ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, September 28, 2023

Serikali, USAID Afya Yangu- RMNCAH waboresha huduma za lishe mkoani Mara

 

Zaidi ya watoto elfu moja wamepatiwa matibabu ya ugonjwa wa utapiamlo mkoani Mara katika kipindi cha mwaka 2022/23 ambapo kati yao, zaidi ya watoto 600 tayari wamepona ugonjwa huo.

Mganga Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt. Zabrone Masatu ameyasema hayo wakati akielezea jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kutoa elimu kwa jamii na kuboresha huduma za afya katika vituo vya afya na hospitali mkoani humo.

Dkt. Masatu amesema Serikali kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH wamefanikiwa kutoa matibabu ya utapiamlo kwa watoto 1,090 ambapo kati yao watoto 608 tayari wamepona kabisa ugonjwa huo unaotokana na lishe duni hususani kwa watoto.

Amesema baadhi ya watoto wenye utapiamlo wamekuwa wakichelewa kupata matibabu kutokana na wazazi kuamini imani za kishirikina na hivyo kuwapeleka kwa waganga wa tiba asili wakidhani wamelogwa na hivyo kuchelewa kupata tiba sahihi ya chakula lishe.

Dkt. Masatu amesema kutokana na imani hiyo, zaidi ya watoto 20 waliobainika kuwa na ugonjwa wa utapiamlo wamekatisha matibabu ambapo jitihada za kuwafuatilia zinaendelea kupitia kwa watoa huduma za afya ngazi ya jamii ambao wamepewa mafunzo na wamekuwa wakiwabaini pia watoto wenye utapiamlo.

“Tumekuwa tukifanya kazi na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH ili kuhakikisha tunaboresha afya ya watoto ambapo tumewajengea uwezo watumishi wetu na wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wanatusaidia kuwatambua watoto wenye utapiamlo na kuwaunganisha na tiba” amesema Dkt. Masatu;

“Pia kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH tumepata vibao 52 kwa ajili ya kutusaidia kupima viashiria vya utapiamlo kwa watoto katika vituo vyetu vya afya, tunashukuru Serikali kupitia mradi huu kila Halmashauri katika Mkoa wetu sasa ina Afisa Lishe anayesaidia kwenye utoaji huduma na kuwaelimisha wananchi kuandaa chakula lishe” ameongeza Dkt. Masatu.

Naye Afisa Lishe wa Halmashauri ya Bunda Mji katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Lucy Mwaluwyo amesema wakati mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH unaanza, kwa mwezi zaidi ya watoto 16 walikuwa wakitibiwa katika hospitali ya Bunda DDH na Manyamanyama tofauti na sasa ambapo idadi hiyo imepungua kwa wastani wa watoto sita hadi nane kwa mwezi.

Mwaluwyo amesema tayari amefanya kikao na waganga wa kienyeji na kuwaelimisha ili wanapoona mtoto mwenye dalili za utapiamlo ambazo ni pamoja na mtoto kunyong’onyea na mwili kuishiwa nguvu wawashauri wazazi kuwapeleka hospitalini.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Guta wilayani Bunda, Regina Samson amesema baada ya mwanae kuugua utapiamlo, hakujua ni ugonjwa gani hivyo ndugu walimshauri ampeleke kwa mganga wa kienyeji ambapo hata hivyo baada ya kumfikisha huko mtoto hakupona na hali yake ilizidi kuwa mbaya.

Baada ya Regina kuona hali ya mwanae inazidi kubadilika alimpeleka katika Hospitali ya Bunda DDH ambapo alibainika kuwa na ugonjwa wa utapiamlo na kuanzishiwa tiba ya chakula lishe iliyomsaidia mwanae kupona kabisa baada ya muda wa wiki tatu.

Hata hivyo hatua ya Regina kumtoa mwanae kwa mganga wa kienyeji na kumpeleka hospitalini ilipokelewa tofauti na mama mkwe wake aliyeamua kumtorosha mjukuu wake hospitalini ili kumrudisha kwa mganga wa kienyeji lakini kutokana na jitihada za watoa huduma za afya walimfuatilia na kumresha kwenye matibabu huku mvutano huo ukisababisha ndoa yake inayotajwa kuwa ya ‘nyumba ntobhu’ kuvunjika na hivyo kurejea nyumbani.

Mkasa mwingine kama huo umemsibu Remi Mayenga mkazi wa Kijiji cha Nyatwali wilayani Bunda aliyebaini mtoto wa kaka yake mwenye umri wa miaka miwili mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu amepelekwa kwa mganga wa kienyeji baada ya afya yake kudhoofika ambapo baada ya kumchukua na kumfikisha hospitalini alibainika kuwa na utapiamlo.

“Nilimpeleka katika Hospitali ya Bunda DDH akapatiwa matibabu kwa muda wa wiki tatu na sasa amepona. Wahudumu walitufundisha jinsi ya kutengeneza uji wa lishe kwa kutumia mtama, mchele, mbegu za maboga, michembe, karanga, soya na ufuta. Sasa anaendelea vizuri, nawashauri wananchi wenzangu kwamba si kila kitu ni kukimbilia kwenye mitishamba ama kwa waganga wa kienyeji” amesema Regina.

Mganga Mkuu mkoani Mara, Dkt. Zabrone Masatu amebainisha kuwa kabla ya mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH kuanza, matibabu ya utapiamlo yalipatikana katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara iliyopo wilayani Msoma na ile ya Shirati iliyopo wilayani Rorya lakini baada ya mradi huo, matibabu yanapatikana katika vituo vinne vya afya na hospitali 11 hatua ambayo imeondoa hatari kwa watoto chini ya miaka mitano kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Dkt. Masatu amesema kupitia mradi huo wa USAID Afya Yangu- RMNCAH, pia wanajamii wamefundishwa namna ya kuandaa vyakula vyenye lishe ambavyo vinapatikana katika mazingira yanayowazunguka ikiwemo dagaa, mtama, karanga, mhogo na mahindi hatua hatua iliyosaidia idadi ya watoto wanaougua utapia mlo kupungua.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mtoto akinywa uji wa lishe.
Mkazi wa Kijiji cha Nyatwali Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Remi Manabu akieleza jinsi tiba ya chakula lishe ilivyomsaidia mtoto wa kaka yake.
Bibi Mang'era Mang'era (62) mkazi wa Kijiji cha Guta Wilaya ya Bunda mkoani Mara akieleza namna tiba ya chakula lishe inayotolewa na hospitali ya Bunda DDH ilivyomsaidia mjukuu wake kupona ugonjwa wa utapiamlo.
Bibi Mang'era Mang'era (62) mkazi wa Kijiji cha Guta Wilaya ya Bunda mkoani Mara akiwa na mjukuu wake aliyepata tiba ya chakula lishe katika Hospitali ya Bunda DDH. Bibi Mang'era ndiye mama mzazi wa Regina Samson/ mama mzazi wa mtoto.
Bibi Mang'era Mang'era (62) mkazi wa Kijiji cha Guta Wilaya ya Bunda mkoani Mara akiwa na mjukuu wake aliyepata tiba ya chakula lishe.
Afisa Lishe Halmashauri ya Bunda Mji katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Lucy Mwaluwyo akieleza jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH kuimarisha huduma ya tibalishe kwa ajili ya watoto wenye utapiamlo katika hospitali ya Bunda DDH na Manyamanyama.

Wednesday, September 27, 2023

ZAIDI YA WAGONJWA 1000 WAFANYIWA UCHUNGUZI NA KUPATIWA MATIBABU KAMBI YA MADAKTARI BINGWA TANGA

 

Mratibu wa Kambi hiyo ambaye pia ni Mhazini wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt Mathew Shao kulia akiteta wakati wa kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa wa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga.

Wananchi wakiendelea kupatiwa huduma mbalimbali wakati wa kambi hiyo inayoendelea kwenye viwanja vya CCM Mkwakwani Jijini Tanga


Na Oscar Assenga, TANGA

ZAIDI ya wagonjwa 1000 wamefanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu katika kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa wa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga.

Kambi hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga Mhe. Ummy Mwalimu iliyoanza Septemba 25 mwaka huu na inayotarajiwa kumalizika leo tarehe 27 September ilikuwa ikitoa huduma za kibingwa katika magonjwa mbalimbali.

Akizungumza leo Mratibu wa Kambi hiyo ambaye pia ni Mhazini wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt Mathew Shao alisema mwamko wa wananchi umekuwa kuridhisha kutokana na kuongezeka idadi yao kila siku.

Dkt Shao ambaye pia ni Daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa alitaja magonjwa hayo ya kibingwa ni Moyo,Sukari,Mifupa,Pua/koo,masikio,wanawake na uzazi,kinywa na meno,watoto ,mfumo wa mkojo(Urojolia) na Macho.

Aliyataja magonjwa mengine ni ya Upasuaji,utoaji wa dawa na vipimo vya sukari,moyo-Echo,ECG,Utrasound,Sickle Cell,Uzito na urefu,hali ya lishe,ukimwi/TB,Ushauri na nasaha na elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza (NCD)

Tuesday, September 26, 2023

WATOROSHAJI MADINI KUKIONA SERIKALI YAJA NA MBINU MPYA ZAIDI SASA KUTUMIA GPS.

 NA ALBERT G. SENGO/MWANZA

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kuongeza udhibiti wa utoroshaji wa madini sambamba na kufanya kazi kwa kufuata Sheria ya Madini, kanuni zake na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali hivyo Sekta ya Madini kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025. Mavunde ameyasema hayo leo Septemba 26, 2023 jijini Mwanza kwenye kikao chake na menejimenti ya Tume ya Madini kilichoshirikisha Wakurugenzi, mameneja na maafisa madini wakazi wa mikoa. Viongozi walioshiriki ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Madini Nchini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba. Amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa udhibiti wa utoroshaji wa madini, maboresho ya mfumo wa usimamizi wa Leseni za Madini, biashara ya madini na kufanya tafiti za madini katika maeneo yote nchini kabla ya mwaka 2030 ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Madini ya Mwaka 2030 ya “Madini ni Maisha na Utajiri.” “Kwenye suala la utoroshaji wa madini Serikali haitamfumbia macho mfanyabiashara au mtu yeyote atakayebainika anatorosha madini, mkakati ni kuhakikisha madini yote yanauzwa kupitia masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini na Serikali kupata kodi itakayotumika kuboresha Sekta nyingine muhimu,” amesema Mavunde. Katika hatua nyingine, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kutatua migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini badala ya kusubiri kutatuliwa katika ngazi za juu. Aidha, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kufanya kazi kwa kushirikiana kwa upendo na kuongeza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zote katika Sekta ya Madini. Pia amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu wa hali ya juu na kusisitiza kuwa utendaji wao utapimwa kupitia matokeo yanayoonekana hususan kwenye maeneo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

WIZARA YA MADINI KURUSHA NDEGE YA UTAFITI NCHI NZIMA 'MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI'

 NA ALBERT G. SENGO/MWANZA

"Utajiri wa Sekta ya Madini ni taarifa hakuna uchawi mwingine wowote" 'MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI' fuatilia ufafanuzi wa kauli hii kutoka kwa Waziri wa Madini Mhe. Anthony Peter Mavunde (mbunge) aliyoitoa katika 'Kikao Kazi' cha Waziri huyo na Menejimbenti ya Tume ya Madini, kilichofanyika katika ukumbi wa BOT jijini Mwanza leo Tarehe 26 September 2023. "Unayoyaona yote haya kama matunda ya sekta hii yanatokana na eneo dogo sana lililofanyiwa utafiti, tumejiwekea malengo ifikapo mwaka 20230 tuwe tumelipitia eneo la nchi nzima kwaajili ya kufanya utafiti na tupate viashiria vya madini mengine tofauti tofauti ili tuongeze wigo na mchango wa Sekta hii katika uchumi wa Tanzania" alisema Waziri Mavunde na kuongeza "Tumedhamiria tutakwenda kufanya utafiti wa kina kwa kurusha ndege, helkopta na drones kupata picha za miamba yote kwa maeneo yote nchini yaani kufanya HIGH-RESOLUTION GEOPHYSICAL (HRG) SURVEYS ambayo itatupa picha kama hatua ya awali ya viashiria ili baadaye tuendelee na shughuli za uchorongaji na kuweza kubaini madini tuliyonayo" alisema Waziri Mavunde na kuongeza "Lakini hatua ya kwanza ni ya upigaji wa picha" #jembefm #samiasuluhuhassan #kaziiendelee #mwanza #mavunde

Monday, September 25, 2023

MAMIA YA WANANCHI WAJITOKEZA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA UCHUNGUZI TANGA

 

Huduma Matibabu ya Kibingwa zikiendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga 
Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Moi Dkt Hellena Mwijage akizungumza kuhusiana na kambi hiyo ya matibabu
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Jijini Tanga wakipatiwa huduma 

Huduma za upimaji urefu zikiendelea katika kambi hiyo
Sehemu ya Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo wakiendelea wakiwa tayari kuwahudumia wananchi kwenye kambi hiyo


Na Oscar Assenga, TANGA.

MAMIA ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Jijini Tanga wamejitokeza kwa wingi kwenye kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa kwa Uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani.

Kambi hiyo ya Huduma za Madaktari Bingwa imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ambapo siku ya kwanza ya zoezi hilo mwitikio wa wananchi walijitokeza kwa wingi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kupata matibabu wananchi hao walifurahia huduma hiyo huku wakikipongeza chama cha madaktari kwa kuwa na utaratibu huo mzuri kwa wananchi.

Akizungumza mmoja wa wananchi hao Jonas Mwakifuo ambaye ni Mkazi wa Mwanzange Jijini Tanga alisema kwamba huduma ambazo zinatolewa ni nzuri kwa sababu wananchi wengi wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali lakini hawana fedha za kuweza kugharamia matibabu.

Alisema hivi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la magonjwa mbalimbali ikiwemo tezi dume na mfumo wa mkojo na figo ambayo yamekuwa yakiwatesa wananchi wengi hivyo uwepo wa madaktari hao utawasaidia kuweza kupata matibabu ya kibingwa.

“Kwa kweli tunawashukuru madaktari Bingwa hawa maana hii imekuwa ni faraja kubwa sana kwetu kwa sababu tunapata huduma kwa hakika niwapongeeza madaktari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya”Alisema

Kwa upande wake mkazi wa Sahare Jijini Tanga Zuhura Omari alisema kwamba kambi hiyo imekuja wakati muafaka kwani hivi sasa wananchi wengi wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari na uzito mkubwa.

Alisema hivyo huduma hiyo inakwenda kuwa mwarobaini wa kutibu magonjwa hayo hivyo wanashukuru kwa madaktari wote ambao wamefanikisha huduma hiyo muhimu kwao.

Hata hivyo Mariam Saidi ambaye ni mkazi wa Barabara 12 Jijini Tanga alisema kwamba kambi hizo ni muhimu kutokana na kwamba zinawapa fursa wananchi kuweza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yanayowakabili kwa muda mchache.

Akizungumza katika kambi hiyo Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Moi Dkt Hellena Mwijage alisema kambi hiyo ni utaratibu ambao wamekuwa wamejiwekea kila wanapoadhimisha Kongamano la Madaktari nchini wanaanza na shughuli za kijamii.

Mwijage alisema kwa mwaka huu Kongamano hilo linafanyika mkoani Tanga hivyo wameanza na huduma za kijamii na wamepiga kambi kwenye uwanja wa Mkwakwani kwa muda wa siku tatu

Hellena ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) alisema kambi hiyo ya uchunguzi kwa magonjwa mbalimbali itakuwa ya siku tatu huku wananchi wakikaribishwa wajitokeze kuweza kupata huduma na matibabu rasmi na muhimu kutokana na matatizo yao.

Mama koka awakomboa walimu na wanafunzi shule ya msingi mwanalugali

 

Na Victor Masangu,Kibaha 

Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Selina koka katika kuunga mkono juhudi za Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kàtika kuboresha sekta ya elimu ametoa viti na meza  16  katika shule ya msingi Mwanalugali kwa ajili ya kuwasaidia walimu kukaa katika mazingira ambayo ni rafiki.

Selina amesema kwamba lengo lake kubwa ni kuboresha sekta ya elimu hivyo ameamua kutoa viti hivyo ambavyo vitaweza kuwasaidia walimu katika kutimiza majukumu yao ipasavyo na kuondokana na changamoto ambayo walikuwa wanaipata.
Alisema kwamba hatua hiyo ya kutoa viti hivyo ni kutokana na risala ambayo ilitolewa hivi karibuni  wakati wa mahafali ya shule ambapo walibainisha changamoto zao mbali mbali ambazo zinaikabili shule hiyo ikiwemo uhaba wa viti.

Aidha mbali na kutoa viti hivyo ametoa vifaa  mbali mbali  kwa ajili ya kufanyia usafi vikiwemo mafagio,sabuni za maji sulari,pamoja na  fedha kiasi cha shilingi laki mbili  kwa ajili kununua unga kwa ajili ya wanafunzi.

Aidha alibainisha kwamba vifaaa hivyo vitaweza  kuwapa fursa ya shule hiyo kuboresha mazingira ya shule hiyo yawe katika hali ya usafi.

"Nimefika katika shule ya msingi  ya Mwanalugali na nimetoa vifaa mbali mbali ikiwemo viti 16,vifaa vya usafi vikiwemo sabuni pamoja na mafagio ya nje pamoja na mafagio ya ndani na hii yote ni katika kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi na walimu,alisema Selina.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Tumbi mhe.Chokara alimpongeza Mama Selina Koka kwa juhudi zake za kuchangia katika sekta ya elimu na kuleta matokeo chanya katika kuchagiza maendeleo katika nyanja mbali mbali na kuwa karibu katika kuwasaidia wananchi.

Naye Mwenyekiti wa shule ya msingi Mwanalugali amemshukuru mke wa Mbunge Selina Koka kwa kutekeleza ahadi hiyo kwa vitendo kwa kutoa viti hivyo kwa ajili ya walimu.

Katibu wa jumuiya ya wazazi Mkoa wa Pwani alisema Selina Koka amekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Kibaha katia kutekeleza miradi mbali.mbali ya maendeleo.

Alisisitiza kwamba wananchi wanapaswa kuwa na ushirikiano na Mbunge wao lengo ikiwa ni kuleta mabadiliko katika nyanja mbali mbali ikiwemo elimu pamoja na mambo mengine.

Kaimu Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Mwanalugali amempongeza kwa dhati mke wa Mbunge Selina Koka kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta ya elimu.

Nao baadhi ya wazazi waliohudhulia katika halfa hiyo fupi nao hawakusita kutoa shukrani zao kwa msaada ambao ameweza kuutoa katika shule hiyo ikiwemo sukari,meza.mafagio pamoja na fedha