Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza jambo kwa msisitizo wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Kushoto ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula, Leo 8 Julai 2018. (Picha zote Na Mathias Canal-WK)
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza na wazee kijijini Nyamatongo wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Leo 8 julai 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba, Naibu waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa kijiji cha Nyamatongo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Leo 8 Julai 2018.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza jambo wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baada ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Leo 8 Julai 2018.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana (Kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha ushirika Nyamatongo Ndg Willium Elikana mara baada ya kuridhia mgogoro kumalizika.
Na Mathias Canal,
Sengerema-Mwanza
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles
Tizeba pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt
Angeline Mabula wametatua mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi
ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17.
Mgogoro huo umemalizika kwa
maelewano ya pande zote mbili kuwa na kauli moja ambapo Mwenyekiti wa kijiji
hicho amekubali kuketi meza moja na Uongozi wa chama hicho cha ushirika ili
kukubaliana namna bora ya kuchochea Maendeleo katika kijiji na Taifa kwa ujumla
badala ya kuendeleza mgogoro usiokuwa na maslahi kwa pande zote.
Alisisitiza umuhimu wa ushirika
nchini ambapo aliwaeleza wananchi hao kutoendeleza vita ya kutokuwa na
maelewano kwani kufanya hivyo kunarudisha nyuma shughuli za Maendeleo ya kijiji
na Taifa kwa ujumla wake.
Pia, Dkt Tizeba ametangaza Kiama
kwa maafisa ugani wanaokaa maofisini badala ya kuwasaidia wakulima kwenye hatua
muhimu za uandaaji wa shamba na hatimaye wakati wa Kilimo.
Katika mkutano huo Naibu Waziri
wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angelina Mabula aliwataka
wananchi hao kuwa na utamaduni wa kuketi pamoja na kujadili changamoto
zinazowakabili ili kuzitatua kwa manufaa yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa migogoro kama
hiyo haihitaji sintofahamu ya mashitaka ya muda mrefu kwani kufanya hivyo ni
kutengeneza uhasama usio kuwa na sababu ilihali wote ni watanzania.
Dkt Mabula aliongeza kuwa
serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imekusudia kutatua changamoto zote
zinazohusisha wananchi katika migogoro ya ardhi pamoja na kadhia zingine zote.
Mgogoro huo ambao ulianza tangu
mwaka 2001 umekuwa na hatua za kushitakiana baina ya Mwenyekiti wa Kijiji cha
Nyamatongo dhidi ya Chama cha ushirika Nyamatongo katika maeneo mbalimbali
tangu mwaka 2001 ambapo awali ulitolewa maamuzi katika ngazi ya baraza la
kijiji baadae baraza la kata na hatimaye Baraza la Ardhi la Wilaya ya Sengerema
ambalo ndilo liliamua kuvunja maamuzi yote ya baraza la kijiji na Kata ili
kuanza upya usikilizwaji wa kesi hiyo.
Mara baada ya kumalizika kwa
mgogoro huo wananchi kijijini hapo wamempongeza Waziri wa Kilimo Mhe Dkt
Charles Tizeba pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe
Dkt Angelina Mabula kwa kuzuru kijijini hapo hatimaye kutatua mgogoro huo ambao
umekuwa sugu kwa miaka 17.
Aidha, katika mkutano huo
wananchi wamepata nafasi ya kueleza kero mbalimbali zinazowakabili kijijini
hapo ikiwemo ukosekanaji wa maji safi na salama, huku wengine wakieleza
kusikitishwa na maafisa ugani kuketi maofisini pasina kuzuru kwa wakulima ili
kuwafundisha mbinu bora za Kilimo.