezi Wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini na hapendi kuona Chama kinaharibiwa na watu wachache vimelea wanaotengeneza fitna ambao wanashiriki kuleta vurugu ndani ya chama.
Shigino alihamia CHADEMA mwaka 2015 akitokea CCM akiwa Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini na Januari 15,2019 alichaguliwa kuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini.
Hapa ni nje ya ofisi za Chadema wilaya ya Shinyanga Mjini,Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akiwataarifu wanachama wa Chadema juu ya mkutano wao kuzuiwa kufanyika baada ya Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Shinyanga Mjini,Charles Shigino kuandika barua jeshi la polisi kuwa kuna taarifa za uvunjivu wa amani kwenye mkutano wa Chadema uliotakiwa kufanyika leo Januari 21,2020 katika ukumbi wa Ibanza Hoteli Mjini Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akitoa taarifa kwa wanachama wa Chadema kuhusu hatua iliyochukuliwa na Baraza la Uongozi Chadema mkoa kumsimamisha nafasi zote za uongozi Charles Shigino.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akitoa taarifa kwa wanachama wa Chadema kuhusu hatua iliyochukuliwa na Baraza la Uongozi Chadema mkoa kumsimamisha nafasi zote za uongozi Charles Shigino.
Wanachama wa Chadema wakimsikiliza Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akisoma katiba ya Chadema na vifungu alivyokiuka Shigino.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akizungumza na waandishi wa habari ndani ya Ofisi ya CHADEMA Shinyanga Mjini leo Januari 21,2020 na kuwapa taarifa ya kumsimamisha nafasi zote za uongozi Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini, Charles Shigino.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akizungumza na waandishi wa habari ndani ya Ofisi ya CHADEMA Shinyanga Mjini leo Januari 21,2020 na kuwapa taarifa ya kumsimamisha nafasi zote za uongozi Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini, Charles Shigino.Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema mkoa wa Shinyanga Winfrida Mwenula. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Madiwani wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga ,William Shayo akifuatiwa na Katibu wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga,Zacharia Obad.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akionesha barua ya Charles Shigino kuzuia mkutano wa wanachama wa CHADEMA.
Katibu wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga,Zacharia Obad akielezea zaidi kuhusu maamuzi waliyochukua dhidi ya Charles Shigino.
Katibu wa Baraza la Uongozi CHADEMA mkoa wa Shinyanga,Zacharia Obad akielezea zaidi kuhusu maamuzi waliyochukua dhidi ya Charles Shigino.
Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini, Charles Shigino naye akizungumza na waandishi wa habari dhidi ya maamuzi ya Baraza la Uongozi la CHADEMA mkoa wa Shinyanga kumsimamisha nafasi ya Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini ambapo amesema maamuzi hayo ni batili na ataendelea na nafasi hiyo na kubaki kuwa mwanachama mwadilifu wa Chadema.
Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini, Charles Shigino naye akizungumza na waandishi wa habari dhidi ya maamuzi ya Baraza la Uongozi la CHADEMA mkoa wa Shinyanga kumsimamisha nafasi ya Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini ambapo amesema maamuzi hayo ni batili na ataendelea na nafasi hiyo na kubaki kuwa mwanachama mwadilifu wa Chadema.