 |
| Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) Bw. Duan Campbell (kati kati) akipeana mikono na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mh.Martine Shigela (wa tatu kutoka kulia) baada ya kukabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 50 kwa kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma kilichopo mkoani Geita mwishoni mwa wiki. Kituo hicho kimeanzishwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya GGML , Halmashauri ya Geita na Kanisa Katoliki . Wa pili kwa upande wa kulia ni Askofu Flavian Kasala wa Jimbo Katoliki la Geita. |
Na Mwandishi Wetu, GeitaKampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya uwajibikajo kwa jamii kwa kutoa msaada wa hundi ya shilingi milioni 50 kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Moyo wa Huruma wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya 2026 zilizofanyika kituoni hapo, mkoani Geita mwishoni mwa wiki.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mfano wa hundi hiyo kwa uongozi wa kituo hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Bw. Duan Campbell, amesema uwepo wa GGML katika moa wa Geita haujikiti tu katika uchimbaji wa dhahabu bali pia katika kuigusa jamii kwa kujenga jamii yenye afya, matumaini na fursa hasa kwa Watoto walioko katika mazingira magumu.
“Kujenga jamii yenye afya na yenye matumaini ni sehemu ya jukumu letu kama kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini. Uwekezaji wetu katika maendeleo ya kijamii unaendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa ndani, kikanda na kitaifa. Tunajivunia kushirikiana na Moyo wa Huruma na kuona jinsi maisha ya Watoto yanavyobadilika kwa misaada na fursa wanazopata.
“Tunajisikia fahari kuona watoto wanaolelewa katika kituo hiki wanapata mafanikio, ikiwemo wale wanaohitimu katika vyuo vikuu,”
“Hivyo, kama wadau wa maendeleo ya jamii, GGML tutaendelea kuhakikisha kuwa kituo hiki kinapata mafanikio zaidi na kushirikiana na Serikali katika kutokomeza watoto wa mitaani,” amesema Bw. Campbell.
Kituo cha Moyo wa Huruma kilianzishwa mwaka 2006 kupitia ushirikiano kati ya GGML, Jimbo Katoliki la Geita na Halmashauri za Serikali ya mkoa wa Geita, kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kukabiliana na changamoto za watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu—ikiwemo watoto waliopoteza wazazi kutokana na VVU/UKIMWI.
Kupitia mfuko wa GGML Kili Challenge Against HIV & AIDS, GGML imekuwa ikishirkiana na wadau mbalimbali ikiwemo Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kukusanya rasilimali kwa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kusaidia watu wanaoishi na VVU pamoja na taasisi zinazohudumia makundi yaliyo katika hatari, ikiwemo Kituo cha Moyo wa Huruma. Juhudi hizi zimewezesha kujengwa kwa kituo hicho ambacho kimeweza kukua kutoka kulea watoto 12 mwaka 2006 hadi kuwahudumia zaidi ya watoto 100 kwa sasa, wakiwemo wahitimu wa vyuo vikuu na watumishi wa umma.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mh. Martine Shigela ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, ameipongeza GGML kwa kuendelea kusaidia makundi mbalimbali katika jamii.
“Napenda kuwapongeza GGML kwa ibada hii ya kulea kituo hiki chenye watoto wakiwemo watoto wadogo na wakubwa ambao baadhi yao ni wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali wanaosomea masomo ya Sayansi na wale walioajiriwa Serikalini ambao wamepitia katika kituo hiki,” amesema RC Shigela
Akizungumza katika hafla hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Askofu Flavian Kasala amesisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kushirikiana katika kujiepusha na kuzuia vyanzo vinavyopelekea ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao hukosa msaada na hatimaye kutapakaa mitaani.
“Matatizo mbalimbali katika jamii ikiwemo changamoto zinazotokana na uzazi katika umri mdogo, maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na ugumu wa maisha yamepeleka uwepo wa watoto wa mitaani wenye uhitaji kutoka katika jamii”
“Hivyo, kituo kama hiki, kinatupa somo la kuwapa faraja watoto wenye uhitaji na kuweka jitihada za makusudi za kuzuia ongezeko la watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu,” amesema Askofu Kasala.
Akizungumza mara baada ya hafla ya kukabidhi hundi, Mwakilishi wa GGML kutoka idara mahusiano Mussa Shunashu ameeleza majukumu ya GGML katika kituo hicho kilichoanzishwa kwa ushirikiano kati ya GGML, Jimbo Katoliki la Geita na Halmashauri za Mkoa wa Geita.
“GGML katika kuanzisha na kuendeleza kituo hiki, ilikuwa na wajibu wa kutoa fedha na halmashauri wakati huo ilikuwa na wajibu wa kutoa eneo na Jimbo Katoliki la Geita lilikuwa na wajibu wa kusimamia malezi bora na tunashukuru mpaka leo hii kituo hiki kinaendelea kutoa huduma,”
“Kama ilivyo katika mikoa mingine, mkoa wa Geita pia una watoto yatima, ambao walipoteza wazazi/ walezi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa UKIMWI, hivyo, tuliamua kuwa na kituo hiki kwa msaada wa malezi na elimu kwa watoto wenye uhitaji,” amesema.
Katika hafla hiyo ya kuadhimisha Mwaka Mpya 2026, GGML pia ilitoa zawadi mbalimbali, kuandaa burudani, michezo na chakula kwa watoto na walezi wao, pamoja na mazungumzo ya faraja yaliyoimarisha dhana ya malezi ya pamoja na mshikamano wa kijamii.
Mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho (jina limehifadhiwa) amesema msaada unaotolewa na GGML na wadau wengine umewapa nguvu ya kuota ndoto kubwa.
“Tunajisikia kama tupo nyumbani. Tunathamini sana kuona kuna watu wanaojali maisha yetu na mustakabali wetu,” amesema mtoto huyo.
Hatua hii inaendelea kuonesha utekelezaji wa sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ya GGML, inayolenga kuimarisha afya, elimu na ustawi wa watoto na familia katika mkoa wa Geita na Tanzania kwa ujumla, kwa kutambua kuwa maendeleo endelevu huanza na uwekezaji kwa watu.