ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 14, 2025

RAIS SAMIA KUTUA JIJINI MWANZA - RC MTANDA AFUNGUKA JUU YA MAPOKEZI

 NA ALBERT G.SENGO/MWANZA

Mwanza yazidi kung’ara! Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutua jijini Mwanza kwa ziara ya siku tatu yenye uzinduzi, hotuba na shamrashamra za kiutamaduni. RC Said Mtanda atoa wito: Wananchi, jitokezeni kwa wingi kumlaki Mama Samia – amani, mshikamano na uzalendo ndio silaha yetu!

Friday, June 13, 2025

CRDB Bank Foundation, StartHub Africa zaungana kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu

 

Meneja Uendelezaji Biashara Changa wa CRDB Bank Foundation, Sharron Nsule akitoa elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi walioshiriki semina katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Dar es Salaam, Tanzania – June 2025: Katika kuendeleza jitihada za kuinua ujasiriamali na kuwawezesha wanafunzi wabunifu, Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na StartHub Africa imevitembelea vyuo vikuu vitatu nchini na kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanafunzi wanaopenda kumiliki biashara baada ya masomo yao.

Ushirikiano huo unaotekelezwa kupitia programu ya “Uni Launch and Scale” tayari umewafikia zaidi ya wanafunzi 1,000 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Iringa na Taasisi ya Uhasibu Arusha (AIA) na kuwapa fursa ya kupata walezi wa kibiashara na mitaji wezeshi kutoka CRDB Bank Foundation.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema vyuo hivi vitatu ni mwanzo tu kwani lengo lililopo ni kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na kuwawezesha ili wanapohitimu au wakai wanaendelea na masomo yao waanze kushiriki shughuli za kuujenga uchumi baada ya kuwapa elimu ya fedha, mafunzo ya ujasiriamali na uhakika wa kupata mtaji wezeshi.

“Lengo letu ni kuamsha ari ya ujasiriamali iliyomo ndani ya wanafunzi wetu wa vyuo vikuu na kutoa mazingia rafiki kwao kuanzisha biashara zitakazoajiri vijana wenzao badala ya wao wenyewe kuwa waombaji wa kazi wakihitimu. Kupitia ushirikiano huu tunajenga kizazi cha vijana waliowezeshwa kushiriki kuujenga uchumi wa taifa letu,” anasema Tully.

Katika vyuo vitatu ambako wataalamu wa CRDB Bank Foundation na StartHub Africa wamepita, jumla ya biashara 30 zinazomilikiwa na kuendeshwa na wanafunzi zitachaguliwa baada ya kukaguliwa ili kuingizwa kwenye mpango maalumu wa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji biashara, utayari wa kifedha na utimamu wa bidhaa.

“Kwa kushirikiana na StartHub Africa pamoja na vyuo vikuu hivi, tunaamini tunaendeleza juhudi za kukuza ubunifu hasa wa kidijitali miongoni mwa wanafunzi wetu hivyo kujenga msingi imara wa biashara zinazoweza kukua na kuwanufaisha wananchi wengi,” amesema Tully.

Programu ya Uni Launch and Scale ambayo CRDB Bank Foundation inashirikiana na StartHub Africa kuitekeleza inalenga kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kutekeleza uwekezaji wanaoukusudia kwa kuwapa mafunzo, ulezi wa kibiashara na uwezeshaji wa mitaji kupitia Programu ya Imbeju iliyojielekeza kuwainua vijana, wanawake na makundi maalumu.

Meneja Programu wa StartHub Africa, Zagaro Emanuel anasema katika ushirikiano huu wanakusudia kuwawezesha vijana wengi wabunifu kupitia mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha hivyo kuchangia kuujenga uchumi na kusukuma mbele maendeleo ya Tanzania.

“Tunawahamasisha wanafunzi na wahitimu wa vyuo vikuu, tunawandaa waanzilishi wapya wa biashara watakaosaidia kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuimarisha ujasiriamali nchini kwa kushirikiana na vyuo vikuu, wawekezaji na wawezeshaji. Tukiwa pamoja na Taasisi ya CRDB Bank Foundation, tunaamini tutafika mbali na kuwajumuisha wanafunzi wengi zaidi nchini,” anasema Emanuel.

Meneja huyo anaongeza kwamba programu hiyo inawapa wanafunzi jukwaa la kujitangaza katika soko la ndani, kitaifa na kimataifa na wanapowasilisha mawazo ya miradi yao, wanajiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuvutia mitaji huku vyombo vya habari vikiwarahisishia kujulikana kwa biashara zao hivyo kujiongezea umanifu kwa wadau ambalo ni jambo jema kwa kila biashara.

'BOMU LATEGULIWA LIGI KUU' MWENYEKITI AJIUZULU, MTENDAJI MKUU ASIMAMISHWA GHAFLA.

 


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Steven Mnguto, amewasilisha barua ya kujiuzulu wadhifa wake, hatua inayokuja wakati ambapo kumekuwepo na mijadala mingi kuhusu mwenendo wa uendeshaji wa ligi hiyo.

Taarifa ya kujiuzulu kwa Mnguto imethibitishwa leo, Ijumaa Juni 13, 2025 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), likieleza kuwa barua hiyo imepokelewa rasmi na uamuzi huo utazingatiwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni za shirikisho hilo.


Katika hatua nyingine, Rais wa TFF, Wallace Karia, amemsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo, hadi hapo uchunguzi dhidi yake utakapokamilika. Taarifa ya TFF iliyotolewa usiku huu na Katibu Mkuu, Wilfred Kidao, haijaeleza sababu rasmi ya kusimamishwa kwa Kasongo, lakini imesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mchakato wa kiutawala unaolenga kuboresha uendeshaji wa ligi.


Hatua hizi mbili zimekuja wakati kukiwa na mvutano wa mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba ambayo awali ilikuwa ipigwe Machi 8, mwaka huu kabla ya kusogezwa mbele hadi Juni 15 mwaka huu. Hata hivyo wakati kukiwa na mvutano huo huku kila timu ikivutia upande wake, mapema leo bodi ya ligi imetangaza kuwa mchezo huo sasa utapigwa Juni 25.

Ratiba hiyo mpya ya mchezo namba 184 imekuja kufuatia viongozi waandamizi wa timu hizo kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dodoma mapema leo.

KARIAKOO DERBY YASOGEZWA MBELE, KUPIGWA JUNI 25

 


Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imesogeza mbele mechi ya Ligi Kuu namba 184 baina ya Yanga na Simba uliopangwa kuchezwa Juni 15 hadi Juni 25.

Taarifa hiyo imetolewa leo, Ijumaa, Juni 25 na TPLB.

“BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeusogeza mbele mchezo namba 184 wa
Ligi Kuu ya NBC kati ya klabu ya Yanga na klabu ya Simba ambao ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 15, 2025 kuanzia saa 11:00 jioni.


“Mchezo huo sasa utafanyika Juni 25, 2025 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

“Bodi inazitakia mandalizi mema klabu za Yanga na Simba kuelekea mchezo huo,” imefafanua taarifa ya TPLB.


Taarifa hiyo ya TPLB imetolewa muda mfupi baada ya kusambaa kwa picha zinazomuonyesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi wa Simba na Yanga, Ikulu Dodoma baada ya kufanya nao mazungumzo.

MOTO WA MAENDELEO MWANZA DUKA JIPYA LAVUTIA UWEKEZAJI MPYA - BIASHARA YAZIDI KUCHACHAMAA

 NA ALBERT GSENGO/MWANZA

Katika hatua inayoashiria kasi ya ukuaji wa sekta ya ujenzi na biashara jijini Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala, ametoa wito kwa wawekezaji hususan wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi kujitokeza na kuwekeza jijini hapa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa duka jipya la vifaa vya ujenzi la ABC Mwanza Hardware, Masala amesema uwepo wa maduka hayo utapunguza utegemezi wa bidhaa kutoka Dar es Salaam umbali wa wa zaidi ya kilimita 1,200 na kupunguza gharama za usafirishaji kwa wananchi wa Mwanza na mikoa jirani. “Tunahitaji makampuni kama haya kuja zaidi Mwanza. Wananchi wetu wanastahili huduma bora, za haraka na zenye bei nafuu. Uwekezaji huu ni dalili ya uhai wa kiuchumi wa jiji letu,” alisema Masala. Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Constantine Sima, amesisitiza kuwa ujio wa ABC Mwanza Hardware unamaanisha fursa zaidi kwa Kanda ya Ziwa, huku akilitaja jiji la Mwanza kama kitovu cha biashara kwa mikoa ya kaskazini magharibi. Mwakilishi wa kampuni ya ABC Mwanza Hardware, Bwana Sahares amesema wamejipanga kutoa huduma za kiwango cha juu kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kutoa vifaa vya ujenzi kwa bei rafiki, wakilenga kuwahudumia wateja wote wa Kanda ya Ziwa kikamilifu. Mbali na uzinduzi huo, tuangazie pia ni kwa namna gani ujio wa duka hilo jipya la vifaa vya ujenzi utaleta tija kwa wananchi na wafanyabiashara wa jiji la Mwanza. Zulfikar Nanji ni Mkurugenzi wa Kampumi ya Mwanza Huduma, anafafanua kwa kina mafanikio yanayotarajiwa kupitia uwekezaji huu. #samiasuluhuhassan #mwanza

Wednesday, June 11, 2025

UWT KIBAHA MJINI KUNOGILE WAJENGA NYUMBA YA KATIBU NA KUANZISHA MRADI WA MGAHAWA

 


VICTOR MASANGU, KIBAHA

Jumuiya ya  umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini katika kuunnga juhudi za Rais awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo imefanikiwa kuanzisha mradi wa mgahawa ikiwa kama ni moja ya  kitega uchumi kwa ajili ya kuweza kujikwamua kiuchumi  pamoja na mradi wa ujenzi wa  nyumba ya Katibu wa jumuiya hiyo.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Cecilia Ndaru wakati wa kikao cha kikanuni cha baraza hilo ambacho kimeweza kukutana kwa lengo la kujadili masuala mbali mbali ya kimaendeleo, kujiandaa katika kuelekea uchaguzi mkuu, mapokezi ya Mwenyekiti wa UTW Taifa sambamba na kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama  kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 kutoka kwa madiwani wa viti maalumu.

Katibu Ndaru amesema kwamba lengo lao kubwa ni kuweka mikakati madhubuti ya kuendelea kubuni na kunzisha miradi mipya ambayo itaweza kuwa ni mkombozi mkubwa kwa jumuiya hiyo kuweza kujiongezea kipato pamoja na kuweka misingi imara ya kuweza kuimarisha jumuiya hiyo kuanzia ngazi za chini.

Katika kikao hicho cha baraza ambacho kilifunguliwa  na Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Mwalimu Mwajuma Nyamka  ambaye alikuwa mgeni rasmi  amewataka wanawake hao kuhakikisha wanakuwa naa umoja na mshikamano hasa katika kioindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Nyamka katika baraza hilo amewahimiza wanawake kuchangamkia fursa za kugombea nafasi mbali mbali za uongozi ikiwemo katika nafasi ya udiwani pamoja na ubunge na kuwaomba wanampa kura nyingi za kishindo cha hali ya juu  Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi huo mkuu  amebainisha kwamba lengo la chama ni kuhakikisha wanashinda katika nafasi zote.

"Nawapongeza sana wanawake wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini kwa kuweza kuchapa kazi kwa bidii na mimi nimefaarijika sana kuona meweza kusimamia vemaa utekelezaji wa ilani ya chama na pia mmeweza kuanzisha mradi wa mgahawa amabo utaweza kuwa ni chachu ya kujikwamua kuchumi sambamba na ujenzi wa nyumba ya katibu kwa hivyo kitu kikubwa mfanye kazi na viongozi ambao bado wapo madarakani achanane na kampeni amabzo hazina faida kwa kipindi hiki,"amebainisha Nyamka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu kwa kuweza kutenga fedha nyingi ambazo zimekwenda katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu, afya, maji,miundombinu ya barabara pamoja na huduma nyingine za kijamii.

Aidha Mgonja amemshukuru Mbungu wa Jimbo la Kibaha mjini Mhe. Silvestry Koka pamoja na mke wake Mama Selina Koka kwa kuweza kuwa mstari wa mbele kupambana katika kuwasaidia kwa hali na mali kufanikiwa ujenzi wa mradi wa mgahawa pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba ya katibu wa UWT kwa kushirikiana na wadau na viongozi wengine wa chama pamoja na jumuiya zake.


Naye mlezi wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini ambaye pia ni mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Mama Selina Koka amewahimiza wanawake wote kuwa na umoja na mshikamano hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuwaomba kuwa mstari wa mbele katika kupiga kura lengo ikiwa ni kuweza kushika katika nafasi zote za udiwani, ubunge, pamoja na nafasi ya urais.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ambaye amefunga rasmi kikao cha baraza hilo ameishukuru kwa dhati jumiya hiyo ya wanawake kwa kuweza kumpa ushirikiano na sapoti kubwa katika kipindi chote ambacho aliingia madarakani na kuahidi kuendelea kushirikiano nao katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo na kutatua changamoto ambazo wanakumbana nazo.

Koka amebainisha kwamba tangu aingie madarakani mnamo mwaka 2010 ameweza kuwa bega kwa bega na jumuiya ya UWT ambapo wameweza kushirikiana katika baadhi ya miradi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa mradi wa nyumba ya Katibu pamoja naa kiteega uchumi cha mgahawa sambamba na kushirikishwa katika vikao mbali mbali vyebye kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo ikiwemo kutatua kero na changamoto za wananchi.

MKUTANO WA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI NA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DODOMA.

 Mkutano wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji mkuu wa serikali na waandishi wa habari kutoka Jengo jipya la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo - Mtumba, Dodoma.

Tuesday, June 10, 2025

'RUNGU JINGINE CHADEMA' - MAHAKAMA KUU YAIPIGA STOP KUFANYA SHUGHULI ZA KICHAMA.

 


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezuiwa kwa siku 14 kufanya shughuli zozote zile za kichama na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam.

Zuio hilo linatokana na kesi namba 8323/2025 iliyofunguliwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa na wenzake wawili ambayo imetolewa uamuzi leo na Jaji Hamidu Mwanga.

Uamuzi huo umetolewa huku CHADEMA ikikosa muwakilishi wa kisheria baada ya Wakili Jebrah Kambole aliyekuwa akisimamia kesi hiyo kujitoa kabla ya kutolewa uamuzi akidai kutosikilizwa kwa hoja zao.

Hatua ya CHADEMA kuzuiwa kufanya shughuli hizo inatokana na maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la Mawakili wa walalamikaji ya kwamba liwekwe zuio hilo hadi kesi ya msingi itakapoanza kusikilizwa Juni 24, 2025.

Mbali na Mohammed, wengine ni Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu wanaojitambulisha kama wajumbe wa bodi ya wadhamini.

Katika kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, wadai wanaiomba Mahakama hiyo itamke na kuamuru amri za kutamka kuwa, wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na katiba ya chama hicho.

Wamechukua hatua hiyo na kuomba Mahakama iamuru na kutamka hivyo wakidai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.

Pia, wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MWALIMU IKOMBA AMBWAGA LEAH ULAYA URAIS CWT

Mwalimu Suleiman Ikomba.
Mwalimu Suleiman Ikomba.

Hatimaye tambo na majigambo ya wagombea nafasi ya Rais Chama cha Walimu Tanzania (CWT) zimekwisha baada Mwalimu Suleiman Ikomba kutangazwa mshindi akimbwaga kwa mbali aliyekuwa Rais wa chama hicho Mwalimu Leah Ulaya.

Wawili hao walikuwa wamevuta hisia za Walimu na Watanzania kwa ujumla kutokana na nafasi walizokuwa wakizishirikia awali ya mmoja kuwa Rais na Mwingine makamu wa Rais.
 
Tambo za wagombea hao zilisikika mitaani na ndani ya Ukumbi wa Jakaya Kikwete ambao kwa siku tatu ulikuwa na Ulinzi mkali kila kona wa Jeshi la polisi pamoja na Suma JKT.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi huo Halima Liveta amemtangaza hayo alfajiri ya leo Suleiman Mathew Ikomba kuwa amepata kura 608 dhidi ya kura 260 alizozipata aliyekuwa Rais wa awamu iliyopita Leah Ulaya wakati kura moja ikiharibika.
 
Hata hivyo, amesema jumla ya wapiga kura walioripoti kwenye uchaguzi huo walikuwa 914 lakini waliopiga kura walikuwa 868.

Mwalimu Leah Ulaya.


MHE. RAIS DKT. SAMIA AKIPOKEA GAWIO NA MICHANGO KUTOKA KWA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Akishiriki Hafla ya Kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Tasisi na Mashirika ya Umma Ikulu Dar es salaam, leo tarehe 10 Juni, 2025.

Monday, June 9, 2025

YANGA BADO WAKO NA MSIMAMO WAO ULE ULE 'HATUCHEZI'


 Uongozi wa Yanga umesisitiza kuwa hautocheza mechi dhidi ya Simba, Juni 15, 2025 kama matakwa yake hayatofanyiwa kazi licha ya leo Juni 9, 2025 kufanya kikao na uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Utendaji ya Yanga leo, imesema kuwa msimamo wao hautobadilika kama wanayoyaomba hayatashughulikiwa.

“Uongozi wa Young Africans Sports Club, unapenda kuutarifu umma kuwa, tarehe 7 Juni, 2025 tulipokea barua kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kwa ajili ya kuhudhuria kikao maalum cha kujadili masuala yahusuyo mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC, YANGA dhidi ya Simba.


“Uongozi wa Klabu yetu ulitii wito huo na kushiriki kwenye kikao kilichofanyika leo, Jumatatu Juni 9, 2025 kwenye ofisi za Bodi ya Ligi Tanzania zilizopo jengo la NSSF Mafao House, Dar Es Salaam, kuanzia saa 4:00 asubuhi.

“Baada ya majadiliano ya saa kadhaa, Viongozi wa Klabu waliwasilisha msimamo wa Klabu yetu kuwa hatutashiriki mchezo namba 184 uliopangwa kufanyika tarehe 15 Juni 2025 mpaka pale matakwa yetu tuliyoyawasilisha kwa maandishi kwao yatakapotimizwa.

“Tunawatakia kila la heri Bodi ya Ligi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini katika kushughulikia matakwa yetu yenye mustakabali mkubwa

kwenye maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania,” imefafanua taarifa hiyo ya Yanga.

Akizungumza mara baada ya mkutano huo na TPLB uliofanyika katika makao makuu ya Bodi, Ilala, Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji amesema klabu yao imeshiriki kikao hicho kuwasilisha msimamo wa wanachama na mashabiki wao.


Akizungumzia juu ya kukubali

kucheza mechi dhidi ya Simba Arafat amesema Yanga haikuwahi kusema kama itacheza mechi hiyo.

"Tumemaliza mkutano na tulichofanya ni kuwasilisha msimamo wa klabu kutoka kwa wanachama na mashabiki wetu hilo ndio kubwa," amesema Arafat Mara baada ya kusema hayo, Arafat aliondoka eneo hilo sambamba na viongozi wenzake.

Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Karim Boimanda amesema taarifa kamili juu ya mkutano huo itatolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi Almas Kasongo.