ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, August 15, 2023

MBUNGE KATOA MATREKTA BURE VIJANA LIMENI MJIKWAMUE KIUCHUMI - DAFFA

 






Katibu wa Mbunge jimbo la Ulanga mkoani Morogoro Thomas Daffa amewataka vijana wa wilaya hiyo kutumia vyema fursa ya kilimo aliyoitoa Mbunge wa jimbo hilo Mhe Salim Alaudin Hasham ili wainuke kiuchumi.


Daffa amesema ni wakati wa vijana sasa kutumia kilimo kama njia ya kubadilisha maisha yao kiuchumi kwani kwasasa kilimo kimekuwa ni Njia ya mafanikio katika maeneo mengi duniani.

Pia Daffa amesema kwa Fursa ambayo Mbunge wa jimbo hilo ameitoa kwa vijana kuwa atawalimia mashamba yao bure kwa kutumia trekta zake binafsi ni vyema sasa kwa vijana kuacha kukaa vijiweni na kupiga soga badala yake waingie shambani kwani Taifa linawategemea sana.

Siku za hivi karibuni Mbunge Salim Hasham alisema atatoa trekta zake kuwalimia vijana bure mashamba yao hivyo kila kijana anayetaka kulimishiwa basi afike kwenye ofisi yake ili aweze kupatiwa msaada huo kwa lengo la kuhakikisha vijana wanajiajiri na kupunguza tatizo la ajira wilayani humo.

Aidha Daffa amewasisitiza vijana kuacha kutumika kuvuruga amani ya nchi ambayo imetunzwa na waasisi wetu na badala yake ni muda wa kufanya vitu vyenye tija kwa jamii na Taifa letu kwa ujumla.

Daffa pia ameongoza harambee ya ujenzi wa ofisi ya  Chama cha Mapinduzi kata ya kichangani na kuweza kukusanya kiasi cha Mil 3,222,000/= ambayo itaanzisha ujenzi huo ili mpaka kufikia mwezi disemba basi kata hio iweze kupata ofisi ya chama.

Jimbo la Ulanga Lina jumla ya kata 21 na vijiji 159 hivyo chama cha Mapinduzi kinafanya hivyo kujiimarisha kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka  2024 na ule uchaguzi mkuu 2025.

AFYA CHECK KWA KUSHIRIKIANA NA OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA TANGA KUZINDUA KAMBI MAAALUMU YA MATIBABU BURE TANGA

 

 

MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari mapema leo
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Japhet Simeo akizungumza wakati wa mkutano huo

Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shiloo akizungumza


TAASISI ya  Afya Check kwa kushirikiana na ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga wanatarajia kuzindua kambi maalum ya kupima afya  bure kwa wananchi wa Jiji la Tanga  kwa siku tano ikiwa ni mpango wa kuihamasisha  jamii kuwa na desturi ya kupima afya zao mara kwa mara ili pale wanapogundulika kuwa na matatizo mbalimbali waweze kupata matibabu ya haraka.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Waziri wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amesema kambi hiyo itafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia Augost 21 ambapo wananchi 5000 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi katika magonjwa ya Kisukari,  shinikizo la damu, Saratani ya tezi dume,saratani ya mlango wa kizazi.
Waziri Ummy amesema magonjwa yatayopimwa ni yale yanayoambukiza na yasiyoambukizwa na endapo mtu atakutwa na ugonjwa atapatiwa tiba bure na kwa wale ambao watakuwa na magonjwa yatakayohitaji  upasuaji watapatiwa tiba watakapokuja madaktari bingwa huku akiipongeza banki ya CRDB ambao ndio wadhamini wakuu wa kambi hiyo. 

"Takwimu inaonesha wapo watu laki mbili ambao hawajajitambua afya zao katika upimaji wa vvu, tunawashauri na kuwahamasisha watu kupima na kama watu wote ambao wana maambukizi wangekuwa wanafuata masharti ya kumeza dawa tunaweza kuutokomeza kabisa" amesema.
"Niwapongeze sana sana wadau wetu wakubwa CRDB, benki yetu kwa kujitolea na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan,  katika kufadhili huduma zinazowasaidia wananchi" amebainisha.

"Sasa, nitoe wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tanga kujitokeza, wilaya zote kujitokeza kuja kupima katika viwanja vya shule ya sekondari ya Usagara, lengo ni watu 5000 lakini hata tukipata zaidi itakuwa vizuri" amesisitiza.

Awali akizungumza Mratibu mkuu wa Afya check Isack Maro amesema lengo la kuweka kambi mkoani hapa ni kutaka kuwajengea wananchi tabia ya kupima afya kwa hiyari mara kwa mara na hii ni mara baada ya kumaliza mkoani Dar es salaam ambapo zaidi ya wananchi 9324 walifanyiwa vipimo.

"Kitakwimu watanzania tunatumia gharama kubwa sana kujitibu na mara nyingi ni kwa sababu tumechelewa kugundua tatizo sasa kampeni hizi zilianzishwa kuhakikisha kwamba watanzania  wanajenga tabia ya kuoenda kupima afya zao mara kwa mara na hii inaonyesha kuyokana na matukio tunayoyaona  kutokana na hizi kambi ambazo tumezifanya kwa muda mrefu"

"Kwa  sasa hivi ndio tumetoka kumaliza vipimo kwa wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na wilaya zake zote na tukafanikiwa kuwapatia huduma za afya za bure wananchi takriban 9324 walifanikiwa kupatiwa  huduma zote za kibingwa pamoja na hufuma za kawaida  bila kusahau wakapatiwa dawa na vipimo"

Monday, August 14, 2023

MBUNGE UMMY MWALIMU AFANYA ZIARA KATA YA DUGA JIJINI TANGA

 






*Atembelea Kituo Cha Afya Duga 
*Afungua Shina la Wakereketwa 
•Afungua Ofisi ya CCM  kata CCM ya duga .
     
Mbunge wa Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu leo tarehe 12/8/2023 amefanya ziara kata ya Duga. Katika ziara hii mbunge ametembelea kituo Cha Afya duga kukagua utoaji wa huduma ambapo amepongeza watumishi kwa kutokuwa na kifo hata kimoja cha mama mjamzito na watoto wachanga. Mhe Ummy amesema kuwa Rais Samia atatoa gari ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Duga. 

Aidha Mh Ummy amemtaka Mganga Mkuu wa Jiji  kusimamia kwa karibu upatikanaji wa Dawa katika Kituo hicho. Mhe Ummy pia ameutaka Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kufanya ukarabati wa paa la Kituo hicho ili kuepusha madhara kwa wananchi. 
  
Pia Mhe Mbunge  alifungua shina la vijana wa CCM lililopo mtaa wa Magomeni Kirare na  kutoa shilingi milioni 1 kuwaunga mkono vijana hawa na kuahidi kuwatengenezea  turubai moja (tent) .

Pia Mhe Ummy amefungua Ofisi ya CCM kata ya Duga na   kusema ataendelea kujitolea kwa ajili ya Chama. Awali Mhe mbunge amenunua meza 3 na viti 7 kwa ajili ya ofisi hiyo.

Mwisho mbunge Ummy alitembelea makazi ya wazee duga ambayo ni kawaida yake kila mara kuenda eneo hilo au kutuma wasaidizi  wake kuwaona wazee hao na kuwapatia vyakula.

Katika ziara hiyo, Mhe mbunge aliambatana na viongozi wa chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tanga wakiongozwa na Mwenyekiti Meja  mstaafu Hamisi Bakari Mkoba, Mkuu wa wilaya ya Tanga, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe Shillow na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Simon
 
Imetolewa na :
Ofisi ya Mbunge Jimbo la Tanga Mjini

12/8/2023

RAIS MWINYI AIPONGEZA BENKI YA CRDB KWA KUIMARISHA AFYA NCHINI.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi ameiopongeza Benki ya CRDB kwa juhudi inazozionyesha kuboresha afya nchini na kuzitaka kampuni nyingine binafsi kujitoa ili kuongeza nguvu kwani mahitaji ni makubwa.

Rais Mwinyi ametoa pongezi hizo kwenye kilele cha CRDB Bank Marathon kilichofanyika leo Agosti 13 katika viwanja vya The Green vilivyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam na kuwashuhudia washindi wakiondoka na mamilioni ya zawadi baada ya kuonyesha kasi kubwa kuliko wakimbiza upepo wengine zaidi ya 7,000 waliojitokeza na kushiriki.
Akieleza mchango wa CRDB Bank Marathon kwenye sekta ya afya, Rais Mwinyi amesema ni mkubwa na unagusa pande zote za muungano kwa kuwawezesha wasio na uwezo wa kugharimi amatibabu yao pamoja na kuimarisha miundombinu.

“Fedha zinazokusanywa kutoka kwa washiriki wa mbio hizi za hisani zinaelekezwa kwenye matibabu ya Watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na wanawake wenye ujauzito hatarishi. Mwaka huu fedha hizi zitajenga kituo cha afya kule Zanzibar, huu ni mchango mkubwa unaowagusa Watanzania wengi. Nawaomba wadau wengine nao waone namna wanavyoweza kushirikiana na serikali kuboresha huduma za afya,” amesema Rais Mwinyi.
Hata kuratibu mbio hizi zilizokusanya shilingi bilioni moja zitakazoelekezwa kwa walengwa waliokusudiwa mwaka huu, Rais Mwinyi amesema kulihitaji ushiriki wa watu wenye nia moja na akaipongeza kampuni ya Sanlam Insurance ambayo ndio mdhamini mkuu wa mwaka huu.

“Benki ya CRDB inashirikiana na washirika wake kufanikisha mbio hizi. Niwapongeze kampuni ya Sanlam ambao niliwaona ikulu kule Migombani Zanzibar. Homgereni Sanlam kwa kuwa sehemu ya mchango huu mkubwa kwa jamii,” amepongeza Rais.
Akieleza namna mbio za CRDB Bank Marathon zinavyoigusa jamii, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kwa misimu mitatu iliyotanguliwa, fedha zilizokusanywa kutokana na usajili wa washiriki na zile zilizochangwa na washirika, zimewagusa watu wengi.

“Mwaka 2020 wakati tunaanza, zaidi ya watu 4,000 walishiriki na kufanikisha kukusanya shilingi milioni 200 zilizofanikisha upasuaji wa moyo kwa watoto 100 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), pamoja na programu ya utunzaji mazingira ya pendezesha Tanzania,” alsema. 
Aliongeza kuwa mwaka 2021 kulikuwa na washiriki 5,000 na jumla ya shilingi milioni 350 zilikusanywa ambazo zilitumika katika upasuaji wa moyo kwa watoto wengine 100 na kujenga Kituo cha Mawasiliano Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Alifafanua kuwa mwaka jana, jumla ya shilingi milioni 470 zilikusanywa kutoka kwa washiriki 6,000 ambazo zilitumika katika gharama za matibabu ya  wagonjwa watoto 100 JKCI na wanawake wenye ujauzito hatarishi na walio na maradhi ya fistula katika Hospitali ya CCBRT. 
Kutokana na mafanikio hayo, Nsekela amesema msimu huu wa nne wa CRDB Bank Marathon una malengo makuu manne ambayo ni kujenga kituo cha afya ya mama na mtoto visiwani Zanzibar, kuchangia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, kuchangia matibabu ya wanawake wenye ujauzito hatarishi na wanaougua fistula pamoja na kuendelea programu ya pendezesha Tanzania kwa kuimarisha bustani za Zanzibar ikiwamo Bustani ya Jamhuri, Bustani ya Migombani-Botanic Garden, Bustani ya Tenga-Mnazi Mmoja, Bustani ya Mbele ya Ikulu Migombani pamoja na Njia Nne za Michenzani.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Martin Warioba alisema mafanikio ya mbio wanazoziratibu waliyoyapata ndani ya miaka mitatu iliyopita yamevuka mipaka kwani katika mwaka wa pili tu zilitambulika kimataifa na Chama cha Usajili na Upimaji wa Mbio za Kimataifa (AIMS) na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Riadha (World Athletics).

“Hii si tu imekuwa ni heshima kwa Benki yetu lakini pia ni heshima kwa nchi yetu. Kwa utambulisho huu wa kimataifa, mbio za CRDB Bank Marathon zinavutia wakimbiaji kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni hivvo kuzifanya kuwa sehemu ya kutangaza utalii wa nchi yetu,” alisema Warioba.
Warioba alisema kuwa mafanikio ya mbio za mwaka huu yamechangiwa na wadau kadhaa wanaoshirikiana na Benki ya CRDB ambao ni kampuni ya Sanlam Insurance, Alliance Life Insurance, Clouds Media Group Jubilee Allianz & Life Insurance, Heritage Insurance, Britam Insurance, Strategis Insurance, A1 Outdoor, Gardaworld, Mwananchi Communications, IPP Media, Sahara Media, Softnet, BEVCO, Hyatt Regency, na Spik & Span.

Afrika Mashariki wagawana zawadi
Zawadi zenye thamani ya zaidi ya shilingi 100 zilizotolewa kwa washindi wote walioshiriki kilomita 42, kilomita 21, kilomita 10 na kilomita tano pamoja na kilomita 65 kwa waendesha baiskeli zilikwenda kwa wawakilishi kutoka karibu mataifa yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kwenye kilomita 42 (full marathon), Jakline Juma wa Tanzania na Moses Menginch wa Kenya waliongoza makundi yao hivyo kuondoka shilingi milioni 10 walizoshinda huku nafasi ya pili ikienda kwa Paskalia Chipkorir wa Kenya na Jonathan Akankwasa walizawadiwa shilingi milioni 5 na Nancy Cheptegei wa Uganda na Rashid Muna wakiondoka na shilingi milioni 2, baada ya kushika nafasi ya tatu.

Kwenye mbio za kilomita 21 (nusu marathon), Watanzania waling’ara katika makundi yote mawili, yaani wanawake na wanaume baada ya Magdalena Crispin na Josephat Joshua kuongoza. Nafasi ya pili ilikwenda kwa Atalena Napule Gasper wa Sudan na Nangat Willy wa Kenya huku nafasi ya tatu ikikamatwa na Failuna Matanga wa Tanzania na Panuel Mkingo wa Kenya.

Ceclia Panga, Transfora Musa na Neema Kisuda waliwaongoza wanawake kukimbia kilomita 10 huku Shuemery Mohamed, Josephat Tiophil na Jonas John wakifanya hivyo kwa wanaume. John Msigwa, Danidi Kisoni na Justine Mbegu walikuwa moto wa kuotea mbali kwa wavulana waliokimbia kilomita tano.




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi akimvalisha medali ya kushiriki mbio za hisani za CRDB Bank Marathon Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.  Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Alliance Life Assurance, Byford Mutimusakwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Neema Mori. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Martin Warioba, Waziri wa Habari, Vijana na Michezo Zanzibar, Tabia Mwita, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt Pindi Hazara Chana na Mke wa Rais Mwinyi, Mama Mariam  Mwinyi.