ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 17, 2026

MALEMA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA MI-5 JELA

Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini, Julius Malema
Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini, Julius Malema.

 

Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini, Julius Malema, ameripotiwa kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria pamoja na kufyatua risasi hadharani.

Tukio Lilivyotokea

Hukumu hiyo inatokana na tukio la mwaka 2018 wakati wa maadhimisho ya miaka mitano ya chama cha EFF yaliyofanyika katika jimbo la Eastern Cape. Katika tukio hilo, video iliyosambaa mitandaoni ilimuonyesha Malema akifyatua risasi kadhaa hewani kwa kutumia bunduki ya nusu otomatiki mbele ya umati wa wafuasi wake waliokuwa wakishangilia.

Mamlaka za usalama zilichukulia kitendo hicho kama ukiukwaji wa sheria za silaha za moto nchini Afrika Kusini, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa uchunguzi na hatimaye kufunguliwa kwa mashtaka dhidi yake.

Utetezi Wake Mahakamani

Akiwasilisha utetezi wake, Malema alidai kuwa silaha iliyotumika haikuwa mali yake na kwamba kitendo hicho kilikuwa sehemu ya kuhamasisha umati katika tukio la kisiasa. Hata hivyo, upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi ulioridhisha mahakama kwamba kitendo hicho kilikiuka sheria za nchi, na hivyo kumfanya kupatikana na hatia.

Athari za Kisiasa

Hukumu hiyo inatarajiwa kuwa na athari kubwa katika siasa za Afrika Kusini, hasa kutokana na nafasi ya Malema kama mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani. Chama chake cha EFF kimekuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana na tabaka la wafanyakazi, hivyo hukumu hiyo inaweza kuathiri mwenendo wa kisiasa ndani ya chama na taifa kwa ujumla.

Wachambuzi wa siasa wanaamini kuwa kesi hiyo inaweza kufungua mjadala mpana kuhusu nidhamu ya viongozi wa kisiasa, utawala wa sheria na matumizi sahihi ya silaha za moto nchini humo.

KOCHA BILO AFARIKI AKIWA UWANJANI JIJINI MWANZA

aa

  Athuman Bilali maarufu kama Billo.

Picha: Mtandao
Athuman Bilali maarufu kama Billo.

Aliyewahi kuwa kocha wa timu mbalimbali za soka nchini, ikiwamo Stand United ‘Chama la Wana’ na Pamba (sasa Pamba Jiji), Athuman Bilali maarufu kama Billo, amefariki dunia huku chanzo cha kifo chake kikiwa bado hakijafahamika.

Marehemu Billo hadi mauti yanamkuta alikuwa mmiliki wa kituo cha michezo pamoja na timu ya wanawake ya Bilo Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.

Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Leonard Malongo, amethibitisha kifo hicho, akieleza kuwa ni pigo kubwa kwa wadau wa soka mkoani Mwanza na nchini kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Malongo, taarifa za awali zinaeleza kuwa kocha huyo aliendelea na majukumu yake ya kawaida ya mazoezi na timu ya Bilo Queens katika Uwanja wa Shule ya Msingi Nyasaka jijini Mwanza hadi jioni ya Aprili 15, 2026. Hata hivyo, baada ya wachezaji kuondoka, aliachwa akiwa amekaa uwanjani na baadaye alikutwa amefariki eneo hilo asubuhi iliyofuata.

“Jana alikuwa uwanjani akifanya mazoezi na timu yake, lakini hadi wachezaji wanaondoka walimwacha amekaa. Asubuhi ndipo alikutwa amefariki hapohapo. Bado hatujajua chanzo cha kifo, kwani mwili wake umehifadhiwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi,” amesema Malongo.

Ameongeza kuwa taarifa zaidi kuhusu chanzo cha kifo pamoja na ratiba ya mazishi zitatolewa baada ya taratibu za kitabibu kukamilika.

Kifo cha Billo kimeacha pengo kubwa katika maendeleo ya soka, hususan katika kuinua vipaji vya wanawake kupitia timu yake ya Bilo Queens. Wadadau wa michezo wanatarajiwa kuendelea kutoa salamu za rambirambi huku wakikumbuka mchango wake mkubwa katika tasnia ya soka nchini.

Thursday, April 16, 2026

BALAA LA YANGA KWA MBEYA CITY LEO


MABINGWA watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Mabao ya Yanga SC yamefungwa na mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo mawili dakika ya saba na 82, kiungo Muivory Coast, Pacome Peodoh Zouzoua dakika ya 10 na 44, kiungo Mkongo Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 16 na beki mzawa, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ dakika ya 45’+2.

Kwa ushindi huo, Yanga SC wanafikisha pointi 47 katika mchezo wa 19 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi nane zaidi ya watani, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi.

Kwa upande wao Mbeya City baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 17 za mechi 19 pia nafasi ya 13 kwenye ligi ya timu 16.

Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.

Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.  

Wednesday, April 15, 2026

WANANCHI WASHIRIKI UJENZI WA JENGO LA HUDUMA ZA UZAZI

 

Na, Ernest Magashi

Wananchi wa Kata ya Katente, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamejitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la kusafisha eneo litakalojengwa jengo la huduma za uzazi katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe. Ushiriki huo unaakisi mwamko mkubwa wa jamii katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya, hususan kwa mama na mtoto.Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Marycelina Mbohoma, ametoa shukrani za dhati kwa Rais kwa kuidhinisha utoaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo muhimu. Amesema uwekezaji huo ni hatua madhubuti katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.Aidha, Mbohoma amewataka wananchi kuendelea kuwa walinzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.“Mradi huu ni wetu sote. Ni wajibu wetu kuulinda, kuuthamini na kutoa taarifa mapema pale tutakapoona viashiria vya hujuma,” amesisitiza.Kwa upande wake, Mhandisi wa Ujenzi wa Wilaya, Haruni Fashe, amesema jengo hilo la kisasa litagharimu shilingi milioni 660 na linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi minne.Amefafanua kuwa jengo hilo litakuwa na miundombinu muhimu ikiwemo wodi za wazazi, vyumba vya kujifungulia, chumba cha upasuaji, pamoja na huduma za watoto wachanga.Mradi huu unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya wilayani Bukombe, kwa kuhakikisha akina mama wanapata huduma salama na bora wakati wa kujifungua, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyoweza kuzuilika.Ushiriki wa wananchi katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi huu ni ishara ya umiliki wa kweli wa miradi ya maendeleo na msingi imara wa mafanikio endelevu ya sekta ya afya.Mkazi wa Katente, Evodia Simon,alisema wamejitokeza kujitolea nguvu zao kama sehemu ya kuitikia wito wa maendeleo unaotolewa mara kwa mara na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, na viongozi wengine wa serikali katika mikutano ya hadhara.

SIMBA SC YAIBAMIZA FOUNTAIN GATE 3-0

 


TIMU ya Simba SC imeonyesha ubabe wake jioni ya leo kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara uliopigwa kwenye dimba la Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha. 


Simba ilianza kuonesha makali yake mwishoni mwa kipindi cha kwanza, ambapo kiungo fundi kutoka Zambia, Clatous Chama alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 45+7 kwa mpira uliowaacha mabeki wa Fountain Gate wakitazamana. 


Kipindi cha pili hakikuwa na huruma, kwani winga hatari kutoka Senegal, Libasse Gueye aliongeza bao la pili dakika ya 53, akimalizia shambulizi la kasi lililoacha mashabiki wa Simba wakishangilia kwa furaha kubwa. 


Shinikizo la Simba liliendelea kuwa kubwa na kuwavuruga wapinzani wao, hali iliyosababisha kiungo mzawa, Shaaban Mgunda kujifunga dakika ya 71 wakati akijaribu kuokoa hatari langoni kwake—bao lililozika matumaini ya Fountain Gate kabisa. 


Kwa ushindi huo, Simba SC sasa imefikisha pointi 39, ikiendelea kushikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikiwa nyuma kwa pointi tano dhidi ya vinara na mabingwa watetezi, Young Africans SC baada ya kila timu kucheza mechi 18. 


Kwa upande wa Fountain Gate, hali inaendelea kuwa tete baada ya kupoteza mchezo wao wa 10 kati ya 18 walizocheza hadi sasa. 


Wakiwa na sare nne na ushindi nne pekee, wanabaki na pointi 16, wakishika nafasi ya 14 katika ligi yenye timu 16—eneo hatarishi kabisa. 


Vita ya kushuka daraja yazidi kupamba moto 

Kwa mujibu wa kanuni za ligi, timu mbili za mwisho zitashuka moja kwa moja daraja. 

Hata hivyo, zile zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14 zitapata nafasi ya kupambana kujiokoa kupitia mechi za mtoano za nyumbani na ugenini. 

Mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu, huku atakayeshindwa akilazimika kupambana tena na timu kutoka Ligi ya Championship katika hatua nyingine ya mchujo—mapambano ya mwisho yatakayobainisha nani atasalia kwenye ligi kuu msimu ujao.

WIZARA YA MAMBO YA NJE KUANDAA UTARATIBU WA KUVUNA MAARIFA YA MABALOZI WASTAAFU


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetakiwa kutumia hazina ya maarifa na uzoefu kutoka kwa Mabalozi Wastaafu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuimarisha diplomasia ya nchi. 


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati anafungua kikao cha mashauriano kati ya uongozi wa Wizara na Mabalozi Wastaafu kilichofanyika jijini Dar Es Salaam Aprili 15, 2026. 

"Wizara tumeanzisha utaratibu wa kuwa na vikao vya mara kwa mara na Mabalozi Wastaafu ili kuvuna maarifa na uzoefu wao kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia ili ulete nanufaa katika nyanja mbalimbali kama vile, siasa, ulinzi na usalama, uchumi, biashara, uwekezaji na utalii". Balozi Kombo alisema.


Balozi Kombo ametaja mifano ya maeneo ambayo angependa Mabalozi Wastaafu wachangie maarifa na uzoefu walio kuwa nao ili maeneo hayo yaendelee kuwa na manufaa zaidi kwenye nchi..


Maeneo hayo ni pamoja na mwenendo wa ufanyaji wa biashara baina ya Tanzania na nchi nyingine, hususan zilizopo barani Afrika.


Utekelezaji wa Dira 2050 ambayo inalenga uchumi wa Dola bilioni moja, ni eneo lingine muhimu ambalo maarifa ya Mabalozi Wastaafu yanahitajika ili kuhakikisha 

utekelezaji wake unakuwa wa ufanisi.


Waziri Kombo ameongeza kuwa mabadiliko yanayoendelea duniani 

hususan, maendeleo ya kidigitali yanahitaji mikakati thabiti ili nchi iweze kunufaika na kuwa na mipango madhubuti ya kukabiliana na athari zake. Haya yote yanahitaji mawazo ya pamoja ili kuyaendeea kwa ufanisi.


Eneo lingine ambalo Waziri  Kombo alisisitiza umuhimu wa kupata uzoefu wa Mabalozi Wastaafu ni siasa za ulimwengu ambazo zimekuwa hazitabiriki na zinasababisha madhara mbalimbali, hususan katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.


Aidha, uzoefu wa Mabalozi Wastaafu unahitajika katika kuendeleza na kuimarisha taswira nzuri ya nchi na hasa nchi inapopewa dhamana ya majukumu ya kimataifa. Balozi Kombo alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika mwaka 2028 na hivyo maarifa yao ni muhimu ili kuhakikisha nchi inatekeleza jukumu hilo kwa ufanisi. 

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo alisema Wizara inaangalia uwezekano wa kuanzisha utaratibu rasmi kupitia   Ofisi ya Rais-UTUMISHI ili ushirikishwaji wa Mabalozi Wastaafu uwe unatambulika rasmi.



Monday, April 13, 2026

HORMUZ | MAZUNGUMZO YA HORMUZ NI "MECHI ILIYOISHA KABLA HAIJAANZA"

 AZAM MEDIA LTD