ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, December 24, 2021

JELA MIAKA 30 KWA KUMBAKA BINTI WA MIAKA 12

 


Mahakama ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro imemuhukumu kwenda jela miaka 30, Elitumain John Elitumain miaka 31 mkazi wa kitongoji cha Majengo Kata ya Hedaru Wilayani hapa Kwa kosa la kumbaka binti wa miaka 12.


Akitoa hukumu hiyo leo Desemba 24, hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Mussa Hamza amesema mtuhumiwa alifikishwa mahakamani hapo akiwa na kesi ya kumbaka binti huyo ambaye alikuwa mfanyakazi wa ndani nyumbani kwake.


Hakimu Hamza amesema kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na Jamuhuri wakiongozwa na waendesha mashtaka wa Serikali, Frank Masese na Samweli Flavian wamethibisha pasipo shaka kuwa kosa hilo lilitendeka Oktoba 27, 2021 huko nyumbani kwa mshtakiwa.


Mshtakiwa ametiwa hatiani kwa kosa hilo kwa mujibu wa kifungu cha sheria 130 (2) (e) na 131(1) vyote vikiwa ni kanuni ya adhabu mapitio ya mwaka 2019 shauri la jinai 132/2021.

TANZANIA YAWEKEWA MASHARTI YA KUPIMA UVIKO - 19

 


Nchi nne zimeiwekea masharti Tanzania ambapo kuanzia sasa wasafari wanaoelekea nchi hizo watatakiwa kupima ugonjwa wa Uviko-19 saa sita kabla hawajapanda kwenye ndege.


Hii pia itawahusu wasafiri kutoka nchi mbalimbali wanaokuja kuunganisha ndege Tanzania.


Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alipozungumza na waandishi wa habari Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).


Profesa Makubi alizitaja nchi hizo kuwa ni Marekanai, India, Dubai na baadhi ya nchi za Ulaya, kwamba hatua hiyo ni mbali na kutakiwa kuwa na cheti cha kupima Covid 19.


"Katika masharti haya hata kama tayari una cheti ulichopimwa covid, utapaswa ukifika hapa upime tena saa sita kabla hujasafiri.


" Hivyo nawasihi wananchi ukitaka kusafiri kwenda nchi hizo muhakikishe mnawahi hapa uwanja wa ndege saa saba kabla ili mchukuliwe kipimo hicho ili  kuepuka usumbufu ikiwamo kukatazwa kusafiri "amesema  Profesa Makubi.


Amesema masharti haya yanakuja baada ya kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya ugonjwa huo ambapo mpaka kufika Desemba 23 mwaka huu watu milioni 276.4 duniani wanaugua ugonjwa huo huku milioni 5.3 wamefariki.


Kufuatia maagizo hayo Katibu huyo aliwataka wananchi kukubali kuwa ugonjwa huo bado upo na kuwasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari za kuepuka ugonjwa huo kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono na maji tiririka, kuchanja na kufanya mazoezi.


" Mbali na tahadhari hizo pia nawakumbusha wananchi kuepuka kutumia vyeti feki ya kuonyesha wamepima Covid kumbe sio kweli kwa kuwa hatua kali dhidi yao zitachukuliwa,"alitahadharisha Profesa Makubi.


Wakati kukiwa tetesi za Wabunge wa nchi za Kenya na Uganda wanaosadikiwa kupata Uviko-19 covid baada ya kumalizika kwa mashindano ya mabunge ya nchi za Africa Mashariki nchini, amesema  wanafuatilia kujua ukweli.

SERIKALI YAPOKEA DOZI 376,320 ZA MODERNA

 Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Dorothy Gwajima, akiongea na Waandishi wa Habari katika Uwanja wa Ndege wa Mwl. Julius Nyerere wakati wa mapokezi ya Chanjo ya Modena

 Uongozi wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania ambao ni wadau wakubwa wa mapambano dhidi ya Uviko 19, ukiwa, umeambatana na Waziri wa Afya wakati wa mapokezi ya Chanjo ya Modena

Na WAMJW-DSM


Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea Dozi 376,320 za Moderna ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha ikiwakinga Wananchi wake dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Hafla fupi ya mapokezi  imefanyika 24 Disemba 2021 na kuongozwa na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam  na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Ubalozi na Taasisi zisizo za kiserikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt.  Gwajima amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imelenga kuwakinga jumla ya Watanzania 249,795 kutokana na kupokea Chanjo dozi 376,320 za Moderna zilizoingia kupitia mpango wa COVAX Facility zitakinga watanzania 188,160 ikiwa ni awamu ya kwanza kupokea aina ya Chanjo za Moderna.

"Mapokezi ya chanjo hizi za leo yanafanya jumla ya chanjo tulizopokea hapa nchini tangu tuanze kutoa chanjo za chanjo dhidi ya UVIKO 19 hadi sasa zimefikia dozi 6,408,950 zikijumuisha (Sinopharm, Janssen, Pfizer), na leo Moderna ambazo zinatosha kuchanja jumla ya watanzania 3,204,475
hivyo niwaombe wanaohusika na zoezi hilo kuwajibika kwa kasi kubwa ili kuwawezesha watanzania wengi kupata chanjo mapema iwezekanavyo amesema Mhe.Dkt Gwajima.

Aidha,Mhe.Dkt.Gwajima amesema kuwa Wizara imetoa Mwongozo wa Chanjo unaofafanua vyema taratibu za utoaji wa chanjo hizi wenye lengo la kufikia uchanjaji wa asilimia 60 ya watanzania ili kudhibiti ugonjwa wa uviko 19.


Wednesday, December 22, 2021

Narco Yapunguza Bei Ya Kondoo, Mbuzi Kuelekea Krismasi

 


KATIKA kuelekea Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya, Serikali imetangaza punguzo la asilimia 33 ya bei ya mbuzi na kondoo waliopo katika Ranchi za Taifa (NARCO) katika msimu huu wa sikukuu ili kuhamasisha wananchi kula nyama na kuongeza wigo wa soko la ndani.


Akitangaza punguzo hilo, Ofisa Masoko wa Narco, Emmanuel Mnzava alisema Serikali imeamua kutoa ofa ya Krismasi na mwaka mpya kwa wananchi wake ambapo mbuzi 3,000 na kondoo 1,000 watauzwa kwa bei ya punguzo.


Alisema bei hiyo itakuwa katika ranchi za Kongwa (Dodoma), Ruvu (Pwani), Mkata (Morogoro), West Kilimanjaro (Kilimanjaro) na Missenyi (Kagera).


Alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kutoa ‘ofa’ ya Krismasi na mwaka mpya kwa wananchi wake ambapo ofa hiyo inalenga kuhamasisha ulaji wa nyama ya mbuzi na kondoo hapa nchini na kuongeza soko la bidhaa hiyo ndani ya nchi.


Aliongeza: “Awali mbuzi mmoja katika ranchi hizi alikuwa anauzwa hadi Sh 150, 000 lakini kutokana na punguzo hili sasa watauzwa kwa Sh 120,000 hadi 100,000, kwa mbuzi na kondoo ambaye akichinjwa anatoa kilo 15 hadi 20.”


Ofisa masoko huyo alitaja lengo lingine la kupunguza bei ni kuhamasisha jamii ya Watanzania katika ufugaji wa kisasa na kibiashara wa mbuzi na kondoo ili kukidhi mahitaji ya soko la kigeni pamoja na machinjio na viwanda vya nyama vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa nchini.


Alisema takwimu zinaonesha kuwa ulaji wa nyama ya mbuzi na kondoo hapa nchini bado uko chini ikilinganishwa na ulaji wa nyama ya ng’ombe ambao unaongezeka kila mwaka.


Alisema mahitaji ya nyama ya mbuzi na kondoo katika soko la nje ya nchi na machinjio na viwanda vya nyama vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa nchini yanaongezeka, hivyo kutoa fursa la soko la bidhaa hiyo kwa wafugaji.


Kwa upande wake, Mkazi wa Chamwino, Ramadhani Kiza alisema ulaji wa nyama ya mbuzi unakuwa chini kutokana na upatikanaji wake kwa kuwa ni adimu na gharama yake ni kubwa, hivyo watu wengi kushindwa kumudu.


Alisema ni vyema serikali ikaingilia kati suala hili kwa kuwahamasisha wafugaji kufuga mbuzi kisasa na kibiashara ili kufanya nyama ya mbuzi iwe inapatikana kila mahali kama ilivyo bidhaa nyingine.


“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutushushia bei ya mbuzi na kondoo lakini tunaomba ofa hii isiwe kwa muda mfupi iwe endelevu


ili kila mwananchi awe na uwezo wa kununua na kufurahi na familia yake hasa kipindi hiki ambacho watu wengi wanasherehekea mwaka mpya na Krismasi,” alisema.


Mfanyabiashara wa Soko la Bonanza, Maria Issa aliipongeza serikali kwa kuleta punguzo la bei kwa wakati ambao unahitajika sana na watu.


Alisema sherehe za mwaka mpya na Krismasi wananchi hununua nyama ya ng’ombe na mbuzi kwa ajili ya kusherehekea na ndugu na jamaa zao.

Sunday, December 19, 2021