Mkoa wa Mwanza leo Aprili 26,2023 umeadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuzindua kampeni ya kupanda miti milioni 23 ña kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo dhidi ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika kimkoa Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza kwenye viwanja vya Chuo cha Ufundi Stadi(VETA) kilichopo wilayani humo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amesema lengo ni kuufanya mkoa huo kuwa mfano kitaifa kwa kupanda na kutunza miti pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji.
“Tutakapopanda miti Mwenyekiti na Mtendaji wa wa Kijiji watawajibika kuilinda hatuwezi kuwa tunafanya mchezo kwenye mambo ya muhimu, kama mwananchi atapeleka mifugo yake kuchunga kwenye eneo lililopandwa miti atalipa faini pamoja na kupanda miti iliyoliwa ama kuharibiwa na mifugo wake.
” Tutengeneze elimu chungu kwa wananchi ili watunze mazingira na kuhifadhi miti tunachohitaji ni kukabiiana na ukame pamoja na mabadiliko ya tabianchi wote tuwe na moyo wa kuijenga Tanzania yetu kwa faida yetu na vizazi vijavyo,”amesema Mhe.Malima.
Ameongeza kwamba ili kufanikisha lengo hilo la kupanda miti milioni 23, kila wilaya zimepangiwa kiasi cha miti ya kupanda ambapo amefafanua kwamba Wilaya za Ilemela na Nyamagana kwa kuwa hazina maeneo ya kupanda miti zitalazimika kununua maeneo kwenye wilaya zingine mkoani humo na kupanda miti hiyo kisha zitaimiliki.
Akizungumzia umuhimu wa chanjo za polio, surua, kifua kikuu na homa ya ini kwa watoto wenye umri chini ya miaka miwili Mhe.Malima amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kuandaa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo kwa kundi hilo ili kuwaepusha na madhira mbalimbali yanayoweza kuwapata ikiwemo vifo au ulemavu wakati serikali inazitoa bure ili kuwalinda waweze kujenga taifa la kesho.
Aidha amewataka wananchi wa mkoa huo kuuenzi muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuvumiliana, kustahimiliana, kuheshimiana, kupendana, kusaidiana na kukosoana kwa kuambiana ukweli kwa staha lakini sio kutukanana.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.