ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, September 25, 2023

MAMIA YA WANANCHI WAJITOKEZA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA UCHUNGUZI TANGA

 

Huduma Matibabu ya Kibingwa zikiendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga 
Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Moi Dkt Hellena Mwijage akizungumza kuhusiana na kambi hiyo ya matibabu
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Jijini Tanga wakipatiwa huduma 

Huduma za upimaji urefu zikiendelea katika kambi hiyo
Sehemu ya Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo wakiendelea wakiwa tayari kuwahudumia wananchi kwenye kambi hiyo


Na Oscar Assenga, TANGA.

MAMIA ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Jijini Tanga wamejitokeza kwa wingi kwenye kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa kwa Uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani.

Kambi hiyo ya Huduma za Madaktari Bingwa imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ambapo siku ya kwanza ya zoezi hilo mwitikio wa wananchi walijitokeza kwa wingi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kupata matibabu wananchi hao walifurahia huduma hiyo huku wakikipongeza chama cha madaktari kwa kuwa na utaratibu huo mzuri kwa wananchi.

Akizungumza mmoja wa wananchi hao Jonas Mwakifuo ambaye ni Mkazi wa Mwanzange Jijini Tanga alisema kwamba huduma ambazo zinatolewa ni nzuri kwa sababu wananchi wengi wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali lakini hawana fedha za kuweza kugharamia matibabu.

Alisema hivi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la magonjwa mbalimbali ikiwemo tezi dume na mfumo wa mkojo na figo ambayo yamekuwa yakiwatesa wananchi wengi hivyo uwepo wa madaktari hao utawasaidia kuweza kupata matibabu ya kibingwa.

“Kwa kweli tunawashukuru madaktari Bingwa hawa maana hii imekuwa ni faraja kubwa sana kwetu kwa sababu tunapata huduma kwa hakika niwapongeeza madaktari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya”Alisema

Kwa upande wake mkazi wa Sahare Jijini Tanga Zuhura Omari alisema kwamba kambi hiyo imekuja wakati muafaka kwani hivi sasa wananchi wengi wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari na uzito mkubwa.

Alisema hivyo huduma hiyo inakwenda kuwa mwarobaini wa kutibu magonjwa hayo hivyo wanashukuru kwa madaktari wote ambao wamefanikisha huduma hiyo muhimu kwao.

Hata hivyo Mariam Saidi ambaye ni mkazi wa Barabara 12 Jijini Tanga alisema kwamba kambi hizo ni muhimu kutokana na kwamba zinawapa fursa wananchi kuweza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yanayowakabili kwa muda mchache.

Akizungumza katika kambi hiyo Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Moi Dkt Hellena Mwijage alisema kambi hiyo ni utaratibu ambao wamekuwa wamejiwekea kila wanapoadhimisha Kongamano la Madaktari nchini wanaanza na shughuli za kijamii.

Mwijage alisema kwa mwaka huu Kongamano hilo linafanyika mkoani Tanga hivyo wameanza na huduma za kijamii na wamepiga kambi kwenye uwanja wa Mkwakwani kwa muda wa siku tatu

Hellena ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) alisema kambi hiyo ya uchunguzi kwa magonjwa mbalimbali itakuwa ya siku tatu huku wananchi wakikaribishwa wajitokeze kuweza kupata huduma na matibabu rasmi na muhimu kutokana na matatizo yao.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.