ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, July 19, 2025

DED HALMASHAURI WILAYA YA MBEYA AWEKA MIKAKATI KABAMBE YA KUBORESHA KIWANGO CHA ELIMU

 

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Erica Yegella.

Na Mwandishi wetu, Mbeya

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Erica Yegella amewataka walimu wa shule za awali na msingi kuhakikisha wanawajibika ipasavyo kwa  kuweka misingi mizuri  na imara katika suala zima la  ufundishaji kwa watoto kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kuwa na uelewa wa  kujua kusoma, kuandika pamoja na kuhesabu lengo ikiwa ni katika kuboresha sekta ya elimu kuanzia ngazi za chini.

Yegella ameyasema hayo wakati wa halfa ya ugawaji wa madawati 50 katika  shule mbili za msingi ikiwemo jitegemee pamoja na shule ya msingi  ya Mlimareli zilizopo katika kata ya Utengule Usongwe ambayo yametolewa kwa msaada wa benki ya CRDB ikiwa ni katika kuunga juhudi za serikali ya awamu  ya sita  katika kuboresha kiwango cha  elimu.

Mkurugenzi huyo amesema kwamba watoto wote ambao wanasoma katika elimu ya awali pamoja na wale wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili pindi anapoingia kufanya mitihani yake anapaswa awe tayari anafahamu kusoma, kuandika, na kuhesabu hivyo walimu wanapaswa kulivalia njuga suala hilo ili kuongeza kiwango cha elimu kwa wanafunzi hao.
Aidha Mkurugenzi huyo  amebainisha kwamba madawati hayo yataweza kuwa mkombozi mkubwa kwa wanafunzi hao kuweza kuondokana na adha ya kusoma wakiwa katika mlundikano na kwamba wataweza kusoma katika mazingira ambayo ni rafiki zaidi na yataleta mabadiliko chanya ya kimaendeleio katika nyanja hiyo ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

"Kwa kweli kwa upande wangu mimi kama mkurugenzi nipende kushukuru sana benki ya CRDB kwa kuweza kukubali amaombi yetu ya kutusaidia madawati haya 50 ambayo tutaweza kuyagawanya katika shule mbili na nina imani yataweza kuwa msaada mkubwa kwa watoto wetu ambao ni wanafunzi wa shule mbili,"amesema Mkurugenzi huyo.

WANANCHI NACHINGWEA WANUFAIKA NA MIKOPO NAFUU, WAIKIMBIA "KAUSHA DAMU"

 

Mkurugezi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea Mhandisi chionda Kawawa akimkabidhi bajaji ya mkopo ya asilimia 10 ndugu Hamis Chilumba ikiwa ni sehemu ya shilingi milioni 649,781,998 zilizotolewa na Halmshauri hiyo akiwa sambamba na Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, Bi Stella Kategile
Mkurugezi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea Mhandisi chionda Kawawa akimkabidhi Guta ya mkopo ya asilimia 10 ndugu Zawadi Kanga ikiwa ni sehemu ya shilingi milioni 649,781,998 zilizotolewa na Halmshauri hiyo
Mkurugezi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea Mhandisi chionda Kawawa akiwakabidhi pikipiki za miguu miwili maarufu bodaboda kwa kikundi cha vijana ikiwa ni mkopo wa asilimia 10 ndugu  ikiwa ni sehemu ya shilingi milioni 649,781,998 zilizotolewa na Halmshauri hiyo


Na Fredy Mgunda, Nachingwea, Lindi.


Mikopo yenye riba kubwa, maarufu kama mikopo ya kausha damu, imekuwa kizingiti kikubwa kwa maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wengi nchini, hasa wafanyabiashara wadogo. Riba kubwa na masharti magumu ya urejeshaji yamewafanya wengi kupoteza mitaji na biashara zao.

Hata hivyo, nuru imeonekana kwa baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, baada ya serikali kuanzisha mpango wa utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Wananchi waliopokea mikopo hiyo, wakiwemo Zawadi Kanga, Ashura Chingu, Husura Mponga na Ramadhani Nambunga – wameeleza jinsi fedha hizo zilivyowasaidia kuondokana na adha ya mikopo yenye masharti kandamizi kutoka kwa taasisi binafsi na mabenki.

“Mikopo hii ya asilimia 10 ni tofauti kabisa. Hatunyonywi tena kama zamani. Tunafanya biashara kwa amani na kurejesha kwa mpangilio mzuri,” alisema mmoja wa wanufaika.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi kwa vikundi mbalimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Chionda Kawawa, alisema kuwa mpango huo ni sehemu ya mkakati wa serikali ya awamu ya sita wa kuwawezesha wananchi kiuchumi.

“Mikopo ya kausha damu imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wananchi wetu. Halmashauri imedhamiria kuwa sehemu ya suluhisho kwa kutoa mikopo isiyo na riba ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya wananchi,” alisema Mhandisi Kawawa.

Kwa mujibu wa Kawawa, jumla ya shilingi 649,781,998 zimetolewa kwa vikundi 54 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ili kuwainua kiuchumi na kuchangia pato la taifa kupitia shughuli zao za uzalishaji.

Aidha, aliwataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa uangalifu na kurudisha mikopo kwa wakati ili kuwezesha mzunguko wa fedha kwa vikundi vingine.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, Bi Stella Kategile, aliwakumbusha wanavikundi umuhimu wa uaminifu na nidhamu ya fedha.

“Wakirejesha kwa wakati, watakuwa wamefungua milango kwa wengine kunufaika. Pia, wataweza kukopa zaidi ya walichopata awali,” alisisitiza Bi Kategile.

Mpango huu wa mikopo isiyo na riba unatajwa kuwa mfano wa kuigwa katika kupunguza utegemezi na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi vijijini.


Wednesday, July 16, 2025

LIVE:- MKUTANO WA MKUU WA MKOA WA MWANZA NA WAANDISHI WA HABARI, DODOMA.

 Mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanz, Mhe. Said Mtanda na Waandishi wa Habari wa Jijini Dodoma kueleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan

Sunday, July 13, 2025

CHEGE, MADEE WAHAMASISHA CHAPA YA TANZANIA.

 Chege na Madee

Wasanii mahiri wa muziki wa Bongo Fleva, Chege Chigunda na Madee, maarufu kama ‘Samia Kings’, wamenogesha Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), Sabasaba, kwa kuhamasisha watanzania kuenzi na kununua bidhaa zenye nembo ya ‘Chapa Tanzania’ (Made in Tanzania).

Wasanii hao walipokelewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dk. Kedmon Mapana, katika banda la Karume ambalo linaonesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na watanzania.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Madee amesema ambao hawajafika katika maonesho hayo wafanye hima, ili kushuhudia bidhaa zinazotengenezwa na wazawa.

“Kama bado hujafika kwenye banda letu la ‘Made in Tanzania’, umepata dhambi. Kuna vitu vingi sana vya asili yetu ambavyo huwezi kuviona popote. Hii ni fursa ya kipekee kujifunza na kujivunia vyetu.”

Ameongeza kwa kusimulia kisa alichokutana nacho nje ya nchi aliponunua bidhaa zenye asili ya Afrika lakini zikiwa na nembo ya mataifa mengine:

“Nilinunua nyanya na vitunguu ambavyo nilijua kabisa vimetoka Tanzania, lakini ziliandikwa Made in nchi nyingine. Hii inaumiza. Ndiyo maana huu mpango wa Made in Tanzania ni ukombozi mkubwa kwa sisi waishio nje na wenye mapenzi na bidhaa za nyumbani.”

Kwa upande wake, Chege, amesisitiza kuwa Sabasaba inafanyika nyumbani kwake yaani Temeke, akijutia kutomleta binti yake Jada, kwenye maonesho hayo.

“Ningekuja naye tungenunua bidhaa nyingi za Kitanzania. Watoto wana mapema. Nawaomba wazazi wenzangu tuwalete watoto wetu, ndiyo kizazi cha kesho,” alisema.

Chege ameeleza kuvutiwa na ubunifu wa mavazi, viatu na bidhaa nyingine za viwandani vinavyotengenezwa hapa hapa nchini.

Msanii kutoka Afrika Kusini, amesema amevutiwa na ubora wa bidhaa za Tanzania na kuahidi kuwa balozi wa kuzitangaza kwa wenzake nyumbani..

Dk. Mapana, amewahimiza watanzania kutumia fursa ya Sabasaba kutembelea banda la Karume kujionea ubunifu wa ndani na kushiriki kukuza uchumi wa nchi kupitia bidhaa za ndani.


PINDA ATAKA HAKI MCHAKATO WA WAGOMBEA






Na Oscar Assenga,TANGA

WAZIRI Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Mizengo Pinda amehimiza viongozi waliopewa dhamana ya mamlaka ya kusimamia mchakato wa uteuzi wa wagombea kuhakikisha wanatenda haki kwa wale wote waliojitokeza kwenye kinyang’anyiro hicho .

Pinda aliyasema hayo leo mara baada ya kutembelea ukarabati wa ofisi ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga ambao umefikia asilimia 99 uliofanywa ikiwa ni ndoto za Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Rajab Abduhaman kuona jengo hilo linakuwa na muonekana mzuri kwa ajili ya kuwahudumia wana CCM.

Akiwa katika eneo hilo mara baada ya kutembelea ukarabati wa jingo hilo aliupongeza uongozi wa CCM kutokana na kazi nzuri walioifanya ya kukarabati jengo hilo na hivyo kuwa na muonekana mpya.

Alisema wakati nchi ikielekea kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu Octoba mwaka huu tayari maandalizi yameshaanza na waliochukua fomu Udiwani na Ubunge wameshafanya na kazi ya chama ni kuhimiza viongozi waliopewa dhamana ya mamlaka ya kusimamia mchakato watende haki.

“ Bahati nzuri kamati yenu mlisimamie kikamilifu ili mtu asipate sababu ya kupiga kelele wakati hakuna sababu ya kufanya hivyo kwa wananchi tunaomba wakati wa kupiga kura tumieni haki yenu tena kwa uhuru wenu wenyewe”Alisema

Aidha alisema pia kupitia utaratibu uliowekwa kabla ya kutoka kwenda kupambana na vyama vyengine lazima wampate mgombea wa chama atakayekwenda kupambana na vyama vyengine vya siasa tumieni haki yenu vizuri mtupe mgombea ambaye mnaamini anaweza kutuvusha kwa haraka zaidi.

Hata hivyo Waziri Mkuu Mstaafu Pinda alisema kwamba wanaendelea kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu na kumpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya nchi ipo kwenye utulivu na amani na mambo yanasonga mbele.

“Tanga kuna maneno nimesikia Rais hana deni na sisi na octoba tunatiki niombeni wana Tanga na wana CCM hilo jambo lipo mbele yenu na Tanga mlikuwa wapambanaji sana lazima jitihada kuhakikisha mnaongoza kwenye kura za Rais na Ubunge kwenye chaguzi zijazo”Alisema

Pinda aliwataka viongozi wa mkoa huo kuendelea kuchapa kazi pamoja na mshikamano kwa kuhakikisha wanaendelea kudumisha amani na ulitulivu ambao wanao mpaka sasa kutokana na kwamba haukudondoka tu angani bali umejengwa hivyo waendelee kumuomba mwenyezi Mungu aendelee kuisimamia.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abdurhaman amesema ukarabati wa ofisi hiyo ni maelekezo ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Dkt Samia Suluhu kuhakikisha mali za chama yakiwemo majengo ya chama ya ofisi na menginevyo wanayalinda na kuyafanyia ukarabati mkubwa ili yaendelee kutumika miaka mingi kadri inavyowezekana.

Aidha alisema kwamba alifanya ziara kwenye mkoa wa Tanga na katikati pita pita yake aliona jengo lao namna lilivyokuwa na kutoa maelekezo kuhakikisha jengo hilo linafanyiwa ukarabati mkubwa na hayo ni matunda ya Mwenyekiti wa Taifa na maelekeo yake.

“Tulipopata maelekezo hayo tukasema lazima tufanye kwa sababu haki na heshima ya CCM kwenye nchi na mkoa wa Tanga ni kubwa haiwezekani viongozi wa CCM wanaovyoonekana uzuri lakini mahali wanapofanyia kazi hapafanani na nasi tukasema hapana lazima watii maelekezo hayo na tunashukuru wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa na Kamisaa wao kwa umoja na mshikamano wao ndio umewezesha kutekeleza maelekezo hayo ya Rais”Alisema

Naye kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi ,Dkt Batilda Burian amesema wa wamefarijika uwepo wa Waziri Mkuu huyo na wanamshukru Mwenyekiti Taifa kwa kazi kubwa aliyoifanya wakati wa ziara yake na wana Tanga wanaendelea kumshukuru kwa mambo mengi makubwa ya kimaendeleo aliyofanya kwa mkoa huo.

“Kutokanana na hilo tunasema kwamba Mama Hana deni na Octoba tunatiki na kura zitajaa na kumwagika kutokana na kasi kubwa ya maendeleo aliyoyafanya katika mkoa wa Tanga na hivyo kuufungua kiuchumi”Alisema

Hata hivyo,Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Mfaume Kizigo alisema chama hicho kimepata kiongozi wa kwelikweli na kinachoonekana hapo ni sehemu ya maendeleo makubwa yaliyofanywa na Mwenyekiti huyo kutokana na kila wilaya amejenga byumba za watumishi kuanzia chama na Jumuiya zake zote na amefanya hivyo kila alipokwenda kuishauri kamati ya siasa.



Mwisho.