ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 28, 2023

ALIYEMLEA NA KUMSOMESHA MILEMBE ASIMULIA NAMNA ALIVYOISHI NA MAREHEMU


NA ALBERT G.SENGO/MISUNGWI Sospeter Mkakaru ni shemeji wa marehemu Milembe Suleiman ambaye alimsomesha marehemu katika ngazi ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza. Mwili wa marehemu, Milembe Suleiman, aliyekuwa Afisa Ugavi wa Kampuni ya Madini ya dhahabu ya Geita Gold Mine (GGM) umeagwa hii leo katika kitongoji cha Nyashimba, kijiji cha Sanjo kata ya Usagara wilayani Misungwi mkoani Mwanza ambapo baadaye umesafirishwa kuelekea mkoani #Geita kwaajili ya mazishi.

Thursday, April 27, 2023

Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akutana na kuzungumza na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame, Ikulu Jijini Dar es Salaam


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame mara baada ya Kuwasili katika ukumbi wa Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Aprili, 2023.


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Aprili, 2023. Rais wa Rwanda Mhe. Kagame amewasili nchini kwa ajili ya ziara ya Kikazi ya Siku 2.

 


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mgeni wake Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Aprili, 2023

 



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mgeni wake Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Aprili, 2023

WATOTO 1871 KUPATA CHANJO WILAYA YA NACHINGWEA

 

Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo akimpatia matone ya chanjo mmoja ya watoto waliofika katika hospital ya wilaya ya Nachingwea kuwapeleka Watoto wao kupata chanjo.

Na Fredy Mgunda, Nachingwea.

MKUU wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo amezindua wiki ya chanjo kwa Watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wasichana wenye umri wa miaka 14 kupata chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi.

Akizungumza wakati uzinduzi wa wiki ya chanjo, Moyo alisema kuwa wilaya ya Nachingwea wanatarajia kuwafikia walengwa wa chanjo wapatao 1871 kwa lengo la kuwakiga na magonjwa mbalimbali.

Moyo alisema kuwa serikali ya wilaya ya Nachingwea imejipanga vikivyo kuhakikisha walengwa wote wanaotakiwa kupata chanjo wanapata katika maeneo husika ili kufanikisha kuwakinga Watoto na magonjwa mbalimbali.

Aliwaomba wazazi wote wilaya ya Nachingwea kuwapeleka Watoto wao kupata chanjo Kwenye vituo vya afya, zahanati na hospital yoyote iliyopo karibu yao.

Moyo alisema kuwa mtoto asiyepata chanjo ni hatari kwa maisha yake na kwa jamii inayomzunguka kwa kuwa atakuwa na uwezo wa kuwaambukiza wengine ugonjwa alionaa kwasababu hana kinga za kutosha kuulinda ugonjwa huo.

Alisema kuwa ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha anamlinda mtoto wake kwa kumpeleka Kwenye vituo vya afya, zahanati na hospital yoyote ile mtoto wake akapate chanjo ya Kinga.

JIJI LA TANGA LAMPONGEZA RAIS DKT SAMIA SULUHU KWA KUONYESHA UONGOZI ULIOTUKUKA

 

Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shillow akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la Robo tatu kilichoketi leo kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Pili Mnyema na kulia ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt Sipora Liana


Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Meja Mstaafu Hamisi Mkoba akizungumza wakati wa kikao hicho


Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt Sipora Liana akizungumza wakati wa kikao hicho
Sehemu ya madiwani wakiwa kwenye kikao hicho
Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga wakiwa kwenye baraza hilo
Sehemu wa madiwani wakifuatilia hoja mbalimbali



Na Oscar Assenga, Tanga. 

HALMASHAURI ya Jiji la Tanga limepongeza Rais Dkt Samia Suluhu kwa kutimiza miaka miwili madarakani kwa kuonyesha uongozi uliotukuka katika mambo mbalimbali ikiwemo kuendeleza miradi mikubwa iliyoacha na mtangulizi wake hayati Dkt John Magufuli. 

Pongezi hizo zimetolewa leo na Mshtahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shilloo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha Robo ya tatu ambapo alisema licha ya kuendeleza miradi lakini pia ameanzisha mingine mikubwa ikiendana na kupelekea fedha nyingi kwenye ngazi ya Halmashauri ikiwemo Tanga Jiji ambao pia wamenufaina nazo. 

Shillow alisema pamoja na hayo lakini Rais Dkt Samia Suluhu amefungua upya milango ya ajira kwa watumishi wa umma baada ya kuingia madarakani kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma na kuwapatia unaafuu katika kodi mbalimbali ili waweze kukidhi mahitaji yao na kudumu masiaha yao. 

“Lakini jambo jingine ni Rais Dkt Samia Suluhu kuongeza mikopo ya elimu ya juu, kuondosha riba kwa wanafunzi kwenye mikopo hiyo sambamba na kufungua milango ya demokrasia kwa kuenzi utanzania umoja, mshikamano na undugu kwa watanzania bila kujali tofauti za kiitikadi “Alisema Mshtahiki Meya huyo. 

Hata hivyo alisema kwamba wanampongeza pia kwakutoa matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanywa kidigitali kwa mara ya kwanza tokeo nchi ipate uhuru ikiwemo kugawa vishikwambi vilivyotumika katika sensa kwenye idara ya elimu sekondari na msingi za Halmashauri nchini ili kuimarisha elimu na uwekaji wa takwimu za elimu pamoja na kuifungua nchi kwenye mambo ya utalii na mahusiano ya kikanda na kimataifa.

MAMA KOKA AFANYA KWELI AWAFUNGULIA AKAUNTI ZA BENKI WANAWAKE WA UWT KUJIKWAMUA KIUCHUMI

 


Na Victor Masangu,Kibaha.


Mke wa mbunge wa jimbo la Kibaha mjini Selina Koka ameahidi kuwainua kiuchumi wanawake wa kata ya misugusugu na kongowe kwa kuwawezesha kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali pamoja na kuwapatia mitaji ya fedha ili kuondokana na umasikini.

Selina ambaye pia ni mlezi wa UWT Wilaya ya Kibaha mji amesema lengo lake kubwa kuwapambania wanawake wote was uwt kwenye Jimbo la Kibaha kwa kuwasaidia waweze kufanikiwa katika shuguli zao mbali mbali za ujasiriamali.


"Ninachotaka kukifanya ni kuwawezesha wanawake wajasiriamali ili waweze kuanzisha biashara zao ambazo zitawasaidia kujipatia fedha na kujikwamua kiuchumi na kwamba nitasaidia katika kata zote 14 za Jimbo hili,"alisema Mgonja.

Alifafanua zaidi Selina Koka aliongeza kuwa mikakati yake ni kuwafungulia akaunti wanawake wa UWT kwa kuwapa kiasi cha shilingi laki tano ili waweze kuanzisha biashara.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mji Elina Mgonja amebainisha kwa kwa sasa katika kata ya misugusugu kumekuwa na maendeleo katika sekta mbali mbali.

Aliongeza kuwa Mbunge Koka amekuwa mstari wa  mbele katika kusikiliza kero na changamoto mbali mbali zinazowakali na kuzifanyia kazi katika maeneo ya afya,elimu pamoja na miundombinu ya barabara.

"Kitu kitubwa  sisi wanawake inabidi tuachane kabisa na mambo ya makando kando na kuwahimiza watu kulipa ada kwa wakati lengo ikiwa ni kujizatiti katika kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,"alisema Mgonja.

Katika hatua nyingine alimpongeza kwa dhati mlezi wa UWT Selina Mgonja kwa juhudi zake za kusaidia wanawake katika kuwawezesha ili kuweza kujikwamua  kiuchumi na kwamba ziara yake ni kuangalia uhai wa chama.

Wednesday, April 26, 2023

MWENYEKITI UWT KIBAHA AWAASA WANAWAKE KUSHIKAMANA KUKIJENGA CHAMA

 


Na Victor Masangu,Kibaha


Mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mji Elina Mgonja amewahimiza wanawake kushikamana kwa pamoja kwa lengo la kukiimarisha chama  ili kiweze kushinda katika chaguzi zake mbali mbali ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024.


Mgonja ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kutembelea wanachama  viongozi wa mbali mbali wa ccm ikiwemo pamoja na kuzungumza nao ili kubaini changamoto zinazowakabili ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi.

Mwenyekiti huyo alibainisha kwamba lengo lake kubwa ya kufanya ziara hiyo ni kwa ajili ya kukiimarisha chama pamoja na kupata taarifa mbali mbali za utekelezaji wa Ilani ya chama.


Pia aliwaasa viongozi mbali mbali wa ccm katika ngazi zote pamoja na kuwahimiza viongozi wa serikali za mitaa Kuhakikisha wanahudhulia katika vikao mbali mbali ili kuweza kutambua mambo ambayo yametekelezwa katika maeneo yao.

Kadhalika aliwaomba viongozi kuwa na utamaduni wa kuyasemea mambo ambayo yanatekelezwa na madiwani pamoja na kazi za maendeleo ambazo zinafanywa na Mbunge wa kibaha mjini Silvestry Koka.


"Kwa Sasa inabidi tujipange kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa hivyo viongozi wenzangu inatakiwa kushikamano kwa pamoja ili tuweze kusinda kwa kishindo katika uchaguzi huo bila kupoteza nafasi hata moja,"alisema Mngonja.

Kadhalika alimpongeza mlezi wa UWT Selina Koka kwa kuweza kuwasaidia wanawake katika nyanja mbali mbali ikiwemo kiuchumi na kuwaondoa katika wimbi la umasiki.

Kwa upande mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Selina Koka ambaye pia ni mlezi wa umoja huo alibainisha kuwa ataendelea kuwasaidia kwa hali na mali ili waweze kujikwamua kiuchumi.


Ziara ya Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mji pamoja na kamati ya utekelezaji imewajumuisha viongozi mbali mbali wa chama  pamoja na jumuiya zake lengo kubwa ikiwa ni kukiimarisha chama  ili kiweze kushinda katika chaguzi mbali mbali

LITA BILIONI 6 ZA MAJI TAYARI ZIMEINGIZWA BWAWA LA MWALIMU NYERERE

 NA ALBERT G.SENGO/PWANI

KASI ya ujazaji maji bwawa la Mwalimu Nyerere imefikia ujazo wa lita za maji bilioni sita huku ikibaki mita kumi na tatu tu kufikia kiwango cha maji yatakayoweza kuzungusha mitambo ya kufua umeme ambapo hatua hiyo imetajwa kuwa ni kiwango kizuri kutokana na kuzidi matarajio yaliyopo katika ujazaji wa bwawa hilo. Waziri wa Nishati, January Makamba amefika kwenye mradi wa bwawa kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere Hydro Power Project iliopo Rufiji Mkoa wa #Pwani kukagua hatua na maendeleo mbalimbali yanayoendelea kufanyika kwenye mradi huo. Waziri Makamba amesema Maendeleo ya mradi ni mazuri kwa sasa, Na kwa mujibu wa takwimu za kiwango cha uingiaji wa maji ni kikubwa kuliko kiwango cha Maji cha mwaka 2019/2020 kilicholeta mafuriko kwa mikoa ya Pwani na Morogoro. Kasi ya ujazaji maji katika bwawa hilo inaenda sambamba na kasi usukaji na usimikaji wa mitambo ya kufua umeme pamoja na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme. #samiasuluhuhassan #ikulumawasiliano #makamba

MKOA WA MWANZA WAADHIMISHA MIAKA 59 YA MUUNGANO KWA KUZINDUA KAMPENI YA UHIFADHI MAZINGIRA NA CHANJO

 

 

Mkoa wa Mwanza leo Aprili 26,2023 umeadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuzindua kampeni ya kupanda miti milioni 23 ña kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo dhidi ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika kimkoa Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza kwenye viwanja vya Chuo cha Ufundi Stadi(VETA) kilichopo wilayani humo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amesema lengo ni kuufanya mkoa huo kuwa mfano kitaifa kwa kupanda na kutunza miti pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji.

“Tutakapopanda miti Mwenyekiti na Mtendaji wa wa Kijiji watawajibika kuilinda hatuwezi kuwa tunafanya mchezo kwenye mambo ya muhimu, kama mwananchi atapeleka mifugo yake kuchunga kwenye eneo lililopandwa miti atalipa faini pamoja na kupanda miti iliyoliwa ama kuharibiwa na mifugo wake.

” Tutengeneze elimu chungu kwa wananchi ili watunze mazingira na kuhifadhi miti tunachohitaji ni kukabiiana na ukame pamoja na mabadiliko ya tabianchi wote tuwe na moyo wa kuijenga Tanzania yetu kwa faida yetu na vizazi vijavyo,”amesema Mhe.Malima.

Ameongeza kwamba ili kufanikisha lengo hilo la kupanda miti milioni 23, kila wilaya zimepangiwa kiasi cha miti ya kupanda ambapo amefafanua kwamba Wilaya za Ilemela na Nyamagana kwa kuwa hazina maeneo ya kupanda miti zitalazimika kununua maeneo kwenye wilaya zingine mkoani humo na kupanda miti hiyo kisha zitaimiliki.

Akizungumzia umuhimu wa chanjo za polio, surua, kifua kikuu na homa ya ini kwa watoto wenye umri chini ya miaka miwili Mhe.Malima amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kuandaa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo kwa kundi hilo ili kuwaepusha na madhira mbalimbali yanayoweza kuwapata ikiwemo vifo au ulemavu wakati serikali inazitoa bure ili kuwalinda waweze kujenga taifa la kesho.

Aidha amewataka wananchi wa mkoa huo kuuenzi muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuvumiliana, kustahimiliana, kuheshimiana, kupendana, kusaidiana na kukosoana kwa kuambiana ukweli kwa staha lakini sio kutukanana.

MSHIKAJI NYOKA MAARUFU AFARIKI BAADA YA KUNG'ATWA NA NYOKA MWENYE SUMU


Mshikaji mashuhuri wa nyoka nchini Uganda ambaye pia alikuwa muuzaji wa mnyama, huyo amefariki dunia baada ya kuumwa na nyoka mwenye sumu akiwa katika mawindo.

Kulingana na mkewe, Abdallah Kalule mwenye umri wa miaka 38, aliona nyoka likiingia kwenye kichuguu karibu na nyumba yao na kama kawaida alimfuata.

Kalule aliwinda nyoka na kuwauza zaidi kwa waganga wa kienyeji kwa Ksh.5,400 sawa na (93,466.13)

Nyoka huyo alimuuma na kutoroka wakati wa misheni yake ya uwindaji, na kumwacha akipambana na sumu.

Mjomba wake Kalule ambaye ni Mariam, amesema Kama kawaida, alichukua jembe na kuanza kuchimba kichuguu kikubwa. Uchimbaji ulichukua muda na nyoka kutoonekana

John Jjingo, aliongeza kuwa japo familia yake wana historia ndefu ya kukamata na kuuza nyoka, wameamua kuachana na biashara hiyo baada ya kifo cha Kalule.

Marehemu Kalule alikuwa amekamata kwa muda mrefu nyoka ambao baadhi yao walikuwa wakubwa kuliko waliomuua.

Hatuwezi kuendelea na biashara hatari kama hii ambayo inaweza kutufanya kupoteza maisha yetu.

Tutajikita katika shughuli nyingine kama vile nyanya na mahindi,” alisema Jjingo.

Tuesday, April 25, 2023

WABUNGE WA AZIMIO NCHINI KENYA WAMUAGIZA RUTO KUMKAMATA PIA YESU WA TONGAREN

 NA ALBERT G.SENGO

Wakati taarifa za mwanzilishi wa kanisa la Good News International Paul Mackenzie zikiwa zimegonga vichwa vya habari kwa takribani wiki moja sasa huku mtumishi huyo akiwa ameswekwa ndani, bunge la nchini Kenya limemtaka Rais wa nchi hiyo William Ruto kumkamata pia mchungaji maarufu kama Yesu wa Tongaren kwani naye anadaiwa kuwa ni mmpotoshaji.

BIBI ADAKWA NJAMA KUMUUZA MJUKUU WAKE SH7 MILIONI

 

Mwanamke mmoja (jina limehifadhiwa) jijini Nairobi nchini Kenya ameshtakiwa kwa kosa la kula njama ya kumuuza mjukuu wake kwa Sh400,000 ya nchini humo (Sh6.9 milioni).

Mwanamke huyo mwenye miaka 39 alikamatwa Aprili 9, 2023 na polisi ambao walijifanya wana nia ya kumnunua mtoto huyo mdogo mwenye siku tano.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la nchini humo limeripoti kuwa mtuhumiwa huyo alimchumkua mjukuu wake Kaunti ya Kakamega baada ya mtoto wake mwenye umri wa miaka 16 kujifungua na kumtaka akamlee mjini Nairobi ili binti yake aendelee na masomo.

Baada ya kufika Nairobi, mwanamke huyo alianza kutafuta mteja wa kumuuzia mtoto huyo kabla hajatiwa mikononi mwa polisi

“Walipanga kukutana kwenye mgahawa mmoja jijini Nairobi na hatimaye kuwakamata, wakamwokoa mtoto huyo na kumpeleka kwenye kituo cha kulelea watoto,” tovuti ya Daily Nation imeripoti.

Mshukiwa huyo yupo rumande tangu akamatwe baada ya polisi kupata agizo hilo kutoka mahakamani.

MBUZI WAKOROFI WASHINDA KESI YA UZURURAJI NA KUACHILIWA NCHINI UINGEREZA.


Kundi kubwa la mbuzi wakorofi wenye tabia ya kuzurura katikati ya mji nchini Uingereza wameachiliwa huru baada ya kushinda kesi ya uzururaji.

Mbuzi hao wamekuwa wakizurura mitaani kwa zaidi ya miaka 100 wakiwa na tabia mbovu za kula mimea na uzio wa nyumba za watu.

Isitoshe, mbuzi hao wenye pembe ndefu waliingia kwenye hoteli, wakipanga foleni nje ya nyumba ya utunzaji wakati wa chakula cha jioni wakitarajia chakula na kutembelea kituo cha huduma cha ndani.

Baraza la Halmashauri ya Llandudno, North Wales iliamuru mbuzi hao kuachiliwa licha ya tabia zao mbovu, likisema ni jukumu la wamiliki wa ardhi kulinda mali zao kutoka kwa genge la wanyama hao badala ya kuzuiliwa, Daily Star limeripoti.

Hata hivyo, pendekezo hilo lilikataliwa kufuatia maandamano makubwa ya umma mjini Bodlondeb.

Mbuzi hao walipata umaarufu mwaka wa 2020 walipovamia mitaa iliyoachwa tupu wakati wa janga la kimataifa la COVID-19.

Zaidi ya mbuzi 200 huondoka mara kwa mara kwenye eneo la Orme Mkuu kurandaranda mitaani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Halmashauri, hakuna mtu au shirika moja ambalo linawajibika kisheria kwa idadi ya mbuzi hao ambao Malkia Victoria alitoa kama zawadi kwa kiongozi wa eneo hilo.

INASIKITISHA WATOTO MAPACHA WAFARIKI KWENYE BWAWA LA KUNYWESHEA MIFUGO

 


NA ALBERT G.SENGO/MWANZA Watoto wawili mapacha wamekufa maji baada ya kutumbukia kwenye lambo la maji yaliyokuwa yametuama mita chache kutoka kwenye nyumba yao wakati wanacheza. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea jumapili ya Tarehe 23.04.2023 majira ya saa 14:00 mchana, huko katika kijiji cha Runele, Kata ya Hungumalwa, Tarafa ya Nyamilama Wilaya ya kwimba. Taarifa zaidi zinaarifu kuwa watoto hao wawili wa jinsia ya kiume ambao ni Kulwa Jimoku na Doto Jimoku, wote wakiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi sita, ambapo wazazi wao ni Jimuku Rozalia, miaka 28 na Avelina Nkwaya, Miaka 20, wote wakulima na wakazi wa kijiji cha Runele walikufa maji wakati wanacheza nje kidogo ya nyumba yao ambapo walitumbukia kwenye lambo la maji lililopo Mita 30 kutoka kwenye nyumba yao. Kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa lambo hilo limetengenezwa na wazazi hao kwa lengo la kuhifadhia maji ya kunyweshea mifugo yao. Kamanda amekitaja chanzo cha tukio hilo kuwa ni michezo ya watoto na uzembe wa wazazi kutokuwa makini kwa kuangalia watoto hao wadogo wanaohitaji kuwa na uangalizi wa karibu kutokana na umri wao kwani wakati tukio linatokea wazazi hao walikuwa wanaendelea na shughuli za kilimo . Miili ya marehemu hao Kulwa na Doto imefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya wilaya ya #Kwimba na kukabidhiwa kwa ndugu kwa mazishi.

'ENERGY DRINKS' TISHIO KWA AFYA


Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imetoa angalizo kwa wale wanaopenda kutumia vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini maarufu 'Energy drinks'.

Imesema katika utafiti wake mpya umebaini unywaji wa vinywaji hivyo kwa wingi unaweza kuleta madhara kwenye mishipa ya moyo ya kuziba ghafla na hata kusababisha vifo vya ghafla.

Hivyo, imeonya kuwa mtu asinywe zaidi ya kopo moja lenye ujazo wa mililita 250 ndani ya saa 24, huku ikisisitiza kama kuna uwezekano wa kuviepuka, ifanyike hivyo kulinda afya ya mhusika.

Baadhi ya vinywaji hivyo ndani yake kuna maji, sukari, ladha, caffein, mitishamba, tauline (amino acid), protini, vitamini, madini. Inaelezwa kuwa caffeine pamoja na mambo mengine, inafanya kazi ya kuzuia uzalishwaji wa kichocheo cha mwili kinachohusika na kulala ama kuhisi uchovu.

Utafiti huo wa kisayansi umehusisha unywaji wake na matatizo ya moyo na mishipa kuziba ghafla inayowakumba watu wa rika zote wanaovitumia hivi sasa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo JKCI, Pedro Palangyo alisema utafiti huo uliochapishwa juzi katika jarida moja maarufu la kisayansi nchini Marekani, unamhusisha kijana wa Kitanzania ambaye mshipa wake mkubwa wa moyo uliziba ghafla.

Hata hivyo, alisema miezi ya hivi karibuni JKCI imekuwa ikipokea vijana wengi hospitalini hapo wanaofika kutibiwa wakikabiliwa na changamoto mfanano na hizo, huku wakiwa na historia ya kutumia vinywaji hivyo.

Ongezeko la matumizi

Dk Pedro alisema matumizi ya vinywaji vya kuongeza nguvu yamekuwa makubwa katika jamii na yanaongezeka huku vijana wengi wakivitumia si kwa sababu ya kujipa nguvu, bali kwa kupenda ladha yake.

"Energy drinks husababisha damu kuwa nzito kuliko inavyopaswa na ikiwa nzito inaweza kusababisha damu kuganda kama ilivyokuwa katika kisa hiki, kwa hiyo ni muhimu kuendelea kupaza sauti kwa jamii zetu na kwa wale wanaviotumia ni vizuri wakaacha kabisa," alisema Dk Pedro.

Alisema takwimu za hivi karibuni za taasisi hiyo zinaonyesha wanapata wagonjwa wengi wa mishipa kuziba kwa watu wenye umri mdogo ambao katika hali ya kawaida ya ugonjwa huo umri mdogo ni mtu yeyote chini ya miaka 45.
 

Ukubwa wa tatizo

Wanamichezo, wanafunzi na watu wanaofanyakazi ngumu ndiyo wanaotajwa zaidi kutumia vinywaji hivyo wakiamini huwaondolea usingizi, uchovu na kuwapa nguvu zaidi.

Wapo wanamichezo ambao hutumia saa chache kabla ya kuingia mchezoni au mara baada ya kucheza wakiamini itawafanya kupata nguvu za ziada na kucheza kwa kiwango.

Huku wanafunzi na madereva wakivitumia siku za mitihani ili kuuondoa usingizi na wanywaji wa pombe kali aina ya spiriti na whiskey hutumia kuchanganyia.

Hata hivyo, wataalamu walisema iwapo mwili umechoka na unaulazimisha kwa kutumia visaidizi ina madhara.

"Ni kweli caffein husisimua mfumo wa fahamu na kumfanya mtumiaji kuhisi kuchangamka na kuondoa uchovu. Caffein huainishwa kisayansi kama kundi la opiod yaani dawa ya kulevya aina ya kichangamshi kiwango chake katika vinywaji hivi kinakubalika ni salama kwa matumizi ya binadamu lakini unapoulazimisha mwili unauchosha zaidi na unapozidisha lazima upate madhara na hatushauri kuchanganya na pombe kali ina madhara makubwa," anasema daktari wa bingwa wa magonjwa ya moyo, Enock Erick.

DARAJA LAFUNGWA BAADA YA ATHARI ZA MVUA.


Kamati ya Ulinzi Wilayani Malinyi limefunga kwa muda matumizi ya daraja la BUTU linalounganisha Tarafa za Ngoheranga na Malinyi kutokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha.


Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Sebastian Waryuba na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na usalama wametembelea maeneo ambayo yanatajwa kuathiriwa na mvua za masika zinazoendelea kunyesha Wilayani humo


Kulingana na kufungwa kwa daraja hilo Mawasiliano kati ya Tarafa za Ngoheranga,Malinyi na Mtimbira yamekatika.


Mkuu wa Wilaya amewashauri wananchi kipindi hiki Cha mvua wasifanye safari ambazo sio za lazima wakati serikali inaendelea kutatua tatizo la daraja BUTU.


Athari hizo za madaraja na maji kujaa katika maeneo mbalimbali zinatokana na mvua za masika zinaendelea kunyesha Wilayani humo.


Tutaendelea kukujuza kwa maeneo mengine yaliyoathiriwa na mvua hizo.

Monday, April 24, 2023

'KWA WIZI HUU WA FEDHA ZA SERIKALI TUNAAMBIWA SUBIRI HADI MWEZI WA 11?' HECHE ANG'AKA AKIICHAMBUA RIPOTI YA CAG

 NA ALBERT G.SENGO/MWANZA

Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, John Heche ameendelea kuwachongea kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Mawaziri, viongozi na watendaji wa wizara, mashirika na taasisi za umma zinazotajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akitaka wawajibishwe. Heche ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amemshauri Rais Samia kuanza kwa kuiwajibisha kwa kuiondoa ofisini manejimenti ya Shirika la Reli nchini (TRC) kama alivyofanya kwa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo baada ya ripoti ya CAG kuibua kashfa ya hasara ya Sh1.7 trilioni kwa kutoa zabuni bila ushindani.

MBUNGE UMMY AWAPA POLE WAATHIRIKA WA MVUA MAKORORA TANGA

  

Mbunge wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya katikati akimuonyesha kitu Afisa Mazingira wa Jiji la Tanga Kizito Mkwambi wakati alipofanya ziara kuangalia athari za mafuriko iliyotokana na mvua


MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya katikati akimsikiliza Afisa Mazingira wa Jiji la Tanga Kizito Mkwambi kulia wakati alipofanya ziara kuangalia athari za mafuriko iliyotokana na mvua

Na Oscar Assenga,Tanga. 


Mbunge wa Tanga Mhe Ummy Mwalimu leo tarehe 23/4/2023 akiambatana na Afisa Mazingira wa Jiji la Tanga,  Kizito Mkwambi amekagua baadhi ya miundombinu iliyoathirika na mafuriko jijini Tanga, ikiwemo eneo la Ziwani, Kata ya Usagara na Mzingani. 


Mhe Ummy ambaye pia ni Waziri wa Afya amelitaka Jiji na Tarura Wilaya ya Tanga kuangalia namna ya kuzibua mirefeji iliyoziba haraka ili kuondoa kero ya mafuriko eneo hilo na maeneo mengine ya Jiji. 

Aidha Mhe Ummy ameeleza kuwa Suluhisho la kudumu la kuondoa kero sugu ya mafuriko eneo la Ziwani ni kutafuta fedha ili kuchimba mfereji wa kupitisha maji yanayotuama katika eneo hilo. 

KOKA AFANYA KWELI AMWAGA MIFUKO 100 UJENZI WA OFISI YA BAKWATA KIBAHA.

 


Na Victor Masangu,Kibaha 

Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ametekeleza ahadi yake kwa vitendo kwa kuamua kuchangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuanza  ujenzi wa ofisi za Bakwata Wilaya ya Kibaha.

Koka ameyasema hayo wakati wa Baraza kuu la Eid Wilaya ya Kibaha ambalo lilifanyika katika viwanja vya shule ya msingi kongowe na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa kiislamu kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Mkoa.

Mbunge huyo alisema kwamba amekuwa  kushirikiana bega kwa bega na Baraza kuu la waislamu kuanzia ngazi ya Wilaya kwa kipindi kirefu tangu mnamo mwaka 2015 na kwamba amechangia mifuko hiyo ikiwa ni moja ya utekelezaji wa ahadi yake kwa vitendo.

"Mimi Kama Mbunge katika kipindi Cha Baraza lililopita nilipokea maombi kuhusu ukosefu wa kuwa ña ofisi ya Bakwata Wilaya ya Kibaha kwa hivyo nikawaambia watafute eneo kwa ajili ya ujenzi na leo nimefurahi kwani nimekwenda kulitembelea na ndio maana nimeanza na mifuko 100,,"alisema Koka.


Pia Koka pia katika Baraza hilo aliungwa mkono na mjumbe wa halmashauri ya ya chama cha mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mansoor Musa ambaye na yeye kuchangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo.


Katika hatua nyingine Koka aliwaasa wawazi na walezi Kuhakikisha wanaweka misingi imara katika kuendelea kuzilinda mila na desturi pàmoja na kuimarisha maadili katika jamii inayotuzunguka.


Kwa Upande wake  kaimu Sheikh Zuberi Chamgunda alimpongeza kwa dhati Mbunge Koka kwa kushirikiana na jamii kwa hali na mali ikiwemo kutekeleza ahadi yake ya kuchangia mifuko 100 ya saruji.


Nao baadhi ya waislamu ambao walishiriki katika Baraza hilo la Eid walisema kuwa kupatikana kwa ofisi ya Bakwata Wilaya itakuwa ni mkombozi kwao hivyo wamewaomba wadau wengine kuiga juhudi za Mbunge Koka kujitolea kwa moyo katika shughuli za kijamii.