Nchi nne zimeiwekea masharti Tanzania ambapo kuanzia sasa wasafari wanaoelekea nchi hizo watatakiwa kupima ugonjwa wa Uviko-19 saa sita kabla hawajapanda kwenye ndege.
Hii pia itawahusu wasafiri kutoka nchi mbalimbali wanaokuja kuunganisha ndege Tanzania.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alipozungumza na waandishi wa habari Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Profesa Makubi alizitaja nchi hizo kuwa ni Marekanai, India, Dubai na baadhi ya nchi za Ulaya, kwamba hatua hiyo ni mbali na kutakiwa kuwa na cheti cha kupima Covid 19.
"Katika masharti haya hata kama tayari una cheti ulichopimwa covid, utapaswa ukifika hapa upime tena saa sita kabla hujasafiri.
" Hivyo nawasihi wananchi ukitaka kusafiri kwenda nchi hizo muhakikishe mnawahi hapa uwanja wa ndege saa saba kabla ili mchukuliwe kipimo hicho ili kuepuka usumbufu ikiwamo kukatazwa kusafiri "amesema Profesa Makubi.
Amesema masharti haya yanakuja baada ya kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya ugonjwa huo ambapo mpaka kufika Desemba 23 mwaka huu watu milioni 276.4 duniani wanaugua ugonjwa huo huku milioni 5.3 wamefariki.
Kufuatia maagizo hayo Katibu huyo aliwataka wananchi kukubali kuwa ugonjwa huo bado upo na kuwasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari za kuepuka ugonjwa huo kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono na maji tiririka, kuchanja na kufanya mazoezi.
" Mbali na tahadhari hizo pia nawakumbusha wananchi kuepuka kutumia vyeti feki ya kuonyesha wamepima Covid kumbe sio kweli kwa kuwa hatua kali dhidi yao zitachukuliwa,"alitahadharisha Profesa Makubi.
Wakati kukiwa tetesi za Wabunge wa nchi za Kenya na Uganda wanaosadikiwa kupata Uviko-19 covid baada ya kumalizika kwa mashindano ya mabunge ya nchi za Africa Mashariki nchini, amesema wanafuatilia kujua ukweli.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.