ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, March 21, 2025

SAMIA MGENI RASMI UAPISHO RAIS MTEULE NAMIBIA.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia Suluhu Hassan, atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za uapisho wa Rais mteule wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, zitakazofanyika leo Machi 21,2025.

Rais Samia Suluhu Hassan, atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za uapisho wa Rais mteule wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, zitakazofanyika leo Machi 21,2025.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Mei 20,2025 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais. Samia atahutubia kwenye sherehe hizo za uapisho zitakazofanyika sambamba na Maadhimisho ya Miaka 35 ya Uhuru wa Namibia.

Aidha, taarifa hiyo imefafanua kuwa mahusiano baina ya Tanzania na Namibia ni ya kidugu na kihistoria ambayo yaliasisiwa na Hayati Julius Nyerere na Hayati Sam Nujoma kipindi cha harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa bara la Afrika.


“Mahusiano haya yameendelea kukuzwa na kulelewa na Viongozi wote wakuu waliowafuatia katika nyanja mbali mbali,”imefafanua taarifa hiyo.


Kadhalika, mbali na kuhudhuria sherehe hizo Rais Samia atapata fursa ya kusalimiana na mwenyeji wake na kufanya mazungumzo ya kukuza na kuimarisha mahusiano.

“Kwa mara ya kwanza Namibia itapata Rais Mwanamke hivyo kufanya idadi ya Marais Wanawake barani Afrika kuwa wawili akiwemo Rais Samia,”imefafanua.

MRADI MKUBWA WA MAJI KATA YA PANGANI KUANZA RASMI UTEKELEZAJI APRIL 15 MWAKA 2025

 


VICTOR MASANGU, KIBAHA

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Pangani ilyopo katika Halmashauri ya mji Kibaha mkoani Pwani wanatarajiwa kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama baada ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutenga kiasi cha shilingi bilioni 8.9 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji ambao utakwenda kuwa ni  mkombozi mkubwa kwa wananchi hao na maeneo mengine ya jirani.



Hayo yamebainishwa na Meneja wa Dawasa Wilaya ya Kibaha  Halfa Ambokile wakati  wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Panagni ambao umendaliwa na Jumuiya ya umoja wa wanawake Wilaya ya Kibaha mji kwa lengo la kuweza kuzungumza na wananchi ikiwa pamoja na kusikiliza kero na chanagmoto zinazowakabili kwa ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi ikiwemo suala la huduma ya maji katika eneo hilo.

Meneja huyo amesema kwamba  kwa sasa wameshaanza maandalizi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo mkubwa ambao umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.9 amabzo zimetolewa na serikali na kwamba wanatarajia kuanza rasmi zoezi zima la utekelezaji ifikapo Aprili 15 mwaka huu na kwamba mradi huo utaweza kusambaza maji katika mitaa ipatayo sita pamoja na maeneo mengine ya jirani.

"Kwa sasa tumeshaanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa ambapo tunatarajiwa kujenga tanki kubwa lenye ujazo wa  milioni 6 amabapo mradi huo utekelezaji wake utatumia muda wa miezi nane hadi 12 kumalizika na baada ya hapo wananchi wataanza rasmi kupata huduma ya maji safi na salama katika mitaa saba ya kata ya Pangani ambayo iliyokuwa  badio haina huduma ya maji,"amesema Meneja huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amesema kwamba juhudi kubwa zimefanywa na Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassa kwa kuweza  kutenga fedha mbali mbali ambazo zimekwenda kutekeleza miradi ya maendeleo katika kata ya pangani ikiwemo, afya, elimu, miundombinu na barabara pamoja na mradi mkubwa wa maji ambao utaweza kutatua kero na changamoto za wananchi hao.


Aidha Mgonja amemshukuru kwa dhati Mbunge  wa  Jimbo  la Kibaha  mjini Mhe: Silvestry Koka kwa kuweza kuwapambania wananchi wa kata hiyo katika suala la kuwaletea maendeleo katika nyanja mbali mbali ikiwa sambamba na kuweza  kusikiliza changamoto mbali mbali za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi .  

Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Pangani Jitihada Hussen amempongeza Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutenga kiasi cha shilingi bilioni 8.9 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji ambao utakwenda kuondoa kabisa changamoto ambazo zilikuwa zinawakabili wananchi  kwa kipindi kirefu.

"Kwa kweli mimi kama mwenyekiti nampongeza kwa dhati  Rais wetu kwa juhudi zake za kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo suala zima la kutuangalia wananchi wa Pangani kwa jicho la tatu kwa kutenga fedha hizo  kiasi cha shilingi bilioni 8.9 kwa ajili ya kutekeleza miradi mkiubwa ya maji ikiwa sambamba na Mbunge wetu wa Jimbo la Kibaha mjini kwa kusikiliza kero za wananchi,"alisema Mwenyekiti huyo.


Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Pangani hawakusita kumpongeza kwa dhati Mbunge wao wa Jimbo la Kibaha mjini kwa kuweza kuwa mstari mbele katika katika kuhakikisha anatekeleza ilani ya chama kwa vitendo ikiwa sambamba na kulivalia njuga suala la kuwepo kwa mradi mkubwa wa maji ambao utaweza kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kata ya Pangani na maeneo ya jirani.
Kukamilika kwa mradi wa Pangani uliopo  katika Halmashauri ya Mji Kibaha, Mkoa wa Pwani unatarajiwa kuanza utekeezaji wake rasmi  kuanzia Aprili 15 mwaka huu  ambao utaweza kuondoa kero na chanagmoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa baadhi ya  wananchi  ambao walikuwa wanakosa huduma hiyo kwa kipindi kirefu.

TANGA UWASA WAELEZA MBINU ZA KUKABILIANA NA MAJI YANAYOPOTEA

 






Na Oscar Assenga, TANGA.

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ( Tanga Uwasa) imebuni mbinu mpya za kukabiliana na maji yanayopotea kila siku ambao utakuwa chachu ya kuwarahisishia kupata taarifa kwa wakati na kufikia kwa haraka kuitatua .

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Mamlaka hiyo Mhandisi Salum Hamis wakati wa kikao cha wadau wiki ya Maji 2025 kilichofanyika leo Jijini Tanga .

Katika kikao hicho mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo hali ya huduma,mapitio ya mkataba wa huduma kwa wateja na udhibiti wa maji yanayopotea.

Ambapo katika kukabiliana nalo wameandaa mfumo huo ambao utakuwa ukitumika kwa wale wenye simu janga utawasaidia popote wanatapokuwa wakiingia kwenye mfumo wanapiga picha eneo lenye mvujo na kuingia kwenye mfumo na kuandika mvujo.

Alisema baada ya kuandika kupitia mfumo huo utaonekana ukiwa umeripotiwa muda gani na kama umechelewa kufanyiwa kazi itaonekana na kuwarahisishia wao kama wanataka kutoa adhabu kwa watendaji wazembe kuwachukulia hatua watajua kutokana na mfumo kuwaonyesha.

“Mpaka sasa kuna kiasi kikubwa cha maji yanayopotea na tuna zaidi ya asilimia 30 ya maji wanayozalisha kwa mwezi yanapotea hii maana yake ni pesa maana hayo maji tunakuwa tayari tumeyagharamia kwa upande wa kuyawekea dawa na umeme”Alisema

“Kwetu hili ni hasara kubwa sana na ndio maana wanathamini Taarifa za mivujo ya maji tukifanikiwa wa kupunguza maji yanayopotea hata kwetu gharama za uendeshaji zitapungua kwa kiasi kikubwa”Alisema Mhandisi Hamisi.

Katika hilo tumejipanga pia kuongeza vitendea kazi kwa watumishi ikiwemo kugawa pikipiki kuwasambaza zaidi kuhakikisha kila eneo kunakuwa na watu wao ikiwemo magari au pikipiki na bajaji ili kuhakikisha wanakabiliana na upotevu huo kwa hali na mali

“Lakini niwaambie kwamba mfumo huo utawasaidia wadau, wananchi kuweza kuripoti taarifa zao za mivujo na hivyo kuwa rahisi kuweza kufanyiwa kazi na mtu aliyekabidhiwa eneo lake la utendaji kazi na namna anavyo hudumia wateja na kama hawajibiki mfumo utawaonyesha na kuona namna ya kumchukulia hatua”Alisema

Awali akizungumza wakati akifungua kikao hicho Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Victor Mollel amewataka wadau kuendelea kuwapatia taarifa za changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo kwa sababu zinawasaidia katika kuboresha taarifa zao za utendaji wa kazi.

Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ya maji ni uhifadhi uoto asili kwa uhakika wa maji wao wanajua chanzo cha maji cha Jiji la Tanga yanatoka Amani Muheza kwenye Mto Zigi hivyo kuna jitihada mbalimbali yanaendelea kwa ajili ya uhifadhi wa Mazingira.

Naye kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa Wateja Daudi Mkumbo alisema katika mkataba au rasimu ya mkataba mpya ya huduma kwa mteja Tanga Uwasa inaowajibu wa kutowakatia wateja huduma ya maji kwa siku za mapumziko kama Jumamosi, Jumapili na Ijumaa kuaza saa sita mchana

Mkumbo ambaye pia ni Meneja wa Huduma kwa Wateja alisema hiyo inatokana na kwamba katika wakati huo wakazi wa Tanga wengi wapo kwenye ibada hiyo itawawia vigumu katika kushughulia kurudisha maji, siku za mapumziko wahudumu wakiwemo mafundi kuwa kwenye mapumziko.

Thursday, March 20, 2025

TANRODS PWANI YAANIKA UKWELI MPUTU SAKATA LA BINTI DEREVA ALIYEKAMATWA MIZANI YA VIGWAZA

 NA VICTOR MASANGU,VIGWAZA PWANI..TV..TANRODS 


WAKALA wa barabara nchini (TANROAD) Mkoa wa Pwani umewataka baadhi ya   madereva wa vyombo vya moto hasa magari makubwa  kufuata sheria na  utaratibu  uliowekwa katika changamoto zao zinazowakabili kuliko kutoa  taarifa ambazo sio sahihi kwa  kutumia mitandao ya kijamii na kuzua taaruki na sintofahau kwa jamii. 

Uongozi wa Tanroad Mkoa wa Pwani  umetoa kauli hiyo kufuatia  malalamiko yaliyotolewa  na mmoja wa  dereva kutoka  Kampuni ya Simba logistic  Pamela James ambaye alidai  kubambikiwa uzito katika mizani ya vigwaza mkoani Pwani tarehe 13 Machi wakati akiwa amebeba  mzigo wa kopa akitokea  nchini  Kongo.

INSERT 1
.TV PAMELA LUKUMBI 
Dereva wa Malori Makubwa aliyekamatwa.
 
Kwa upande wake Meneja wa Tanrod Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage kwa niaba ya mtendaji mkuu wa Tanrods Tanzania  hakusita kuweka banaya  changamoto kubwa iliyopelekea gari hiyo kuzuiliwa katika mizani ya  Vigwaza.

INSERT..2 TV Mhandisi BARAKA MWAMBANGE
Meneja wa TANROAD Mkoa wa  Pwani.

VICENT TARIMO ni mkuu wa kitengo kinachosimamia masuala ya mizani kutoka Tanrod Makao makuu hapa anaweka wazi makosa yaliyopelekea gari hilo kukamatwa.

INSERT..3 TV VICENT TARMO Tanrod makao makuu 
 kitengo cha usimamizi wa mizani.

Hivi karibuni kumekuwepo na baadhi ya madereva kukwepa Sheria ya udhibiti   wa magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayomtaka msafirishaji mwenye gari inayoanzia tani tatu na nusu kupitia katika vituo vya mizani kwa ajili ya kuhakikisha uzito wa magari yao.

Wednesday, March 19, 2025

TUJIEPUSHE KUIGA TABIA ZA KIGENI ZISIZOKUWA NA MAADILI KWA TAIFA-MAJALIWA


▪️Amsifu Askofu Kilaini asema ni kielelezo cha ujasiri, imani thabiti na kujitoa kwa jamii

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema jamii inahitaji kufundishwa, kutambua na kuenzi mila za Kitanzania, pamoja na kujiepusha na vishawishi vya kuiga tabia za kigeni ambazo hazina manufaa kwa ustawi wa Taifa.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Machi 19, 2025) katika Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Msaidizi Mstaafu wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Bukoba Askofu Method Kilaini.


“Sote tumekua tukishuhudia ongezeko la vitendo vya ukosefu wa maadili katika jamii. Vitendo hivi vinatokana na malezi hafifu lakini pia watu kuiga mila na desturi kutoka mataifa mengine ambazo haziendani na tamaduni na maadili yetu ya Kitanzania.”


Waziri Mkuu amesema hali hiyo imeathiri mwenendo wa jamii, hususan kwa vijana ambapo wanashuhudia mabadiliko katika misingi ya familia, jamii, na Taifa kwa ujumla. “Nitumie fursa hii kuliomba Kanisa kuendelea kuwa nguzo ya maadili bora, kwa kutoa mwongozo wa kiroho na kijamii.”


Amesema Kanisa lina nafasi ya pekee katika kuhakikisha Taifa linarudisha maadili ya kweli ya Kitanzania yanayofundisha kuheshimu utu, haki, na amani. “Serikali, tunatambua mchango mkubwa wa Kanisa katika hili na tutashirikiana nalo ili kuleta mabadiliko chanya kwa kizazi cha sasa na kijacho.”


Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa madhebu ya dini ikiwemo Kanisa Katoliki katika kuboresha ustawi wa jamii.amii yetu., hivyo amewaomba viongozi wa dini nchini waendelee kuwa nguzo ya maadili bora, kwa kutoa mwongozo wa kiroho na kijamii.


Akizungumza kuhusu Askofu Kilaini, Mheshimiwa Majaliwa amesema ni kielelezo cha ujasiri, imani thabiti, na huduma ya kujitolea kwa Kanisa na jamii ya Watanzania, ameonesha nguvu ya uvumilivu, akiwa na michango mikubwa katika maisha ya kanisa.


Amesema pamoja na changamoto nyingi alizokutana nazo, hakukata tamaa, bali aliendelea kuwa mwanga kwa wengi. “Ninatambua kuwa katika kipindi cha uongozi wake, alifanya kazi muhimu katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akiwa Katibu Mkuu kwa miaka tisa na nusu, akisaidia kuimarisha huduma za jamii na kuendeleza taasisi mbalimbali za Kanisa, ikiwemo hospitali ya Bugando na Chuo Kikuu cha Nyegezi.”


“Kama Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alijizatiti katika kuimarisha utawala wa fedha za Kanisa na kusaidia kuanzisha Radio Tumaini, hatua muhimu katika mawasiliano ya kiroho. Kwa ushirikiano wake na viongozi wa Kanisa, alisaidia pia kuanzisha Television ya Tumaini, akionesha uongozi wa kimapokeo na kisasa.”


Akimzungumzia Askofu Msaidizi Mstaafu. Method Kilaini Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa amesema Askofu huyo ni hazina kubwa ya mkoa wa Kagera kwani licha ya kutoa huduma za kiroho mara nyingi amekuwa akishiriki katika matukio mabalimbali yanayofanywa na Serikali. "Amekuwa mshauri mzuri katika masula mbalimbali hasa yanayohusu amani na maendeleo ya Taifa letu.”

Naye, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu Angelo Accaltino amesema anafurahishwa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya kanisa Katoliki na Serikali ya Tanzania na uwepo wa Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Jubilei hiyo ni ushahidi. “Natamani kuona ushirikiano huu unadumu na kuendelea kukua.”


Kwa upande wake,  Askofu Msaidizi Method Kilaini amesema anamshukuru Mungu kati ya mambo mengi aliyoyafanya aliguswa sana na ushirikiano alioupata kutoka kwa Sheikh wa Mkoa wa Kagera Haruna Kichwabute katika kutafuta amani na maridhiano kati ya Wakristo na Waislamu mkoani Kagera.


“Tumefanikiwa sana kuwaunganisha Wakristo na Waislamu mkoani kwetu, sisi ni ndugu sisi ni wamoja na ndio maana leo hii namuona Sheikh wetu wa Mkoa yupo hapa kanisani akishirikiana nasi katika Jubilei hii”

POLISI MWANZA INAWASHIKILIA WATU WAWILI KWA TUHUMA ZA MAUWAJI

 NA ALBERT G.SENGO/MWANZA

Taarifa kutoka Jeshi la Polisi mkoani Mwanza.

Tuesday, March 18, 2025

HAYA NI MAAJABU 'MAFIGA MATATU' NGARA ENEO MOJA LENYE MILIMA MITATU YA NCHI TATU TOFAUTI

 NA ALBERT G.SENGO

Karibu Halmashauri ya wilaya ya Ngara, sehemu yenye amani na watu wakarimu. eneo lenye utajiri wa utalii wa kipekee kama maporomoko ya Rusumo na Mafiga Matatu. Mafiga Matatu eneo moja lenye vilima vitatu vinavyopatikana nchi tatu tofauti, kilima kimoja kikiwa Rwanda, kingine cha pili Burundi na cha tatu Tanzania. Mwandishi wetu Jofrey John 'Suzuki Drumdrum' anasafiri zaidi ya umbali wa kilometa 391.4 hadi kijiji cha Kasange kata ya Kilusha wilayani Ngara kujionea tunu hii hazina ya utalii Tanzania.

YANGA PRINCESS YAIBABUA SIMBA QUEENS 1-0

 

TIMU ya Yanga Princess imeibuka na ushindi wa bao 1-0 na watani wao, Simba Queens katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji wa Kimataifa wa Rwanda, Jeannine Mukandayisenga dakika ya 49 akimchambua kipa wa Kimataifa wa Kenya,  Winfrida Seda Ouko.

Kwa ushindi huo, Yanga Princess inafikisha pointi 27, ingawa inabaki nafasi ya tatu ikizidiwa pointi saba na vinara, Simba Queens ambao pia ni mabingwa watetezi baada ya wote kucheza mechi 12.

JKT Queens ipo katikati yao, Simba Queens na Yanga Princess ikiwa na pointi 32 katika nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 12 — na kesho inacheza na Mashujaa Queens Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam. 

KARIAKOO DERBY WANAWAKE | Goli pekee la Jeannnine Mukandayisenga dakika ya 49 limeipa Yanga ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba Queens, katika mchezo wa ligi kuu ya Wanawake, uliopigwa kwenye Dimba la KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam.

TANGA UWASA KUBORESHA UWEZO WA UZALISHAJI MAJI KUFIKIA LITA MILIONI 60

 



Na Oscar Assenga,TANGA

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) imeweka bayana mpango mkakati wao wa kuboresha uwezo wa uzalishaji wa maji kutoka Lita Milioni 45 mpaka kufikia Lita Milioni 60 pamoja na kuongeza mtandao wa bomba la usambazaji wa maji kwa umbali wa kilomita 60

Mpango huo uliwekwa bayana leo na Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) Alawi Ahmadi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya maji iliyoanza Machi 16 hadi Machi 22, 2025 yenye kauli mbiu “Uhifadhi wa uoto wa asili kwa uhakika wa Maji”

Alisema kwamba lengo la mipango hiyo ni kuhakikisha huduma inafika kwa wakazi wote pamoja na utekelezajii wa miradi mkubwa wa uboreshaji wa miundombinu kuanzia eneo la Bwawani,Mtambo wa kutibu maji pamoja na kuendeleza mtandao wa usambazaji maji katika maeneo mbalimbali .

“Tutaboresha uwezo wa kuzalisha maji kwa asilimia 25 ukilinganisha na mahitaji kwa sasa tunaweza kuzalisha maji lita milioni 45 tunataka kuzalisha maji lita milioni 60 kutakuwa na ongezeko la maji lita milioni 15 kwenye uwezo uliopo wa mtambo wetu”Alisema

Aidha alisema kwamba wataongeza pia mtandao wa bomba la usambazaji maji kwa kilomita 60 sasa hivi wana urefu wa kilomita 862 lakini wataongeza kilimota 60 ili kufikia watu wote waliopo kwenye eneo lao lka huduma,

Alisema kwamba mradi huo ulianza tokea mwezi Julai mwaka jana na unatarajia kuisha Desemba mwaka huu ambapao kwa sasa umefikia asilimia 15 kwa maana vifaa vyote vinayotakiwa kutekeleza mradi huo vimewasili eneo la mradi na wakandarasi wamekwisha kuanza kazi kwa maeneo mbalimbali.

“Mradi huu vifaa vyote vinavyotakiwa vimewasili na gharama za mradi huo ni Sh.Bilioni 53.12 ambazo walizipata kwa kuuza hati fungani na kwa sasa utoaji huduma umefikia asilimia 93 ya wakazi wa Jiji ya Tanga, Muheza na Pangani”Alisema

Alisema kupitia kauli mbiu hiyo Tanga Uwasa inapanga kufanya tathimini na kuweka vipaumbele kwenye mambo mbalimbali ikiwemo jitahida zinazofanyika na matokeo ya uhifadhi wa mazingira ili kufanikisha kutunza vyanzo vya maji ili viweze kuwa endelevu.

“Lakini kupunguza athari za uchafuzi wa vyanzo vya maji ili kupunguza athari zake kwa watumiaji na kupunguza gharama za kuyasafisha pamoja na utekelezaji wa miradi ya kuboresha hali ya huduma kwa upande wa maji safi na taka”Alisema

Alisema pia kuendelea na utatuzi wa kero za huduma zinazowapata wananchi kwa sasa katika maeneo mbalimbali ya huduma pamoja na kutoa elimu kwa wateja juu ya huduma kwa kutumia vyombo vya habari, madawati ya huduma kwa wateja.

“Katika wiki ya maadhimisho ya wiki ya maji Tanga Uwasa imejipanga kutoa elimu kwa wateja kuhusu masuala mtambuka ya maji kutumia vyombo vya habari, madawati maalumu ya huduma kwa wateja na kuwatembelea majumbani pamoja na kutoa msahama wa tozo ya kurejesha huduma kwa wateja ambao wamesitishiwa huduma ya maji pamoja na kuruhusiwa kuweka mikataba ya kulipa madeni yao kwa awamu yaani kidogo kidogo”Alisema

Awali akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Tanga Uwasa Mhandisi Salum Hamis alisema wana mradi mkubwa wa hati fungani ambapo wana maeneo makubwa manne ambayo yatasaidia kumaliza shida ya maji katika Jiji la Tanga na miji ya Muheza na Pangani.

Alisema kwenye huo mradi wanakwenda kuupanua mtambo wa kusukuma maji mabayani kutoka uwezo wa sasa wa kusumua maji kutoka Lita 42,000 kwa siku mpaka kufika 60,000 kwa siku ikiwemo kujenga bomba linguine kubwa kutoka mabayani mpaka kituo chao cha kusafisha maji Mowe lenye kipenyo cha Milimita 600.

“Sasa hivi wana Bombo lenye milimita 600 na wanaongeza la pili na lingine ni kituo cha kusafisha na kutibu maji Mowe kwa sasa kina uwezo wa kusafisha na kutibu maji kwa uwezo wa mita za ujazo 45,000 kwa siku kwenye huo mradi tunakwenda kukiongeza kufikia uwezo wa mita za ujazo 60,000 kwa siku “Alisema

Monday, March 17, 2025

VETA TANGA WAADHIMISHA MIAKA 30 YA KUANZISHA KWAKE KWA KUFANYA UKARABATI SHULE YA MSINGI CHANGA

 



Na Oscar Assenga,TANGA

CHUO cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Jijini Tanga katika kuadhimisha miaka 30 ya kuanzishwa kwake wamefanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya ukarabati wa majengo ,Miundombinu ya Umeme ,Tehama pamoja na kwashonea sare wanafunzi wa Shule ya Msingi Changa ya Jijini Tanga.

Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo Mkuu wa VETA kituo cha Tanga,Gideon Lairumbe alisema kwamba wameamua kuadhimisha katika shule hiyo kutokana na kwamba ni miongoni mwa wanufaika wa maadhimisho ya VETA ambayo kitaifa kilele chake kitafanyika Jijini Dar es salaam kuanzia Machi 17 hadi 21 mwaka huu mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Alisema kwa ngazi ya kituo cha Tanga,VETA imefanya ukarabati darasa la awali kujenga sakafu ya nje ya shule,mfumo wa umeme,Tehama na kuziba maeneo hatarishi maeneo hatarishi ya mmomonyoko wa udongo wakati wa mvua .

Eneo jingine ambalo shule hiyo imenufaika na VETAni kuwashonea sare wanaf unzi 150,kupiga rangi na kukarabati mfumo wa jiko la kupikia zikiwamo sufuria.

Shule nyingine iliyonufaika na VETA katika maadhimisho hayo ni ya Msingi Juhudi wa mamambayo wanafunzi wenye mahitaji maalumu wameshonewa sare na kwa upande wa Mama lishe katika mitaa mbalimbali wamepewa kofia na vizibao vya kuwahudumia wateja.

“Tumefanya hivi ikiwa ni jithada za VETA kurejesha imani kwa jamii ambayo imekuwa ikiihudumia kwa kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake lakini pia kuwavuta vijana kujiunga katika mafunzo yake ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira”amesema Lairumbe.

Yussuph Ilias ambaye ni mzazi wa wanafunzi wawili wanaosoma shule ya Msingi Changa amesema ukarabati uliofanywa na VETA umesaidia kwani imebadilika na kuwa ya kisasa na kuwawezesha awanafunzi kusoma bila wasiwasi.

“Kwa mfano upande wa baharini shule ya Changa inapakana na bahari ya Hindi..kule chini kulikuw na mmompnyoko ambao ulikuwa ukitutia wasiwasi wazazi kuhusu usalama wa watoto,lakini VETA wameweka vifusi na hali imekuwa nzuri”amesema Ilias.

Makamu Mwenyekiti wa wanafunzi wa Chuo cha VETA Tanga,Mariam Hashim amewaomba wazazi kuwapeleka vijana wao waliohitimu shule za Sekondari na vyuo mbalimbali ili kupata mafunzo ya ufundi yatakayowasaidia kujiajiri.

“Mfano ni mimi nimehitimu chuo kikuu lakini nimeamua kuja VETA kupata ujuzi wa ufundi wa umakenika na kabla sijamaliza mwaka wangu wa pili tayari kuna mashirika matatu yamenifuata na yameahidi kunipa kazi”amesema Mariam.

WADAU MWANZA KUFUTURISHA WATOTO YATIMA, RC MTANDA AIPONGEZA BENKI YA NBC

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ameelezea dhamira ya uongozi wa mkoa huo kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kuandaa hafla kubwa ya futari mahususi kwa makundi maalum wakiwemo watoto yatima zaidi ya 600 kutoka vituo vyote vya kulelea watoto ili kutoa wasaa kwao kufurahia pamoja mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mtanda alielezea dhamira hiyo mwisho mwa wiki aliposhiriki hafla ya futari iliyoandaliwa na benki ya NBC mahususi kwa wateja wake wa Kiislamu jijini Mwanza.Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dini, wateja, viongozi wa serikali pamoja wafanyakazi wa benki ya NBC huku Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Rayson Foya akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, heobald Sabi kwenye hafla hiyo.

Akizungumzia mpango wa hafla ya watoto yatima jijini humo mbele ya wageni waalikwa, Mtanda alisema itahusisha jumla ya vituo 16 vya kulelea watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu ili kutoa wasaa wa kwa wadau mbalimbali jijini humo ikiwemo benki ya NBC kushiriki futari ya pamoja na watoto hao.

“Baada ya hafla hii ya NBC mahususi kwa ajili ya wateja wao hatua inayofuata ni kushiriki pamoja futari kama hii na moja ya kundi lenye uhitaji kama ambavyo miongozo ya dini yetu inavyotuongoza. Badala ya kila taasisi kuandaa shughuli kama hizi kwa kujitegemea peke yao tumeona ni vema wote tuwe na shughuli ya pamoja ili kutoa wasaa kwa wadau wenye nia kama NBC kuweza kuwafikia walengwa wenye uhitaji haswa’’ alisema.

Pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa ushirikiano wake na wateja wake wenye imani ya kiislamu hususani katika mwezi huu wa Ramadhani huku akisisitiza umuhimu wa mahusiano yanayogusa na kuheshimu misingi ya imani za dini kwa wateja wa benki, Mtanda pia aliishukuru benki hiyo kupitia matawi yake ya Mwanza na Nyanza kwa namna inavyoshirikiana na serikali katika kufanikisha mipango ya maendeleo hususani katika nyanja ya elimu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Rayson Foya alisisitiza juu ya umuhimu wa uhusiano mzuri kati ya benki hiyo na wadau wake muhimu ikiwemo Serikali na wateja. Alitumia fursa hiyo kuzungumzia huduma maalum inayotolewa na Benki ya NBC kwa wateja wa Kiislamu inayojulikana kama La Riba, ambayo inazingatia mafundisho ya Kiislamu kuhusu riba.

“NBC tunatambua kuwa Ramadhan ni nguzo muhimu ya imani ya Kiislamu, wakati wa ibada, upendo, na sadaka. Hivyo kwa kutambua thamani hiyo, futari hii ni ishara ya kuthamini mahusiano yetu sisi, wateja wetu na wadau wetu wote ikiwemo serikali, ikiwa ni njia mojawapo ya kushirikiana pamoja baraka za mwezi huu’’ alisema Foyaa

Kwa mujibu wa Foya, ushirikiano umekuwa ukiambatana na utoaji wa huduma bora kwa wateja wa benki hiyo kwa kuzingatia mahitaji maalum.

“Katika kuthibitisha dhamira yetu hii ni hivi karibuni tu tulitambulisha rasmi ‘App yetu ya NBC Kiganjani ikiwa na maboresho makubwa zaidi kulingana na mahitaji ya wateja wetu ambao sasa wanaweza kufungua akaunti popote walipo, kufanya malipo ya serikali (GEPG), kununua umeme (LUKU), na kulipa ankara mbalimbali kwa urahisi.’’ alisema.

Hafla hiyo pia ilihusisha utoaji wa zawadi kwa wageni waalikwa. Kwa wateja wa Kiislamu wa benki ya NBC jijini Mwanza, hafla hiyo ilikuwa fursa nzuri ya kufurahi pamoja na kujenga uhusiano mzuri miongoni mwao na benki hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda (kulia) akipokea zawadi maalum kutoka kwa Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Rayson Foya (katikati) wakati wa hafla futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Meneja wa benki ya NBC Tawi la Mwanza, Thomas Lijaj.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda (kushoto) akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya NBC kwa ajili ya wateja wake jijini Mwanza. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda (kushoto) akiwaongoza wageni waalikwa kupata futari wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya NBC kwa ajili ya wateja wake jijini Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda (kulia), akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC Rayson Foya (wa pili kulia), Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Sheikh Othman Ndaki (wa pili kushoto) na Meneja wa NBC Tawi la Nyanza Innocent Ngavatula (kushoto) wakati wa hafla ya Iftar iliyoandaliwa na NBC.
Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Rayson Foya (pichani) akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya NBC kwa ajili ya wateja wake jijini Mwanza. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Sheikh Othman Ndaki (wa pili kulia walioketi), viongozi waadamizi wa benki ya NBC na wafanyakazi wa benki ya NBC matawi ya Mwanza na Nyanza jijini Mwanza wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake jijini humo. 
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dini, wateja, viongozi wa serikali pamoja wafanyakazi wa benki ya NBC jijini Mwanza.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dini, wateja, viongozi wa serikali pamoja wafanyakazi wa benki ya NBC jijini Mwanza.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, dini, wateja, viongozi wa serikali na wafanyakazi wa benki ya NBC jijini Mwanza.