ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, April 15, 2026

SIMBA SC YAIBAMIZA FOUNTAIN GATE 3-0

 


TIMU ya Simba SC imeonyesha ubabe wake jioni ya leo kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara uliopigwa kwenye dimba la Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha. 


Simba ilianza kuonesha makali yake mwishoni mwa kipindi cha kwanza, ambapo kiungo fundi kutoka Zambia, Clatous Chama alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 45+7 kwa mpira uliowaacha mabeki wa Fountain Gate wakitazamana. 


Kipindi cha pili hakikuwa na huruma, kwani winga hatari kutoka Senegal, Libasse Gueye aliongeza bao la pili dakika ya 53, akimalizia shambulizi la kasi lililoacha mashabiki wa Simba wakishangilia kwa furaha kubwa. 


Shinikizo la Simba liliendelea kuwa kubwa na kuwavuruga wapinzani wao, hali iliyosababisha kiungo mzawa, Shaaban Mgunda kujifunga dakika ya 71 wakati akijaribu kuokoa hatari langoni kwake—bao lililozika matumaini ya Fountain Gate kabisa. 


Kwa ushindi huo, Simba SC sasa imefikisha pointi 39, ikiendelea kushikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikiwa nyuma kwa pointi tano dhidi ya vinara na mabingwa watetezi, Young Africans SC baada ya kila timu kucheza mechi 18. 


Kwa upande wa Fountain Gate, hali inaendelea kuwa tete baada ya kupoteza mchezo wao wa 10 kati ya 18 walizocheza hadi sasa. 


Wakiwa na sare nne na ushindi nne pekee, wanabaki na pointi 16, wakishika nafasi ya 14 katika ligi yenye timu 16—eneo hatarishi kabisa. 


Vita ya kushuka daraja yazidi kupamba moto 

Kwa mujibu wa kanuni za ligi, timu mbili za mwisho zitashuka moja kwa moja daraja. 

Hata hivyo, zile zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14 zitapata nafasi ya kupambana kujiokoa kupitia mechi za mtoano za nyumbani na ugenini. 

Mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu, huku atakayeshindwa akilazimika kupambana tena na timu kutoka Ligi ya Championship katika hatua nyingine ya mchujo—mapambano ya mwisho yatakayobainisha nani atasalia kwenye ligi kuu msimu ujao.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment