|
Mbunge wa Jimbo la Sengerema William Ngeleja. |
NA PETER FABIAN, SENGEREMA.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Sengerema kutekeleza miradi 10 ya maji kwa gharama ya shilingi bilioni 29.1kutoka katika chanzo cha maji cha ziwa Victoria.
Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara nyakati tofauti wananchi wa Kata za Nyamatongo na Busisi wakati wa ziara yake ya kikazi, Mbunge wa Jimbo la Sengerema William Ngeleja aliwaeleza wananchi hao kwamba Halmashauri hiyo imepitisha kiasi cha fedha Shilingi bilioni 29.1 katika bajeti za fedha za mwaka 2013/2014 na 2014/2015 kutekeleza miradi hiyo.
“Baada ya kumaliza kero ya upatikanaji wa umeme kwenye maeneo mbalimbali ya vijiji sasa tunashughulika na kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yanayokabiliwa na uhaba katika baadhi ya Kata ikiwemo Mji wetu wa Sengerema ambapo utekelezaji wake unaendelea,”alieleza.
Ngeleja aliwaeleza wananchi hao kuwa katika utekelezaji wa miradi hiyo iliyogawanywa sehemu kumi imelenga kumaliza kabisa kero hiyo ya maji ifikapo mwishoni mwa mwaka 2015 kama ilivyokusudiwa ili wanananchi katika maeneo hayo wapate maji safi na salama.
Katika kata ya Nyamatongo Mbunge alitoa kiasi cha shilingi 200,000. kwa ajili ya kununulia vipuli vipya vya Pampu ya kusukuma maji ambavyo vimeharibika na kusababisha kuwepo kero ya upatikanaji wa maji katani humo huku katika Kata ya Busisi akiahidi kufatilia.
Halmashauri ili kurejesha mashine mpya iliyokuwepo baada ya kuondolewa na kuretwa mashine mbovu na kusababisha maji kuwa tatizo.
Mbunge huyo akiwa Kata ya Busisi alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuhusu miradi iliyokwishakuanza kutekelezwa itakayotekelezwa kupitia fedha za bajeti zilizopangwa kwa miaka miwili ambapo aliitaja maeneo ilipo na gharama itakatotumika.
Ngeleja aliwaeleza wananchi hao kuwa miradi 10 ya maji inayotekelezwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 29.1 kutoka ziwa Victoria katika Kata za Nyasigu hadi Ngoma kwa gharama ya bilioni 1.6, Kata ya Chamabanda hadi Kasomeko kwa gharama shilingi milioni 500, Kata ya Nyatakubwa hadi Kasungamile kwa shilingi milioni 250.5.
Miradi mingine ni ilie iliyopo Kata ya Buyagu hadi Bitoto wa gharama ya bilioni 1.3, Kataya Chamabanda hadi Nyantakubwa wa gharama ya shilingi milioni 713.2, Kata ya Katunguru hadi Nyamutelela wa shilingi milioni 794.7, Kata ya Kakumulo hadi Nyampande wa shilingi milioni 408, Kata ya Chifumfu wa shilingi milioni 140.
Ngeleja alitaja mingine kuwa ni mradi wa maji wa Kata ya Kamanga hadi Nyamatongo wa shilingi milioni 405 na mradi mkubwa wa maji wa mjini Sengerema kutoka chanzo cha maji kilichopo kijiji cha Nyamazugo utakaogharimu kiasi cha bilioni 23sawa na USD milioni 14 ambapo baadhi itakamilika mwishoni mwa mwaka huu na mingine katikati ya mwaka 2015.
"Tutaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzitafutia ufumbuzi kero na changamoto ambazo zitaonekana kukwamisha utekelezaji wa miradi hiyo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati na zenye kiwango ambacho kinakubalika na hatuna muda wa kujadili baadhi ya maneno ya wapinzani wetu yanayolenga kutukatisha tamaa ili tusifikie lengo,"alisisitiza